Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Njia nne za kumaliza vita vya Iran
Katika uchambuzi wetu tunaangazia njia tofauti wa jinsi vita vya Iran vinaweza kutamatika, huku kukiwa na hofu wa Iran kugeuza vita hivi kuwa "vita vya rasilimali ya maji" dhidi ya jirani zake eneo la ghuba.
Katika gazeti la Marekani la The New York Times, taarifa ya uchambuzi wa "vita hivi vitaisha vipi?" inaelezea njia nne ambazo vita hivi vinaweza kumalizika.
Njia ya kwanza kulingana na uchambuzi huo ni kubadilishwa kwa utawala wa Iran.
Hii inaweza kufanyika iwapo kutakuwa na maandamano makubwa yatakayoungwa mkono na jeshi na polisi wa Iran wakiungwa mkono na Marekani na Israel ili kuipindua serikali ya taifa hilo.
Gazeti hilo linasema "wazo hili halifai kupuuziliwa, ila si ya kutegemewa, kwa sababu utawala wa Iran una uwezo wa kusalia madarakani."
Njia ya pili ni mabadiliko katika utawala. Hii ni kumaanisha kuwa utawala unasalia ulivyo lakini unafuata matakwa ya Israel na Marekani. Ila hili huenda likakuwa vigumu kuafikiwa kutokana na msimamo wa kiongozi mkuu wa sasa Mojtaba Khamenei. Ni vigumu kujua iwapo kiongozi wa sasa atakubali kusalimisha silaha za nyuklia, makombora na kusitisha ufadhili wa makundi tofauti kama Hezbollah.
Njia ya tatu ambayo vita hivyo vinaweza kumalizika, ni kwa pande zote kujitangaza mshindi. Uchambuzi wa gazeti hilo la The New York Times linasema kuwa Trump na Netanyahu hawajaafikia malengo yao ya vita hivyo.
"Ni vigumu kufikiria kuwa vita hivyo vitakamilika kabla ya Marekani na Israel kushambulia maeneo yaliyo na silaha ya nyuklia yaliyosalia nchini Iran, na huenda hii ikaleta mabadiliko katika uongozi wa taifa hilo."
Njia nyingine ni "kuangusha serikali ya Iran". Hii ni kama kile kilichotokea Syria.
Kulemaza shughuli za serikali ambapo maeneo tofauti yatakuwa na serikali huku maeneo mengine yatakuwa yanajitawala, na hii itachochea taifa hilo kuingiliwa kijeshi na mauaji ya kimbari kutokea.
Mwandishi wa uchambuzi huo anasema hili ni wazo ambalo Israel inaweza kutekeleza, ila huenda likapingwa na Marekani na mataifa ya ghuba, kwani Iran kuingiliwa kijeshi kutaharibu amani ilioko mashariki ya kati.
Njia ya mwisho ni iwapo Marekani itaiteka kisiwa cha Kharg, ambacho hutumika kusafirisha 90% ya mafuta ya Iran, na kupunguza mapato ya serikali ya Iran yanayotokana na mafuta. Hii itaifanya Iran kushindwa kuindesha serikali yake, kutowalipa wafanyikazi wake mishahara pamoja na wanajeshi.
Hakuna uwezekano wa Putin kushinda vita hivi
Katika uchambuzi wa gazeti la Uingereza la The Telegraph, katika taarifa inayosema "Putin hashindi vita hivi, dunia inaporomoka mbele yake" inachambua athari ya vita vya Israel na Marekani dhidi ya Iran kwa Urusi, ikielezea kuwa "ni mchanganyiko wa "wakati mzuri na mbaya"
Gazeti hilo linasema kwamba ongezeko la bei ya mafuta linaongeza mapato ya Urusi. Anabashiri kwamba bei ya pipa la mafuta ya Urusi inaweza kufikia dola 80, jambo ambalo linaweza kuleta faida ya ziada ya kati ya dola 5 hadi 6 kwa kila pipa.
Alisema kwamba "mwelekeo wa bei ya mafuta unategemea kuendelea kwa mzozo katika mlango wa bahari wa Hormuz, iwapo utasalia kufungwa au kuwa wazi"
Uchambuzi huo unaongezea kuwa "faida hii ni ndogo sana ikilinganishwa na hasara ya vita vya Iran kwa Putin, kwani rais wa Urusi anawapoteza washirika wake na hawezi kuwaokoa," ikirejelea serikali za Venezuela, Iran, na Syria.
Uchambuzi huo unaongezea kuwa "Vikosi vya serikali mbili muhimu kwa Moscow, Venezuela na sasa Iran, vimeathirika pakubwa. Vilevile, imesalia muda mchache kabla utawala wa kikomunisti huko Cuba kuanguka, hiki kikiwa kisiwa ambacho Putin anakiona kama mshirika wake wa karibu."
Aidha vita vya Ukraine vimedhoofisha nguvu za kijeshi na ushawishi wa kidiplomasia wa Urusi duniani, na kupunguza uwezo wa Urusi wa kutuma vikosi vyake kwa haraka maeneo mbali mbali.
Hii inaipa nguvu China na sasa "Moscow haiwezi kushindana na utajiri wa Beijing."
Vita vya rasilimali ya maji
Mwandishi Roger Boyes anasema "vita vya maji vya Tehran ni mfano wa kutisha"
Mwandishi huyo anaelezea kuwa Iran "iko karibu kuanguka," kwa sababu "vikosi vyake vimechoka na vituo vyake vya kijeshi viko "wazi" kwa mashambulizi ya Marekani na Israeli."
Pia anaonya juu ya uwezekano kwamba Tehran inaweza kutumia "vita visivyo sawa," hii inamaanisha kulenga miundombinu ya kiuchumi katika mataifa ya ghuba.
"Nchi za Ghuba ndizo kiungo dhaifu zaidi katika muungano wa mataifa ya Magharibi dhidi ya Iran, ni mataifa tajiri lakini dhaifu. Kwa hivyo, Tehran inataka kuchochea vita ndani ya nchi hizi na kuharibu sifa zao kama eneo salama. Pia inataka kufunga njia za baharini, na kuharibu uchumi wa dunia."
Uchambuzi huo pia unaonya kuwa "kukata usambazaji wa maji safi kwa nchi za Ghuba,kunaweza kufanya maji kuwa silaha ya vita"
Mwandishi wa uchambuzi huo alitaja shambulio la Iran kwenye kituo cha maji nchini Bahrain mwishoni mwa wiki hii, pamoja na uharibifu wa miundombinu mingine ya kuondoa chumvi kwa maji huko Kuwait na Falme za Kiarabu, kunaonyesha "kuibuka kwa njia mpya ya vita kati ya Iran na majirani zake eneo la Ghuba."
Uchambuzi huo unamalizia kwa kusema kuwa "kiongozi mpya wa Iran anaonekana tayari kufanya maji kuwa silaha ya vita katika eneo hilo."
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula