Kenya inavyosogea kwenye siasa za maneno ya nguoni

    • Author, Asha Juma
    • Nafasi, BBC Nairobi
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Tahadhari: Kwa sababu zisizoepukika, makala hii imetumia maneno unayoweza kuyachukuliwa kuwa matusi ya nguoni.

Nchini Kenya, ushindani wa kisiasa sio tu kwamba unahusisha sera au utendakazi, la hasha, unazidi kuwa ni nani anayeweza kuwa na matusi makubwa zaidi ya mwingine.

Kuanzia mikutano ya kampeni hadi bungeni huku mitandao ya kijamii ikiwa haijasazwa, tabaka la kisiasa nchini limeendeleza utamaduni wa kufanyiana dhihaka na kutupiana maneno ya nguoni. Maneno haya kwa hadhi ya viongozi wanaohusishwa yanatajwa kama matusi ama maneno ya nguoni kwa ukali wake.

Kile kinachopaswa kuwa mashindano ya mawazo ya kuleta mabadiliko nchini, yamegeuka kuwa ukumbi wa maneno machafu na ya nguoni.

Matukio ya hivi karibuni zaidi yakionyesha jinsi hali hii inavyoendelea kuwa donga sugu. Rais William Ruto ameonekana hadharani akirushiana cheche za maneno makali na kambi ya upinzani kiasi cha kuanza kukosolewa vikali na makundi mbali mbali yaliyoonekana kukerwa na tabia hiyo. Lakini kwanini wanasiasa wa Kenya wameamua kutumia maneno haya badala ya sera?

Utumiaji wa maneno ya nguoni kwa wanasiasa

Yanatumiwa kama zana za kudhalilisha watu. Wanasiasa mara nyingi hutumia dhihaka, majina ya kejeli, na lugha za kukashifu ili kudhoofisha uaminifu wa wapinzani. Kwa kufanya hivyo, viongozi hujaribu kutengeneza mtazamo wao kwa umma bila kuhusisha masuala muhimu na kutumika kama njia ya mkato katika mawasiliano ya kisiasa ambayo ni rahisi kukumbuka kuliko mabishano ya kisera na masuala ya msingi zaidi yanayohusu hadhira.

Matusi hufanya kazi kama njia ya uhamasishaji. Katika mikutano ya hadhara na mikusanyiko ya watu, lugha zenye msisimko wa aina hii huvutia wafuasi. Na matokeo yake, kicheko na hasira inakuwa sehemu ya utendaji, na kuwa utambulisho wa kundi fulani. Mwanasiasa anapomtusi mpinzani, inakuwa ni kama kuchora mstari wa wazi kati ya "sisi" na "wao," na bila shaka yoyote, kunafifisha msisimko wa kuelezea sera alizonazo dhidi ya upande mwingine.

Mazingira ya kisiasa ya Kenya kihistoria yamezingirwa na mifarakano ya kikabila, na wakati mwingine yanatokana na dhana potofu au lugha ya siri. Hata kama si ya kikabila kwa uwazi, wakati mwingine hueleweka zaidi na hadhira ya eneo husika. Hili hufanya matusi kuwa na nguvu zaidi—na vile vile hatari—kwa sababu yanaweza kuzidisha migawanyiko na kuongeza uhasama kati ya pande mbili.

Cheche za matusi

Katika matukio ya hivi karibuni zaidi, kumeshuhudiwa mojawapo ya kampeni mbaya zaidi za kisiasa nchini Kenya zilizogonga vichwa vya habari, viongozi wakuu wa nchi walianza kurushiana matusi ya nguoni, kutukanana hadharani na kudhalilishana kwa kurushiana maneno machafu.

Rais Ruto na Kiongozi wa chama cha The Democracy for the Citizens Party (DCP) ambaye pia alikuwa naibu wake wa zamani Rigathi Gachagua walikuwa mstari wa mbele kwa aibu hii hasa kwa wale ambao wamekuwa wakiwachukulia kama kioo cha jamii.

Gachagua alionekana kukosoa uongozi wa Rais Ruto.

Rigathi Gachagua alitoa kauli kali dhidi ya Rais Williama Ruto kwa madai kuwa ni upinzani kufichua kile anachoeleza kuwa uongozi mbovu na ufisadi uliokithiri hasa katika sekta ya afya.

Gachagua, alimshutumu Rais Ruto kwa kuhusika na madai ya kutaka "kuiiba" au kuimiliki Nairobi Hospital, moja ya hospitali tajika ya kibanfsi katika Afrika Mashariki na Kati inayosimamiwa na Chama cha Hospitali cha Kenya.

"Tukikubalia wewe uibe Nairobi hospital, utakuja kuiba makafani ya Lee na hatutaki tufike hapo," Gachagua alisema.

Nairobi Hospital imejikuta katika sakata ya kile kinachodaiwa kuwa ufisadi na Rais kwa upande wake alijitokeza na kuapa kulinda Hospitali ya Nairobi kutokana na kile anachokiita walaghai na wadanganyifu.

Hata hivyo, upinzani umedai kuwa hautakoma kumfuatilia Rais William Ruto hadi utakapomuondoa afisini katika uchaguzi ujao wa urais.

''Tutahakikisha William Ruto hutalala, kwa muda wa miezi 15 ijayo. Utalala ukifikia Sugoi, Tutakuanika na hawa vijana wangu. Si unaona vile amekonda, mpaka masikio inafanya nini?... Na bado, Bado…, Gachagua alisema.

Na kama haitoshi, Gachagua aliendelea kutoa maneno makali dhidi ya Rais Ruto.

"Tunapoua nyoka, tunaua hata mayai, tutamwondoa Kasongo na watu wake wote, ndiyo maana tulianzisha kampeni ya 'fagia wote'," alisema Gachagua.

Lakini kwa sababu siasa ni mchezo mchafu wa nipe nikupe, baada ya madai hayo, Ruto aliamua naye kurusha cheche zake.

"Mtu mwenye ana Pepo ya ukabila na Chuki, na kisirani anatuambia nini kama Wakenya", Ruto alijibu.

"Mtu ambaye ameenda kwa kitanda cha ndugu yake ambaye alikuwa anakufa, anaenda kumlaghai katika Wosia wake", Ruto alisema akiendelea kumjibu Gachagua.

"Wezi, mnaiba kutoka kwa ndugu zenu wenyewe, yatima na wajane. Unataka kutupa msomo. Unazunguka makanisani, barabara, mazishini ati unatuongelesha. Unatuongelesha kitu gani"? Ruto aliendelea kutupa cheche zake.

Lakini pia, Rais Ruto alionekana kumlenga mwanasiasa mwingine wa upinzani ambaye hakumtaja jina.

"Nyinyi munakula mpaka tumbo linapasuka. Mumekula mpaka kichwa kimevimba na kiburi. Nataka niwaambie, tafadhali nendeni mujiangalie kwenye kioo. Muende muangalie mnavyokaa. Kichwa kimevimba, tumbo ndio hilo karibu linararua mashati. Tafuteni gym kwanza muende kufanya mazoezi kidogo. Na mupunguze kula chakula kingi. Ndiyo muache kulala kwenye mikutano. Hata munaharibu hewa huko kwa mikutano mukiwa mumelala, bure kabisa", Ruto alisema.

Hata ingawa hakutajwa jina, lakini yupo aliyesimama na kumjibu Rais Ruto.

"Kwanza kabisa mimi sili chakula kwa bibi yako, ama kwa watu wako. Mimi nala ndizi kule Kisii kwetu… Sasa kama hiyo ndiyo inakusumbua. Mbona mimi sijakuja kukuuliza wewe mbona umekonda," Fred Matiang'i, mgombea urais wa chama cha Jubilee alijitokeza na kujibu madai ya Rais Ruto.

Lakini ikumbumbukwe kuwa utamaduni huu wa kurushiana cheche za matusi sio jambo geni kwa siasa za Kenya. Kabla ya maridhiano nchini Kenya mwaka 2018 maarufu kama 'handshake', Raila Odinga na Uhuru Kenyatta pia nayo waligonga vichwa cha habari kwa kurushiana maneno makali wakati wa kipindi kigumu cha baada ya uchaguzi wa mwaka 2017.

'Handshake' kwa kiasi fulani, ilichochewa na dhana kwamba uhasama wa kisiasa ulikuwa unaongezeka ikiwa ni pamoja na matusi na kulikuwa na dhana kuwa nchi inaelekea kwenye ukosefu wa utulivu.

Hata hivyo, miaka kadhaa baadaye, tabia hii bado inaendelea kujitokeza.

Gharama ya siasa za matusi

Wakati tabia hii inaendelea kujitokeza, ukweli usiopingika ni kwamba inagharama.

Wanasiasa wanapojitumbikiza katika siasa za matusi, kuna uwezekano mkubwa wa kuondoa mijadala ya mambo ya msingi ambayo watu wangependa kusikia na kuibadilisha kuwa migogoro ya kibinafsi.

Pia wananchi wanakosa fursa ya kufahamu ukweli wa mambo ya msingi wanayostahili kufanya maamuzi kwa uelewa. Na pale tabia hii inapozidi, umma unakosa uaminifu kwa taasisi zake na kufanya tabia ya kurushiana matusi kuwa jambo la kawaida.

Wanasiasa kutumia lugha ya matusi, hasa katika siasa za Kenya, ni wakati ambapo wananchi hupata fursa ya kufahamu mambo yaliyokuwa yamefanywa kisiri, lakini sasa yanatolewa paruwanja kwa sababu kila mmoja yuko mbioni kutaka mwenzake adhalilike kwa ile ile tu nia moja, hila ya kutaka kuharibiana sifa.

Na inapofika hatua hii, bila shaka, wanasiasa wanaweza kupelekana mahakamani. Kwa mfano, Raila Odinga vs Samuel Kivuitu (zama za 2007–2010).

Dai: Taarifa zinazoashiria Raila Odinga alihusika katika makosa ya kiuchaguzi.

Matokeo: Mahakama ilitoza fidia ya mamilioni na pengine funzo likiwa shutuma kali za kisiasa lazima ziungwe mkono na ushahidi, vinginevyo, mtu anaweza kujipata kwenye mkono wa sheria.

Lakini pia cheche za namna hii zinaweza kutafsiriwa kama maneno ya chuki dhidi ya mwingine au jamii fulani. Na vile vile ukajipata mashakani kisheria.

Lakini, kuna wale waliokataa kukaa kimya na kujitokeza kushutumu maneno ya Rais Ruto kwa mabadilishano ya matusi ikiwa ni pamoja na viongozi wa kidini, makundi ya kiraia na hata viongozi wa upinzani.

Hata hivyo, Rais Ruto kwa upande wake, ameonekana kuwasuta kwa kukaa kimya wakati upinzani ulikuwa unamshambulia kwa maneno machafu na kusema kuwa palipofikia, hatanyamaza tena.

Ruto alisema amekuwa kimya kwa muda mrefu sana, msimamo alioubainisha kuwa ulichukuliwa kimakosa na upinzani kuwa udhaifu.

"Wale nitawashughulikia. Wamenitukana kwa miaka miwili mfululizo. Juzi nimewajibu tu siku moja, na hata si kuwajibu ipasavyo, niliwaambia tu kuwa tabia yenu sio nzuri," alisema.

Hadi kufikia sasa, viongozi wa kisiasa wanachaguo la kuamua kuendelea kutumia matusi kama silaha yao au kuanzisha utamaduni wa majadiliano yenye tija, sera na kadhalika ili hakikisha uwajibikaji na udumishaji wa heshima miongoni mwao.

Maneno yanayozungumzwa na wanasiasa kwao yanaweza kuwa jukwaa la kisiasa tu lakini athari yake kwa umma ni zaidi ya hilo. Yanaweza kuongoza umma katika masuala ya msingi, kuashiria maadili ya taifa ya njia ya uongozi.

Lakini umma pia, unajukumu katika kusikiliza kinachosemwa na kujifanyia maamuzi ama ni cha msingi kwao au la, na iwapo watasimamia misimamo yao. Hili linaweza kusaidia kuamua aina ya siasa wanayotaka.

Lakini hadi Kenya itakapofikia kiwango hicho, kuna hatari ya siasa za nchi kuendelea kwa mtindo unaoshuhudiwa, sio tu mashindani ya madaraka lakini pia nani mwenye matusi makali zaidi ya mwingine.