Je, wajua hatari ya kutumia dawa za kupunguza maumivu bila ushauri wa daktari?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwenye mitandao ya kijamii katika siku za hivi karibuni, haswa kitengo cha kuacha maoni kwenye Facebook,Instagram na Tiktok, msemo 'umemeza Brufen' umesheheni pakubwa.
Nchini Kenya msemo huu ulipata umaarufu baada ya mchekashaji mmoja kutania jinsi kina mama wakiafrika hutumia dawa ya kupunguza maumivu aina ya Brufen kutibu kila maumivu ya mwili kabla ya ugonjwa kuzidi.
Dawa aina ya Brufen, ambayo huenda ka jina la utengenezaji ibuprofen mara nyingi hununuliwa katika duka la dawa na hutumika kupunguza maumivu ya mwili, maumivu ambayo huletwa na hedhi, maumivu ya meno, maumivu ya misuli na kichwa.
Lakini je wajua hatari ya kutumia dawa za kupunguza maumivu ya mwili mara kwa mara bila maelekezo ya daktari?
Daktari Goody Gor kutoka nchini Kenya, anasema kuwa mtu anafaa kumeza dawa hizi za kupunguza maumivu iwapo tu maumivu yamezidi. "Kama unaweza kuvumilia uchungu si lazima umeze dawa hizi lakini maumivu yakizidi ni vyema upate ushauri wa daktari"
Ila wengi huogopa kufika hospitalini kwa sababu ya maumivu ambayo yanaweza kusuluhishwa kwa kumeza vidonge ambavyo vanapatikana dukani.
Maumivu ya kichwa hutokana na msongo wa mawazo, shinikizo la damu, kufanya kazi kwa muda mwingi, kutokula lishe bora, kutokunywa maji ya kutosha, na iwapo unajipata unameza dawa hizi mara kwa mara au kila siku ili mwili wako ufanye kazi ni vyema basi kuna tatizo anaema Dkt Gor.
Katika utafiti uliofanywa na wanasayansi kutoka chuo kikuu cha Liverpool na London nchini Uingereza na kuchapishwa kwenye jarida la The Lancet,wanaonya kuwa matumizi ya dawa za kupunguza maumivu miongoni mwa vijana kwa muda mrefu, huenda ikaathiri afya yao ya akili.
Kulingana na ripoti hiyo iliyotolewa mwaka wa 2023, vijana chini ya umri wa miaka 25, ambao wanamauimivu kupita kiasi, 29% kati yao huwa na matatizo ya afya ya akili katika maisha yao ya mbeleni.

Chanzo cha picha, Getty Images
Matumizi ya dawa aina ya Paracetamol (Panadol) kwa muda mrefu huleta uvimbe wa tumbo au 'gastritis.'
Asprin huathiri jinsi ini hufanya kazi. "Iwapo utachukua tembe nane za asprin kila siku, basi ini lako hapo baadaye litapata matatizo. Ini lina majukumu mengi mwilini, na iwapo itapata changamoto, basi viungo vingine vya mwili vitaathirika kama misuli ya mwili, moyo na akili"
Matumizi ya Brufen

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Matumizi ya Brufen kwa wingi huleta uvimbe wa tumbo na baadaye vidonda vya tumbo. Dawa hii pia husababisha kiungulio "heartburn", maumivu ya tumbo, kutapika, kuendesha na hali ya kufungana kwa choo.
Iwapo Brufen itatumika kwa muda mrefu, baadaye huathiri figo na kulemaza kazi ya figo, baadaye mtu hushuhudia kufura kwa miguu, shinikizo la damu na maradhi ya moyo.
Matumizi ya dawa hizi pia hupunguza uzito wa mifupa ya mwili, kwa hivyo mtu huwa katika hatari ya kuvunjika viungo na huchukua muda kupona.
"Brufen huathiri afya ya utumbo, moyo, figo,ngozi,mifupa, huathiri kazi ya dawa zingine unazotumia, mzunguko wa hedhi,homoni kwa hivyo dawa hizi zinafaa kutumiwa iwapo kuna ulazima"
Ubongo pia huathirika kutokana na matumizi ya madawa haya bila maelekezo ya daktari huleta ukungu katika ubongo,mabadiliko ya hisia.
Katika chapisho lingine la The Lancet, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Oxford walichunguza madhara yanayoletwa na matumizi ya dawa ya kupunguza maumivu kupita kiasi.
Watafiti hao walichunguza zaidi ya rekodi 353,000 za wagonjwa kutoka vituo 639 tofaut vya afya, ili kutathmini athari za dawa za kupunguza maumivu ambayo hayana kiungo cha kusisimua misuli 'steroids'
Watafiti hao waliwachunguza wagonjwa waliopewa dozi ya miligramu 150 ya diclofenac na miligramu 2400 ya ibuprofen kwa siku.
Matokeo yao yalibaini kuwa kati ya watu elfu moja waliotumia dawa hizo watatu kati yao walipata mashambulizi mabaya ya moyo, na moyo kushindwa kufanya majukumu yake.
"Dawa bandia"
Kutokana na kutokuwa na umakini wa maafisa wa kudhibiti viwango vya dawa, dawa nyingi bandia zinapatikana katika duka za dawa kulingana na Dkt Goody Gor, anaelezea kuwa iwapo mtu atatumia dawa hizi kwa wingi, madhara yake yatakuwa mabaya.
"Ukimeza dawa bandia utajipata unatumia dawa zaidi kutibu madhara ya dawa za awali, kisha dawa hizi pia zina madhara yake, kwa hivyo unajipata katika mzunguko wa kumeza dawa"
Dawa ipi bora ya kupunguza maumivu?

Chanzo cha picha, Getty Images
Goody Gor anashauri kuwa njia bora ya kukabiliana na maumivu ya mara kwa mara ni kuhakikisha unapata lishe bora na kutumia njia asili haswa kutibu maumivu ya kichwa.
"Hakuna dawa salama, ila Paracetamol, au acetaminophen, si hatari sana kwa afya yako iwapo itatumika kwa viwango vya chini. Mtu anafaa kutumia gramu mbili kwa siku, hizo ni tembe nne kwa siku, ili kutodhuru ini lako"
Kufanya mazoezi kila mara pia kunapendekezwa ili kunyorosha misuli ya mwili na kuzuia maumivu.
Kunywa maji mengi pia husaidia kuboresha afya ya mifupa yako na kuzuia maumivu.
Nafaa kutumia dawa ya kupunguza maumivu kwa muda gani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Iwapo umepata maumivu kutokana na kufanya kazi nyingi, Dkt. Goody Gor anashauri kupumzika kwanza kabla ya kumeza dawa na kutumia njia mbadala kama kupata usingizi wa kutosha nakunywa maji mengi.
"Iwapo ni maumivu ya kichwa kutokana na uchovu wa kawaida, kumeza dawa mara moja kwa siku inafaa kutosheleza kumaliza maumivu hayo ila maumivu yakizi ni bora mtu atafute ushauri wa daktari"
Iwapo maumivu yatadumu zaidi ya siku moja ni vyema kumwona daktari ili kubaini chanzo cha maumivu hayo.
Njia sahihi ya kumeza dawa za kupunguza maumivu

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na Dkt Goody Gor, wakati wa kumeza dawa hutofautiana.
Anaelezea kuwa kuna dawa ambazo hufanya kazi haraka iwapo itamezwa kabla ya kula au baada ya kula lakini ni bora kumeza kwa kutumia maji mengi.
"Kwa maumivu ya kichwa unaweza kumeza dawa kwa kutumia chai au kahawa ili kuharakisha utendaji kazi wake. Ila maji ndio hutumika kwa sana"
Kuna dawa za kupunguza maumivu ambazo zinadhibitiwa kama vile Opioids ambazo matumizi yake huenda yakaleta uraibu iwapo yatatumiwa bila maelekezo ya daktari.
"Dawa ya Tramadol ambayo mara nyingi hutumiwa vibaya, dawa hii hupunguza kiwango cha damu inayoelekezwa kwenye figo, na husababisha figo kubakisha maji mengi mwilini na pia kuchochea shinikizo la damu. Iwapo utachukua dawa hii na pombe, utakuwa unaathiri ini lako. Dawa ya Codeine ambayo hupatikana katika dawa ya kutibu homa au mafua huleta uraibu na huathiri afya ya mtu"
Kumeza dawa za kupunguza maumivu ni suluhisho la muda kwa tatizo kubwa. Ili kutotegemea dawa hizi kila siku ya maisha yako, Gor anashauri kujua kiini cha maumivu yako ya mwili ili kukabiliana nalo.














