Mambo 5 makubwa yaliyofichuliwa kutoka kwenye mamilioni ya faili za Epstein

Chanzo cha picha, Getty Images
Wizara ya Sheria ya Marekani imetoa mamilioni ya faili mpya zinazohusiana na marehemu Jeffrey Epstein, ikionesha idadi kubwa zaidi ya nyaraka zilizotolewa na serikali tangu sheria ilipoamuru kutolewa kwake mwaka jana.
Kurasa milioni tatu, picha 180,000, na video 2,000 zilichapishwa Ijumaa.
Ufichuzi huo unakuja wiki sita baada ya Rais Donald Trump, kuamuru kwamba nyaraka zote zinazohusiana na Epstein zitolewe kwa umma.
"Kutolewa kwa leo kunaashiria mwisho wa mchakato kamili wa kutambua na kupitia nyaraka ili kuhakikisha uwazi na kufuata sheria kwa watu wa Marekani," alisema Mwanasheria Mkuu Msaidizi Todd Blanche.
Nyaraka hizo zinajumuisha maelezo kuhusu muda wa Jeffrey Epstein gerezani, ikiwa ni pamoja na ripoti ya kisaikolojia na kifo chake akiwa gerezani, pamoja na rekodi kutoka kwa uchunguzi wa Ghislaine Maxwell, mshirika wa Epstein ambaye alihukumiwa kwa kumsaidia kusafirisha wasichana walio na umri mdogo.
Pia zinajumuisha barua pepe kati ya Epstein na watu mashuhuri.
Barua pepe na nyaraka nyingi zinaanzia zaidi ya muongo mmoja, zikiangazia uhusiano wa Epstein wakati wa matatizo yake ya kisheria.
Alihukumiwa mwaka wa 2008 huko Florida kwa kuomba ngono kutoka kwa msichana wa miaka 14 baada ya kufikia makubaliano yenye utata.
Alifariki Agosti 2019 akiwa gerezani kwa mashtaka katika kesi kubwa ya biashara haramu ya ngono.
Epstein alimwalika 'The Duke' kukutana na mwanamke wa Urusi
Nyaraka hizo zinaangazia uhusiano wa karibu wa mfadhili huyo aliyefedheheshwa na wasomi wa Uingereza.
Zinajumuisha barua pepe kati ya Epstein na mtu anayeitwa "The Duke", anayeaminika kuwa Andrew Mountbatten-Windsor, kaka wa Mfalme Charles III, akimaanisha chakula cha jioni katika Jumba la Buckingham, ambapo kulikuwa na "faragha".
Ujumbe mwingine kutoka kwa Epstein unajumuisha pendekezo la kumtambulisha "The Duke" kwa mwanamke wa Urusi mwenye umri wa miaka 26.
Barua pepe hizo zimesainiwa kwa herufi "A," na sahihi inayoonekana kusomeka "Mtukufu wa Kifalme The Duke wa York KG." Zilibadilishwa mnamo Agosti 2010, miaka miwili baada ya Epstein kukiri hatia ya kuomba ngono kutoka kwa mtoto mdogo.
Barua pepe hizo hazioneshi ukiukwaji wowote.

Chanzo cha picha, U.S. Department of Justice
BBC imewasiliana na Andrew, ambaye hapo awali alijulikana kama Duke wa York, kwa ajili ya kutoa maoni. Mountbatten-Windsor amekuwa akichunguzwa kwa miaka mingi kuhusu urafiki wake wa zamani na Epstein. Amekana mara kwa mara makosa yoyote.
Baadhi ya barua pepe katika chapisho la hivi karibuni zinaonekana kuwa kati ya Epstein na Sarah Ferguson, mke wa zamani wa Andrew.
Barua pepe ya tarehe 4 Aprili, 2009 ilisainiwa: "Love, Sarah, the redhead!"
Anasema angekuwa Palm Beach, Florida, na alitaka kunywa chai. Barua pepe hiyo inaendelea kujadili mawazo ya kampuni ya Ferguson. Duchess wa zamani wa York anamtaja Epstein kama "Rafiki yangu mpendwa, wa kuvutia, na wa pekee Jeffrey."
Anamwita "mahiri" na kusema, "Ninajivunia sana wewe."
Mfadhili huyo alikuwa bado chini ya kifungo cha nyumbani kwa hukumu yake ya 2008 wakati mawasiliano ya barua pepe yalipofanyika.
Trump anatajwa mara nyingi
Rais wa Marekani anatajwa mara nyingi katika faili zilizotolewa hivi karibuni. Trump alidumisha urafiki na Epstein, lakini anadai uliharibika miaka mingi iliyopita na amekana kujua lolote kuhusu uhalifu wake wa kingono.
Miongoni mwa hati mpya ni orodha iliyokusanywa na FBI mwaka jana ya madai dhidi ya Trump yaliyotolewa na watu walioita mstari wa ushauri wa Kituo cha Uendeshaji wa Vitisho cha Kitaifa. Mengi ya haya yanaonekana kutegemea ripoti ambazo hazijathibitishwa zilizopokelewa na shirika hilo na zilitolewa bila ushahidi.
Orodha hiyo inajumuisha madai mengi ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya Trump, Epstein, na watu wengine mashuhuri.

Chanzo cha picha, Getty Images
Trump amekuwa akikanusha mara kwa mara makosa yoyote yanayohusiana na Epstein, na waathiriwa wa Epstein hawajamshtaki Trump kwa uhalifu wowote.
Walipoulizwa kuhusu madai ya hivi karibuni, Ikulu ya White House na Wizara ya Sheria walitaja kifungu katika taarifa kwa vyombo vya habari kinachoambatana na seti mpya ya faili.
"Baadhi ya hati zina madai ya uwongo na ya kusisimua dhidi ya Rais Trump ambayo yaliwasilishwa kwa FBI muda mfupi kabla ya uchaguzi wa 2020," Wizara ya Sheria ya Marekani ilisema.
"Ili kuwa wazi, madai hayo hayana msingi na ni ya uwongo, na kama kungekuwa na uaminifu kidogo, bila shaka yangekuwa tayari yametumika dhidi ya Rais Trump."
Elon Musk alimuuliza Epstein ni lini 'sherehe yake itafanyika' kisiwani kwake
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nyaraka hizo pia zinajumuisha mawasiliano ya barua pepe kati ya Epstein na bilionea wa teknolojia Elon Musk.
Musk, ambaye hajashtakiwa kwa uhalifu wowote katika kesi hiyo, hapo awali alisema kwamba Epstein alikuwa amemwalika kwenye kisiwa chake, lakini alikataa.
Barua pepe mpya zinaonesha kwamba Musk alikuwa amejadili kusafiri huko zaidi ya mara moja, ikiwa ni pamoja na safari iliyopendekezwa mnamo 2012, ambapo alimuuliza Epstein: "Ni siku gani itakuwa sherehe kwenye kisiwa chako?"
Ujumbe kutoka Novemba 2012 unaonesha kwamba Epstein alimuuliza Musk ni watu wangapi angehitaji kuwasafirisha kwa helikopta hadi kisiwani, na Musk akajibu kwamba angekuwa yeye na mkewe wa wakati huo, Talulah Riley pekee.
Katika barua pepe ambayo Musk alituma kwa Epstein wakati wa Krismasi mnamo 2012, Musk aliuliza ikiwa mfadhili alikuwa amepanga sherehe zozote kwa sababu alihitaji "kujiachilia".
"Nimekuwa nikifanya kazi kwa kiwango cha hali ya juu mwaka huu, na kwa hivyo mara tu watoto wangu wanaporudi nyumbani baada ya Krismasi, nataka sana kutoka nje na kusherehekea huko St. Barts au mahali pengine na kupumzika," anaandika, akiongeza kwamba "uzoefu wa kisiwa tulivu" ni kinyume cha anachotaka.
Katika barua pepe nyingine kutoka mwishoni mwa mwaka 2013, Musk na Epstein wanajadili ziara ya kisiwa cha mfadhili na wanafanyia kazi vifaa na tarehe.
Hakuna ushahidi kwamba Musk aliishia kusafiri hadi kisiwa cha Epstein.
BBC imewasiliana na wawakilishi wa Musk katika makampuni yake ili kuwafahamisha kuhusu barua pepe hizo mpya.
Katika chapisho kwenye X Jumamosi hii, Musk alibainisha kuwa "alikuwa anajua sana kwamba baadhi ya barua pepe na (Epstein) zinaweza kutafsiriwa vibaya na kutumiwa na wakosoaji ili kuchafua jina langu."
"Sijali kuhusu hilo, lakini ninachojali ni kwamba angalau tujaribu kuwashtaki wale waliofanya uhalifu mkubwa na Epstein, hasa kuhusu unyonyaji mbaya wa wasichana walio chini ya umri," aliongeza.
Madai ya kashfa ya Epstein kuhusu Bill Gates
Msemaji wa mwanzilishi mwenza wa Microsoft, Bill Gates, amejibu madai ya kutisha yaliyomo katika faili za hivi karibuni za Epstein, ikiwa ni pamoja na kwamba aliambukizwa ugonjwa wa zinaa, akiziita "upuuzi kabisa na uongo kabisa."
Barua pepe mbili za tarehe 18 Julai, 2013, zinaonekana kuandikwa na Epstein, lakini haijulikani kama ziliwahi kutumwa kwa Gates.
Zote zilitumwa kutoka kwa akaunti ya barua pepe ya Epstein na kurudishwa kwenye akaunti hiyohiyo, ingawa hakuna akaunti inayohusiana na Gates inayoonekana na hakuna barua pepe iliyosainiwa.
Moja imeandikwa kama barua ya kujiuzulu kutoka kwa Wakfu wa Bill na Melinda Gates na analalamika kuhusu kulazimika kupata dawa kwa Gates "ili kukabiliana na matokeo ya kufanya mapenzi na wasichana wa Urusi."
Nyingine, inayoanza na "mpendwa Bill", inalalamika kwamba Gates ameumaliza urafiki na inadai kwamba Gates amejaribu kuficha maambukizi ya zinaa, ikiwa ni pamoja na ya mke wake wa wakati huo, Melinda.
Msemaji wa Gates aliiambia BBC: "Madai haya, kutoka kwa mwongo aliyekasirika na aliyethibitishwa, ni ya kipuuzi kabisa na ya uongo kabisa."
Aliongeza: "Kitu pekee ambacho nyaraka hizi zinaonesha ni kuchanganyikiwa kwa Epstein kwa kutodumisha uhusiano endelevu na Gates na jinsi angeenda mbali ili kuweka mtego na kumchafua."

Chanzo cha picha, Reuters
Udhibiti na utambuzi wa waathiriwa
Nyaraka nyingi zilizotolewa Ijumaa zinajumuisha upunguzaji mkubwa wa yaliyomo. Sheria inahitaji upunguzaji ufanywe tu ili kuwalinda waathiriwa au taarifa zinazochunguzwa. Pia inahitaji muhtasari wa kile kilichopunguzwa na msingi wa kisheria wa upunguzaji huo.
Msaidizi wa Mwanasheria Mkuu Todd Blanche alisema kwamba upunguzaji huo ulikusudiwa kuwalinda waathiriwa na kwamba Idara ya Sheria ilikuwa imewapa mamia ya wafanyakazi kazi ya kupitia hati hizo kwa zaidi ya miezi miwili ili kuhakikisha zinaachiliwa haraka.
Gloria Allred, wakili wa haki za wanawake ambaye amewawakilisha waathiriwa wengi wa Epstein, aliiambia BBC kwamba taarifa ya hivi karibuni ilifichua majina ya waathiriwa wengi, wakiwemo baadhi ambao hawakuwa wametambuliwa hadharani hapo awali.
Allred alikosoa matumaini ya Blanche kwamba chapisho hilo "lingefunga kesi" kwa waathiriwa, akiita "ujinga."
"Wamewaangamiza wengi wa waathiriwa hawa kwa kufichua majina yao hadharani," Allred alisema.
"Katika baadhi ya matukio... wana mstari unaopita majina lakini bado yanaweza kusomwa.
"Katika visa vingine, wameonesha picha za waathiriwa, manusura ambao hawajawahi kuhojiwa, hawajawahi kutoa majina yao hadharani."

Chanzo cha picha, Reuters
Wakili huyo aliongeza kwamba wakati timu yake ya kisheria ilikuwa ikifanya kazi ya kuifahamisha wizara hiyo ambapo udhibiti zaidi unahitajika ili kulinda utambulisho wa waathiriwa, "watu wengi tayari wamepakua faili hizo."
Allred alielezea hali hiyo kama "janga kubwa," akisema idara hiyo "imefikia kiwango cha juu" na "inapaswa kujionea aibu."
BBC imewasiliana na Idara ya Sheria kwa maoni zaidi.
Mwisho wa sakata?
Haijulikani kama huu utakuwa mwisho wa sakata la kuchapishwa kwa hati za Epstein.
Msaidizi wa Jaji Mkuu Blanche alisema kwamba ufichuzi wa siku ya Ijumaa umemaliza kazi ya Wizara ya sheria ya Marekani ya kutambua na kupitia nyaraka."
Hata hivyo, wabunge wa chama cha Democratic wanaendelea kusema kwamba wizara hiyo imeficha nyaraka nyingi sana (labda karibu milioni mbili na nusu) bila sababu inayokubaliwa, na kwamba hii inazua maswali.
Wengi, hata ndani ya kambi ya Trump, wameamini kwa muda mrefu kwamba kulikuwa na njama ya kuwalinda matajiri na wenye nguvu waliokuwa na uhusiano na Epstein.
Blanche alikiri kwamba kutoa nyaraka hizi hakutakidhi hitaji la taarifa zaidi. Alidai kwamba faili hizo hazina majina maalum ya wanaume waliowanyanyasa wanawake na kwamba, ikiwa wizara hiyo ingekuwa na majina hayo, wanaume hao wangeshtakiwa.
"Sidhani kama umma utagundua wanaume waliowanyanyasa wanawake katika faili za Epstein, kwa bahati mbaya."















