Maisha ya wafugaji Kenya, Somalia yalivyo hatarini ukame ukizidi kusambaa

V

Chanzo cha picha, REUTERS/Thomas Mukoya

    • Author, Vincent Mumo Nzilani
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Ukame unaoendelea katika Pembe ya Afrika sasa umeenea hadi maeneo ambayo hapo awali hayakuwa yakikumbwa sana na majanga ya ukame, hali inayowaacha wafugaji wengi wakipoteza chanzo chao kikuu cha maisha na kukabiliwa na njaa.

Katika kijiji cha Shompole, kaunti ya Kajiado kusini mwa Kenya, mizoga ya ng'ombe na mbuzi waliokufa imetapakaa katika boma la familia ya Maria Katanga, ishara ya athari mbaya za ukame unaodumu kwa miezi kadhaa. Tangu mwezi Agosti mwaka jana, mfugaji huyo wa Kimaasai mwenye umri wa miaka 24 amesema amepoteza zaidi ya ng'ombe 100 na mbuzi 300.

Wanyama waliobaki wamekonda kupita kiasi, kiasi cha kushindwa kutoa maziwa, hali inayozidi kuathiri upatikanaji wa chakula kwa familia inayotegemea mifugo kwa maisha yake ya kila siku.

Kenya imewahi kukumbwa na ukame hapo awali, ikiwemo mwaka 2022 wakati ambapo ukame uliovunja rekodi uliua idadi kubwa ya mifugo na kusababisha mgogoro mkubwa wa njaa katika maeneo ya kaskazini na kaskazini-mashariki mwa nchi. Hata hivyo, tofauti na misimu iliyopita, athari za sasa zimeenea hadi kaunti kama Kajiado, inayopakana na jiji la Nairobi na ambayo kihistoria haijakuwa katika maeneo hatarishi ya ukame.

Thamani ya mifugo yashuka kwa kasi

C

Chanzo cha picha, REUTERS/Thomas Mukoya

Kadri mifugo inavyoendelea kudhoofika, ndivyo pia thamani yake inavyozidi kuporomoka sokoni. Emmanuel Loshipae, kijana wa miaka 19 kutoka familia ya Katanga, amesema wafugaji wanalazimika kuuza mifugo kwa bei ya hasara ili kuokoa angalau sehemu ya maisha yao.

"Ng'ombe aliyekuwa akiuzwa kati ya shilingi 60,000 hadi 70,000 kabla ya ukame, sasa anauzwa kwa shilingi 5,000 tu," amesema.

Familia nyingi zimesema zimelazimika kufanya mauzo ya dharura ili kupata fedha za kununua chakula cha mifugo au kusaidia mahitaji ya msingi ya nyumbani, huku maeneo ya malisho yakikauka kabisa.

Afisa wa utawala wa eneo hilo, Lemaiyan Samuel Kureko, amesema baadhi ya wafugaji sasa wanasafiri umbali mrefu kutafuta maji na nyasi, huku wengine wakivuka mpaka wa Kenya kuingia Tanzania.

"Kumekuwa na ukame hapo awali katika eneo hili, lakini huu ni mbaya kuliko yote tuliyowahi kushuhudia," amesema.

Hatari ya migogoro kuongezeka, Somalia ikiathirika

Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame (NDMA) ya Kenya imeonya kuwa ukame unaojirudia mara kwa mara unaongeza ushindani wa rasilimali chache kama maji na malisho, hali inayoongeza hatari ya migogoro kati ya jamii za wafugaji.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, mabadiliko ya tabianchi yamefanya majanga kama haya kuwa ya mara kwa mara zaidi na yenye athari pana kuliko ilivyokuwa awali.

Wakati huo huo, Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya imetabiri kuwa msimu wa mvua wa Machi hadi Mei katika kaunti ya Kajiado utakuwa wa wastani au chini ya wastani, hali inayozidisha hofu ya kuendelea kwa ukame.

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bishar Maalim Mohammed, mwenye umri wa miaka 60, akiwa amesimama katikati ya mizoga ya mbuzi waliokufa nje ya boma lake katika kijiji cha Jabi-bar karibu na mji wa Rhamu, 21 Januari 2026.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mgogoro wa ukame haujaikumba Kenya pekee. Somalia ilitangaza hali ya dharura ya kitaifa mwezi Novemba mwaka jana kufuatia misimu mfululizo ya mvua duni.

Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wa Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mamilioni ya Wasomali wanakabiliwa na njaa kali, huku kupungua kwa misaada ya kimataifa kukipunguza uwezo wa mashirika ya kibinadamu kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka.

"Utapiamlo uko katika kiwango cha kutisha, karibu nusu ya watoto wote nchini Somalia wakiwa na utapiamlo na kuhitaji matibabu ya haraka," WFP imesema katika taarifa yake.

Nchini Kenya, NDMA imesema imetoa msaada wa fedha taslimu kwa zaidi ya kaya 130,000 katika kaunti ambazo kihistoria zimekuwa zikikumbwa na ukame, hasa maeneo ya kaskazini. Hata hivyo, kaunti ya Kajiado haikujumuishwa katika mpango huo wa dharura.

Kwa wafugaji walioko huko, hali inaendelea kuwa ngumu kila siku.

"Hakuna watu waliokufa bado, lakini mifugo imeangamia na jua linaendelea kuwa kali zaidi kila siku," amesema afisa Kureko.

"Tumekata tamaa kiasi kwamba kilichobaki ni kumuomba Mungu atusaidie."

Habari hii ya Vincent Mumo Nzilani (Reuters) imetayarishwa na Yusuph Mazimu