Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uvamizi wa Israel nchini Lebanon: Operesheni sita za kijeshi
Jeshi la Israeli lilitangaza kupanua operesheni zake za ardhini na angani nchini Lebanon dhidi ya Hezbollah. Hilo linakuja huku Israel ikizidisha mashambulizi yake, baada ya Hezbollah inayoungwa mkono na Iran kufyatua makombora mapema mwezi huu, kufuatia kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Shambulio la anga la Israeli Jumapili lililenga Daraja la Qasmiyeh karibu na mji wa pwani wa Tyre, moja ya njia kubwa inayounganisha kusini mwa Lebanon na katikati.
Mwandishi wa BBC Mashariki ya Kati Hugo Bashega anasema Israel inasema Hezbollah inatumia madaraja haya kuhamisha vikosi vya kijeshi kuelekea kusini.
Ameongeza: "Haya ni madaraja ya kraia na miundombinu muhimu ya serikali, watu wanayategemea kwa usafiri wao. Na kuna hofu kwamba huu ni mpango wa kuitenganisha kusini na sehemu nyingine za nchi, katika maandalizi ya operesheni kubwa ya ardhini.”
Walebanoni wengi wanaogopa kwamba Israel itaanzisha eneo la kijeshi kusini mwa nchi, sawa na lile lililokuwepo miaka ya 1980 na 1990.
Tangu kuanza kwa mashambulizi ya anga ya Israel, zaidi ya watu milioni moja wameyakimbia makazi yao, huku kukiwa na hofu kwamba familia nyingi hazitaweza kurudi makwao.
Katika miongo kadhaa ya makabiliano kati ya Israel na Hezbollah, Israel imewahi kufanya operesheni kubwa za kijeshi ndani ya Lebanon kwa angalau mara sita.
Operesheni Litani1978
Machi 14, Israeli ilianzisha operesheni ya kijeshi yenye lengo la kuwafukuza wapiganaji wa Kundi la Ukombozi wa Palestina (PLO) waliokuwa Lebanon wakati huo kutoka mpakani, kufuatia shambulio la majini la wanachama wa PLO ambalo liliwaua takriban raia 30 kaskazini mwa Israeli.
PLO ilianzisha makao yake makuu nchini Lebanon baada ya kuondoka Jordan mwaka 1970.
Vikosi vya Israeli vilisonga mbele kuelekea kaskazini hadi kingo za Mto Litani, bila kushiriki katika mapigano ya moja kwa moja na wapiganaji wa shirika hilo, ambao polepole waliondoka kadri vikosi hivyo vilivyosonga mbele.
PLO ilitangaza kusitisha mapigano wiki mbili baadaye, na vikosi vya Israeli viliondoka baadaye mwaka huo, vikiunga mkono wanamgambo washirika wa Kikristo, Jeshi la Lebanon Kusini, kudhibiti maeneo ya mpaka.
Inakadiriwa kuwa idadi ya vifo kutokana na Operesheni Litani, kufikia Juni, ilikuwa imezidi vifo 1,100 kwa Walebanoni na Wapalestina.
Chini ya azimio lililotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL, kiliwekwa kando ya mpaka kati ya nchi hizo mbili, unaojulikana kama Mstari wa Bluu.
Zaidi ya wafanyakazi 300 wa mataifa tofauti wameuawa wakitekeleza majukumu yao tangu mwaka 1978, na kuifanya kuwa mojawapo ya misheni hatari zaidi za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.
Operation Peace for Galilee 1982
Operesheni ya Litani haikumaliza mapigano kati ya wapiganaji wa PLO na vikosi vya Israeli kwenye mpaka. Kufuatia kujeruhiwa balozi wa Israel huko London na kundi la Wapalestina Juni 3, 1982, Israeli, chini ya uongozi wa Waziri wa Ulinzi wa wakati huo Ariel Sharon, ilianzisha operesheni kubwa ya kijeshi iliyohusisha maelfu ya wanajeshi na mamia ya magari.
Shambulio hilo lilianza Juni 6, na ndani ya siku chache vikosi vya Israel vilikuwa vimefika viungani mwa Beirut na kuanza kushambulia sehemu ya magharibi ya mji mkuu.
Baada ya kuzingirwa kwa zaidi ya miezi miwili, maelfu ya wapiganaji wa Kipalestina walihamishwa kwa njia ya baharini.
Jeshi la Israeli pia lilipambana na vikosi vya Syria mashariki mwa nchi, na kuangusha ndege kadhaa katika moja ya mapigano makubwa zaidi ya angani katika eneo hilo.
Serikali ya Lebanon inakadiria kwamba vita hivyo vilisababisha vifo vya takriban raia na wanajeshi 19,000 wa Lebanon, Palestina, na Syria, huku jeshi la Israeli likitangaza vifo vya wanajeshi wake 376 kati ya Juni na Septemba 1982.
Operesheni hazikuishia hapo. Baada ya kuuawa kwa rais wa Lebanon Septemba 14 kwa bomu lililotegwa kwenye gari, jeshi la Israel liliwaruhusu wanamgambo Wakristo kuingia katika kambi za wakimbizi wa Kipalestina za Sabra na Shatila, ambapo mauaji yalitokea na idadi ya wahanga inakadiriwa kuwa kati ya raia 700 na 3,500.
Mwaka uliofuata, Israeli iliondoa vikosi vyake kutoka katikati mwa Lebanon, lakini ilidumisha uwepo wa jeshi ndani ya eneo la kilomita 19 kusini mwa nchi tangu 1985, na haikuondoka kabisa hadi miaka 18 baadaye.
Katika kipindi hicho, Hezbollah iliibuka kama jeshi linaloungwa mkono na Iran, ambayo iliipa silaha na ufadhili, kwa lengo la kukabiliana na uwepo wa jeshi la Israeli nchini Lebanon.
Operation Accountability 1993
Ndege za kivita za Israeli zililenga maeneo kadhaa ya Hezbollah katika shambulio la wiki moja lililoanza Julai 25. Israeli ilisema mashambulizi hayo yalikuwa ni kujibu mashambulizi ya roketi kwenye maeneo yake huko Lebanon na kaskazini mwa Israeli, ikisisitiza kwamba lengo lao lilikuwa "kuizuia Hezbollah kugeuza kusini mwa Lebanon kuwa ngome yao ya kigaidi."
Kwa upande mwingine, Hezbollah ilisema ilirusha makombora yake kujibu mashambulizi ya awali ya helikopta za Israeli.
Wakati wa kampeni hiyo, jeshi la Israeli lilifyatua maelfu ya makombora na kusema liliwaua wapiganaji 50 ambao liliwaelezea kama "magaidi".
Uvamizi huo pia ulisababisha uharibifu wa maelfu ya majengo, na Umoja wa Mataifa unakadiria idadi ya vifo vya raia kuwa takriban 130, pamoja na watu wapatao 300,000 waliokimbia makazi yao.
Jeshi la Israeli liliripoti kwamba mwanajeshi mmoja wa Israeli na raia wawili waliuawa wakati wa operesheni hiyo.
Operation Grapes of Wrath 1996
Mapigano yalianza tena mwezi Aprili, kufuatia shambulio la roketi dhidi ya Israeli, ilijibu kufanya mashambulizi makubwa ya makombora na kuua zaidi ya watu 200, wengi wao wakiwa raia, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Zaidi ya watu 100 waliuawa katika shambulio la bomu lililolenga eneo la Umoja wa Mataifa huko Qana, ambapo raia walikuwa wamekimbilia.
Israel ilisema ililenga vijiji vya Washia kusini mwa Lebanon kwa lengo la kuwalazimisha wakazi kukimbilia kaskazini kuelekea Beirut, ili kuishinikiza serikali za Lebanon na Syria kuchukua hatua dhidi ya shughuli za Hezbollah.
Kwa kujibu, Hezbollah ilirusha mamia ya makombora kuelekea Israeli, na kuwajeruhi raia wapatao 55, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Mgogoro huo ulisababisha maelfu ya Walebanoni kuhama makazi yao, pamoja na maelfu ya Waisraeli.
Aprili 27, pande hizo mbili zilifikia makubaliano ya kusitisha mapigano, na kukomesha raundi hii ya mapigano.
Vita vya Pili vya Lebanoni 2006
Jeshi la Israeli lilianzisha mashambulizi ya ardhini, baharini na angani ambayo yalidumu kwa zaidi ya mwezi mmoja, yakilenga kusini mwa Lebanon na Beirut, baada ya Hezbollah kuwakamata wanajeshi wawili wa Israeli Julai 12.
Mashambulizi hayo yalipanuka na kujumuisha maeneo ya chama hicho, na pia yalilenga miundombinu ya kiraia, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beirut.
Usitishaji mapigano uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa ulianza Agosti 14. Azimio la kimataifa lilitoa agizo la kupelekwa kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa na jeshi la Lebanon kusini mwa Mto Litani, lakini hili halikutekelezwa kikamilifu.
Mgogoro huo wa siku 34 ulisababisha vifo vya zaidi ya Walebanoni 1,125, wengi wao wakiwa raia, pamoja na wanajeshi 119 na raia 45 nchini Israeli.
2023
Hezbollah ilizindua shambulio la roketi kwenye maeneo ya Israeli katika eneo la mpaka ili kuwaunga mkono Wapalestina huko Gaza, kufuatia shambulio la Hamas kusini mwa Israeli Oktoba 7. Oktoba 9, kundi hilo lilipanua mashambulizi yake hadi kujumuisha kaskazini mwa Israeli.
Mapigano ya pande zote mbili yaliendelea hadi Septemba 17, 2024, yalipozidi kuwa mabaya baada ya Israeli kulipua vifaa vya mawasiliano vinavyotumiwa na wanachama wa Hezbollah, na kisha kulipua vifaa tena vifaa vingine vya mawasiliano siku iliyofuata, na kusababisha vifo vya watu 39 na kujeruhiwa maelfu kote nchini.
Wiki moja baadaye, Israeli ilianzisha operesheni ya kijeshi inayoitwa "Northern Arrows," ambapo ilifanya mashambulizi makali ya anga dhidi ya ngome za Hezbollah, ikifuatiwa na mashambulizi ya ardhini mwezi Oktoba.
Ilisema kwamba lengo lilikuwa ni kuhakikisha wakazi wapatao 60,000 wa kaskazini mwa Israeli ambao walikuwa wameyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya roketi wanarudi.
Balozi wa Israeli katika Umoja wa Mataifa alisema Septemba 2024 kwamba Hezbollah iliusha zaidi ya makombora 8,000 kuelekea kaskazini mwa Israeli na Milima ya Golan tangu mashambulizi ya Oktoba 7, 2023.
Vita hivyo vilisababisha vifo vya takriban watu 4,000 nchini Lebanon na 120 nchini Israeli, huku Hezbollah ikipata pigo ambalo liliidhoofisha kwa kiasi kikubwa uwepo wake.
Mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah aliuawa katika shambulio la anga Septemba 2024, baada ya miaka 32 kuongoza chama hicho.
Chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani na Ufaransa, Hezbollah ilikubali kuondoa silaha kusini mwa Mto Litani, yapata kilomita 30 kutoka mpaka na Israeli, na Israeli ilikubali kuondoa vikosi vyake kutoka eneo hilo.
Tangu kuanza kutumika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, pande zote mbili zimeshutumuana kwa kukiuka makubaliano hayo. Israel iliishutumu Hezbollah kwa kujaribu kujenga upya uwezo wake wa kijeshi, ikiwemo kusini.
Jeshi la Israel pia lilifanya mashambulizi ya karibu kila siku, ambayo lilisema yalilenga maeneo yanayohusiana na kundi hilo, huku vikosi vyake vikiendelea kuwekwa katika angalau maeneo matano kusini mwa Lebanon.