Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Achana na mafuta: Zijue bidhaa nyingine zinazoathirika kwa kufungwa Mlango wa Bahari wa Hormuz
- Author, Ben Chu
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kusitishwa kwa usambazaji wa mafuta na gesi kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz kutokana na vita kati ya Marekani na Israel na Iran kumeongeza bei za nishati duniani kwa kiasi kikubwa.
Petroli tayari imepanda na bili za mafuta, gesi na umeme ndani ya Uingereza zinakaribia kuongezeka.
Lakini si mafuta pekee yaliyoathiriwa na mzozo huo. Kemikali, gesi na bidhaa zingine muhimu kwa kawaida huingia kwenye minyororo ya usambazaji wa kimataifa kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
BBC Verify imegundua kuwa bei ya bidhaa nyingi - kuanzia chakula, simu janja, hadi dawa - inaweza kuathiriwa, kwani idadi ya meli zinazopita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz imeshuka kutoka zaidi ya 100 kwa siku moja kabla ya vita hadi chache tu.
Mbolea (Chakula)
Kemikali za petrokemikali hutokana na mafuta na gesi na huzalishwa kwa wingi kwa ajili ya kusafirishwa nje na nchi katika eneo la Ghuba. Na moja ya mbolea muhimu kwa wa kilimo duniani.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, karibu theluthi moja ya mbolea duniani - kama vile urea, potashi, amonia na fosfeti - kwa kawaida hupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Takwimu kutoka Shirika la Biashara Duniani zinaonyesha, tangu mgogoro uanze, usafirishaji wa bidhaa zinazohusiana na mbolea kupitia njia ya maji umepungua.
Wachambuzi wameonya kwamba uhaba wa viambato hivi vya mbolea huenda ukaathiri sana kilimo kwa sababu Machi na Aprili ni msimu wa upandaji kwa nchi zilizo katika kizio cha kaskazini cha dunia na hilo litaathiri mavuno ya baadaye mwakani.
Wataalamu wanasema kufungwa kabisa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kunaweza kuongeza bei za ngano duniani kwa 4.2% na bei za matunda na mboga mboga kwa 5.2%.
Na inakadiria kwamba nchi zitakazo athirika zaidi na ongezeko la bei za vyakula zitakuwa Zambia (31%), Sri Lanka (15%), Taiwan (12%) na Pakistan (11%).
Urusi kwa kawaida hutoa karibu moja ya tano ya mauzo ya nje ya mbolea duniani na wachambuzi wanasema inaweza kuongeza uzalishaji ili kujaza pengo hilo.
Mjumbe maalum wa Vladimir Putin, Kirill Dmitriev, amesema Urusi, mzalishaji mkuu wa bidhaa kama vile mbolea, iko " katika nafasi nzuri.
Gesi ya Heliamu
Theluthi moja ya gesi ya heliamu duniani kwa kawaida hutoka Qatar na hupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Hii inatokana na gesi asilia na hutumika katika utengenezaji wa semikondakta, ambazo hufanywa kuwa microchips zinazotumika katika kompyuta, magari na vifaa vya nyumbani.
Heliamu pia hutumika kupoeza sumaku katika skana za Upigaji Picha wa Mwangwi wa Magnetic (MRI) zinazotumika hospitalini.
Kiwanda kikubwa cha Ras Laffan nchini Qatar, kinachozalisha gesi hiyo, kimefunga uzalishaji baada ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran kushambulia.
Na serikali ya Qatar imeonya kwamba itachukua miaka mitatu hadi mitano kurekebisha uharibifu huo, na kuzua hofu kuhusu uzalishaji wake.
2023, Chama cha Sekta ya Semiconductor cha Marekani kilionya kuhusu "kuongezeka kwa bei" ikiwa usambazaji wa heliamu duniani utavurugwa.
Wachambuzi wameonya kwamba athari kubwa ya kufungwa kwa Hormuz inaweza ongeza bei ya teknolojia nyingi za kisasa, kuanzia simu hadi vituo vya data.
Prashant Yadav, mtafiti mkuu wa afya ya kimataifa katika Baraza la Mahusiano ya Kigeni, ameonya kuwa bei za MRI zinaweza kuathiriwa ikiwa kutakuwa na uhaba wa muda mrefu wa heliamu.
"Mashine za MRI zinahitaji kati ya lita 1,500 hadi 2,000 za heliamu ili kupoza sumaku. Kila wakati unapofanya skani, kiasi kidogo cha hicho huchemka au kuyeyuka."
"Watu hupenda kufikiria matumizi makubwa ya heliamu ni katika vituo vya data, semiconductors na kupoza mashine za AI na sekta ya data. Lakini hatuwezi kusahau kwamba heliamu ni muhimu sana kwa MRIs na kwa matibabu mengine," ameiambia BBC Verify.
Dawa
Kemikali za methanoli na ethilini ambazo hutokana na petrokemikali - ni nyenzo muhimu katika uzalishaji wa dawa duniani, ikiwa ni pamoja na dawa za kutuliza maumivu, viuavijasumu na chanjo.
Nchi za Ghuba - Saudi Arabia, Qatar, Oman, Falme za Kiarabu, Kuwait na Bahrain - zinakadiriwa kuchangia takriban 6% ya uwezo wa uzalishaji wa petrokemikali duniani.
Mataifa haya hutumia hasa Mlango-Bahari wa Hormuz kusafirisha kemikali hizi kwa ulimwengu, huku karibu nusu zikienda Asia.
India ambayo ni mzalishaji mkubwa wa dawa duniani, na nyingi ya dawa hizo hutumwa Marekani na Ulaya.
Dawa hizi pia husafirishwa hadi masoko ya kimataifa kupitia viwanja vya ndege vya Ghuba, hasa Dubai, ambavyo vimevurugwa na mzozo huo.
Baadhi ya wachambuzi wameonya kuhusu uwezekano wa bei za juu za dawa kwa kaya kutokana na usumbufu katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Vyuma na Betri
Salfa ni bidhaa nyingine inayotokana na mafuta ghafi na gesi asilia na huzalishwa kwa wingi kwa ajili ya kusafirishwa nje kutoka eneo la Ghuba.
Karibu nusu ya biashara ya salfa duniani kote kwa kawaida hupitia Mlango-Bahari wa Hormuz. Matumizi yake makuu ni katika mbolea, lakini pia ni muhimu kwa uchakataji wa chuma.
Salfa hutumika kutengeneza asidi ya salfa, ambayo hutumika kwa ajili ya kuchakata shaba, kobalti na nikeli na pia kwa ajili ya uchimbaji wa lithiamu.
Vyuma hivyo vyote vinahitajika kwa ajili ya utengenezaji wa betri, ambazo hutumika katika kila kitu kuanzia vifaa vya nyumbani hadi magari ya umeme hadi vifaa vya kijeshi kama vile ndege zisizo na rubani.
Wachambuzi wanaonya kwamba ikiwa usambazaji wa salfa utaendelea kukatizwa, matokeo yake yanaweza kuwa ni kupandisha bei kwa watumiaji wa bidhaa zenye betri.