Iran ina nguvu kiasi gani?

Wataalamu wengi wanakubali kwamba vita kamili haiko katika ajenda ya upande wowote

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wataalamu wengi wanakubali kwamba vita kamili haiko katika ajenda ya upande wowote
    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Siku chache zilizopita zimekuwa kama safari ya kupanda na kushuka, zikijaa matukio na kauli kutoka Iran na Marekani.

Maandamano nchini Iran yanaendelea kuongezeka siku hadi siku, mengi tukiyaona kupitia vyombo vya habari vya Magharibi pekee, na hakuna anayeweza kuthibitisha kwa uhakika picha kamili ya kinachoendelea kwa sababu ya kuminywa kwa intaneti na kufungwa kwa mtandao.

Kwa upande mwingine, mamlaka za Iran zimekuwa zikidai mara kwa mara kwamba mataifa ya kigeni yako nyuma ya maandamano hayo, na lawama nyingi zinaelekezwa waziwazi kwa Israel.

Wakati huohuo, Trump alianza kwa kuitishia Iran kuingilia kijeshi, kisha akachapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii anaoupenda wa 'Truth social' akisema kuwa msaada ulikuwa njiani kwa waandamanaji.

Baadaye akasema ameambiwa kuwa mauaji ya waandamanaji yamesitishwa, lakini hali hiyo ingeendelea kufuatiliwa kwa karibu.

Hivyo basi, ni nini hasa kinaendelea? Na ni nini kuhusu Iran kinachomfanya Trump kufikiria chaguo zake kwa umakini mkubwa kiasi hiki? Je, kweli anaweza kuwasaidia waandamanaji wa Iran kushughulikia malalamiko yao? Na uingiliaji wa kijeshi wa Marekani nchini Iran ungekuwaje, na ungefanikisha nini hasa?

Je, uingiliaji wa kijeshi wa Marekani ungefanikisha nini?

fd

Chanzo cha picha, Getty Images

Tayari tumeona mifano ya uingiliaji wa kijeshi wa Marekani hapo awali, Iraq, Libya, Syria, Afghanistan, ambapo iliahidiwa kuwa hatua za uingiliaji wa nje pekee zingeweza kurekebisha machafuko ya ndani.

Lakini ni vigumu kusema hivyo kwa Iran.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ukirudi nyuma na kuangalia historia ya Iran, jamii yake na muundo wake wa kisiasa, unaona kwamba kuingia Iran si jambo rahisi kama linavyosikika.

Kwa mfano, nguvu zake zilionekana hata ilipojibu Israel kwa shambulio la moja kwa moja katika kipindi kifupi cha mapigano mwaka jana. Hii ni kwa sababu Iran si nchi nyingine tu ya Mashariki ya Kati inayokumbwa na misukosuko.

Ni mojawapo ya nchi zilizo na mwendelezo mrefu wa kihistoria, umuhimu mkubwa wa kimkakati, na uimara wa kisiasa duniani.

Kwa hiyo, katika uchambuzi wa leo, hebu tuchambue kwa nini Iran mara kwa mara huwapinga wale wa nje wanaotarajia kuona ikidhoofika. Kwanza, tuangalie muktadha wa maandamano ya sasa.

Mwishoni mwa mwezi Desemba, wafanyabiashara katika Bazaar Kuu ya Tehran walikataa kufungua maduka yao.

Bazaar kihistoria imekuwa mojawapo ya taasisi zenye nguvu zaidi nchini Iran kiuchumi, kijamii na hata kisiasa. Hivyo, mgomo wa wafanyabiashara unaashiria zaidi ya hasira ya kawaida.

Kwa mujibu wa ripoti, mfumuko wa bei ulikuwa umefikia kiwango cha juu kabisa, sarafu ilikuwa imedhoofika vibaya, na viwanda vilivyohusiana na minyororo ya ugavi ya bazaar vilikuwa vikifungwa.

Kutoka hapo, maandamano yalisambaa kwa kasi, si Tehran pekee bali kila jimbo, kuanzia miji midogo ya mbali iliyokumbwa na ukosefu wa ajira na kutelekezwa, hadi miji mikubwa.

Majibu ya serikali ya Iran

Mfumo wa ulinzi wa makombora wa Iron Dome wa Israel ulisaidia kuharibu zaidi ya makombora 300 na ndege zisizokuwa na rubani zilizofyatuliwa na Iran mwishoni mwa wiki

Chanzo cha picha, Amir Cohen / Reuters

Maelezo ya picha, Mfumo wa ulinzi wa makombora wa Iron Dome wa Israel ulisaidia kuharibu zaidi ya makombora 300 na ndege zisizokuwa na rubani zilizofyatuliwa na Iran mwishoni mwa wiki

Huku haya yakiendelea, Donald Trump alizungumza waziwazi kuhusu uwezekano wa hatua za kijeshi dhidi ya Iran.

Mwanzoni mwa karne ya 20, umuhimu wa Iran uliongezeka kwa kugunduliwa kwa mafuta. Na bila shaka, hapo ndipo matatizo pia yalipoanza. Mwaka 1908, Uingereza iligundua mafuta nchini Iran na kuunda Kampuni ya Anglo-Persian Oil, inayojulikana leo kama BP. Jambo lililoipa Uingereza ushawishi mkubwa sana juu ya uchumi wa Iran.

Lakini mwanzoni mwa miaka ya 1950, waziri mkuu wa Iran aliyechaguliwa kidemokrasia, Mohammad Mossadegh, aliamua kutaifisha sekta ya mafuta ya Iran, akisema kuwa Iran inapaswa kudhibiti rasilimali zake yenyewe. Uingereza ilijibu kwa vikwazo na vita vya kiuchumi. Kisha mwaka 1953, Marekani na Uingereza ziliandaa mapinduzi ya kumuondoa Mossadegh madarakani.

Kuanzia hapo, utawala wa kifalme ulionekana na Wairani wengi kuwa wa kisasa, lakini usio halali.

Ayatollah Ruhollah Khomeini alijenga uasi wake juu ya tukio hilo. Ujumbe wake ulikuwa rahisi lakini wenye nguvu: Shah hakutawala kwa ajili ya Iran, bali kwa ajili ya Magharibi. Hoja hiyo iliwagusa wengi, na hatimaye ikasababisha mapinduzi ya 1979 yaliyomaliza utawala wa kifalme.

Kwa mujibu wa Profesa Nargis Bajoghli, mapinduzi hayakufaulu kwa sababu Wairani walikuwa na hasira kwa miongo mingi. Yalifaulu kwa sababu mihimili mitatu ya nguvu iliungana: wananchi, wanazuoni wa dini, na wafanyabiashara wa bazaar.

Kupitia mitandao ya misikiti, upangaji wa wafanyakazi, na nguvu za kiuchumi, taasisi hizo zilisonga pamoja. Muungano huo ulipotimia, ufalme ulianguka. Kutokana na misukosuko hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ilizaliwa.

Baada ya hapo, Iran ilikumbana na kutengwa na kisha vita.

Mwaka 1980, Iraq iliivamia Iran. Vita vilidumu miaka minane. Mamia ya maelfu walikufa, silaha za kemikali zilitumika, na miji iliharibiwa. Lakini Iran iliishi. Uhai huo ukawa msingi wa utambulisho wake. Uvumilivu chini ya shinikizo ukawa sehemu ya nafsi ya Iran.

Tangu wakati huo, Iran imevumilia miongo ya vikwazo, mashambulizi ya mtandaoni, mauaji ya kulenga watu, operesheni za siri, na mawimbi ya maandamano. Hata hivyo, mfumo umeendelea kuwepo. Uimara huo si wa bahati mbaya. Unadumishwa na muundo tata wa nguvu, hasa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

IRGC iliundwa baada ya mapinduzi kulinda mfumo. Inawajibika moja kwa moja kwa Kiongozi Mkuu. Kadri muda ulivyopita, imekua na kuwa nguvu kubwa ya kijeshi, kijasusi, mtandaoni na kiuchumi, ikidhibiti makombora, droni, mitandao ya ujasusi, na sekta kubwa za uchumi. Muundo huu unaipa serikali ya Iran uimara mkubwa. Hata chini ya shinikizo kali, mfumo hauitegemei taasisi moja inayoweza kupasuka kirahisi.

Marekani iliorodhesha IRGC kama kundi la Kigaidi na kisha imeungwa hivi majuzi na Uingereza kuwataja kama magaidi.

Vikwazo viliidhoofisha Iran, lakini pia vilibadilisha uchumi wake. Wasomi waliounganishwa na IRGC wakawa wahusika wakuu wa kukwepa vikwazo, wakidhibiti uagizaji, mtiririko wa fedha, na upatikanaji wa bidhaa zilizozuiliwa. Hivyo, mamlaka yakajikita zaidi.

Hapa ndipo tunaporejea kwa bazaar. Mwaka 1979, bazaar ilikuwa na uhuru mkubwa wa kiuchumi. Leo, biashara nyingi za bazaar zinategemea mitandao inayohusishwa na serikali na IRGC ili kuendelea kuishi. Kwa hiyo, wafanyabiashara wanapogoma leo, inaashiria hali ya kukata tamaa, lakini si nguvu ile ile ya taasisi huru iliyomwangusha Shah.

Ndiyo maana, kwa mujibu wa wachambuzi kama Narges Bajoghli, kulinganisha hali ya sasa na 1979 ni kupotosha.

Marekani inataka nini hasa kutoka Iran?

Marekani na Iran zimekuwa katika pande zinazopingana tangu mapinduzi ya Iran

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Marekani na Iran zimekuwa katika pande zinazopingana tangu mapinduzi ya Iran

Hakuna aliye na uhakika Marekani inataka nini kutoka kwa Iran. Inashangaza kwasababu katika mfano wa hivi karibuni wa Venezuela Marekani haikuogopa wala kusita kueleza nia yake na nchi hiyo ya karibiani na pia huko Greenland.

Na mabadiliko yoyote ya utawala yangehitaji uongozi mbadala.

Hadi sasa, hakuna jina kubwa lililotajwa isipokuwa Reza Pahlavi, ambaye pia anakabiliwa na maswali mengi kuhusu uhusiano wake na Magharibi. Anasema kwamba katika diplomasia, uhusiano na Marekani utarejeshwa katika hali ya kawaida, urafiki na Marekani na watu wake utaimarishwa, Israel itatambuliwa mara moja, na juhudi zitafanywa kupanua Makubaliano ya Abraham kuwa Makubaliano ya Cyrus, yakileta pamoja Iran huru, Israel na ulimwengu wa Kiarabu.

Hata hivyo, wachambuzi wanachambua kuwa Marekani ina malengo mengine: kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia; kupunguza ushawishi wake wa kikanda na kuilinda Israel na washirika wa Ghuba; kuhakikisha Mkono wa bahari wa Hormuz unabaki wazi; na hatimaye, kuepuka vita vya kikanda.

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa haitafuti kutengeneza silaha za nyuklia, lakini nchi nyingi na shirika la kimataifa la kudhibiti nyuklia, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), haziamini.

Mashaka kuhusu nia ya Iran yalizuka mwaka 2002 ilipogundulika kuwa nchi hiyo ina vifaa vya siri vya nyuklia. NPT inaruhusu nchi kutumia teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni yasiyo ya kijeshi kama vile dawa, kilimo na nishati, lakini hairuhusu uundaji wa silaha za nyuklia.

Na hili lilisababisha mvutano na hadi Marekai kuvamia baadhi ya miundo mbinu ya nyuklia ya Iran mwaka jana 2025 Juni.

Baadhi wanaamini mashambulizi madogo yanaweza kuishtua serikali au kuwapa ujasiri waandamanaji. Wengine wanaonya kwamba hatua hizo zingekuwa na athari kinyume, zikichochea utaifa. Hatari zote mbili ni za kweli. Iran pia imeahidi kujibu shambulio lolote, na kumbuka bado ina hazina kubwa ya makombora. Kwa hiyo, mzozo usingebaki katika mipaka midogo.

Ndani ya Iran, wanaharakati wengi wanaelewa hili kuliko mtu yeyote. Wanajua kuwa vita vingewarudisha nyuma kwa miongo kadhaa, na mapinduzi ya vurugu yangekuwa maafa makubwa.

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ameonya kwamba shambulio lolote la Marekani litasababisha vita vya kikanda, huku Marekani ikiendelea kuimarisha uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo.

"Wamarekani wanapaswa kufahamu kuwa wakianzisha vita, safari hii haitakuwa vita ya kawaida, bali vita ya kikanda," alisema Khamenei, kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim.

Iran inaweza kupigana na Israel?

g

Chanzo cha picha, Getty Images

BBC imepima swali hili kwa kutumia vyanzo vilivyoorodheshwa hapa chini, ingawa kila nchi inaweza kuwa na uwezo mkubwa ambao umefichwa.

Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati (IISS) inalinganisha nguvu ya mashambulizi ya majeshi ya mataifa yote mawili, kwa kutumia njia mbalimbali rasmi na za wazi ili kupata makadirio bora iwezekanavyo.

Mashirika mengine, kama vile Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm, pia hufanya tathmini, lakini usahihi unaweza kutofautiana kwa nchi ambazo mara nyingi hazitoi takwimu.

Hata hivyo, Nicholas Marsh, kutoka Taasisi ya Utafiti wa Amani Oslo (PRIO), anasema IISS inaonekana kama alama ya kutathmini nguvu za kijeshi za nchi duniani kote.

IISS inasema Israel ina matumizi ya juu zaidi katika bajeti yake ya ulinzi kuliko Iran, na kuipa nguvu kubwa katika mzozo wowote unaoweza kutokea.

IISS inasema bajeti ya ulinzi ya Iran ilikuwa karibu $7.4bn mwaka 2022 na 2023, wakati Israel ilikuwa na zaidi ya mara mbili ya bajeti hiyo, karibu $ 19bn.

Matumizi ya ulinzi wa Israel ikilinganishwa na Pato la Taifa (kipimo cha pato lake la kiuchumi) pia ni mara mbili ya Iran.

Israel hivi majuzi kupitia Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imeeleza iko tayari kuishambulia Iran iwapo Tehran watathubutu kuivamia na kuongezea kuwa wamejipanga vya kutosha bila kutegemea msaada wa Trump.

Mtaalamu wa Masuala ya Asia Magharibi katika Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru, Delhi, Profesa Ashwini Mahabatra, anasema:

"Iran imeendelea katika uwanja wa teknolojia kuliko hapo awali. Wana droni na makombora ya masafa marefu. Ingawa Israel inaweza kukabiliana nayo, ila inapendelea kuepuka mzozo na Iran.''

Ashwini Mohapatra anasema, "Marekani na Israel hazitaki ushawishi wa Iran uongezeke katika eneo la Asia Magharibi. Ndio maana inataka kuiweka pembeni Iran."

Iran ni nchi kubwa kuliko Israel na idadi ya watu wake (karibu milioni 89) ni karibu mara tisa ya ile ya Israeli (karibu milioni 10).

Pia ina askari mara sita zaidi ya wanajeshi wa Israeli. Kuna wanajeshi 600,000 nchini Iran, wakati Israel ina wanajeshi 170,000, inasema IISS.

Na hili ndilo jambo la mwisho: Iran si dhaifu. Imechoka, imeelemewa, na iko chini ya shinikizo kubwa. Lakini bado ina nguvu, ina uwezo wa kuzoea, na imeundwa kwa kina na kumbukumbu zake. Ni ustaarabu unaokumbuka himaya, uvamizi, unyonyaji wa mafuta, mapinduzi ya kijeshi, mapinduzi ya wananchi, vita, na hatimaye, kuendelea kuishi.

Pia, Geranmayeh, kama wataalam wengi wanavyokubali kwamba vita kamili haiko katika ajenda ya upande wowote.