Kituo kipya cha watoto njiti chatoa matumaini kwa familia za Kwimba
- Author, Elizabeth kazibure
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Tanzania
- Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, kwa muda mrefu familia zenye watoto waliozaliwa kabla ya wakati, yaani watoto njiti, zililazimika kusafiri umbali mrefu wa karibu kilomita 100 katika barabara zisizo nzuri ili kupata huduma maalum za matibabu. Mara nyingi kuchelewa kufika hospitalini kuligharimu maisha ya watoto wengi wachanga.
Watoto hawa ni kama wanajeshi wadogo wanaopigana vita vikubwa tangu pale wanapozaliwa.
Katika Wilaya ya Kwimba, baadhi ya watoto huzaliwa mapema wakiwa na uzani mdogo sana, wakati mwingine chini ya kilo mbili, hali inayoweka maisha yao hatarini.
Lakini sasa, kuna matumaini mapya.

Wilaya ya Kwimba imezindua kituo chake cha kwanza cha kutoa huduma maalum kwa watoto njiti.
Kwa kina mama kama Maria, ambaye amejifungua watoto mapacha njiti, kituo hiki tayari kinaonyesha tofauti kubwa katika maisha ya familia yake.
"Baada ya kujifungua watoto walikuwa na shida ya kupumua, ndio maana wauguzi waliniambia nikae hapa kwasababu walikuwa na vifaa vya kuwahudumia ili waweze kuwa salama, ili na mimi niweze kuondoka nao nyumbani. Na sasa wanaendelea vizuri," anasema Maria.
Hapo awali, wazazi wengi kama Elizabeth Robert na Ntanguta Francis Mwanziwa katika eneo hilo walikabiliwa na maamuzi magumu kuhusu jinsi ya kupata huduma kwa watoto wao wachanga, hasa pale walipohitaji matibabu ya haraka.
Bi Elizabeth anasema: "Nilijifungua mtoto wangu akiwa na kilo moja pointi mbili, mpaka sasa hivi mtoto wangu anaendelea vizuri. Nashukuru sana jengo hili na vifaa vya hapa."
Na mume wa Elizabeth anaongeza kwa kusema: "Nina matumaini kuwa mtoto wangu ataendelea vizuri na maisha yake yatakuwa sawa, kwasababu nikiangalia kule alikotoka, alikuwa kwenye sehemu siyo nzuri. Kwahiyo kuzaa mtoto kama huyu usiseme kwamba huyu mtoto hawezi kuishi, usimkatie tamaa. Yaani endelea kujipa moyo, endelea kumuombea, atapita tu."
Kituo hicho kina vitanda maalum 15 kwa watoto njiti pamoja na vifaa muhimu vya kisasa, ikiwemo mashine za kusaidia kupumua na vifaa vya kutoa joto kwa watoto wachanga. Pia kuna vyumba maalum vya huduma ya kangaroo, ambapo mama hugusana na mtoto ngozi kwa ngozi kifuani ili kusaidia ukuaji wake, pamoja na vyumba vya kunyonyesha na kutoa ushauri wa lishe.
Kwa viongozi wa afya duniani, kituo hiki ni zaidi ya jengo tu.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) barani Afrika, Profesa Mohamed Janabi, anasema mradi huu unaweza kuwa mfano muhimu kwa maeneo mengine ya vijijini barani Afrika.
"Ni kweli kwamba katika bara letu, hasa katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, viwango vya vifo vya watoto wachanga na watoto njiti, bado ni vya juu. Tulichoshuhudia hapa Kwimba, ambapo Taasisi ya Doris Mollel, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Serikali ya Tanzania wamezindua kituo hiki, ni hatua ya moja kwa moja ya kukabiliana na changamoto hiyo. Kituo hiki kinaimarisha huduma za afya za msingi ambazo ndizo nguzo kuu ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wote. Na muhimu zaidi, hatuko katika jiji kubwa, tuko hapa katika jamii yenyewe. Kwa uwezo wake na ari kubwa tuliyoiona kutoka kwa jamii, ni kweli kabisa kuwa kituo hiki ni cha kuokoa maisha. Ni mradi muhimu sana," anaeleza Profesa Janabi.
Kwa mujibu wa Profesa Janabi, vituo kama hivi vinaweza kusaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kuhakikisha huduma maalum zinapatikana karibu na jamii badala ya wazazi kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.
Zaidi ya miundombinu na vifaa, kituo hiki kina hadithi ya kibinafsi iliyo nyuma yake.
Doris Mollel ni mwanamke aliyekuwa nyuma ya maono ya mradi huu. Ujenzi wa kituo hiki ni matokeo ya miaka mingi ya uanaharakati kuhusu watoto njiti. Alianza kwa kuhamasisha jamii kuhusu changamoto zinazowakabili watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, na sasa juhudi zake zimezaa matunda kwa kuanzishwa kwa kituo kinachookoa maisha ya watoto hao.
"Watoto njiti wanaweza kuishi wanapopata uangalizi sahihi, hivyo huu ni ujumbe kwa jamii kwamba sisi ndio tuna jukumu la kuhakikisha wanapata huduma sahihi. Tulikuja na maono, tukatafuta washirika, tukaihusisha jamii, na kila mtu ana nafasi yake katika kuhakikisha jamii inahudumiwa vizuri." anasema Doris Mollel.
Madaktari wanasema siku 28 za kwanza baada ya kuzaliwa ndizo muhimu zaidi kwa mtoto mchanga. Bila huduma ya haraka ya kitabibu, matatizo yanayotokana na kuzaliwa kabla ya wakati yanaweza kuwa hatari sana.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Doris Mollel, zaidi ya watoto 1,300 wanatarajiwa kuokolewa kila mwaka kutokana na kuboreshwa kwa huduma na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya matibabu.
Hii inaleta matumaini mapya kwa familia nyingi na mwanzo bora wa maisha kwa maelfu ya watoto katika jamii.
Mkoa wa Mwanza una wakaazi zaidi ya milioni 3.5, lakini kwa muda mrefu huduma maalum kwa watoto njiti zilikuwa zinapatikana zaidi katika mji mkuu wa mkoa huo pekee.
Kwa miaka mingi, kuzaliwa kabla ya wakati katika Wilaya ya Kwimba kulimaanisha kupigania maisha yako mbali na nyumbani.
Sasa mapambano hayo yanaanza hapo hapo wilayani, yakizungukwa na uangalizi wa karibu wa wataalamu wa afya, vifaa vya kisasa na, zaidi ya yote, matumaini mapya.














