Wabunge wa Cameroon waidhinisha kuundwa kwa nafasi ya makamu wa rais
Bunge la Cameroon limeidhinisha muswada wa kurejesha wadhifa wa Makamu wa rais, ambao ulifutwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, huku seneta mmoja wa chama tawala akielezea mchakato huo kama "wa haraka" na "wa kutiliwa shaka."
Wakati wa kikao cha leo, wajumbe 200 wa bunge la juu na la chini vilivyotawaliwa na chama tawala cha CPDM cha Biya walipiga kura kuunga mkono marekebisho ya katiba, 18 walipiga kura ya Hapana, wanne hawakupiga kura.
Kwa mujibu wa muswada huo ambao BBC imeuona, nafasi hiyo ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa shughuli za serikali, kuboresha uwakilishi pale ambapo kiongozi anahitajika kumwakilisha Rais nje ya nchi, na pia kupunguza mzigo wa urithi wa uongozi kutoka kwa Seneti ili iweze kuzingatia majukumu yake ya kutunga sheria.
Kabla ya marekebisho hayo, katiba ilimtaja kiongozi wa Seneti kuwa ndiye anayechukua madaraka kwa muda mfupi iwapo Rais atafariki, ataacha madaraka, au atashindwa kuyatekeleza.
Muswada uliopitishwa sasa unaeleza kuwa makamu wa rais atateuliwa na kuondolewa na rais, na ndiye atakayemrithi mkuu wa nchi.
Hata hivyo, akiwa rais wa mpito, hataruhusiwa kurekebisha katiba wala kugombea urais.
“Katika kusubiri kutiwa saini na rais wa Jamhuri, nafasi ya makamu wa rais sasa imeanzishwa rasmi nchini Cameroon,” alisema Spika wa Bunge la Taifa, Théodore Datouo, baada ya kura hiyo.
Upinzani umeukosoa muswada huo, ukisema uliwasilishwa bila mashauriano ya kutosha.
Wabunge wa chama cha Social Democratic Front (SDF) walisusia upigaji kura huo. Walikuwa wamependekeza marekebisho yawe kwa mfumo wa makamu wa rais kuchaguliwa pamoja na rais, badala ya kuteuliwa.
Unaweza kusoma pia: