Bei ya kondomu huenda ikapanda kutokana na vita vya Iran, Marekani na Israel

Muda wa kusoma: Dakika 4

Vita vya Iran vimetikisa viwanda vingi na athari zake zinaonekana na huenda komdomu zikaathirika pia. Usumbufu katika usambazaji wa amonia na mafuta ya silikoni, bidhaa zinazotoka na petroli zinazotumika katika utengenezaji wa kondomu, umesababisha hatari ya kupanda kwa bei. Hilo inaweza pia kuathiri mauzo ya rejareja.

Kuna dalili za kutosha kutoka kwa wauzaji nchini India, kwamba bei ya amonia inaweza kuongezeka kwa asilimia 40-50, kutokana na kutokana na hilo bei ya mafuta ya silikoni inaweza pia kuongezeka.

Afisa mmoja anayehusika na biashara hiyo ameiambia BBC Hindi kwa sharti la kutotajwa jina, "hakuna mtu aliyefikiria kwamba kungekuwa na tatizo lolote katika kondomu.”

Amonia hutumika kuimarisha mpira na kuondoa protini iliyozidi. Mafuta ya silikoni hufanya kazi kama mafuta ya kulainisha kondomu.

Lakini ongezeko la bei na athari zake kwenye mauzo ya rejareja si jambo pekee linalotia wasiwasi. Athari za tatizo hili pia zinaleta wasiwasi kwa wale wanaohusika katika tafiti za idadi ya watu na afya (kama vile programu za uzazi wa mpango na programu za kudhibiti UKIMWI).

Poonam Mutreja, mkurugenzi mtendaji wa Population Foundation of India, amase,a, "Kuimarisha upatikanaji wa njia za uzazi wa mpango ni muhimu kwa kufikia matokeo bora ya kiafya. Kwa hivyo, uhaba wa kondomu au kupanda kwa bei zao pia kunaweza kusababisha ongezeko la mimba za utotoni."

Kwa nini bei inaweza kupanda?

Sababu kuu ya tatizo hili ni matatizo yanayohusiana na usambazaji kutokana na vita. Uhaba wa makontena ya usafirishaji duniani unachelewesha usafirishaji kwa wateja nje ya nchi.

Muda wa usafirishaji wa meli umeongezeka kwa sababu meli kubwa zimezuiwa kusafiri kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.

Usafirishaji kupitia Cape of Good Hope unachukua siku 15-20 zaidi. Vikwazo vya anga Mashariki ya Kati vimepunguza uwezo wa usafirishaji wa anga, na kusababisha mrundikano wa mizigo ya bidhaa.

Vyanzo kutoka sekta hiyo vinasema, "Kwa sasa, ni vigumu kukadiria kwa usahihi uhaba katika usambazaji wa komdomu. Kwanza, kuna suala la nyenzo za kuingiza. Gharama ya kuingiza, kisha gharama ya bidhaa, na kisha usumbufu katika usambazaji. Ni wazi, hii itakuwa na athari kwenye usambazaji."

Kampuni ya Cupid Limited, iliyoko Malegaon, Maharashtra, India inasema, kupitia R. Babu, meneja mkuu mkuu wa Cupid Limited, "Bei za mafuta ya silikoni na karatasi ya alumini zimepanda. Bei za mpira pia zinapanda. Kwa hivyo, hii inaathiri gharama za utengenezaji. Shida ni kwamba hatuwezi kuwapa wachuuzi bidhaa za bei kubwa kwa sababu hawako tayari kwa hilo. Kwa hivyo hili ni tatizo kubwa."

R. Babu anasema, "Tunasafirisha nje asilimia 80 ya jumla ya uzalishaji wetu, hasa Urusi, Afrika Kusini, Ulaya na Brazili. Pia tunakabiliwa na ugumu wa kupata meli za usafirishaji kusafirisha bidhaa kwenda maeneo haya."

Wasiwasi kuhusu dawa

Kutokuwa na uhakika katika sekta ya kondomu pia kunaonekana katika sekta ya dawa kwa ujumla. Sekta hii inakabiliwa na changamoto mbili.

Viranchi Shah, msemaji wa Chama cha Watengenezaji wa Dawa India (IDMA), anasema, "Changamoto moja iko upande wa usafirishaji. Kuna tatizo kubwa kuhusu upatikanaji wa meli za kusafirisha kwenda Afrika, Mashariki ya Kati na Ulaya, iwe ni kwa njia ya baharini au angani. Sababu kuu ya hili ni kwamba upatikanaji wa meli umepungua. Kwa kuwa mzunguko umepungua, gharama imeongezeka."

"Hili ni eneo linalohitaji kufuatiliwa. Athari inaonekana wazi," Shah anasema. "Lakini kuhusu upatikanaji wa dawa nchini India hakuna changamoto."

Lakini changamoto inayokabili tasnia hii ni kwamba dawa nyingi zina viambato vinavyotokana na kemikali za petroli.

"Kuna wimbi la uvumi unaoendelea hivi sasa. Uvumi huu umesababisha hofu kwamba kunaweza kuwa na uhaba. Hii ndiyo sababu bei zimepanda. Hivi sasa, zaidi na uvumi kuliko uhaba halisi," anasema Shah kutoka Ahmedabad.

Anasema, "Kuna mazingira ya hofu. Kwa kweli, watu hawana uhakika kitakachotokea kesho."