Iran yailaumu Marekani kwa kuvunjika mazungumzo ya kusaka amani

Iran yasema kuwepo kwa matakwa mengi ya Marekani ndio yamesababisha mazungumzo ya amani kushindwa huko Islamabad

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. Watu wenye silaha wavamia kituo cha watoto yatima Nigeria na kuwateka nyara watoto

    Hj

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Magenge ya wahalifu mara nyingi huwateka watu kwa ajili ya fidia nchini Nigeria

    Watoto wanane bado hawajulikani walipo baada ya watu wenye silaha kuvamia kituo cha watoto yatima ambacho hakijasajiliwa katika Jimbo la Kogi kaskazini-kati mwa Nigeria na kuwateka nyara watoto 23, mamlaka zimesema.

    Kamishna wa habari wa Kogi, Kingsley Fanwo, amesema watoto 15 waliokolewa katika operesheni ya haraka ya mashirika ya usalama.

    Ameongeza kuwa shambulio la Jumapili pia lilishuhudia mmiliki wa kituo hicho akitekwa.

    Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo, lakini vyanzo vya usalama vinasema jimbo hilo lina wapiganaji wa Boko Haram, na kumekuwa na mashambulizi kadhaa ya vurugu katika eneo hilo.

    Nigeria pia inakabiliwa na mgogoro wa utekaji nyara katika sehemu nyingi za nchi, huku magenge ya wahalifu yakiwateka watu kwa ajili ya fidia. Serikali imefanya malipo ya fidia kuwa kinyume cha sheria lakini hii haijazuia utekaji nyara huo.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Watawa wa Sri Lanka wakamatwa na kilo 110 za bangi kwenye mizigo yao

    Hj

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Watawa ishirini na wawili wamekamatwa katika uwanja wa ndege nchini Sri Lanka baada ya maafisa kugundua kilo 110 (pauni 242) za bangi zilizofichwa kwenye mizigo yao.

    Maafisa wa forodha walisema kila mtawa alipatikana na takriban kilo 5 kwenye mizigo walipofika katika mji mkuu wa Colombo siku ya Jumamosi.

    Watawa hao, ambao wengi wao walikuwa wanafunzi, walikuwa wakirudi kutoka Thailand baada ya kupewa likizo ya siku nne chini ya mfadhili asiyejulikana.

    Mtawa wa 23, anayeaminika kuandaa safari hiyo, amekamatwa katika kitongoji cha Colombo, polisi waliiambia BBC Sinhala.

    Kulingana na kaimu msemaji wa polisi, mtawa huyo - ambaye hakujiunga na safari hiyo - aliwaambia watawa wengine kwamba "vifurushi hivi ni mchango" na gari la kubeba mizigo litakuja kuchukua vifurushi hivyo.

    Ofisi ya Dawa za Kulevya ya Polisi ya Sri Lanka iligundua picha na video kwenye simu za mkononi za baadhi ya watawa, kutoka mahekalu ya Sri Lanka, zikiwaonyesha wakifurahia mapumziko yao wakiwa wamevaa nguo za kawaida.

    Watawa hao 22 waliwekwa rumande kwa siku saba kwa mahojiano zaidi baada ya kufika mahakamani siku ya Jumapili.

    Polisi waliiambia BBC Sinhala wanaamini watawa hao huenda hawakujua walichokuwa wamebeba.

    Dawa hizo zilipatikana kwenye vifaa vya shule na peremende.

    Inadhaniwa kuwa ni mara ya kwanza kundi la watawa kukamatwa kwa tuhuma za kuingiza dawa za kulevya nchini kupitia uwanja wa ndege.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Asasi za kiraia zapinga ripoti ya Jaji Chande

    OL

    Chanzo cha picha, LHRC

    Maelezo ya picha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga

    Asasi za kiraia na watetezi wa haki za binadamu wamepinga ripoti ya Jaji Mohamed Chande Othman, juu ya matukio ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 na kuelezea mapungufu ya ripoti hiyo.

    Asasi hizo kumi na nne zinaikosoa tume kwa kutumia Polisi na vyombo vya usalama vingine katika uchunguzi wao, kwani vyombo hivyo vinalalamikiwa kuhusika katika kuua, kuteka, kuondoa miili ya watu au majeruhi kwenye vituo vya afya na mahospitali na kuipeleka kusikojulikana, hivyo haviwezi kuwa chanzo cha kuaminika katika uchunguzi.

    Vilevile asasi hizo zinaikosoa tume kwa na kigugumizi katika kuwataja waliohusika kwani tume imekiri kuwepo kwa vitendo vya utekaji na kupotea kwa watu, lakini haijaweza kueleza kwa kina nani wanaohusika na vitendo hivyo, wala nani anayetoa amri ya utekelezaji wake.

    Kwa upande mwingine, zinasema tume imeeleza kuwa waliohusika na vurugua walipewa pesa, lakini haijasema ni nani aliyetoa fedha hizo, licha ya kudai kuwa na ushahidi.

    Tume iliyoundwa wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu kuchunguza matukio ya vurugu na vifo, ilitoa taarifa yake tarehe 23/04/2026, ambapo jumla ya watu 518 walifariki katika vurugu hizo.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Wapiganaji wa Urusi waondoka kaskazini mwa Mali baada ya mashambulizi ya waasi

    p

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kikosi cha Urusi cha Afrika kilifikia makubaliano na waasi wa FLA (kwenye picha) kuondoka Kidal

    Baada ya wikendi ya mashambulizi yaliyoratibiwa kote Mali na wapiganaji wanaotaka kujitenga na wanamgambo wa Kiislamu, vikosi vya Urusi vilivyoko nchini humo vikisaidia kuilinda serikali ya kijeshi vimethibitisha kuwa vimeondoka katika mji wa kaskazini wa Kidal.

    Katika mfululizo wa machapisho kwenye mitandao ya kijamii, Kikosi cha Afrika cha Urusi kilisema "wameondoka katika eneo hilo" pamoja na wanajeshi wa Mali.

    Kundi la Azawad Liberation Front (FLA) linalotaka kujitenga lilisema Jumapili kwamba wanajeshi wa Urusi wamekubali kujiondoa, na kudai udhibiti wa Kidal, wakitangaza "sasa iko huru".

    Mali imekabiliwa na uasi kwa miaka mingi kutoka kwa waasi wanaotaka kujitenga kaskazini, na makundi yenye uhusiano na al-Qaeda na kundi la Islamic State.

    Siku ya Jumamosi, milipuko na milio ya risasi iliripotiwa katika sehemu nyingi za Mali, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Bamako.

    Mashambulizi pia yaliripotiwa katika miji ya kati ya Sevare na Mopti, pamoja na Gao na Kidal kaskazini, kwenye ukingo wa kusini wa jangwa la Sahara.

    Huko Kati - mji ulio karibu na mji mkuu na makao makuu ya kambi kubwa ya kijeshi - Waziri wa Ulinzi wa Mali Sadio Camara aliuawa katika shambulio la bomu la gari la kujitoa mhanga nyumbani kwake.

    Ripoti zinaonyesha kuwa mashambulio ya FLA yalifanyika katika maeneo ya kaskazini yanayotawaliwa na Watuareg, huku kundi la jihadist Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) likifanya mashambulizi katika maeneo mengi.

    Mapigano yalianza tena huko Kidal siku ya Jumapili, lakini muda mfupi baadaye, msemaji wa FLA Mohamed Elmaouloud Ramamane alisema makubaliano yamefikiwa kati yao na Jeshi la Afrika la Urusi kwa "lengo la kuhakikisha wanaondoka salama katika eneo hilo."

    Kundi hilo linasema limechukua udhibiti wa mji huo, ambao ulikuwa makao makuu yasiyo rasmi ya harakati ya kujitenga kwa zaidi ya muongo mmoja kabla ya kutekwa na jeshi la Mali kwa msaada wa mamluki wa Urusi mwishoni mwa mwaka 2023.

    Ingawa Jeshi la Afrika la Urusi limethibitisha kujiondoa Kidal, limesema shughuli zao zitaendelea kwingineko.

    Wapiganaji wengi wa Kikosi cha Urusi Afrika walikuwa wa kundi la mamluki wa Urusi la Wagner. Kufuatia kifo cha kiongozi wao Yevgeni Prigozhin 2023, shughuli nyingi za kundi hilo zilichukuliwa na wizara ya ulinzi ya Urusi, ambayo iliunda Kikosi kipya cha Afrika.

    Kikosi cha Afrika kinasimamiwa na Naibu Waziri wa Ulinzi wa Urusi Yunus-Bek Yevkurov, huku shughuli zake zikiendeshwa na Meja Jenerali Andrey Averyanov, mtu muhimu katika shirika la ujasusi wa kijeshi la GRU.

    Jukumu la Urusi ni kuzisaidia serikali kubaki madarakani, hilo huenda sanjari na kupata rasilimali muhimu za asili, kama vile dhahabu, almasi na urani.

    Kama Wagner, kikosi cha Afrika kimeshutumiwa kufanya ukatili dhidi ya raia.

    Nchini Mali, wanachama wa Africa Corps wanaripotiwa kulipwa $3,000 (£2,200) kwa mwezi.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Colombia yatangaza zawadi ya dola milioni 1.4 kwa taarifa za mshukiwa wa shambulio la bomu

    o

    Chanzo cha picha, Colombian Defence Ministry

    Maelezo ya picha, Waziri wa ulinzi anamshutumu 'Marlon' kwa kuhusika na mashambulizi

    Waziri wa Ulinzi wa Colombia, Pedro Sánchez ametangaza zawadi kubwa kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa kiongozi wa waasi anayejulikana kama "Marlon."

    "Marlon", ambaye jina lake halisi ni Iván Jacob Idrobo Arredondo, anashukiwa kuamuru shambulio la bomu la Jumamosi kwenye Barabara Kuu ya Pan-American, ambapo watu 20 waliuawa.

    Shambulio hilo ni mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi dhidi ya raia na linakuja zaidi ya mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 31 Mei.

    Sánchez alisema zawadi hiyo ni peso bilioni 5 (sawa na dola za kimarekani milioni 1.4; £1m).

    Waziri wa ulinzi anamshutumu "Marlon" kwa kuhusika na shambulio la Jumamosi pamoja na mfululizo wa mashambulizi mengine katika majimbo ya Cauca na Valle del Cauca, kusini-magharibi mwa Colombia, mwishoni mwa wiki.

    Hakuna ushahidi au maelezo yaliyotolewa.

    Katika tukio baya zaidi kati ya haya, wanawake 15 na wanaume watano waliuawa kwenye barabara kuu inayounganisha miji ya Cali na Popayán, gavana wa jimbo la Cauca alisema.

    Mabasi kadhaa na magari mengine yaliharibiwa katika mlipuko huo, ambao ulisababisha shimo kubwa.

    "Marlon" ni wa kundi lenye silaha linaloongozwa na muasi anayejulikana kwa jina la utani la Iván Mordisco, mtu anayetafutwa sana nchini Colombia.

    Mordisco aliwahi kuwa sehemu ya Kikosi cha Wanajeshi wa Mapinduzi cha Colombia (Farc) lakini alijitenga na kundi la waasi lilipokuwa likijadiliana kuhusu makubaliano ya amani ya 2016 na serikali.

    Anachukuliwa kuwa kiongozi wa waasi mwenye nguvu zaidi nchini Colombia. Kundi lake linajihusisha na uchimbaji madini na ujambazi pamoja na biashara haramu ya dawa za kulevya.

    Rais Gustavo Petro aliwaelezea wahusika kama "magaidi, wafashisti na wafanyabiashara wa dawa za kulevya" na akaamuru kupelekwa wanajeshi wa ziada katika eneo hilo.

    Muhula wa Petro unaisha Agosti mwaka huu. Akizuiwa na katiba kugombea muhula wa pili, amemuunga mkono mgombea wa mrengo wa kushoto, Iván Cepeda.

    Rais mpya anatarajiwa kuchaguliwa tarehe 31 Mei, huku uchaguzi wa marudio ukitarajiwa kufanyika tarehe 21 Juni.

  6. Maharamia wateka meli nyingine karibu na pwani ya Somalia

    l

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka za baharini zinaonya kuhusu tishio kwa meli zinazopita katika pwani ya Somalia baada ya meli ya mizigo kukamatwa katika kitendo kinachoshukiwa kuwa cha uharamia.

    Kituo cha Biashara za Baharini cha Uingereza (UKMTO) kimeongeza kiwango cha tishio katika eneo hilo baada ya watu kuiteka meli na kuilekeza iende kwenye maji ya eneo la Somalia siku ya Jumapili.

    Meli nne zimetekwa katika matukio yanayoshukiwa kuwa ya uharamia katika wiki iliyopita ikiwemo meli ya uvuvi na meli ya mafuta.

    Miaka mitatu iliyopita uharamia ulikuwa umetoweka katika eneo hili la Bahari ya Hindi ambalo hapo awali lilikuwa maarufu kwa utekaji nyara.

    "Kutokana na tishio la uharamia meli zinashauriwa kusafiri kwa tahadhari," UKMTO ambayo inahusika na masuala ya usalama baharini imesema katika taarifa yake.

    UKMTO ilisema katika taarifa kwamba utekaji nyara huo wa siku ya Jumapili ulitokea maili sita kutoka Garacad, Somalia. Hakuna maelezo zaidi yaliyoripotiwa.

    UKMTO pia ilitoa onyo kuhusu utekaji nyara mwingine kando ya pwani ya Mareeyo, kaskazini mwa Somalia uliotokea tarehe 21 Aprili.

    Maharamia pia waliteka nyara meli ya mafuta, Honour 25, ikiwa na wafanyakazi 17 iliyokuwa ikisafiri karibu na pwani ya Somalia Aprili 22, kulingana na maafisa kadhaa wa usalama waliozungumza na BBC .

    UKMTO pia iliripoti kwamba meli ya uvuvi yenye bendera ya Somalia ilitekwa Alhamisi.

    Watu wawili wenye silaha pia walijaribu kupanda meli ya mizigo kutoka kwenye boti ndogo siku ya Alhamisi, UKMTO iliripoti, ingawa walishuka baada ya wafanyakazi wa meli hiyo kufyatua risasi za onyo.

    Kati ya mwaka 2005 na 2012, maharamia kutoka Pembe ya Afrika walipata kati ya dola milioni 339 (£266m) na dola milioni 413 (£325) kwa kuwashikilia mateka wafanyakazi na kudai malipo ya fidia, kwa mujibu wa makadirio ya Benki ya Dunia.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Watu 42 wauawa Chad katika mzozo kuhusu kisima cha maji

    p

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kuna mivutano ya mara kwa mara kuhusu maji nchini Chad

    Maafisa wanasema watu wasiopungua 42 wameuawa na 10 kujeruhiwa katika mapigano kati ya makabila hasimu mashariki mwa Chad katika mzozo ulioanza kuhusu kisima cha maji.

    Mgogoro katika jimbo la Wadi Fira, ambao mwanzoni ulikuwa kati ya familia mbili, uliongezeka na kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyoenea katika eneo kubwa, huku vijiji vikiteketezwa.

    Serikali ya Chad ilisema siku nya Jumapili kwamba ujumbe ulioongozwa na naibu Waziri Mkuu Limane Mahamat umetumwa katika eneo hilo na hali imedhibitiwa.

    Mapigano makali ya kijamii ni ya kawaida katika taifa hilo la Afrika ya Kati, huku kukiwa na mzozo wa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na mivutano ya kikabila.

    Mapigano hayo mara nyingi husababishwa maji na ardhi ya malisho.

    Kuwasili kwa wakimbizi waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi jirani ya Sudan katika miezi ya hivi karibuni kumeongeza mvutano zaidi kuhusu rasilimali na usalama.

    Siku ya Jumapili, naibu waziri mkuu alisema serikali inachukua hatua zote muhimu kuzuia mzozo nchini Sudan usivuruge eneo la mpaka.

    Mapigano ya kijamii nchini Chad yamesababisha vifo vya mamia ya watu katika miaka ya hivi karibuni, wakiwemo 33 waliouawa mwezi Novemba kutokana na kisima kilichokuwa kinagombaniwa huko Dibebe, kusini-magharibi.

    Kulingana na shirika la kimataifa la kukabiliana na mizozo, watu 1,000 waliuawa na wengine 2,000 kujeruhiwa katika mapigano takriban 100 kati ya mwaka 2021 na 2024.

    Kundi la Haki za Binadamu la Amnesty International mwaka jana lilisema limerekodi matukio saba ya vurugu kati ya wafugaji na wakulima kati ya 2022 na 2024, na kusababisha vifo 98.

    Mapigano hayo yalisababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na masuala mengine, na licha ya vurugu zinazojirudia, serikali imeshindwa kuwalinda watu.

    Amnesty inasema mara nyingi majibu ya vikosi vya usalama huchelewa na wahusika hawawajibishwi.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Mashambulizi ya Israel yaua 14 Lebanon wakiwemo watoto wawili

    k

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Jeshi la Israeli limetetea mashambulizi yake ya siku ya Jumapili, likisema lilikuwa likiwalenga wapiganaji wa Hezbollah katika maeneo yake kusini mwa Lebanon.

    Wizara ya afya ya Lebanon inasema mashambulizi ya Israeli siku ya Jumapili yamewaua watu 14 , wakiwemo watoto wawili na wanawake wawili.

    Jeshi la Israeli (IDF) lilifanya mashambulizi ya angani kwenye maeneo ambayo lilidai yalitumika "kuendeleza mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa IDF".

    Katika taarifa tofauti, jeshi la Israeli linasema mwanajeshi wa IDF mwenye umri wa miaka 19 ameuawa na wengine sita kujeruhiwa na shambulio la ndege zisizo na rubani za Hezbollah nchini Lebanon.

    Mapigano kati ya Hezbollah na Israel nchini Lebanon yameendelea huku kukiwa na usitishaji mapigano.

    Mkataba wa kusitisha mapigano ulianza kutekelezwa tarehe 16 Aprili, na tangu wakati huo umeongezwa kwa wiki tatu.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Iran yailaumu Marekani kwa kuvunjika mazungumzo ya kusaka amani

    ]

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Waziri wa mambo ya nje wa Iran Araghchi amewasili leo Urusi

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi anasema wingi wa matakwa ya Marekani kumesababisha mazungumzo ya amani kushindwa huko Islamabad, Pakistan, amewaambia waandishi wa habari baada ya kuwasili Urusi.

    Akiwasili St Petersburg, Araghchi anasema atashauriana na washirika wake wa Urusi kuhusu vita vya Mashariki ya Kati, katika mahojiano kwa lugha ya Kiajemi na kuchapishwa kwenye chaneli yake ya Telegram.

    Kuwasili kwa Araghchi nchini Urusi kunakuja baada ya mazungumzo na wapatanishi wa Pakistan huko Islamabad. Aliwaambia waandishi wa habari majadiliano hayo yalishughulikia masharti ambayo yanaweza kubeba mazungumzo ya kusaka amani.

    Waziri wa mambo ya nje pia alitaja kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz akisema suala hilo bado ni suala la kimataifa na anatoa wito kwa majirani ikiwemo Oman kufanya kazi na Iran kwa maslahi yao ya pamoja kwa ajili ya mlango huo.

    Kauli ya Araghchi inakuja baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuvunja safari iliyopangwa ya maafisa wa Marekani kwenda Pakistani mwishoni mwa wiki kwa ajili ya mazungumzo kuhusu vita vya Mashariki ya Kati, akidai itakuwa ni kupoteza "muda."

    Pia unaweza kusoma:

  10. Gachagua afika mahakamani katika kesi ya kupinga kuondolewa madarakani

    ]

    Chanzo cha picha, citizen

    Maelezo ya picha, Kiongozi wa Chama cha Demokrasia kwa Wananchi (DCP) Rigathi Gachagua akiwa ameambatana na mkewe Dorcas Rigathi katika Mahakama Kuu Aprili 27, 2026

    Vikao vya kusikiliza mashauri ya kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa Niabu wa Rais wa Kenya Rigathi Gachagua Rigathi Gachagua kutaka uamuzi wa kumuondoa madarkani ubatilishwa vimeanza leo Jumatatu jijini Nairobi.

    Mawakili wake wameiambia Mahakama Kuu kuwa mchakato wa kumuondoa madarakani ulikuwa na mapungufu mengi.

    Kiongozi wa Chama cha Demokrasia kwa Wananchi (DCP) aliwasili mahakamani Jumatatu, akifuatana na mkewe Dorcas Rigathi, wanawe wawili na timu yake ya mawakili.

    Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu.

    Gachagua aliwasilisha kesi mahakamani kupinga uhalali na uhalali wa kikatiba wa mchakato wa kumshtaki uliosababisha kuondolewa kwake madarakani kama Naibu Rais.

    Anasema mchakato huo ulikiuka taratibu, ukiukwaji wa ulinzi wa kikatiba, na kunyimwa haki yake ya kusikilizwa.

    Kesi hiyo pia inatilia shaka maamuzi na hatua zilizochukuliwa wakati na baada ya uongozi wake, huku timu yake ya wanasheria ikisisitiza baadhi ya hatua zilizochukuliwa dhidi yake zilichochewa kisiasa na hazikuwa na msingi wa kisheria.

    Kesi hiyo inatarajiwa kushughulikia maswali muhimu ya kikatiba kuhusu kuondolewa kwa Naibu Rais, mgawanyo wa madaraka, na maamuzi ya mahakama katika shughuli za bunge.

    Gachagua, alipokuwa akizungumza Mombasa siku ya Jumapili, alisema amejenga kesi ngumu kuthibitisha kwamba alifukuzwa kazi kwa misingi isiyo ya kikatiba, akionyesha imani kwa Mahakama kumpa haki.

    Gachagua aliondolewa madarakani Oktoba 2024, na kuwa naibu rais wa kwanza wa Kenya kushtakiwa, na tangu wakati huo amedai kwamba hongo zilitumika katika Bunge la Kitaifa na Seneti ili kuunga mkono kuondolewa kwake madarakani.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Kipa wa Real Zaragoza apoteza udhibiti, na kumpiga mpinzani uwanjani

    hh

    Chanzo cha picha, LaLiga TV

    Kipa wa Real Zaragoza, Esteban Andrada, anakabiliwa na adhabu kali baada ya kumpiga mpinzani wake katika mechi ya mchuano mkali wa daraja la pili nchini Hispania dhidi ya Huesca, licha ya kuwa tayari alikuwa amefukuzwa uwanjani.

    Mchezaji huyo raia wa Argentina alipokea kadi ya pili ya njano baada ya kumdondosha mchezaji wa Huesca katika dakika za nyongeza za mchezo uliokuwa mkali wa kuamua kuepuka kushuka daraja.

    Baada ya hapo alikimbia moja kwa moja kuelekea kwa nahodha wa Huesca, Jorge Pulido, na kumpiga ngumi usoni.

    Tukio hilo lilisababisha vurugu kubwa uwanjani, na kupelekea pia kipa wa Huesca Dani Jiménez na mchezaji wa Zaragoza Dani Tasende kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

    Baadaye Andrada aliomba radhi akisema “alipoteza umakini” na yuko tayari kupokea adhabu yoyote itakayotolewa.

    Klabu ya Zaragoza pia ilitoa taarifa ikilaani vikali tukio hilo na kusema itachukua hatua za kinidhamu.

    “Tulishuhudia matukio yasiyofaa katika mchezo huu na ambayo hayakupaswa kutokea,” ilisema klabu hiyo.

    “Imeongeza kuwa matukio hayo hayaakisi maadili ya Real Zaragoza wala mashabiki wake, ambao kihistoria wamejulikana kwa nidhamu, ujasiri na heshima kwa wapinzani.”

    Kocha mkuu wa Huesca José Luis alisema baada ya mchezo kuwa tukio hilo ni “kupoteza udhibiti kabisa” na kwamba licha ya hali ya mchezo kuwa ya presha kubwa, halikubaliki.

    Huesca ilishinda mchezo huo kwa bao 1-0 kupitia Oscar Sielva, huku timu zote mbili zikiendelea kubaki katika eneo la kushuka daraja zikiwa na mechi tano zilizobaki msimu huu.

    Soma zaidi:

  12. DRC yaanzisha kikosi cha kijeshi kulinda migodi ya madini

    Mmoja wa maofisa hao alisema hilo ni wazo la Rais Félix Tshisekedi lenye lengo la kuleta mageuzi katika sekta ya madini na kupambana na ubadhirifu wa madini ya thamani.

    Chanzo cha picha, Presidence RDC

    Maelezo ya picha, Mmoja wa maofisa hao alisema hilo ni wazo la Rais Félix Tshisekedi lenye lengo la kuleta mageuzi katika sekta ya madini na kupambana na ubadhirifu wa madini ya thamani.

    Mamlaka ya madini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo imezindua kikosi cha wanamgambo kitakachohusika na kulinda migodi, kutekeleza sheria zake na kufuatilia kwa ukaribu uzalishaji wa madini.

    Rafael Kabengele, mkuu wa shirika la madini, amesema kikosi hicho ni wazo la Rais Félix Tshisekedi kama sehemu ya mageuzi ya sekta hiyo na mapambano dhidi ya usimamizi mbovu wa madini ya thamani.

    Awamu ya kwanza ya kikosi hicho cha kijeshi itakuwa na wanajeshi kati ya 2,500 na 3,000 ambao wanatarajiwa kuanza kazi Desemba 2026 baada ya mafunzo.

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi yenye utajiri mkubwa wa rasilimali za asili, lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa za kuhakikisha wananchi wananufaika nazo.

    Kufikia mwaka 2028, inatarajiwa kuwa watu 20,000 watakuwa wameajiriwa katika kikosi hicho kusimamia hadi migodi 22 katika maeneo mbalimbali ya nchi.

    Baadhi ya migodi, kama Rubaya mojawapo ya migodi mikubwa zaidi ya koltani duniani kwa sasa iko chini ya udhibiti wa muungano wa AFC M23.

    Kikosi hicho kipya cha dola milioni 100, kinachoitwa Walinzi wa Migodi, kitachukua nafasi ya wanajeshi wa kawaida waliokuwa wakilinda migodi, na kimefadhiliwa na Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu.

    Wanachama wake watasimamia uchimbaji na usafirishaji wa madini ya thamani hadi yanapotoka nchini.

    Inakadiriwa kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina utajiri wa madini usiotumika wenye thamani ya dola trilioni 25, lakini sehemu kubwa ya wananchi wake bado wanaishi katika umaskini mkubwa na vita vinavyoendelea mashariki mwa nchi.

    Soma zaidi:

  13. Ziara ya Mfalme Charles Marekani kuendelea kama ilivyopangwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kasri la Buckingham linasema ziara ya kiserikali ya Mfalme Charles III nchini Marekani - ambayo inaanza baadaye leo - "itaendelea kama ilivyopangwa", japo kuna marekebisho madogo.

    Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya majadiliano kufanywa pande zote mbili za Atlantiki na ushauri kutoka kwa serikali, kulingana na taarifa ya Jumapili.

    Ikulu ilisema Mfalme "amefarijika sana" kusikia rais wa Marekani, Melania Trump na wageni wengine hawakujeruhiwa katika tukio la Wanshington.

    Mfalme Charles anatarajiwa kuhutubia mabunge yote mawili ya Congress, kutembelea ukumbusho wa 9/11 huko New York na kuhudhuria uwekaji wa shada la maua kuwaenzi wanajeshi waliokufa wa Marekani na Uingereza huko Virginia.

    Bado haijabainika ni marekebisho gani yamefanywa kwenye safari hiyo.

    Inatarajiwa kufanyika siku chache baada ya ripoti kuibuka kwamba Marekani inaweza kuktathmini msimamo wake juu ya uhuru wa Uingereza juu ya Visiwa vya Falklands.

  14. 'Tunaishi katika ulimwengu wa ajabu' - asema Trump baada ya jaribio la mauaji dhidi yake

    .

    Chanzo cha picha, reu

    Tukio la shambulio la risasi kwenye dhdifa ya Waandishi wa White House linaonekana kuwa jaribio la tatu la mauaji dhidi ya Donald Trump, kufuatia matukio ya Butler, Pennsylvania mnamo Julai 2024, na katika klabu yake ya gofu huko Florida mnamo Septemba mwaka huo.

    Lakini katika mahojiano na 60 Minutes jana, Trump alisema: "Sikuwa na wasiwasi. Ninaelewa maisha. Tunaishi katika ulimwengu wa ajabu."

    Alipoulizwa kuhusu kilichojiri - ambapo JD Vance aliondolewa wa kwanza ukumbini - Trump alisema "haikuwa rahisi" kwa maafisa wa usalama kumuondoa kwenye chumba hicho.

    "Nilitaka kuona kinachofanyika.. nilitaka kuona kinachoendelea. Na kufikia wakati huo ndipo tulibaini, labda kuna kitu kibaya kimetokea."

    Alipoulizwa kuhusu "kushuka" alipokuwa akiongozwa kutoka ukumbini, Trump alijibu: "Nilianza kutembea nao [maafisa wa usalama]. Niligeuka, nikaanza kutembea, wakasema, 'Tafadhali shuka. Tafadhali shuka chini.'

    "Kwa hiyo nilishuka na yule mwanamke wa kwanza akashuka pia."

    CBS, mshirika wa habari wa BBC imeona hati iliyoandikwa inayoaminika kuhusishwa na mshukiwa, Cole Allen, ikisema alitaka kuwalenga wanachama wa utawala wa Trump "kutoka ngazi ya juu hadi chini".

    Wakati wa mahojiano ya Dakika 60, Trump alikasirishwa na mwandishi wa habari Norah O'Donnell baada ya kuuliza juu ya yaliyomo kwenye dondoo, ambayo ni yalijumuisha maneno kama vile "mnyanyasaji, mbakaji na msaliti".

    Alimsuta O'Donnell kwa kumuuliza juu ya dondoo hizo, na kuongeza kuwa "unapaswa kuona aibu kusema hivyo, kwa sababu mimi sihusiki na mambo hayo".

    Maelezo zaidi:

  15. Bei ya mafuta yapanda baada ya mazungumzo ya amani ya Marekani na Iran kukwama

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bei ya mafuta imepanda baada ya duru ya pili ya mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Iran kukwama tena.

    Mafuta ya Brent ilipanda hadi dola 107.26 kwa pipa, wakati mafuta yasiyosafishwa ya Marekani yalipanda kwa 1% kwa dola 95.40.

    Haya yanajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema Jumamosi kwamba Washington iliahirisha mpango wa kutuma ujumbe wake nchini Pakistan kwa mazungumzo na wenzao wa Iran.

    Ugavi wa nishati duniani umekuwa chini ya shinikizo kubwa tangu kuanza kwa vita vya Iran kwani njia kuu ya baharini ya Hormuz imefungwa.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi alisema Jumapili kwamba "majadiliano muhimu juu ya masuala ya nchi mbili na maendeleo ya kikanda" yanaendelea na Oman.

    Alichapisha kwenye mtandao wa kijamii: "Lengo letu lilijumuisha njia za kuhakikisha usafiri salama ambao ni wa kufaidisha majirani wote wapendwa na ulimwengu.

    Majirani zetu ndio kipaumbele chetu." Araghchi amewasili St Petersburg, Urusi leo Jumatatu "kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin", shirika la habari la serikali ya Iran Irna liliripoti.

    Takriban thuluthi moja ya mafuta ghafi na gesi asilia (LNG) hupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Maelzo zaidi:

  16. Vita vya Iran: Araqchi awasili Urusi kwa mazungumzo na Putin

    Putin na Araqchi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi amewasili St. Petersburg, Urusi ambapo anatarajiwa kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow, shirika la habari la Iran, limeripoti likimnukuu balozi wa Iran nchini Urusi, Kazem Jalali.

    Bwana Araghchi alisafiri kwa ndege ya "Minab Flight 168" kuwakumbuka watoto waliouawa katika shule ya Minab, Mkoa wa Hormozgan, waliouawa katika shambulio la Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Madhumuni ya ziara ya Bw. Araqchi inaelezwa kuwa "kukutana na kujadiliana na Rais wa Urusi Vladimir Putin."

    .

    Chanzo cha picha, TELEGRAM/REUTERS

    Siku ya Jumapili, baada ya kusafiri hadi Muscat na kukutana na maafisa wa Oman, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alielekea Islamabad kwa mara ya pili katika siku tatu zilizopita, na kukutana na maafisa wa Pakistan kabla ya kuondoka kwenda Moscow.

    Maelezo ya ziara hizi na sababu ya kurejea kwake Oman na Pakistan bado haijafichuliwa.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Watu 14 wauawa Lebanon licha ya mpango wa usitishaji mapigano kufikiwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya Afya ya Lebanon inasema kuwa watu 14 wakiwemo watoto wawili waliuawa Jumapili katika mashambulizi ya Israel.

    Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) hapo awali alitoa ilani ya kuhama kwa wakaazi kutoka vijiji kadhaa kusini mwa Lebanon, na kuonya kuwa wa kupuuza ilani hiyo "kungelihatarisha maisha yao".

    IDF baadaye ilisema ilifanya "mashambulizi ya angani" kuwalenga wanamgambo wa Hezbollah katika maeneo ya kusini mwa Lebanon ambayo inadai yanatumiwa "kuendeleza mashambulizi dhidi ya wanajeshiwa Israel".

    Pia imesema mwanajeshi wa IDF mwenye umri wa miaka 19 ameuawa na wengine sita kujeruhiwa na shambulio la ndege isiyo na rubani ya Hezbollah nchini Lebanon.

    Hezbollah ilirusha ndege tatu zisizo na rubani kuelekea Israeli, IDF iliripoti, huku ikiongeza kuwa ziliangushwa na jeshi la anga la Israeli kabla ya kuvuka mpaka.

    Nchi hizo mbili zilifikia mpango wa usitishaji mapigano, ambao ulianza kutekelezwa tarehe 16 Aprili na kuongezwa muda kwa wiki tatu Alhamisi wiki iliyopita.

    Chini ya makubaliano hayo, Israel inasalia na "haki yake ya kuchukua hatua zote za kujilinda, wakati wowote, dhidi ya mashambulizi yaliyopangwa, yanayokaribia, au yanayoendelea".

    Akizungumza katika mkutano wa serikali, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema IDF "inaendelea, na inafanya kazi kwa nguvu" nchini Lebanon, akisema hatua za Hezbollah "zinasambaratisha usitishaji mapigano".

    Soma zaidi:

  18. Traoré alaani mashambulizi ya Mali na kuyataja kuwa 'ya kinyama'

    Kapteni Ibrahim Traoré

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kapteni Ibrahim Traoré, rais wa muungano wa Mataifa ya Sahel (AES), amelaani mashambulizi ya kupangwa nchi ya Mali, takribani saa 48 baada ya matukio hayo.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumapili usiku, alitaja mashambulizi hayo kama "ya kinyama " na kusema "yanaungwa mkono na maadui wa mapambano ya ukombozi wa Sahel".

    Traoré aliongeza kuwa mashambulizi hayawezi "kuyumbisha nia ya watu mashujaa wa Sahel kuishi kwa uhuru, amani na heshima". Pia alitoa salamu za rambirambi kwa walioathirika.

    Alisema mashambulizi hayo yaliyoratibiwa yalipangwa kwa muda mrefu kwa madhumuni ya kuathiri vikosi vya usalama vya Mali na kuwatia hofu raia.

    Kapteni Traoré alichukua urais wa zamu wa AES mwezi Desemba, akichukua nafasi ya kiongozi wa kijeshi wa Mali, Jenerali Assimi Goïta.

    AES inayaleta pamoja mataifa ya Mali, Niger na Burkina Faso, ambayo yanaongozwa na serikali za kijeshi zilizoingia madarakani kufuatia mapinduzi katika miaka ya hivi karibuni.

    Nchi hizo tatu zilijiondoa katika Jumuiya ya kikanda ya Ecowas na tangu wakati huo zimeimarisha ushirikiano chini ya muungano huo.

    Ubia huo unalenga kuimarisha uratibu wa usalama, kuunganisha rasilimali na kukuza utangamano wa kiuchumi, ikijumuisha mipango ya miundomsingi ya pamoja, usafiri huria wa watu, na, kwa muda mrefu, soko la pamoja na sarafu.

    Soam pia:

  19. Trump na maafisa wake 'huenda' ndio walengwa wa shambulio la risasi Washington - Mamlaka

    Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump na maafisa wake ndio "huenda" walengwa wa mtu anayeshukiwa kuwa na bunduki ambaye alijaribu kuvamia dhifa ya Waandishi wa White House, kaimu Mwanasheria Mkuu wa Marekani Todd Blanche amesema.

    Mshukiwa huyo, aliyetambuliwa na vyombo vya habari vya Marekani kama Cole Tomas Allen mwenye umri wa miaka 31, alikamatwa baada ya polisi kusema alifyatua risasi karibu na kituo cha ukaguzi wakati wa tukio katika hoteli ya Washington DC siku ya Jumamosi.

    Blanche, akizungumza na NBC News, alisema nia ya mtu anayedaiwa kuwa na bunduki bado inachunguzwa, lakini matokeo ya "awali" yanaonyesha kuwa alikuwa akiwalenga maafisa wa utawala.

    Kikosi kazi cha FBI cha kitengo cha uhalifu na ugaidi kinachunguza tukio hilo.

    Baada ya kuondolewa jukwaani na kupelekwa mahali salama, Trump baadaye aliwaambia waandishi wa habari katika kikao fupi siku ya Jumamosi: "Nadhani hakuna taaluma ambayo ni hatari zaidi".

    Katika taarifa ya Jumapili, Ikulu ya White House ilisema Trump "yuko imara" baada ya kunusurika, pamoja na wajumbe wa baraza la mawaziri, "jaribio la mauaji wakati risasi zilifyatuliwa".

    Rais wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Ikulu ya White House, Weijia Jiang, alitaja shambulio hilo kuwa "la kutisha".

    Maelezo zaidi:

  20. Natumai hujambo. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja leo Jumatatu 27.04.2026

Trending Now