Je, vita vya Iran vitaweza kuiokoa bajeti ya Urusi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Dmitry Peskov, msemaji wa rais wa Urusi, amesema kuwa kupanda kwa bei ya mafuta na kulegezwa kwa muda kwa vikwazo vya Marekani kutawawezesha wauzaji wa nishati wa Urusi kupata mapato zaidi, jambo ambalo litaongeza mapato ya bajeti ya nchi hiyo.
Urusi imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kifedha katika miezi ya hivi karibuni. Je, vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran vinaweza kutatua matatizo haya? Jibu la swali hili linategemea kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa vita katika Mashariki ya Kati na muda ambao bei ya juu ya mafuta itaendelea kushuhudiwa.
Katika wiki ya kwanza ya vita, soko la mafuta lilionekana kuwa tulivu kwa kiasi Fulani, bei zilikuwa zinapanda polepole, lakini hakukuwa na hofu wala ongezeko la ghafla la bei. Wachambuzi wengi walitarajia vita vitaisha haraka.
Lakini kadri mzozo huo unavyoendelea, wasiwasi unaongezeka kuhusu uwezekano wa vita vya muda mrefu, na kufungwa kwa Mlango wa bahari wa Hormuz moja ya njia muhimu zaidi za biashara ya mafuta duniani unaongeza wasiwasi huo.
Bei ya mafuta ya Urusi aina ya Urals pia imeongezeka, kulingana na shirika la uchambuzi la Argus ambalo lililiambia BBC kuwa bei ya mafuta haya imeongezeka kwa zaidi ya 70% tangu vita hivyo kuanza.
Bei ya usafirishaji wa mafuta ya Urusi kwenda India imeongezeka zaidi. Bei ya mafuta ghafi ya Urusi aina ya Urals yanayowasilishwa katika bandari za India imefikia zaidi ya dola 98 kwa pipa.
Mafuta ya Iran yanachangia takribani 3.5% ya usambazaji wa mafuta duniani, na changamoto katika mauzo yake ya nje haiwezi kuwa na athari kubwa katika soko la kimataifa la mafuta.
Kwa sasa, jambo muhimu zaidi linaloathiri hali ya soko ya mafuta ni kusitishwa kwa usafiri wa meli katika Mlango wa bahari wa Hormuz. Kufikia mwaka 2025, takribani robo ya biashara ya mafuta inayosafirishwa kwa njia ya bahari duniani hupitia mlango huo, na uwezekano wa kusafirisha mafuta kupitia njia mbadala ni mdogo sana.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mara tu baada ya kuzuka kwa vita tarehe 28 Februari, usafirishaji wa meli kupitia Mlango wa Hormuz ulisimama kabisa. Kampuni za bima zilipandisha viwango vya bima au zilikataa kabisa kutoa bima kwa meli zinazopita katika njia hiyo. Ada za bima dhidi ya hatari za vita pia ziliongezeka kwa kiasi kikubwa.
Wachambuzi wanasema kuwa ni idadi ndogo tu ya meli za kubeba mafuta ambazo bado zinapita katika mlango huo, na baadhi ziko chini ya vikwazo.
Kulingana na kampuni ya uchambuzi ya Clapper, ambayo pia hufuatilia soko la biashara ya mafuta ya kimataifa, kufungwa kwa Mlango wa bahari wa Hormuz imeleta changamoto kubwa katika usambazaji wa mafuta ghafi katika historia ya kisasa.
Kwa miaka mingi, Iran imekuwa ikiweka shinikizo kwa wapinzani wake kwa vitisho vya kufunga Mlango wa bahari wa Hormuz, lakini haijawahi kutekeleza tishio hilo, na hadi sasa mlango huo haujafungwa rasmi.
Kampuni ya utafiti ya Clapper inaona uwezekano wa kufungwa rasmi kwa Mlango wa Hormuz kuwa mdogo sana. Ikiwa hilo litatokea, huenda Marekani ikachukua hatua za kijeshi kuishinikiza Iran kufungua mlango huo wa bahari.
Aidha, kufungwa rasmi kwa mlango huo kunaweza pia kuleta mvutano kati ya China na Iran, kwani 38% ya mafuta yanayoingizwa China kwa njia ya bahari hupitia Ghuba ya Uajemi.
Nchi za Asia ndizo zinazotegemea zaidi usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa bahari wa Hormuz. Kufikia mwaka 2025, takribani 80% ya mafuta na bidhaa za petroli zinazopita katika mlango huo huelekezwa eneo hilo.
Tishio la pili kwa soko la mafuta linaweza kuwa mashambulizi yanayolenga miundombinu ya usafirishaji wa mafuta ya Iran, ikiwemo Kisiwa cha Kharg, ambako kuna kituo kikubwa zaidi cha mafuta cha Iran na mifumo ya kupakia mafuta baharini.
Kulingana na Vertexa, mashambulizi kama hayo yanaweza kuharibu kwa haraka usambazaji wa mafuta katika masoko ya kimataifa.
Nini kinaweza kutokea baadaye katika soko la mafuta?
Hali ya soko la mafuta inategemea kwa kiasi kikubwa muda ambao Mlango wa bahari wa Hormuz utaendelea kufungwa. Wataalamu wametoa utabiri tofauti, na mengi ya makadirio hayo yanategemea mwelekeo wa vita Mashariki ya Kati.
Katika makadirio yao yanayoonekana kuwa na uwezekano mkubwa zaidi, wachambuzi wa Clapper wanatabiri kuwa vita havitasambaa hadi nchi jirani za Iran na vita hivyo vitaendelea hadi mwisho wa Machi au katikati ya mwezi Aprili. Wanakadiria kuwa wastani wa bei ya mafuta ya Brent mwaka huu utakuwa takribani dola 66.8 kwa pipa.
Ongezeko la bei katika wiki ya kwanza ya vita lilikuwa sambamba na matarajio ya wachambuzi. Ongezeko hilo lilikuwa la kiwango cha chini.
Mwezi huu wa Machi, soko la mafuta linaweza kushuhudia mabadiliko ya kupanda kwa ghafla kwa bei ya mafuta, kulingana na wachambuzi wa Clapper. Hali itakuwa mbaya zaidi, ikiwa usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz utaendelea kuzuiliwa kwa zaidi ya wiki nne, bei ya mafuta inaweza kupanda hadi dola 150 kwa pipa.
Wachambuzi wa kampuni hiyo pia wanaeleza kuwa uchaguzi wa katikati ya muhula utakaofanyika nchini Marekani mwezi Novemba mwaka huu, Rais wa Marekani, Donald Trump, anataka kuzuia kupanda kwa bei ya mafuta nchini humo, na hili huenda likachangia kupunguka kwa mapigano na mvutano uliopo.
Shirika la Bloomberg linatabiri kuwa ikiwa Mlango wa bahari wa Hormuz utaendelea kufungwa kwa muda mrefu, bei ya mafuta inaweza kupanda na kufikia dolla 108.
Iwapo mapigano yatapungua,bei ya mafuta itakuwa ikibadilika ndani ya kiwango cha karibu dola 80 kwa pipa, na ikiwa Marekani na Iran watafikia makubaliano ya kusitisha vita, bei inaweza kushuka hadi takribani dola 65.

Chanzo cha picha, Reuters
Kulingana na Vertexa, iwapo kutatokea changamoto kubwa katika usambazaji wa mafuta, shehena za mafuta kutoka Marekani, Amerika Kusini na Afrika Magharibi zinaweza kusaidia kufidia upungufu utakaoshuhudiwa.
Kwa sasa, India inaonekana kukabiliwa na changamoto zaidi kuliko nchi nyingine, akiba yake ya mafuta inaweza kudumu kwa takribani siku 20 tu.

Hali hii itaathiri vipi bajeti ya Urusi?
Serikali ya Urusi inatabiri kushuhudia upungufu wa bajeti yake kwa zaidi ya trilioni 3.7 za ruble (dolla million 46) mwaka huu wa 2026. Serikali hiyo imeongeza kodi inayotozwa ili kujaribu kuongeza mapato yake.
Januari 2026, Urusi ilikosa kufikia 31.7% ya mapato yake yaliyotarajiwa kutoka mafuta na gesi, na mwezi Februari, kiwango hicho kilishuka hadi 2.2%.
Hii inahusiana na vikwazo ambavyo taifa hilo limewekewa. Marekani imewawekea vikwazo wauzaji wakuu wa mafuta wa Urusi, Rosneft na Lukoil, hatua ambayo ilisababisha punguzo kubwa la bei ya mafuta ya Urusi. Mapema mwaka huu, Rais wa Marekani, Donald Trump, alitangaza kwamba India, mmoja wa washirika wakubwa wa kibiashara wa Urusi, imeacha kununua mafuta ya Urusi.
Kulingana na wachambuzi wa Clapper, nafasi ya Urusi katika masoko ya mafuta ghafi imeimarishwa sana kufuatia vita na Iran. Vertexa inakubaliana na tathmini hii.
Kwa mfano, mnamo Machi tarehe 6, wizara ya fedha ya Marekani iliruhusu makampuni ya India kununua mafuta ya Urusi yaliyopakiwa kwenye meli kwa matumizi yao wenyewe.
"Hatua hii, ambayo ni ya muda mfupi, haitatoa faida kubwa ya kifedha kwa maafisa wa Urusi kwa sababu inaruhusu tu ununuzi na uuzaji wa mafuta ambayo tayari yamepakiwa kwenye meli na kwa sasa yako baharini," alisema waziri wa fedha wa Marekani Scott Bessent.
Meli mbili ya mafuta ya Urusi zilikaribia bandari za India hata kabla ya kauli za Bessent kukawia.
Urusi iko tayari kunufaika na hali ya sasa.
Vladimir Putin hivi karibuni alifanya mkutano kuhusu hali ya soko la mafuta na gesi duniani. Alitangaza kwamba Urusi iko tayari kuongeza mauzo kwa "washirika wa kuaminika" akilenga mataifa ya bara Asia, na pia baadhi ya nchi za Ulaya Mashariki kama Hungary na Slovakia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya vita na Iran, mafuta ya Urals yanaendelea kuuzwa kwa bei ya chini kuliko Brent kutokana na vikwazo vilivyowekewa Urusi.
Kulingana na mwanauchumi Yevgeny Nadurshin, bei ya sasa ya mafuta ya Urals bado haijatosha kufidia pengo lililoko katika bajeti ya Urusi.
Anaamini kwamba kipindi hiki kifupi cha kupanda kwa bei ya mafuta hakutabadilisha sana hali ya kifedha ya Urusi.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula










