Iran yatishia kufunga kabisa Mlango wa Hormuz baada ya onyo la Marekani

Onyo hilo linakuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuipa Iran muda wa saa 48 kufungua mlango huo muhimu wa usafirishaji wa mafuta, akionya kuwa Marekani “itaiangamiza” iwapo haitatii.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Iran yatishia kufunga kabisa Mlango wa Hormuz baada ya onyo la Marekani

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Iran imesema itaufunga kabisa Mlango wa Bahari wa Hormuz iwapo Marekani itatekeleza tishio lake la kushambulia miundombinu ya nishati ya nchi hiyo.

    Katika taarifa iliyotangazwa na vyombo vya habari vya Iran, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimesema kitafanya hivyo endapo mashambulizi hayo yatafanyika.

    Onyo hilo linakuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuipa Iran muda wa saa 48 kufungua tena mlango huo muhimu wa usafirishaji wa mafuta, akionya kuwa Marekani “itaiangamiza” Iran kwa kuanza na mitambo yake ya umeme iwapo haitatii.

    Iran kwa upande wake imeonya kuwa endapo miundombinu yake ya mafuta na nishati itashambuliwa, italipiza kisasi kwa kulenga miundombinu ya nishati inayohusishwa na Marekani katika eneo hilo.

    Idadi ya meli zinazopita eneo hilo zimepungua kwa 98% tangu kuanza kwa vita tarehe 28 mwezi Februari. Iran ikihodhi mlango huo kwa usalama.

    Kabla ya vita, takriban meli 138 zilikuwa zinapita katika mlango wa bahari wa Hormuz kila siku kulingana na taasisi ya Joint Maritime Information Centre.. Hali hii inakuja pia kufuatia mashambulizi ya Iran kusini mwa Israel, ambapo zaidi ya watu 160 walijeruhiwa katika miji ya Dimona na Arad.

  2. "Vita vya Mashariki ya Kati ni fedheha kwa ubinadamu"- Papa Leo

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Pope Leo, amesema leo Jumapili kuwa vifo na mateso yanayosababishwa na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati ni “fedheha dhidi ya binadamu”, huku akitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano.

    Akiwa anaongoza sala ya Angelus katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican, Papa Leo alisema anaendelea kufuatilia kwa masikitiko makubwa hali ya vita inayoendelea Mashariki ya Kati na maeneo mengine yaliyoathiriwa na migogoro na vurugu.

    Alisisitiza kuwa dunia haiwezi kunyamaza mbele ya mateso ya watu wengi wasiokuwa na hatia, akisema: “Hatuwezi kukaa kimya tunapoona mateso ya watu wengi, waathirika wasio na ulinzi wa migogoro hii. Kinachowaumiza wao kinaumiza ubinadamu wote.”

    Papa Leo alitoa wito wa kuendelea na sala na juhudi za amani, akisisitiza umuhimu wa kusitisha mapigano ili kufungua njia ya kufikiwa kwa amani ya kudumu katika eneo hilo.

  3. Iran haiwezi kuishambulia Uingereza kwa makombora ya masafa marefu – Waziri

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Hakuna tathmini yoyote inayothibitisha madai ya Israel kwamba Iran ina makombora ya masafa marefu yanayoweza kufika London, amesema Waziri anayeshughulikia makazi nchini Uingereza.

    Steve Reed, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hakuna ushahidi kwamba Iran itaweza kuishambulia Uingereza au kwamba ingeweza kufanya hivyo kama ingependa. Kauli yake inajibu madai ya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) kwamba Tehran ina silaha zenye uwezo wa kufikia umbali wa kilomita 4,000 (maili 2,485).

    Hii inajiri baada ya Iran kushambulia kituo cha kijeshi cha pamoja cha Marekani na Uingereza katika Visiwa vya Chagos Islands, kilichoko takriban km 3,800 kutoka Iran.

    Iran ilirusha makombora mawili kuelekea Diego Garcia – moja liligonga mwamba na lingine likashambuliwa na mifumo ya ulinzi ya Marekani na Uingereza. Reed hakutaja umbali halisi wa makombora kwa sababu ni taarifa za kioperesheni.

    Reed pia alisisitiza kuwa, hata kama Iran ingeweza kurusha makombora kwa umbali huo, vikosi vya Uingereza vina uwezo wa kulinda nchi na raia wake. Kwa sasa, makombora ya masafa marefu zaidi yanayojulikana katika Arsenal ya Iran yanaweza kusafiri umbali wa takriban km 2,000, ambao ni chini ya umbali unaohitajika kufikia Diego Garcia au London.

  4. Watu 64 wauawa kwenye shambulizi la hospitalini Sudan – WHO

    s

    Chanzo cha picha, DrTedros via Sky

    Shambulio kwenye hospitali ya Al Deain Teaching Hospital huko Al Deain, Mashariki mwa Sudan limeua angalau watu 64, kwa mujibu wa Reuters

    Miongoni mwa waliouawa ni watoto, wafanyakazi wa hospitali na wagonjwa, imesema Shirika la Afya Duniani (WHO) Jumamosi.

    Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, kupitia chapisho kwenye mtandao wa X.

    Shambulio hilo lililotokea Ijumaa na kuisambaratisha kabisa hiyo na kusitisha huduma muhimu za afya kwa wakazi wa mji huo.

    WHO imesema hali hiyo inasababisha changamoto kubwa kwa wagonjwa waliokuwa wakihitaji matibabu ya dharura.

  5. Picha za uharibifu katika miji miwili kusini mwa Israel kufuatia mashambulizi ya Iran

    g

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Kombora la Iran lilipiga na kuchaka makazi ya watu huko Dimona, Israel

    Huduma za dharura nchini Israel zimeripoti kuwa watu wasiopungua 88 walijeruhiwa kufuatia shambulizi la Iran katika mji wa kusini wa Arad.

    Wakati huo huo, Redio ya Jeshi la Israel, ikinukuu Hospitali ya Soroka, iliripoti Jumapili asubuhi kuwa watu 150 walijeruhiwa katika miji ya Arad na Dimona, baada ya makombora ya Iran kupiga maeneo hayo Jumamosi.

    Mashambulizi hayo yameelezwa kuwa miongoni mwa makali zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu kuanza kwa vita.

    b

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Jiji la Dimona limekumbwa na mashambulizi makubwa
    d

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Maafisa wa Ulinzi walionekana kubaki mwenye mabaki ya majengo
    s

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Timu ya waokoaji ikiendelea na shughuli za uokoaji katika eneo la Arad.
  6. Zaidi ya watu 4,500 wajeruhiwa tangu kuanza kwa vita na Iran - Israel

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya Afya ya Israel imesema idadi ya watu waliojeruhiwa na kupelekwa hospitalini tangu kuanza kwa vita na Iran hadi Jumapili asubuhi imefikia 4,564.

    Wizara hiyo imeeleza kuwa kati ya majeruhi hao, watu 124 bado wamelazwa hospitalini, akiwemo mmoja aliye katika hali mahututi, 13 wenye majeraha mabaya na 26 walio katika hali ya kati.

    Katika saa 24 zilizopita pekee, watu 303 walipelekwa hospitalini, wakiwemo 8 walio katika hali mbaya na 29 katika hali ya kati, kufuatia mashambulizi mawili ya makombora ya Iran katika miji ya kusini ya Arad na Dimona.

  7. Mlango wa Hormuz - kwa nini ni muhimu?

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Iran imezuia kwa kiasi kikubwa kutumika kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambao ni moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani, tangu Marekani na Israel zilipoishambulia nchi hiyo Februari 28.

    Mlango huu wa bahari unapakana na Iran upande wa kaskazini, na nchi za Oman pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) upande wa kusini. Unaunganisha Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Arabia, ukiwa na upana wa takriban kilomita 50 kwenye sehemu zake za kuingia na kutoka, na karibu kilomita 33 katika sehemu yake nyembamba zaidi.

    Takriban asilimia 20 ya mafuta duniani pamoja na gesi asilia iliyoyeyushwa hupitia katika mlango huu, ikiwa ni pamoja na mafuta yanayosafirishwa kutoka Iran na nchi nyingine za Ghuba ya Uajemi kama Iraq, Kuwait, Qatar, Saudi Arabia na UAE.

    Madhara ya kufungwa kwa mlango huu

    Kwa kawaida, karibu meli 3,000 hupita katika Mlango wa Hormuz kila mwezi, lakini idadi hiyo imepungua kwa kasi katika siku za hivi karibuni kufuatia vitisho vya Iran kushambulia meli za mafuta na vyombo vingine vya majini.

    Kwa mujibu wa takwimu za AFP hadi Machi 18, angalau meli 21 zimeripotiwa kushambuliwa tangu kuanza kwa vita.

    Kutokana na hali hiyo, bei za mafuta duniani zimepanda kwa kasi, huku bei ya mafuta ghafi ikivuka dola 100 kwa pipa – ongezeko la karibu asilimia 70 tangu mwanzo wa mwaka, na takriban asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

  8. Tunakabiliana na tishio la makombora kutoka Iran - UAE

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jumapili, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ilitangaza kuwa inakabiliana na mashambulio kutoka Iran.

    Wizara ya Ulinzi ya UAE ilisema kwenye taarifa:"Sasa hivi mifumo yetu ya ulinzi wa anga inakabiliana na tishio la makombora na ndege zisizo na rubani 'drones' zinazoletwa na Iran."

    Kwa mujibu wa wizara hiyo, "sauti zilizosikika zilitokana na mifumo ya ulinzi wa anga ikipunguza kasi ya makombora na drones hizo."

    Msemaji wa Wizara ya Ulinzi pia alitangaza kuwa 'drones' tatu zilikamatwa na kuharibiwa katika mkoa wa mashariki wa nchi hiyo.

  9. Trump afurahia kifo cha Robert Mueller, aliyekuwa mkuu wa FBI

    S

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Robert Mueller, mshauri maalum aliyeongoza uchunguzi kuhusu kuingilia kati kwa Urusi katika uchaguzi wa Marekani wa 2016, na ambaye uchunguzi wake ulitikisa sehemu kubwa ya awamu ya kwanza ya utawala wa Donald Trump madarakani, amefariki akiwa na miaka 81.

    Sababu ya kifo chake haijajulikana mara moja. CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, imethibitisha kifo chake.

    “Kwa huzuni kubwa, tunatoa taarifa kwamba Bob amefariki,” familia yake ilisema katika taarifa kwenda AP Jumatano usiku. “Familia yake inawaomba waheshimu faragha yao.”

    Mueller hapo awali aliongoza FBI kuanzia 2001 hadi 2013, akiwa ameteuliwa siku chache kabla ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001. Ana sifa ya kuibadilisha FBI kuwa shirika la kisasa la kukabiliana na ugaidi.

    Uchunguzi wake uligusa kampeni ya Trump mwaka 2016 na kusababisha ukosoaji mkali kutoka kwa rais huyo.

    Rais Donald Trump aliandika Jumamosi kwenye mtandao wake: “Ninafurahi amefariki. Huwezi tena kuumiza watu wasio na hatia!”

    Waajiri wake wa zamani na wafanyakazi wenzake walimpongeza kama mtumishi wa umma wa muda mrefu.

    Marais wote wawili aliowahudumia akiwa mkurugenzi wa FBI - George W. Bush na Barack Obama - walitoa heshima kwa kifo chake.

  10. Uharibifu mkubwa umetokea Israel kufuatia mashambulizi ya Iran

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Waokoaji wakiwa eneo la tukio muda mfupi baada ya kombora la Iran kutua Arad Israel

    Jumamosi, kombora la Iran lilitua Arad, mji mdogo kusini mwa Israel, baada ya mifumo ya ulinzi wa anga kushindwa kulizuia.

    Huduma za dharura nchini Israel zimesema watu 88 walipelekwa hospitali baada ya shambulizi hilo, huku 10 kati yao wakiwa wamejeruhiwa vibaya.

    Watu wengine wengi pia walijeruhiwa katika mji wa kusini wa Dimona, umbali wa kilomita 13 tu kutoka kituo cha nyuklia.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameueleza tukio hilo kama “jioni ngumu sana” kwa taifa hilo.

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

  11. Marekani yaipa saa 48 Iran kufungua mlango wa Hormuz, la sivyo itaiangamiza

    S

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump ameipa Iran muda mpya wa saa 48 kufungua tena mlango wa Bahari wa Hormuz, akisema isipofanya hivyo Marekani “itaiangamiza” Iran kwa kuanza na mitambo yake ya umeme.

    Iran kwa upande wake imesema endapo miundombinu yake ya mafuta na nishati itashambuliwa, italipiza kisasi kwa kushambulia miundombinu ya nishati inayohusishwa na Marekani katika eneo hilo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

    Katika saa chache zilizopita, pia kumekuwa na taarifa za ajali ya helikopta ya kijeshi nchini Qatar, pamoja na “tukio” la kombora kwenye chombo kimoja cha majini karibu na pwani ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

    Hayo yamefuatia mashambulizi ya Iran kusini mwa Israel, ambapo zaidi ya watu 120 wameripotiwa kujeruhiwa katika miji ya Dimona na Arad.

  12. Habari na karibu kwenye taarifa zetu za moja kwa moja leo Jumapili ya Machi 22

Trending Now