Meli zipi zinaruhusiwa kupita Mlango Bahari wa Hormuz licha ya hofu ya mashambulizi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Karibu meli 100 zimepita katika mlango wa bahari wa Hormuz mwezi Machi, kulingana na data iliyochambuliwa na BBC Verify, licha ya mashambulizi ya mara kwa mara inayotekelezwa na Iran eneo hilo.
Ingawa kuna meli za kusafirisha mafuta na bidhaa za kila siku ambazo zinapitia eneo hilo, idadi ya meli zinazopita eneo hilo zimepungua kwa 98% tangu kuanza kwa vita tarehe 28 mwezi Februari.
Kabla ya vita, takriban meli 138 zilikuwa zinapita katika mlango wa bahari wa Hormuz kila siku kulingana na taasisi ya Joint Maritime Information Centre.
Data iliyotolewa na wachambuzi wa usafiri wa maji Kpler inaonyesha kuwa meli 99 zimepitia mlango wa bahari wa Hormuz mwezi huu, kwa wastan ikiwa meli tano au sita kwa siku.
BBC Verify inachunguza meli zinazopitia eneo hilo na hatari wanazokabiliana nazo.
Uchambuzi wetu unaonyesha kuwa takriban theluthi moja ya meli zilizopita eneo hilo hivi karibuni zilikuwa na uhusiano na Iran.
Hii ni pamoja na meli 14 zinazoendesha safari zake zikiwa na bendera ya Iran licha ya Iran kuwekewa vikwazo vya mafuta.
Meli nyingine tisa zinazohusiana na China zilipita eneo hilo, huku sita zikielekea India.
Uchambuzi wetu pia unaonyesha kuwa meli kadhaa zisizo na uhusiano na Iran zimepakia kwenye bandari ya nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na meli zinazomilikiwa na kampuni ya Ugiriki.
Baadhi ya meli zinazoonekana kufanikiwa kupita mlango huo wa Hormuz zinafuata njia ndefu kuliko ya kawaida.
Bradley Martin, mtafiti katika taasisi ya RAND Corporation, alituambia kuwa meli zinazotumia njia ndefu huenda zinafuata maagizo kutoka Iran.
Anasema njia hiyo wanayoichukua inaweza kuonyesha uwepo wa mabomu ya baharini, au ni jitihada za maafisa wa Iran kufanya meli iwe rahisi kutambuliwa.
Michael Connell kutoka Center for Naval Analyses inayofadhiliwa na Marekani anakubaliana na utafiti kuwa meli zinachukua njia tofauti.
"Huenda wana mkataba fulani na mamlaka za Iran kwamba ikiwa watatumia njia wanayoambiwa watakuwa salama."
Vitisho vinne katika usafiri wa baharini
Tangu mgogoro ulipoanza, BBC Verify imethibitisha kuwa meli 20 za kibiashara zimeshambuliwa karibu na pwani ya Iran.
Tarehe 11 mwezi Machi, meli ya mizigo yenye bendera ya Thailand, Mayuree Naree, ilishambuliwa ikijaribu kupita katika mlango huo wa bahari.

Chanzo cha picha, EPA
Watu watatu kati ya wafanyakazi 23 bado hawajulikani waliko, wakiaminika kuwa walikwama katika chumba cha injini meli iliposhambuliwa.
Wamiliki wa meli hiyo waliiambia BBC Verify kuwa wahudumu wa meli hiyo "wameathirika kisaikolojia baada ya kushambuliwa"
Meli nyingine mbili ya Star Gwyneth inayomilikiwa na Wagiriki na MT Safesea Vishnu inayomilikiwa na Marekani pia zilishambuliwa siku hiyo.
"Njia za usafirishaji wa bidhaa za kibiashara haziwezi kuwa maeneo ya mapigano," mmiliki wa MT Safesea Vishnu aliambia BBC Verify.
Mtu mmoja alifariki katika shambulio hilo wakati meli hiyo ilipotia nanga kando ya pwani ya Iraq. Wafanyakazi wote 28 walilazimika kuruka majini ili kuepuka kuchomeka meli hiyo ilipowaka moto, alisema Bwana S V Anchan.












