Jinsi Marekani inavyoweza kujaribu kuteka kisiwa cha Kharg cha Iran

Muonekano wa kituo cha mafuta cha Kisiwa cha Kharg, ukionyesha safu ya mabomba yanayonyooshwa kwa umbali kuelekea eneo lililoinuliwa la ardhi ambapo silo kadhaa hukaa, moja wapo ina maneno "Ghuba ya Uajemi" upande wake.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Takriban 90% ya mauzo ya mafuta ya Iran yanapitia Kisiwa cha Kharg
    • Author, Frank Gardner
    • Nafasi, Security correspondent
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameashiria uwezekano wa kutuma wanajeshi ili kudhibiti kituo muhimu cha usafirishaji wa mafuta cha Iran kilichopo katika Kisiwa cha Kharg, kaskazini mwa Ghuba. Hivyo basi, ni nini kilicho nyuma ya hatua hii, ingeendeshwaje, na hatari zake ni zipi?

Kisiwa cha Kharg kwa muda mrefu kimekuwa njia kuu ya Iran kusafirisha mafuta yake nje ya nchi. Kisiwa hiki kiko baharini, na kina maji yenye kina cha kutosha kuruhusu upakiaji wa mafuta kwenye meli kubwa sana za kubeba mafuta (VLCC), ambazo zinaweza kubeba takriban mapipa milioni mbili. Takribani asilimia 90 ya mauzo ya mafuta ya Iran hupitia Kharg.

Wakati wa Vita vya Iran na Iraq, kisiwa hiki kilishambuliwa mara kwa mara na Jeshi la Anga la Iraq, na tarehe 13 Machi mwaka huu Marekani ilishambulia maeneo 90 ya kijeshi kwenye kisiwa hicho, ingawa haikugusa miundombinu ya mafuta.

Iwapo Marekani itaamua kuvamia Kisiwa cha Kharg, hatua hiyo huenda ikawa ya muda mfupi, ikilenga kuiwekea Iran shinikizo kwa kukatiza usafirishaji wake wa mafuta hadi itakapoachana na udhibiti wake juu ya Mlango wa Hormuz, moja ya njia zenye shughuli nyingi zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani na kukubali matakwa ya Washington.

Kwa kuzingatia uthabiti na msimamo mkali wa utawala wa Iran, kuna mashaka makubwa kama mkakati huu utafanikiwa.

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ameonya kwamba majeshi ya nchi yake "yatamiminia moto" dhidi ya vikosi vyovyote vya Marekani vitakavyovamia. Inaaminika Iran imeimarisha ulinzi wake kisiwani humo, ikiwa ni pamoja na mifumo ya makombora ya ardhini kwenda angani.

Picha ya setilaiti ya Kisiwa cha Kharg na ramani inayoonyesha eneo lake katika Ghuba
Maelezo ya picha, Picha ya setilaiti ya Kisiwa cha Kharg na ramani inayoonyesha eneo lake katika Ghuba

Iran pia imeishutumu Marekani kwa unafiki, kwa kupendekeza mazungumzo ya amani huku wakati huohuo ikituma wanajeshi katika eneo hilo.

Vikosi hivyo vinajumuisha karibu wanamaji wa Marekani 5,000 na takriban wanajeshi 2,000 wa anga kutoka 82nd Airborne Division.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hali hii imechochea uvumi kwamba vikosi hivyo vinaweza kutumika kutwaa na kushikilia Kharg.

Kimsingi, wanajeshi wa anga wanaweza kufanya shambulio la ghafla kutoka hewani, huenda usiku, ili kudhibiti maeneo muhimu ya kisiwa hicho kidogo chenye ukubwa wa takriban kilomita za mraba 20.

Kwa upande mwingine, wanamaji wa Marekani wanaweza kuwasili kutoka melini kwa kutumia ndege za Osprey na vyombo vya kutua baharini. Hata hivyo, kwanza meli hizo zingelazimika kupita katika Mlango wa Hormuz unaodhibitiwa na Iran, kisha kusafiri ndani ya Ghuba huku zikikabiliwa na hatari ya mashambulizi kutoka vituo vya siri vya makombora na droni vya Iran.

Shambulio lolote, iwe kwa njia ya anga au bahari, linatarajiwa kukutana na mabomu ya ardhini dhidi ya watu pamoja na makundi ya droni. Ingawa nguvu ya kijeshi ya vikosi vya Marekani ni kubwa na huenda vikashinda, ushindi huo unaweza kuja kwa gharama ya majeruhi wengi.

Baada ya hapo, Marekani itakabiliwa na changamoto ya kudhibiti eneo hilo kwa muda usiojulikana huku ikishambuliwa kutoka bara la Iran.

Mfano unaofanana ni Kisiwa cha Nyoka katika Bahari Nyeusi, ambacho Urusi ilikiteka mapema baada ya uvamizi wake mkubwa mwaka 2022, lakini baadaye ikalazimika kukiacha kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka Ukraine.

Aidha, uvamizi wa muda mrefu wa Marekani katika ardhi ya Iran unaweza kukosa uungwaji mkono ndani ya Marekani yenyewe, hata miongoni mwa baadhi ya wafuasi wa Trump waliomchagua kwa ahadi ya kuepuka migogoro ya aina hii. Pia, inawezekana kelele nyingi kuhusu uvamizi wa Kharg ni sehemu ya mkakati wa upotoshaji.

Hakuna shaka kuhusu thamani ya kimkakati ya kisiwa hiki kwa Iran na jeshi lake la Islamic Revolutionary Guard Corps. Hata hivyo, kuna visiwa vingine katika Ghuba ambavyo vinaweza pia kulengwa na Marekani.

Miongoni mwa hivyo ni Kisiwa cha Larak karibu na bandari muhimu ya Bandar Abbas, kilichopo moja kwa moja kwenye Mlango wa Hormuz. Iran inadaiwa kuwalazimisha meli kupita karibu na kisiwa hiki kwa ukaguzi, na kuripotiwa kutoza ada ya dola milioni mbili kuvuka.

Pia kuna Kisiwa cha Qeshm, ambacho ni kikubwa zaidi katika Ghuba kikiwa mara 75 ya ukubwa wa Kharg ambapo Iran inashukiwa kuwa na vituo vya siri vya makombora na droni chini ya ardhi.

Vilevile, kuna visiwa vitatu Abu Musa pamoja na Tunb Kubwa na Tunb Ndogo, ambavyo vinagombaniwa umiliki kati ya Iran na Falme za Kiarabu (UAE), lakini vyote vinadhibitiwa na Iran.

Kwa pamoja, visiwa hivi vinaunda ngome ya kinga kwa Iran, inayoweza kutishia usafirishaji wa baharini na kuipa faida ya kijiografia inayosaidia kupunguza pengo la nguvu za kijeshi kati yake na Marekani.

Hata hivyo, kuna uwezekano pia kwamba hakuna kati ya haya yatakayotokea.

Wakati huohuo wa kupeleka wanajeshi zaidi katika eneo na kuashiria uwezekano wa operesheni ya ardhini, Trump alisema tena Jumatatu kwamba Marekani iko katika "mazungumzo makini" na Iran ambayo yanaweza "kumaliza operesheni za kijeshi".

Kadiri vita vinavyoingia wiki ya tano, kauli za umma za Trump hazitoi dalili wazi kuhusu hatua yake inayofuata. Hata hivyo, kufikiwa kwa makubaliano ambayo wengi wanaamini Trump anayahitaji zaidi kuliko Iran kutahitaji kuziba pengo kubwa lililopo kati ya misimamo ya pande hizo mbili.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid