Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, sura ya kifahari ya Dubai imetikiswa na vita?
Stephanie Baker alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa na marafiki zake eneo la Palm Jumeirah, kisiwa bandia mjini Dubai ambako ni nyumbani kwa majumba ya kifahari na maeneo ya burudani yaliyoko karibu na ufuo wa bahari.
Ila wakati yeye na marafiki zake walikuwa wanaondoka eneo hilo, waliona kitu kisichokuwa cha kawaida angani.
Muda mchache baadaye vifusi vikaanguka karibu na hoteli ya kifahari ya Fairmont Hotel, wakati Baker walikuwa wamesimama barabarani wakitazama.
"Sote tulikuwa tumeogopa, hatukutarajia kuona kitu kama hicho" alisema Baker.
Mwanamke huyo kutoka Uingereza ambaye huuza nyumba za kifahari, alihamia mjini Dubai mwaka mmoja uliopita, na anasema yeye huiona mji huo kama eneo salama.
Ila wiki mbili baada ya makombora na ndege zisizo na rubani kulenga mji huo kutoka Iran, Baker anasema hana nia ya kuhama mji huo.
"Jinsi hali imedhibitiwa eneo hili, inafanya nihisi salama" alisema.
Dubai ina mamilioni ya watu ambao wanatoka mataifa ya kigeni, ikiwemo raia wa Uingereza 240,000 huku raia wa Falame za Kiarabu wakiwa tu 10% ya wakaazi wa mji huo.
Kwa miaka mingi mji huo umejitengenezea sifa ya kuwa eneo salama na tulivu Mashariki ya Kati. Anga zake zimejaa maghorofa marefu, huku wengi wanaofanya kazi huko wakifurahia kupata mshahara ambao hautozwi ushuru.
Usalama wa mji huo umefanya wengi kuwekeza biashara zao huko huku ikiwa kitovu cha utalii kwa watu wengi wanaotaka kuzuru Mashariki ya Kati.
Kulingana na mamlaka za Falme za Kiarabu, tangu vita vya Iran kuanza, makombora ya kibalistiki 285, makombora ya meli 15 na ndege zisizo na rubani 1,567 zimerushwa eneo hilo, huku wakiweza kudungua 90% ya silaha hizo.
Baadhi ya vifusi vya makombora yaliyodunguliwa yalikuwa yakianguka kwenye makazi ya watu, karibu na uwanja wa ndege n ahata hoteli za kifahari kulingana na video zilizosambaa mitandaoni.
Kufikia sasa mamlaka za Falme za Kiarabu zinasema watu 6 wamefariki kutokana na mashambulizi hayo, huku 141 wakijeruhiwa kote duniani.
BBC ilizungumza na zaidi ya wakazi 20 ambao wameishi Dubai wengine kwa miongo kadhaa, wengi wakisema wameshtushwa na kile ambacho kimetokea katika siku za hivi karibuni, lakini hawana nia ya kuuhama mji huo.
"Hii ni mara ya kwanza naona kitu kama hiki" anasema Eti Bhasin, raia wa India ambaye anasimami biashara ya familia yake na ameishi Dubai miaka yake yote.
"Dubai imekuwa mji tajika, na tunaamini mamlaka ya eneo hili. Hili ni taifa langu na tunaliunga mkono" aliongezea
Kwa wakazi wengine wiki za hivi karibuni zimewatia wasiwasi. Adam Callow alihamia Dubai pamoja na mkewe na wanawe wawili kutoka Uingereza mwaka wa 2024, na kilichowavutia zaidi ni usalama wa mji huu.
Katika siku za kwanza za vita, wanafamilia hao walikuwa wanalala katika chumba kimoja, baada ya wanao kuogopa kulala karibu na dirisha kutokana na milio ya makombora.
"Mamlaka zinafanya kila wawezalo kuhakikisha tuko salama, ila bado tuko wasiwasi iwapo hii ndiyo itakuwa hali ya kawaida" anasema Kalu.
Uwanja wa ndege wa Dubai ndiyo uwanja ulionashughuli nyingi kote duniani, mwaka uliopita, abiria million 90 walitumia uwanja huo kusafiri.
Maelfu ya safari za ndege zimehairishwa, huku usafiri ukiathirika pakubwa.
Katika siku za hivi karibuni, usafiri wa ndege umerejelewa ila kwa kiwango kidogo sana. Uwanja huo wa ndege umeathirika wakati ambao unasemakana huu ni msimu wa watu wengi kusafiri.
Waliokuwa wanapanga kusafiri, wengi wamehairisha safari zao na hata kufutilia mbali nafasi ambazo walikuwa wamejifadhi kwenye hoteli za kifahari.
"Kwa bahati mbaya tunaona wengi wakifuta hifadhi zao za hoteli hadi mwezi Mei" Anasema Dkt Naeem Moadad, muanzilishi wa Gates Hospitality na raia wa Australia ambaye amekaa mjini Dubai kwa miongo miwili.
Anaongezea kuwa " Ukianza mwaka vibaya katika biashara, huwa unatumia mwaka mzima kujaribu kurudisha yale uliopoteza"
Sura nyingine ya Dubai
Nafasi za ajira na biashara katika mji huu huja na usawa tofauti. Ingawa Dubai ina sura ya kumetameta mitandaoni, wengi wa wafanyikazi wahamiaji ambao wanachangia ukuaji wa mji huo wanaishi katika makazi duni.
Nafasi za ajira katika Falme za Kiarabu hutegemea sana wahamiaji, huku wafanyikazi wengi wakitoka kusini mwa bara Asia, wengi wakifanya kazi ya ujenzi na kusafrisha bidhaa.
Kwa wengi, vita havijabadilisha Maisha yao pakubwa.
Hamza msafirishaji bidhaa kutoka Pakistan, anasema uagizaji wa vitu uliongezeka katika siku za kwanza za vita, kwani watu wengi walisalia majumbani.
Anaelezea kuwa "familia yangu nyumbani inanitegemea, sina fursa ya kukaa kwa nyumba kwa sababu ya uoga"
Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu zimekuwa zikipaza sauti kuhusu Maisha ya wafinyakazi katika taifa hilo la ghuba, pamoja na mshahara wa chini wanaolipwa.
Ingawa wengi wa wafanyikazi kama Hamza wanasema wataendelea kuishi eneo hilo, kuna baadhi ambao wameamua kurudi makwao wakihofia usalama wao.
Mfanyikazi mmoja anayehudumu katika kampuni ya ndege alirejea nyumbani kwao mjini Melbourne, Australia mapema wiki hii
Anatuelezea kuwa "nilianza kuhisi wasiwasi niliposikia milipuko ambayo ilikuwa inaongezeka kila siku. Kwangu niliona ilikuwa salama kuondoka hadi hali irejee kuwa ya kawaida"
Ila alituelezea kuwa, bado anataka kurejea mjini Dubai
Wakati mataifa ya magharibi yamekuwa yakiweka sheria kali ya uhamiaji, Dubai imekuwa eneo ambalo matakwa yake ya uhamiaji hayana vikwazo vingi.
Falme za kiarabu imejijengea sura ya kuwa eneo ambalo wafanyikazi pamoja na matajiri wanaweza kujijenga, na idadi ya watu wanaohamia mji huo imekuwa ikiongezeka tangu virusi vya Covid 19.
Kupata ajira yenye mapato mazuri kwa wataalam kama wahandisi, madaktari kutoka Misri, wauguzi kutoka Ufilipino, imekuwa rahisi kupata visa ya kufanya kazi mjini Dubai ikilinganishwa na Ulaya au Marekani.
Je, Dubai itaweza kustahimili changamoto za sasa?
Mji huo ambao umejijengea sifa ya kuwa eneo salama, iwapo hilo litarejelewa ni swali ambalo wengi wanajiuliza.
Christopher Davidson, mchambuzi wa uchumi wa kisiasa katika Falme za Kiarbu anasema mvutio wa Dubai utaathirika angalau kwa muda mfupi.
" Vitu vya msingi kama miundo mbinu, hali ya hewa, eneo la jiografia na kuwa mji wa kimkakati bado halijabadilika, baada ya muda mvuto wake bado utakuwepo"
Mamlaka za eneo hilo, zimepongezwa na wakazi kwa kutoa taarifa na habari kwa kile kinachotokea kupitia ujumbe kwa simu za mkononi.
Rais wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed amewahakikishia wakazi wa mji huo kuwa serikali ya taifa hilo itawalinda.
Baadhi ya wakazi wanasema Maisha ya kawaida yanaendelea, ila serikali ya UAE imeweka vikwazo katika mawasiliano haswa kusambaza video za mashambulio yanayotokea.
Mwanaume mmoja raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 60, alifunguliwa mashtaka baada ya kupiga picha kombora la Iran siku ya Alhamisi iliyopita.
Mchambuzi Davidson anafafanua kuwa, Dubai kurejelea utulivu wake na hali ya kawaida itategemea na mwelekeo wa vita vinavyoendelea Iran.