Simulizi ya mtu 'aliyekufa' kwa dakika 40

Kifo hakikumpa maisha mapya Patrick Charnley lakini kilibadilisha kabisa mtazamo wake kuhusu maisha.
Patrick ni mwanasheria wa masuala ya biashara aliyefanikiwa sana, ambaye zamani aliamini kuwa muda wa kupumzika ni kupoteza maisha. Alijituma sana kufikia mafanikio makubwa zaidi.
Mwaka 2021, wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19, akiwa na umri wa miaka 39 akiwa katika hali nzuri kiafya, lakini ghafla alipata mshtuko wa moyo. Moyo wake ulisimama kufanya kazi.
Siku hiyo alikuwa amekaa tu nyumbani kwa utulivu, akila vitafunwa vyake usiku, alianguka ghafla na kukimbizwa hospitalini.
Madaktari waligundua kuwa mshtuko huo ulisababishwa na ugonjwa wa kurithi wa moyo. Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, Patrick "alikufa" kwa dakika 40.
Mke wake alianza kumpa huduma ya kwanza (CPR) mara tu moyo wake uliposimama. Watoto wao walikimbia kuomba msaada. Wahudumu wa dharura walijaribu kumuokoa bila mafanikio mwanzoni. Hatimaye baadaye wakatumia umeme mara kadhaa na sindano ya ''adrenalin'' na kufanikiwa na moyo wake ukaanza kupiga tena.
"Walikuwa wanamshtua kwa umeme mara kwa mara kuamsha moyo wake," mke wake alikumbuka kwa hofu.
Alikaa wiki moja akiwa hajitambui na akipata degedege. Patrick, alikuja kuzinduka baada ya wiki moja. Lakini alikuwa amepata madhara kwenye ubongo. Alipoteza kumbukumbu, uwezo wa kufikiri kwa haraka na nguvu zake.
Hakuweza tena kuishi na kufanya kazi kama zamani.

Chanzo cha picha, Paatriik Chaarnlii
"Nilipoamka sikuweza kuona"
Patrick anasema bado ni vigumu kuamini kilichotokea.
"Nilipoamka sikuweza kuona," anasema. "Nilikuwa naona kitu lakini sikuelewa ni nini."
Upofu wa muda mfupi ulimfanya apate hali iitwayo 'Charles Bonnet Syndrome', ambapo ubongo huunda picha kama ndoto ili kujaza pengo la taarifa za kuona.
Baadhi ya maono aliyoyaona yalikuwa ya kutisha, mengine mazuri na ya kuvutia. Wakati mwingine alihisi yuko hospitali kwenye kilima kilichofunikwa na theluji, akitazama nje dirishani.
Alisema uzoefu huo ulimpa hisia ya amani na furaha.
Kadri uwezo wake wa kuona ulivyorejea, iligundulika kuwa na tatizo lilihusiana na jeraha la ubongo. Vipimo vya awali vilionyesha kumbukumbu na kasi yake ya kuchambua mambo ilikuwa chini ya asilimia 2. Baadaye hali yake ilianza kuimarika, lakini bado hupata shida kukumbuka mambo mengi ya hivi karibuni.
"Naishi maisha yenye thamani"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baada ya kurudi nyumbani, madhara ya jeraha lake yaliendelea kuonekana. Alipoteza nguvu na motisha ya kufanya mambo mbalimbali. Wakati fulani hakuwa na wasiwasi kuhusu chochote, hali iliyohitaji msaada wa kisaikolojia.
Kupitia tiba ya kisaikolojia, alianza kurejesha ari na kuanza kujifunza kukubali maumivu ya kupoteza maisha yake ya zamani.
Anasema hata kama angeambiwa arudi kwenye maisha yake ya awali, asingetaka.
Sasa ameacha kazi yake ya zamani na anataka kuwa mwandishi.
"Naishi maisha ya taratibu sasa, si kwa sababu nilichagua, bali kwa sababu nalazimika. Lakini ninayashukuru maisha haya. Uzuri wa maisha sasa nauona wazi. Polepole, ninaishi maisha yenye utajiri," anasema.
Anasema mtazamo wake umebadilika kabisa.
"Ninashukuru kuwa hai."
Uhusiano wake na familia pia umeimarika.
"Tuko karibu zaidi kuliko zamani. Kilichonipata kimetufanya tuwe na mshikamano mkubwa," anasema.
Ingawa maisha yake yamebadilika sana, anasema bado anayapenda.
"Wengine wanaweza kuona kama muda wangu umebaki ni mfupi. Lakini siwezi kubadilisha kilichotokea. Licha ya changamoto, bado nayapenda maisha yangu. Nafurahia kuwaona watoto wanaporudi nyumbani. Niliacha kukimbizana na mambo bila kupumzika."
Kwa Patrick, kufa kwa dakika 40 hakukumletea maisha mapya bali kulimfundisha jinsi ya kuyaishi kwa thamani zaidi.














