Shahidi amwambia Tundu Lissu 'sikuogopi'

Upande wa serikali umeleta shahidi mmoja P7 shahidi mwingine ameombewa udhuru amefiwa, kesi itaendelea kesho

Muhtasari

Moja kwa moja

Asha Juma & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

  2. Ghana yafichua paspoti ya raia wa Urusi aliyerekodi na kuchapisha picha za wanawake

    L

    Chanzo cha picha, WIZARA

    Waziri wa mawasiliano wa Ghana Samuel Nartey George ametoa picha ya mwanaume raia wa Urusi aliyerekodi kwa siri na kuchapisha picha za kimapenzi za wanawake wa Ghana.

    Nchi hiyo inafuatilia suala hilo ili kuhakikisha anafikishwa mbele ya sheria.

    Waziri wa mambo ya nje wa Ghana alimwita balozi wa Urusi nchini humo na kuripotiwa kuwa nchi hizo mbili "zinafanya kazi pamoja kumfuatilia mtu huyo."

    Katika mkutano na waandishi wa habari huko Accra, waziri wa mawasiliano Samuel George alichapisha pasipoti ya mtu huyo, ambayo ilikuwa na jina la Vladislav Liukov.

    Samuel George amesema "wizara za mawasiliano na jinsia zinamjua bwana huyu ni nani na pasipoti yake aliyoingia nayo nchini."

    Amesema baadhi ya wanawake wamewasilisha malalamiko rasmi ambayo yatawasilishwa katika ofisi ya mwanasheria mkuu kwa hatua.

    Amesema "polisi pamoja na mamlaka ya usalama wa mtandao watalipeleka suala hilo kwa Interpol kutoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa bwana huyo."

    Waziri huyo pia amesema mamlaka ya usalama wa mtandao ambayo imeendesha uchunguzi kuhusu suala hili inajiandaa kumshtaki mshukiwa hayupo.

    Waghana wengi wanataka mshukiwa akamatwe huku baadhi ya watu wanasema waathiriwa walikubali wenyewe.

    Waziri wa jinsia wa Ghana Agness Naa Momo Lartey amesema "sio wanawake wote ambao picha zao zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii walikutana kimapenzi na mshukiwa."

    Alisema "baadhi ya wanawake hawa wanajiua hasa wale ambao hawakuwa na uhusiano wa kimapenzi na mshukiwa."

    Agnes Naa Momo Lartey anataka waathiriwa waonewe huruma huku wizara yake ikiendelea kuwapa msaada wa kisaikolojia wale waliojitokeza.

    Uchunguzi wa awali uliofanywa na mamlaka ya usalama wa mtandao umebaini kuwa mshukiwa alirekodi matukio ya kimapenzi na baadhi ya wanawake na kujipatia pesa kupitia majukwaa ya mtandaoni.

    Sheria ya usalama wa mtandao ya Ghana, 2020 (Sheria ya 1038) inakataza kurekodi na kusambaza picha za kimapenzi bila ridhaa.

    Mtu anayepatikana na hatia anaweza kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka 25 jela.

  3. Chuo Kikuu India chakosolewa kwa kudai umiliki wa roboti iliyotengenezwa China

    p

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Watumiaji wa mitandao walitambua roboti hiyo kama modeli ya Go2 iliyotengenezwa na kampuni ya Kichina ya Unitree Robotics.

    Chuo kikuu cha India kimezua utata katika mkutano wa kilele wa akili mnemba (AI) jijini Delhi baada ya afisa mmoja kudai kwamba roboti ya mbwa iliyetengenezwa China ni uvumbuzi wa chuo hicho.

    Tukio hilo lilifichuliwa baada ya profesa kutoka Chuo Kikuu cha Galgotias kumwambia mtangazaji wa DD News kwamba roboti hiyo inayoitwa "Orion" "ilitengenezwa" katika Kituo chao cha Centre of Excellence. Video ya matamshi yake imesambaa sana.

    Watumiaji mtandaoni baadaye walitambua mashine hiyo kama modeli ya Go2 iliyotengenezwa na kampuni ya Kichina ya Unitree Robotics, ambayo inauzwa kwa takriban rupia 200,000 ($2,200; ÂŁ1,600).

    Katika taarifa siku ya Jumatano, chuo kikuu kilikana kudai kuwa ndicho kilichotengeneza roboti hiyo na kuelezea ukosoaji huo kama "kampeni ya propaganda."

    Neha Singh, profesa aliyeonekana kwenye video hiyo, baadaye aliwaambia waandishi wa habari kwamba matamshi yake hayakueleweka vizuri.

    Tukio hilo linaonekana ni aibu kwa waandaaji wa mkutano huo kwani video hiyo pia ilichapishwa kwenye akaunti rasmi ya Waziri wa IT Ashwini Vaishnaw X.

    Katibu wa TEHAMA wa India S Krishnan alisema utata huo haupaswi "kufunika" kazi iliyofanywa na washiriki wengine katika mkutano huo.

    Mkutano wa Kilele juu ya AI India, uliozinduliwa na Waziri Mkuu Narendra Modi huko Bharat Mandapam Jumatatu, umetangazwa na serikali kama mkutano mkuu ili kuiweka India kama kitovu cha AI duniani.

    Wajumbe kutoka zaidi ya nchi 100, wakiwemo wakuu kadhaa wa serikali, wanahudhuria, pamoja na viongozi wa kampuni kama vile Sundar Pichai wa Google.

    Mkutano huo wa siku tano unaangazia mijadala ya sera, maonyesho ya biashara na mikutano ya faragha kuhusu akili bandia, miundombinu na uvumbuzi.

    Hata hivyo, siku ya ufunguzi wake ilifunikwa na malalamiko ya msongamano wa watu, foleni ndefu na mkanganyiko katika ukumbi huo, na kusababisha waandaaji kuongeza muda wa maonyesho na kuimarisha usimamizi.

  4. Australia yamzuia kurudi nyumbani raia wake aliyejiunga na Dola la Kiislamu nchini Syria

    p

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Australia imemzuia raia mwenye uhusiano na kundi la Islamic State (IS) kuingia nchini humo kwa miaka miwili.

    Mtu huyo ni miongoni mwa kundi la wanawake na watoto 34 raia wa Australia wanaojaribu kurudi nyumbani baada ya kuachiliwa kutoka kambi moja huko Syria mapema wiki hii, lakini amerudishwa Syria.

    Marufuku hiyo ilitolewa "kwa ushauri kutoka mashirika ya usalama," Waziri wa Mambo ya Ndani Tony Burke alisema Jumatano, akiongeza kuwa watu wengine 33 bado hawakidhi "matakwa ya kisheria yanayohitajika" ili kupigwa marufuku.

    Kundi hilo linaaminikiwa kuwa na wake, wajane na watoto wa wapiganaji wa IS. Kuna watoto 23 miongoni mwao.

    Waziri Mkuu Anthony Albanese alisisitiza kwamba familia hizi hazitapokea usaidizi wa serikali ili kurudi nchini.

    "Hawa ni watu waliochagua kwenda ng'ambo kujiunga na itikadi kali na ya kibaguzi inayolenga kudhoofisha na kuharibu mtindo wetu wa maisha."

    Hata hivyo wataalamu wa sheria wameonya kwamba serikali ina wajibu wa kuwapa raia haki ya kurudi, kwani kundi hilo lina pasipoti halali za Australia.

    Kundi hili katika kambi ya al-Roj kaskazini mwa Syria ni miongoni mwa Waaustralia kadhaa ambao wameshikiliwa katika kambi na magereza kote nchini tangu 2019, wakati IS iliposhindwa nchini Syria.

    Kambi ya al-Roj ina zaidi ya watu 2,000 kutoka mataifa 40, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

    Baadhi ya kambi hizi zimegonga vichwa vya habari huku wanawake na watoto wanaoishi humo wakiwa na utapiamlo na hawana uwezo wa kupata rasilimali za msingi.

    Serikali zingine kadhaa za kigeni - ikiwa ni pamoja na Ufaransa, Uholanzi, na Uingereza - pia zimekataa kuwarejesha nyumbani raia wao ambao bado wanashikiliwa Syria.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine yamalizika bila mafanikio

    o

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Wawakilishi wa Urusi, Marekani na Ukraine walikutana Geneva siku ya Jumanne na Jumatano

    Mazungumzo kati ya Urusi, Ukraine na Marekani yenye lengo la kumaliza vita vya Moscow nchini Ukraine yamekamilika bila mafanikio.

    Mikutano ya pande tatu, iliyofanyika Geneva, imeendelea Jumanne usiku na kudumu kwa saa mbili siku ya Jumatano.

    Ingawa mjumbe wa Marekani Steve Witkoff alionyesha matumaini kuhusu mazungumzo hayo, lakini pande zote mbili za Urusi na Ukraine zilionyesha kuwa ni "magumu."

    Ingawa mazungumzo yalikuwa magumu, mjumbe wa Kremlin Vladimir Medinsky aliongeza kwamba mkutano mwingine utafanyika "hivi karibuni."

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pia amesema mazungumzo hayo "sio rahisi" kutokana na tofauti katika misimamo ya pande hizo mbili.

    Ujumbe wa Urusi na Ukraine ulikutana mara ya mwisho katika mazungumzo yaliyosimamiwa na Marekani huko Abu Dhabi mwezi Januari, ambayo yalipelekea ubadilishanaji wa wafungwa wa kwanza.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Mpanda milima ashtakiwa kwa kumwacha mpenzi wake kwenye mlima na kupelekea kufariki

    k

    Chanzo cha picha, www.foto-webcam.eu

    Maelezo ya picha, Kamera inaonyesha picha ya mpenzi wake akiwa na tochi kutoka kileleni

    Zaidi ya mwaka mmoja baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 33 kupigwa na baridi hadi kufa kwenye mlima mrefu zaidi nchini Austria, mpenzi wake anakabiliwa na kesi Alhamisi akituhumiwa kwa mauaji kutokana na uzembe.

    Kerstin G alifariki kutokana na baridi kali katika safari ya kupanda mlima. Mpenzi wake anashutumiwa kwa kumwacha bila kinga, akiwa amechoka karibu na kilele katika hali ya dhoruba asubuhi ya tarehe 19 Januari 2025, wakati alipokwenda kutafuta msaada.

    Waendesha mashtaka wanasema, kwa kuwa mpandaji huyo alikuwa na uzoefu zaidi, anashtakiwa kwa kushindwa kurudi au kupiga simu kuomba msaada kwa wakati ili kumsaidia mpenzi wake.

    Akitambuliwa na vyombo vya habari vya Austria kama Thomas P, anakanusha mashtaka hayo na wakili wake, Kurt Jelinek, ameelezea kifo cha mwanamke huyo kama "ajali mbaya."

    Msiba huo ulitokea baada ya wawili hao kuanza kupanda mlima Grossglockner wenye urefu wa mita 3,798 (futi 12,460).

    Waendesha mashtaka wanamtuhumu Thomas P kwa kufanya makosa tangu mwanzo na wamechapisha orodha ya makosa 9.

  7. Prestianni akanusha kumfanyia ubaguzi Vinicius

    j

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Real Madrid na Benfica zitakutana kwa ajili ya mechi ya marudiano tarehe 25 Februari

    Winga wa Real Madrid, Vinicius Junior, amesema "wabaguzi wa rangi ni waoga" huku kiungo wa Benfica, Gianluca Prestianni, akikana kumtusi raia huyo wa Brazil kwa kauli ya ubaguzi wa rangi.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliripoti madai ya ubaguzi wa rangi uliofanywa na Prestianni kwa mwamuzi Francois Letexier wakati wa mechi ambapo Real Madrid ilishinda bao 1-0 dhidi ya Benfica jijini Lisbon Jumanne.

    Mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa ilisitishwa kwa dakika 10, huku wachezaji wakitoka uwanjani muda mfupi baada ya Vinicius kuipa timu yake bao la uongozi.

    Mshambuliaji huyo, ambaye ni mwathirika wa matukio mengi ya ubaguzi, amesema katika chapisho kwenye Instagram: "Wabaguzi wa rangi, ni waoga. Huweka mashati yao midomoni kujificha ili kuonyesha jinsi walivyo dhaifu."

    "Lakini wana ulinzi kutoka kwa watu ambao, wana wajibu wa kuwaadhibu. Hakuna kilichotokea leo ambacho ni kipya katika maisha yangu au katika maisha ya timu yangu."

    Prestianni, mwenye umri wa miaka 20, amekana kutoa kauli za kibaguzi kwa Vinicius Jr katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii.

    "Nataka kufafanua kwamba hakuna wakati wowote nilipomtusi Vini Jr kwa ubaguzi wa rangi, kwa masikitiko makubwa, alielewa vibaya kile alichokisikia," alisema Prestianni.

    "Sijawahi kuwa mbaguzi wa rangi kwa mtu yeyote na inaumiza vitisho nilivyopokea kutoka kwa wachezaji wa Real Madrid."

    Uefa, ambayo inaendesha Ligi ya Mabingwa, inasema inapitia ripoti za mechi ya jana usiku.

    Mchezaji mwenzake Vinicius katika timu ya Real Madrid, Kylian Mbappe, ametaka winga wa Argentina, Prestianni, asiruhusiwe tena kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kufuatia tukio hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Mazungumzo ya kusaka amani kati ya Ukraine na Urusi yaingia siku ya pili

    j

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine nchini Uswisi yanasimamiwa na Steve Witkoff.

    Mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff amesema mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi "yameleta maendeleo yenye maana" ili kukomesha vita, huku pande zote mbili zikijiandaa kwa siku ya pili ya mazungumzo huko Geneva sikua ya Jumatano.

    Hata hivyo, matumaini ya mafanikio yanabaki kuwa madogo, huku Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akisema "si haki" kwa Rais wa Marekani Donald Trump kuendelea kuitaka nchi yake isalimu amri, akiongeza kwamba "amani haitapatikana ikiwa Urusi itapewa ushindi."

    Hivi karibuni Rais wa Marekani Donald Trump amependekeza kuwa ni jukumu la Ukraine kuhakikisha mazungumzo nchini Uswisi yanafanikiwa, bila kuitaja Urusi.

    "Mafanikio ya Rais Trump katika kuunganisha pande zote mbili za vita hivi yameleta maendeleo yenye maana, na tunajivunia kufanya kazi chini ya uongozi wake kukomesha mauaji katika mzozo huu mbaya," Witkoff aliandika kwenye X baada ya siku ya kwanza ya mazungumzo.

    Urusi inakalia takriban 20% ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa za eneo la mashariki mwa Donbas. Kremlin inataka Ukraine ikabidhi eneo lote lililobaki, Ukraine imekataa.

    Zelensky aliiambia tovuti ya Axios siku ya Jumanne kwamba "sio haki" Trump kuendelea kuitaka Ukraine pekee ifanye makubaliano.”

    Mazungumzo hayo ni duru ya tatu ya mazungumzo ya pande tatu, ambayo yanasimamiwa na Witkoff na Jared Kushner, mkwe wa rais wa Marekani.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Lissu amaliza kumhoji shahidi huku kesi ikiahirishwa

    .

    Chanzo cha picha, MITANDAO

    Lissu: Umeeleza kwamba hapo kwenye ofisi za RCO uliandika maelezo ukapelekwa mahabusu, ukapatana na ndugu zako ukapata dhamana asubuhi ni kweli sio kweli?

    Shahidi: Naomba nirudie hapo

    Lissu: Hapana utaruhusiwa ukiwa unawasimulia ndugu zako wa kirai

    Shahidi: Rudia swali

    Lissu: Swali langu waeleze majaji kama hayo maneno “ulidhaminiwa asubuhi” yapo kwenye karatasi yako ya maelezo?

    Shahidi: Neno gani?

    Lissu: Kwamba ulidhaminiwa asubuhi

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Kwenye kielelezo hicho shahidi umesema hivi siku ya 3/4/2025 ukiwa kijiweni ilianzishwa mada kwenye mitandao kuwa Lissu na CHADEMA wamesema watazuia uchaguzi na watakinukisha. Nieleze umetaja huo mtandao au mitandao?

    Shahidi: Ndiyo nimetaja mtandao wa Youtube

    Lissu: Akaunti ya nani ya Youtube umetaja?

    Shahidi: Sijataja

    Lissu: Waeleze majaji kama katika maelezo yako umetaja akaunti yako sehemu ya mtandao wowote iwe facebook, instagram?

    Shahidi: Ndiyo nimetaja Youtube

    Lissu: Akaunti ya nani?

    Shahidi: Niliingia kupitia akaunti yangu?

    Lissu: Waeleze majaji kama kwenye maelezo yako kama una akaaunti ya Youtube?

    Shahidi: Sikuandika

    Lissu: Mliendelea kusisitizana kama vijana kuhusu alichokisema Lissu kwamba sisi kama vijana tutaunga mkono na tupo tayari kwa atakachotuambia

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Waeleze majaji kama vijana kusisitizana kuunga mkono ni kosa kisheria

    Shahidi: Mimi sijui kwakua mimi sio mwanasheria

    Lissu: Waeleze majaji kama ni makosa kwa mujibu wa sheria za nchi hii kumuunga mkono Lissu na chama chake?

    Shahidi: Nilishakujibu sijui

    Lissu: Umesema mlikuwa mnasisitizana kuunga mkono kauli zangu za kuzuia uchaguzi kwani kutaka kuzuia uchgauzi ni kosa?

    Shahidi: Ni kosa ndiyo maana tukakamatwa

    Lissu: Aaah ni kosa tutakuja kujadili hilo muda sio mrefu…baada ya kukamatwa umesema uliandika maelezo juu ya kosa la kufanya fujo. Eleza kama ulipelekwa mahakamani kwa kosa hilo?

    Shahidi: Sikupelekwa mahakamani

    Lissu: Baada ya kuchukuliwa maelezo siku ya tarehe 3 kama hao mapolisi walihangaika tena na wewe kuhusu kesi ya kufanya fujo?

    Shahidi: Ndiyo maana niliendelea kuripoti mpaka tarehe 17

    Lissu: Ulipokuwa unaripoti polisi walikuwa wanakuambia nini kuhusu hilo kosa?

    Shahidi: Walikuwa wananiambia kufagia na kusaini

    Lissu: Hawakukuambia kwamba wamekukuta na kosa au wamekupeleka mahakamani?

    Shahidi: Ndiyo maana niko hapa

    Lissu: Upo hapa kwa kosa langu

    Shahidi: Kosa lako wewe ndiyo limenisababishia

    Lissu: 17/4/2025 ulikwenda kuripoti polisi ulisema hivi “Tuliambiwa tusubiri tuhojiwe kwa mara nyingine” ni kweli sio kweli

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Kwa nini polisi walikuambia wakuhoji kwa mara nyingine?

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Waeleze majaji kama hawakukuhoji kuwa shahidi wa kesi hii?

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Ukichokiandika 17/4/2024 kilitokana na maswali ya polisi?

    Shahidi: Hapana nilisema kilichotokea

    Lissu: Kwa hiyo haya ni maelezo yako na unakana kuhojiwa na polisi

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Waeleze majaji umekujaje mahakami leo?

    Shahidi: Kwa miguu

    Lissu: Kutoka Kilanyi, Arumeru

    Shahidi: Nilipanda basi

    Lissu: Nani alikulipia nauli

    Shahidi: Mwanamke wangu

    Lissu: Nani analipa gharama kwenye mji huu?

    Shahidi: Nimeshakuambia mwanamke wangu

    Lissu: Tangu ulipohojiwa na polisi 17/4/2025 uliwahi kuwasiliana na polisi?

    Shahidi: Hapana mpaka pale waliponipigia simu nikachukue sammons

    Lissu amemaliza kumhoji shahidi

    Upande wa mashtaka unataka kesi iahirishwe kutokana na kukosekana kwa shahidi mmoja ambaye taarifa yake ilitolewa mapema. Upande wa mshtakiwa umeafiki kesi itaendelea kesho saa 3 asubuhi.

  10. Lissu aanza kumuhoji shahidi

    .

    Chanzo cha picha, CHADEMA

    Lissu: Katika ushahidi wako leo umeileza mahakama kwamba pale kwa Mromboo kijiweni kuna watu wengi kweli sio kweli?

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Waeleze majaji kama kwenye hicho kielelezo ulichoshika mkononi kama haya maneno “kuna watu wengi kama mama ntilie, dereva bajaji na watu wenye maduka ya mahitaji ya nyumbani” yapo kwenye maelezo yako?

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Umeeleza kwenye ushahidi wako leo kuwa ukiwa hapo Mrombo hapo 3/4/2025 mlikuwa mnazunguza mazungumzo ya kawaida ni kweli si kweli?

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Alafu kuja mtu mmoja akasema “CHADEMA watazuia uchaguzi wa mwaka huu” nataka useme kama hayo maelezo yapo kwenye maelezo yako

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Nionyeshe yapo wapi

    Shahidi: Hapo imesema kwamba ameanzisha lakini ilikuwa…

    Lissu: Umeandika hivi “Nikiwa pale kijiweni kwetu kwa Mrombo ikaanzishwa mada kuhusu kauli za Lissu” hayo maneno hayo “Mumesikia CHADEMA wamesema watazuia uchaguzi wa mwaka huu” yapo kwenye maelezo yako

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Lakini pia kwenye maelezo yako tena ukasema huyo mtu mmoja akasema “tena wamesema watakinukisha mbaya” waeleze majaji kama yapo kwenye maelezo yako

    Shahidi: Yapo

    Lissu: Tuoneshe

    Shahidi: Watakinukisha…

    Lissu: Nikusomee ulichokiandika?

    (Lissu anamsomea) hayo maneno yalisemwa na mtu mmoja?

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Katika ushahidi wako wa leo umesema hivi huyu mtu mmoja huyo akasema “Polisi wanaiba kura hata ukienda mahakamani hutapata haki sababu majaji ni vibaraka wa CCM” si ndiyo ushahidi wako wa leo?

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Waeleze majaji katika hayo maelezo yako kama kuna hayo maneno kwenye maelezo yako ya polisi?

    Shahidi: Ulisema majaji hawatendi haki

    Lissu: Hayo maneno “vibaraka wa CCM” yapo?

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Kwenye ushahidi wako umesema huyu mtu akasema “Mwaka 2024 tume walipewa kazi ya kukata majina ya wajumbe wa CHADEMA”

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Waeleze majaji kama hayo maelezo yapo kwenye maelezo yako polisi

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Waeleze majaji kama kwenye maelezo yako umetaja tume ya uchaguzi hata mara moja kwenye maelezo yako

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Waeleze majaji kama katika maelezo yako umetaja uchaguzi mdogo wa 2024

    Shahidi: Hakuna

    Lissu: Umesahau ulichokuwa unaandika polisi?

    Shahidi: Nilikuwa naandika maelezo sio kitabu

    Lissu: Umesema kwenye maelezo yako “ulipata hamasa kutokana na hayo maneno” kweli sio kweli

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Waeleze majaji kama hayo maneno “ulipata hamasa” yapo kwenye maelezo yako

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Kwenye ushahidi wako leo umesema kwamba baada ya kusikia maneno yale kijiweni, ikabidi uingie kwenye mtandao wa YouTube kwa kutumia simu yako janja kweli au sio kweli?

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Waonyeshe majaji kama kwenye maelezo yako kuna sehemu panapoonyesha uliingia mtandao wa Youtube kwa simu yako janja

    Shahidi: Mimi najua ukiwa kwenye mtandao utakuwa na simu

    Lissu: Kwani huwezi kutumia computer

    Shahidi: Mimi sina Computer

    Lissu: Unaweza kuingia mtandaoni kwa kutumia computer hata TV. Sasa swali langu nataka useme kwenye maelezo yako kuna sehemu ulitumia simu yako?

    Shahidi: Hakuna

    Lissu: Umesema uliingia kwenye mtandao wa Youtube wa Jambo?

    Shahidi: Ndiyo sasa waeleze majaji kama kwenye maelezo yako kuna sehemu uliingia kwenye mtandao wa Jambo

    Shahidi: Hakuna

    Lissu: Baada ya kufika kituo cha central baada ya dakika 45 unashtakiwa kwa kosa la kutaka kufanya fujo

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Waeleze majaji kama hayo maneno yapo kwenye karatasi yako ya maelezo?

    Shahidi: Hayapo

  11. Lissu amsomea shahidi maelezo yake

    .

    Chanzo cha picha, MWANANCHI

    Lissu: Maeneo ninayotaka kukuuliza maswali ni haya yafuatao ya kwanza ni pale kwa Mromboo kuna watu wengi wakiwemo madereva wa bajaji, mama ntilie na maduka ya mahitaji mbalimbali…

    Eneo la pili ni unaposema Aprili 3, 2025 ukiwa hapo kwa Mromboo kuna mtu mmoja aliibua maneno mengine. Hiyo habari ya mtu mmoja nataka nikuhoji,

    Eneo la tatu umesema huyo mtu mmoja akasema tena “Watakinukisha” huyo mtu mmoja...

    Eneo la nne ni huyo mtu mmoja alisema “hata ukienda mahakamani hupati haki”

    Eneo la tano ni uliposema ulipata hamasa…

    Eneo la sita ni wewe uliingia kwenye mtandao wa Youtube kwenye maelezo yako haioneshi kama una simu…

    Eneo la saba ulisema uliingia kwenye mtandao wa Youtube wa Jambo ukaona hiyo video yenye maneno ya huyo bwana mmoja…

    Namba nane ni pale ulipopelekwa kwenye ofisi ya RCO kwa kosa la kufanya fujo…

    Eneo la tisa ni uliporipoti kituoni 3/4/2025, kesho yake ulidhaminiwa asubuhi na ndugu zako. Nimeangalia kwenye maelezo yako ya polisi umesema ulidhaminiwa mchana.

  12. Lissu anaanza kuuliza maswali ya dodoso kwa shahidi

    Lissu: Nataka nikuulize maswali kutokana na ushahidi wako nitaomba ujibu maswali yangu kadri nitakavyouliza bila hofu

    Shahidi: Mimi sikuogopi

    Lissu: Ulianza kuandika maelezo yako tarehe 3/4/2025 kwa kosa la kufanya fujo?

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Hayo maelezo yako tarehe 3/4/2025 yako wapi?

    Shahidi: Kama unakumbuka nikisema tarehe 17/4/2025 niliandika maelezo hayo hayo

    Lissu: Tarehe 3/4/2025 uliandika maelezo yaliyohusu tuhuma za kufanya fujo hayo maelezo yako wapi?

    Shahidi: Mimi sio askari mimi niliandikiwa maelezo nikacha hiyo karatasi

    Lissu: Vile vile uliandika maelezo tarehe 17/4/2025 kweli sio kweli?

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Ukioneshwa hayo maelezo utayatambua?

    Shahidi: Ndiyo nitayatambua

    Lissu: Naomba mahakama shahidi apewe maelezo yake aliyoandika 17/4/2025

    Lissu: Umepata enhe?

    Shahidi: Wamenipatia

    Lissu: Yaagalie uwaeleze majaji kama hayo maelezo ni yako uliyoandika 17/4/2025

    Shahidi: Ndiyo yenyewe

    Pia unaweza kusoma:

  13. Kesi ya Tundu Lissu imeanza, Shahidi P7 ahojiwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Karibu katika matangazo ya moja kwa moja kuhusu Kesi ya Tundu Lissu.

    Upande wa serikali umeleta shahidi mmoja P7 shahidi mwingine ameombewa udhuru amefiwa, mawakili wa serikali wameanza kumuhoji.

    Shahidi wa leo (P7) ni wa kificho, ni kijana wa miaka 26 mkristo.

    Wakili wa serikali anamuongoza shahidi kwa maswali ya msingi

    Wakili: Unajishughulisha na nini katika maisha yako ya kila siku?

    Shahidi: Ni dereva naendesha bajaji

    Wakili: Hiyo shughuli unafanyia wapi?

    Shahidi: Kwa mrombo Arusha

    Wakili: Shughuli hizo umefanya kwa muda gani?

    Shahidi: Toka 2023

    Wakili: Hebu iambie mahakama hali ya eneo la kufanyia kazi ikoje?

    Shahidi: Kuna watu wengi. Kuna sisi waendesha bajaji, mama ntilie na kuna duka la mahitaji ya nyumbani

    Wakili: Iambie mahakama tarehe 3/4/2025 majira ya jioni ulikuwa wapi na unafanya nini?

    Shahidi: Nakumbuka tarehe 3/4/2025 majira ya saa za jioni nilikuwa maeneo ya kazini kwangu kijiweni ninakopaki bajaji kwa Mrombo Arusha.

    Wakili: Ukiwa eneo hilo. Nini kiliendelea?

    Shahidi: Tulikuwa kwenye mazungumzo ya kawaida ya kijiweni baada ya hapo kuna mtu mmoja akaibua mazungumzo mengine tofauti na yale ya mwanzo.

    Wakili: Aliibua mazungumzo gani?

    Shahidi: Hivi mmesikia CHADEMA wamesema kwamba watazuia uchaguzi wa mwaka huu…

    Wakili: Nini kiliendelea baada ya hoja hiyo?

    Shahidi: Huyo mtu akasema tena wamesema watakinukisha mbaya

    Wakili: Baada ya hapo?

    Shahidi: Akasema kwamba polisi wanaiba kura

    Wakili: Endelea shahidi

    Shahidi: Akasema kwamba hata ukienda mahakamani hautapata haki

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Akaendelea kusema kuwa hata ukienda mahakamani hutapata haki sababu majaji ni vibaraka wa CCM…akaendelea kusema kwamba mwaka 2024 tume ya uchaguzi ilipewa maelekezo ya kukata wajumbe wa CHADEMA…tukiwa tunaendelea kubishana nilipata hamasa kupitia yale maneno.

    Wakili: Hebu weka vizuri kumbukumbu unasema ulisikia toka kwa mtu aliyeanzisha mada wewe kama wewe ukafanya nini?

    Shahidi: Baada ya kusikia hayo ilibidi niingie kwenye mtandao wa Youtube maana alisema amesikia kwenye mtandao.

    Wakili: Ulingia kwenye mtandao wa YouTube kwa njia gani?

    Shahidi: Nilitumia simu yangu ya janja

    Wakili: Nini kiliendelea ukiwa hapo Youtube?

    Shahidi: Nikafungua chaneli ya Jambo nikakuta anachozungumza yule bwana ni kweli na mimi nilisikia hayo hayo kupitia simu yangu….

    Wakili: Nini kiliendelea baada ya kuwa umejiridhisha?

    Shahidi: Baada ya dakika chache watu walikuja wakatuambia tupo chini ya ulinzi wakatuambia wao ni askari

    Wakili: Endelea

    Shahidi: Wakatuweka chini ya ulinzi kuna baadhi ya watu walikimbia tukakamatwa watu wawili mimi na P4, tukapelekwa kituo cha polisi cha Muriet, baada ya kufika, tulikaa kama dakika 45 tukapelekwa kituo cha Central mjini.

    Wakili: Baada ya kupelekwa kituo cha Polisi cha central, nini kiliendelea?

    Shahidi: Tukaingizwa kwenye ofisi ya RCO nikaambiwa kwamba ninashtakiwa. Niliandika maelezo na kuingizwa mahabusu

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Asubuhi yake nikifuatwa na ndugu zangu nikadhaminiwa nikapewa ratiba ya kwenda kuripoti kwenye kituo cha polisi

    Pia unaweza kusoma:

  14. Kwaresima na Ramadhan zaanza pamoja katika baadhi ya maeneo

    .

    Waumini wa dini ya Kiislamu katika baadhi ya maeneo kama vile Saudi Arabia na Umoja wa Falme za kiarabu leo wameanza mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Lakini katika baadhi ya nchi kama Tanzania na Kenya kuna wale ambao wameanza mfungo huku wengine wakitarajia kuanza kesho kulingana na mwandamo wa mwezi.

    Kwa Wakristo, leo ni Jumatano ya Majivu ikiwa ni ishara ya kuanza kwa Kwaresma.

    Hali ambayo imefanya mifungo hii mitakatifu ya Waislamu Ramadhan na Wakristo Kwaresma kujikuta pamoja.

    Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kiongozi wa kanisa la Katoliki duniani kwa Kwaresima ya mwaka huu 2026, una kichwa cha habari: “Kusikiliza na Kufunga.

    Funga, toba na kusali kumesisitizwa pia na madhehebu mengine katika kipindi hiki.

    Padri Lameck Paul Ndomba anatoka kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam alisema, "Katika mapokeo na mafundisho ya Kanisa, Wakiristo wanaingia katika kufunga, toba na sala kama sehemu ya kujutia dhambi na makosa yao, ili wapate kusamehewa na Mungu na wapate kuishi upya maisha yao ya kiroho na kiimani. Ninawaomba Wakiristo wote, wazingatie yale yote ambayo Mungu anawataka na Kanisa linafundisha juu ya maisha ya usafi, matakatifu, upendo na huruma kwa wengine lakini pia wakisukumwa sana na upendo kwa Mungu wanayemuamini na kumuabudu. "

    Sala, kufunga na kujinyima pamoja na sadaka ni nguzo katika funga hii".

    Herman Nguki ni muumini wa dini ya Kikristo, Tanzania amezungumza na BBC na kusema, "Mfungo wa Kwaresma unaanza siku ya Jumatanoya Majivu na dhima kuu huwa inakuwa ni kutubu dhabi ndio maana huwa tunaongozwa na somo la Injili ya Marko somo la kwanza aya ya kumi na tano. Tunapakwa majivu kama Wakiristo kutukumbusha kuwa sisi na majivu na mavumbini tutarudi. Misingi Mikubwa ya Kwaresma huwa ni Sala ambayo inatufundisha kujiimarisha uhusiano wetu na Mungu, Kufunga na kujinyima ambayo ni zaidi ya chakula. Ni sehemu ya kujikumbusha kwamba unaweza kuachana na vitu kwa ajili ya Kiristo. Na sehemu ya tatu ni matendo ya huruma… ".

    Na kama ilivyo kwa Wakristo, Waumini wa dini ya Kiislamu vilevile, wako kwenye mfungo wa Ramadhan.

    Mould Ahmed ni muumini wa dini ya kiislamu anauelezea mwezi huu wa mfungo wa Ramadhan kwake.

    "Kawaida yangu huwa nafanya ibada lakini Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ibada inaongezeka."

    Kwa hakika mfungo wa Ramadhan na Kwaresma ni miezi ya ibada unayosisitiza unyenyekevu kwa mwenyezi Mungu kupitia sala, kufunga ama kujinyima pamoja na kutoa sadaka.

    Soma zaidi:

  15. Iran yasema imekubaliana na Marekani 'kanuni za mwongozo' katika mazungumzo ya nyuklia

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Iran imesema imefikia makubaliano na Marekani kuhusu "kanuni za mwongozo" ili kutatua mzozo wao kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.

    Akizungumza baada ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja huko Geneva, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi aliongeza kuwa bado kuna mengi ya kufanywa.

    Kwa upande wake, Marekani ilisema "hatua imepigwa".

    Badr Albusaidi, Waziri wa mambo ya nje wa Oman, alisema mazungumzo hayo "yalimalizika kwa kufikiwa kwa hatua kubwa kuelekea kutambua malengo ya pamoja na masuala yenye utata".

    Mkutano huo ulifuatia vitisho vya mara kwa mara vya kijeshi vya Marekani dhidi ya Iran kuhusu msako wake mbaya dhidi ya maandamano ya kupinga serikali na shughuli zake za nyuklia.

    Rais Donald Trump hapo awali alisema anaamini Iran ilitaka kufikia makubaliano.

    Soma zaidi:

  16. Mechi ya Real Madrid ilisitishwa kwa madai ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Vinicius

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mchezo wa hatua ya mtoano wa Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa dhidi ya Benfica ulisitishwa kwa dakika 10 baada ya Vinicius Junior kuripoti madai ya unyanyasaji wa kibaguzi na yeye na wenzake wakaondoka uwanjani.

    Mwamuzi Francois Letexier alifanya ishara ya mikono kupishana kama msalaba kuashiria unyanyasaji wa kibaguzi baada ya mazungumzo na Vinicius.

    Mshambuliaji huyo wa Brazil alikuwa amewaweka wageni hao wa Uhispania kifua mbele kwa bao 1-0 katika kipindi cha pili kwenye Uwanja wa Estadio da Luz, kabla ya kupewa kadi ya njano kwa sababu ya kusherehekea kupita kiasi.

    Kufuatia mazungumzo na Gianluca Prestianni wa Benfica, Vinicius alimkimbilia mwamuzi Letexier huku akimuashiria mchezaji huyo wa upinzani.

    Taarifa ya Real Madrid ilisema Vinicius alimwambia mwamuzi kwamba alikuwa amefanyiwa kitendo cha ubaguzi wa rangi na winga huyo wa Argentina.

    Kisha Vinicius akatoka nje ya uwanja na kufuatiwa na wachezaji wenzake wa Real Madrid, lakini mchezo huo ulianza tena dakika 10 baadaye, katika dakika ya 60.

    Mechi hiyo ilichezwa hadi mwisho, huku Real ikishinda 1-0 baada ya mchezo kusimama ambapo kitu kilichorushwa kutoka kwa umati kilimpiga Vinicius kwenye mkono.

    Baada ya mechi hiyo, Vinicius alitoa taarifa kwenye Instagram akilaani tukio hilo.

    "Wabaguzi wa rangi, ni waoga sana. Wanahitaji kuweka mashati yao midomoni mwao kuonyesha jinsi walivyo dhaifu," alisema Vinicius.

    "Lakini wana ulinzi wa wengine ambao, kinadharia, wana wajibu wa kuwaadhibu. Hakuna kilichotokea leo ambacho ni kipya katika maisha yangu au katika maisha ya timu yangu."

    "Nilipokea kadi ya njano kwa kusherehekea bao. Bado sielewi ni kwa nini. Kwa upande mwingine, ilikuwa ni itifaki iliyotekelezwa vibaya ambayo haikutimiza lengo lolote."

    Mshambulizi wa Benfica Vangelis Pavlidis alimtetea mchezaji mwenzake Prestianni.

    "Sidhani kama Prestianni alimwambia Vinicius jambo kama hilo. Nadhani linahusiana zaidi na ushindani mkali kati ya Brazil na Argentina kuliko kitu kingine chochote," alisema.

    Prestianni bado hajajibu.

    Taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Brazil ilisema: "Ubaguzi wa rangi ni uhalifu. Haikubaliki. Hauwezi kuwepo katika soka au mahali pengine popote."

    "Vini, hauko peke yako. Uamuzi wako wa kushinikiza itifaki ni mfano wa ujasiri na heshima. Tunajivunia kuwa na wewe."

    "Tutabaki imara katika mapambano dhidi ya aina zote za ubaguzi. Tuko upande wako. Daima."

    Ishara ya mikono kupishana kama msalaba kuashiria unyanyasaji wa ubaguzi wa rangi ilianzishwa na Fifa mnamo Mei 2024.

    Inafanywa na mwamuzi uwanjani ikiwa anaona au kupokea ripoti ya unyanyasaji.

    Soma zaidi:

  17. Familia ya Rais wa zamani wa Zambia yapuuza madai ya kuwekewa sumu

    .

    Chanzo cha picha, Photothek/Getty Images

    Familia ya Rais wa zamani wa Zambia Edgar Lungu, ambaye alifariki Afrika Kusini mwezi Juni mwaka jana na bado hajazikwa, imekanusha madai kwamba Edgar Lungu aliwekewa sumu.

    Polisi wa Afrika Kusini pia wanataka wapewe jukumu la utunzaji wa mwili wake kama sehemu ya uchunguzi wao, kulingana na familia ya mwanasiasa huyo marehemu.

    Katika barua kwa polisi, iliyoonekana na BBC, mawakili wao wanasema familia hiyo inashirikiana na "kesi za uhalifu", lakini wanasisitiza kwamba madai hayo "hayana msingi na hayana ushahidi wa kuaminika".

    Ni mabadiliko ya hivi punde kuhusu hatima ya mwili wa Lungu, ambao bado upo katika chumba cha kuhifadhia maiti nchini Afrika Kusini na umekuwa ukikabiliwa na mgogoro wa kisheria unaoendelea kati ya familia yake na serikali ya Zambia kuhusu mahali anapopaswa kuzikwa.

    Polisi nchini Afrika Kusini imekataa kutoa maoni yoyote kuhusu barua iliyotumwa na kampuni ya sheria ya Mashele Attorneys ya Johannesburg, ambayo inawakilisha familia ya Lungu.

    Msemaji wa polisi Brigedia Athlenda Mathe aliambia BBC: "Hili ni jambo nyeti sana ambalo haliwezi kujadiliwa katika hatua hii."

    Lungu alifariki kutokana na ugonjwa ambao haujawekwa wazi akiwa na umri wa miaka 68 katika hospitali moja mjini Pretoria, Afrika Kusini. Alikuwa ameiongoza Zambia kuanzia 2015 hadi 2021, aliposhindwa katika uchaguzi kwa tofauti kubwa na Rais wa sasa Hakainde Hichilema.

    Serikali ya Zambia inataka mabaki ya Lungu yarudishwe nyumbani na afanyiwe mazishi ya kitaifa, kwa heshima kamili ya kitaifa - na mahakama ya Afrika Kusini ilitoa uamuzi ulioiunga mkono mnamo mwezi Agosti.

    Lakini familia ya Lungu inataka mazishi ya faragha nchini Afrika Kusini kwani wanasema rais huyo wa zamani hakutaka Hichilema ahudhurie mazishi yake. Uhusiano kati ya wanasiasa hao wawili ulikumbwa na utata kwa muda mrefu.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Marekani inaendela kumuomboleza mtetezi wa haki za kiraia, Jesse Jackson

    .

    Chanzo cha picha, REUTERS/Evelyn Hockstein/File Photo

    Marekani na dunia inaendela kumlilia mwanzilishi wa haki za kiraia wa Marekani, Jesse Jackson, baada ya kifo chake akiwa na umri wa miaka themanini na minne.

    Kumbukumbu nchini Marekani zimeongozwa na rafiki yake wa muda mrefu Barack Obama ambaye alisema alitengeneza fursa kwa vizazi vya raia wa Marekani wenye asili ya Kiafrika.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alisema Jckson aliongeza juhudi za kimataifa ili kuendeleza utu na usawa.

    Mwanawe, Jesse Jackson Junior, amemtaja babake kama shujaa.

    Bw Jackson alikuwa mfuasi wa Martin Luther King, na baadaye akawa mchungaji katika jiji la Chicago ambako kumbukumbu za umma zimepangwa.

    Jackson alikuwa mzungumzaji mahiri na mpatanishi aliyefanikiwa katika mizozo ya kimataifa.

    Alikuwepo kwa nyakati nyingi za matokeo katika vita vya muda mrefu vya haki na usawa katika suala la ubaguzi wa rangi nchini Marekani, pamoja na Martin Luther King Jr. huko Memphis mwaka wa 1968 wakati kiongozi wa haki za kiraia aliuawa.

    Alilia waziwazi katika umati wa watu Obama alipokuwa akisherehekea uchaguzi wake wa urais wa 2008, na alisimama na familia ya George Floyd mnamo mwaka 2021 baada ya mahakama kumpata na hatia afisa wa polisi kwa mauaji ya mtu mweusi ambaye hakuwa na silaha wakati wa kukamatwa.

    Rais wa chama cha Republican, Donald Trump, ambaye ana rekodi ya hali ya juu katika suala la ubaguzi wa rangi ambaye pia amekuwa akikosoa harakati za haki za kiraia, alimsifu Jackson kama mtu mcheshi na mwenye uelewa sana wa masuala ya mitaani na kwa kumsaidia kabla na baada ya kuwa rais wakati Jackson alipigania kuwawezesha Wamarekani weusi.

    “Jesse alikuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa sana wa asili kama wengine wachache waliomtangulia," Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii.

    Kamala Harris, aliyekuwa makamu rais, ambaye alishindwa katika uchaguzi wa 2024 ambao Trump aliibuka na ushindi, alimsifu Jackson kama "mmoja wa wazalendo wakubwa wa Marekani.

    Rais wa zamani Joe Biden, alisema katika taarifa yake kwamba Jackson "aliamini sana kwa wazo kwamba watu wote wameumbwa sawa na wanastahili kutendewa kwa usawa.

    Biden alimkumbuka Jackson kama "mtu ambaye hakuogopi kazi ya kukomboa taifa letu."

  19. Gabon yapiga marufuku mitandao ya kijamii

    .

    Mdhibiti wa vyombo vya habari nchini Gabon ametangaza kufungwa kwa muda kwa mitandao ya kijamii.

    Katika taarifa kwenye televisheni, msemaji Jean-Claude Mendome amesema mitandao inadhoofisha maadili ya umma, uthabiti wa taasisi na usalama wa taifa.

    WhatsApp, Facebook na TikTok ndiyo majukwaa yanayotumika zaidi nchini humo.

    Kwa sasa Gabon ipo katika mabadiliko ya kutoka kwenye mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Brice Oligui Nguema ambaye alishinda uchaguzi wa urais mwaka jana.

    Kukatwa kwa intaneti pia kumetumiwa na serikali zilizopita.

    Soma zaidi:

  20. Rais wa Peru aondolewa madarakani kwa mikutano ya siri

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Nchi ya Peru imejikuta tena kwenye msukosuko wa kisiasa baada ya rais aliyepo madarakani kuondolewa na bunge, akiwa amehudumu kwa miezi minne ya muhula wake.

    Rais wa saba wa Peru katika muongo mmoja, José Jerí, alipigiwa kura na wengi kumuondoa madarakani kutokana na tuhuma za kufanya mikutano isiyojulikana na mfanyabiashara wa China na uteuzi usio wa kawaida wa wanawake kadhaa katika nyadhifa za kiserikali.

    Jeri, mwenye umri wa miaka 39, alikuwa kiongozi mkuu wa Bunge Julai mwaka jana na alikuwa mrithi wa pili baada ya kuondolewa madarakani kwa Boluarte.

    Lakini kipindi chake cha uongozi kilighubikwa haraka na utata. Kilichojulikana zaidi kilikuwa kuhusu mikutano ya siri na mfanyabiashara wa China Zhihua Yang, ambaye anamiliki maduka, mkataba wa nishati na tayari alikuwa chini ya uangalizi wa serikali.

    Jeri alirekodiwa akiwa amevaa fulana yenye kumfunika kichwa alipokuwa akikutana na Yang katika mgahawa wa Kichina, katika kashfa ambayo ilipata jina la "Chifagate," lililotokana na jina la migahawa ya Kichina.

    Jeri aliomba radhi baada ya mkutano huo na kusema kwamba hakuna kosa lililofanyika. Licha ya hayo, hakuweza kupambana na shinikizo la kisiasa linaloongezeka huku uchaguzi ujao wa rais ukikaribia na wanasiasa wakilenga kupata uungwaji mkono miongoni mwa watu waliokuwa wamekusanyika.

    Jeri amekuwa rais wa tatu mfululizo kuondolewa madarakani, baada ya kuchukua nafasi ya kiongozi wa zamani Dina Boluarte ambaye aliondolewa madarakani Oktoba mwaka jana kwa madai ya ufisadi na kuwa na uhusiano na makundi yanayotekeleza uhalifu wa kupangwa

    Bunge litamchagua kiongozi wake mpya leo hii Jumatano, ambaye atakuwa rais wa mpito wa nchi hiyo.

    Pia unaweza kusoma changamoto iliyopo kuongoza taifa hili👇

Trending Now