Kwa nini mazungumzo ya Iran na Marekani ni nyeti

Chanzo cha picha, Getty Images
Iran na Marekani zimeanza mazungumzo mapya nchini Oman katika mazingira yenye mvutano mkubwa wa kisiasa na kijeshi, yakifuatia kipindi kifupi baada ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran. Haya ni mazungumzo ya kwanza ya moja kwa moja tangu kile kilichoitwa "vita vya siku 12," vilivyoibuka baada ya shambulio la Israel dhidi ya Iran na kuibua hofu ya vita vya kikanda.
Mazungumzo haya yanafanyika huku pande zote mbili zikiwa na misimamo mikali. Iran inasisitiza kuwa iko tayari kujadiliana, lakini kwa masharti yake, huku Marekani ikionya kuwa hatua za kijeshi bado zipo mezani endapo mazungumzo yatashindwa. Kauli hizi zimeongeza hali ya sintofahamu kuhusu kama diplomasia itaweza kuzuia mzozo mkubwa zaidi.
Kwa miaka mingi, uhusiano wa Iran na Marekani umekuwa wa mashaka, ukijengwa juu ya kutokuaminiana, vikwazo vya kiuchumi na vitisho vya kijeshi. Mazungumzo ya Oman yanachukuliwa na wachambuzi kama jaribio la kuzuia hali hiyo isigeuke kuwa vita vya wazi.
Lakini kwa mtu asiye karibu na siasa za kimataifa, swali kubwa analoweza kujiuliza je, mazungumzo haya yanahusu nini hasa, kwanini ni nyeti kiasi hiki, na nini kinaweza kutokea baadaye?
Mazungumzo ni kuhusu nini, na kwanini mvutano ni mkubwa kiasi hiki?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiini cha mazungumzo haya ni mpango wa nyuklia wa Iran. Tehran inasema mpango huo ni wa matumizi ya kiraia, kama uzalishaji wa nishati, lakini Marekani na washirika wake wana hofu kuwa Iran inaweza kuutumia kutengeneza silaha za nyuklia.
Marekani inataka Iran isimamishe au ipunguze kwa kiwango kikubwa urutubishaji wa uranium, ikubali ukaguzi mkali wa kimataifa, na irejee kwenye masharti magumu ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015. Iran, kwa upande wake, inataka vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani viondolewe, ikisema vimeathiri uchumi na maisha ya raia wake.
Chanzo kikubwa cha mvutano ni mpango wa makombora ya balistiki wa Iran. Marekani inasisitiza kuwa suala hilo lazima lijadiliwe kwa kuwa makombora hayo yana uwezo wa kubeba silaha nzito. Iran inakataa kabisa, ikisema makombora hayo ni sehemu ya ulinzi wake wa taifa hilo na ni jambo lisiloguswa.
Mvutano huu unaongezwa na vitisho vya kijeshi. Rais Donald Trump ameonya mara kadhaa kuwa Marekani inaweza kutumia nguvu iwapo mazungumzo yatakwama, huku Iran ikisema shambulio lolote dhidi yake litasababisha ijibu vikali, ikiwemo hatua zinazoweza kuvuruga usafirishaji wa mafuta duniani kupitia Mlango wa bahari wa Hormuz.
Nani wanashiriki mazungumzo na kwanini Iran ilitaka yahamishiwe Oman?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Upande wa Iran unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araqchi, mwanadiplomasia mkongwe aliyeshiriki katika mazungumzo ya awali ya nyuklia. Upande wa Marekani unaongozwa na mjumbe maalum wa Rais Trump kwa Mashariki ya Kati, Steve Wittkopf, anayehusika pia katika masuala mengine nyeti ya kidiplomasia.
Awali, mazungumzo haya yalipangwa kufanyika Uturuki, lakini Iran iliomba yahamishiwe Oman. Kwa miaka mingi, Oman imekuwa mpatanishi wa kimya kimya kati ya Tehran na Washington, hasa katika masuala ya nyuklia.
Kwa Iran, Oman ni eneo salama kidiplomasia, linaloeleweka, na lenye historia ya mazungumzo yasiyo na shinikizo kubwa la kisiasa. Tehran pia ilitaka mazungumzo yawe ya pande mbili pekee, bila kuhusisha nchi nyingine za eneo hilo.
Iran ina wasiwasi kuwa kuhusisha nchi nyingi katika mazungumzo hayo ungesababisha ajenda kuongezeka na kujumuisha masuala kama makombora ya balistiki na ushawishi wake wa kikanda, mambo ambayo inayapinga kwa nguvu.
Nini kinaweza kutokea baada ya mazungumzo haya?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wachambuzi wengi wa masuala ya kimataifa hawatarajii mazungumzo haya kuzaa matunda kwa haraka. Badala yake, yanaonekana kuwa jaribio la kupunguza mvutano na kuzuia mzozo wa kijeshi wa moja kwa moja.
Kwa Iran, lengo ni kusogeza muda, kupunguza vitisho vya kijeshi, na kulinda kile inachoona kama haki yake ya kujilinda. Kwa Marekani, ni kujaribu kuzuia Iran kufikia uwezo wa nyuklia wa kijeshi bila kuingia kwenye vita vipya Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, hatari bado ipo. Endapo mazungumzo yatashindikana, vitisho vya kijeshi vinaweza kutekelezwa, hali ambayo itaathiri usalama wa eneo zima na uchumi wa dunia kupitia kupanda kwa bei ya mafuta. Na vitisho hivyo vinaweza kuanzia kwa Rais Donald Trump.
Kwa sasa, mazungumzo ya Oman yanabaki kuwa mstari mwembamba kati ya diplomasia na mzozo ilikiwa ni jaribio la mwisho la mazungumzo kabla ya uwezekano wa hatua kali zaidi.
Imetayarishwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali














