'Hata inyeshe mvua ya makombora tunaendelea kuishi papa hapa' - Wairani

- Author, Ghoncheh Habibiazad
- Nafasi, BBC Persian
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mvua ya theluji ilinyesha katika sehemu za mji wa Tehran siku ya Jumanne usiku, na kufunika mji mkuu wa Iran na safu nyeupe baada ya mashambulizi ya anga kwenye vituo vya mafuta kusababisha siku za anga na mvua nyeusi.
Lakini maisha yanaendelea, hata kama vita bado vinashuhudiwa.
Sahar, mwanamke aliye katika umri wake wa miaka 20, aliambia BBC Kiajemi kwamba alikuwa akitumia siku nyingi kujificha nyumbani kwake huko Tehran, akipika, akisoma, na kucheza mchezo wa video wa simulizi ya maisha.
"Nafkiri ubunifu wangu umeongezeka wakati wa vita. Nina msongo wa mawazo kila mara na kuishia kujenga nyumba nzuri zaidi katika mchezo huu," alisema.
Sahar - ambaye jina lake, kama ilivyo kwa wachangiaji wengine, limebadilishwa kwa sababu za usalama - aligundua Jumanne kwamba mwanamke ambaye alikuwa amesoma naye shuleni ameuawa.
"Mwili wake haujapatikana. Nilihisi vibaya sana baada ya kuusikia taarifa hizo," alisema.
"Kwa nini tunapaswa kupitia hofu kubwa hivi tunapokuwa katika miaka ya ujana wetu? Nataka tu hili liishe kabla ya Nowruz. Siku ninazopenda zaidi maishani ni siku za mwanzo za majira ya kuchipua."
Zimesalia siku chini ya 10 hadi Nowruz, tamasha la Mwaka Mpya wa Kiajemi, ambalo linaashiria kuwasili kwa majira ya kuchipua.
Lakini mwaka huu hilo halijakuwa hivyo, kulingana na wale wanaoishi Tehran.

"Haionekani kama pilkapilka zinazokuwa kipindi cha Nowruz. Lakini hata inyeshe mvua ya makombora, tunaendelea kuishi papa hapa. Hatuna chaguo ila kuishi," alisema Peyman, mwanamume aliye katika umri wa miaka 30.
"Magari hayana watu. Mitaa ni imetulia sana ... ni tulivu kiasi kwamba unaweza kucheza mpira wa miguu katikati ya barabara," aliongeza.
Mwanamume mwingine mwenye umri wa miaka 30 alisema: "Ratiba yangu ya kulala inategemea mabomu sasa. Ninalala karibu saa kumi na mbili au saa moja asubuhi na kuamka saa nane mchana. Wakati mwingine, inanibidi nitoke nje kununua mboga, lakini mji wa Tehran hauna chochote."
Jiji la Tehran na maeneo yaliyo jirani lina idadi ya watu milioni 14, lakini baadhi ya wakazi wameondoka kutafuta usalama kwingineko tangu Marekani na Israel zilipoanza kushambulia Iran tarehe 28 Februari.
Baadhi walielekea kaskazini mwa Bahari ya Caspian, ambapo kumekuwa na mashambulizi machache.

Chanzo cha picha, Reuters
Mina, mwanamke aliye katika umri wa miaka 20, ni mmoja wao. Sasa yuko katika jiji la Rasht.
"Familia yangu iliendelea kusisitiza tuende Rasht kukaa na bibi yangu, lakini rafiki yangu mkubwa na mwenzangu tunayeishi naye hakutaka kuondoka Tehran. Nilihisi kuhukumika kuondoka bila yeye, kwa hivyo sikutaka tuende," anakumbuka.
"Usiku walipofika kwenye hifadhi ya mafuta, nyumba yetu ilikuwa ikitetemeka hadi mlangoni. Madirisha yote yaliangaza kana kwamba ilikuwa asubuhi."
Aliongeza: "Niliendelea kufikiria kwamba ikiwa chochote kitatokea kwa familia yangu, itakuwa kosa langu kusema hatupaswi kwenda Rasht."
"Siku iliyofuata, hatimaye tulienda Rasht, kwa kutumia gari iliyochafuliwa kwa madoa ya mvua."
"Rafiki yangu mkubwa aliamua kukaa Tehran na familia yake, lakini mimi humpigia simu kila siku. Tunazungumza kwa njia ya simu kuhusu mambo yote ya kusisimua tutakayofanya baada ya vita kuisha. Labda tutapaka rangi nywele zetu baada ya haya."

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bado ni vigumu sana kuwasiliana na wale walio ndani ya Iran kutokana na kuminywa kwa intaneti kulikosababishwa na serikali mwanzoni mwa vita, lakini wakazi wenye ujuzi wa teknolojia wamekuwa wakitumia Starlink na kushirikisha wengine intaneti yao.
Mfumo wa intaneti ya setilaiti umekuwa njia muhimu ya mawasiliano kwa baadhi ya watu wanaojaribu kuwasiliana na ulimwengu wa nje. Unafanya kazi kama mlingoti wa simu angani, ukitumia mkusanyiko wa setilaiti kuwasiliana na vyombo vidogo vilivyo ardhini vyenye WiFi.
Kutumia Starlink nchini Iran kuna adhabu ya hadi miaka miwili jela, na inasemekana mamlaka zimekuwa zikitafuta vyombo hivyo ili kuwazuia watu kuunganishwa na intaneti.
Mehran, mwenye umri wa miaka 20 anayeishi Tehran, alisema alikuwa akishirikisha muunganisho wake wa Starlink na takriban watu wengine 25. Aliongeza kuwa alikuwa ameficha kifaa hicho "mahali mbali" ili kuzuia mamlaka "kukipata au kukizuia kisifanye kazi".
Aliongeza kuwa amewaruhusu wapendwa wake kujiunga na huduma hiyo bila malipo, ingawa intaneti inauzwa kwenye programu ya ujumbe ya Telegram kwa takriban $6 (£4.50) kwa GB 1 ya data - bei kubwa katika nchi ambayo wastani wa mshahara wa kila mwezi unakadiriwa kuwa kati ya $200 na $300.

Shima, mwanamke mwenye umri wa miaka 20 huko Tehran ambaye anatumia muunganisho wa Starlink kupata mtandao, alisema: "Lazima uinunue kutoka kwa mtu unayemwamini, vinginevyo kuna uwezekano wa kukata mtandao wako baada ya kulipa kiasi kikubwa cha pesa."
Shirika la ufuatiliaji la NetBlocks lilisema Jumatano kwamba kukatika kwa intaneti nchini Iran kumeingia siku yake ya 12, huku muunganisho bado ukiwa katika 1% tu ya viwango vya kawaida baada ya saa 264.
"Starlink VPN ya gharama kubwa sana niliyonunua kwa ajili ya dharura inachukua muda mrefu kuunganisha, na kunifanya niwe na shaka kama ilikuwa na thamani ya kunifanya nitumia pesa nyingi hivyo," Shima alisema.
"Lakini angalau naweza kuwaambia wapendwa wangu walio nje ya nchi kwamba bado niko hai."














