Trump asema Marekani na Iran zimefanya mazungumzo ya kuahirisha mashambulizi, Iran yakanusha

Wakati huohuo, Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuahirisha mashambulizi ya mitambo ya kuzalisha umeme.

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Usiku mwema.

  2. Meli tatu zafuatiliwa zikivuka Mlango-Bahari wa Hormuz

    d

    Chanzo cha picha, Reuters

    Idadi ya meli za mafuta zinazopita katika Mlango-Bahari wa Hormuz imepungua sana tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran tarehe 28 Februari.

    Idadi kubwa ya meli zinazothubutu kupita licha ya vitisho vya Iran dhidi ya usafirishaji zimezima vifaa vyao vya ufuatiliaji vya AIS ili kuepuka kugunduliwa. Hata hivyo, baadhi zimeendelea kuwasha vifaa hivyo, jambo linaloashiria kuwa na imani zaidi kwamba hazitashambuliwa.

    Leo, meli tatu zilifanya safari hiyo huku vifaa vyao vya ufuatiliaji vikiwa vimewashwa, kulingana na takwimu za Trafiki ya Baharini. Meli hizo zilionekana zikisafiri kwa ukaribu na kuchukua njia isiyotumika sana, karibu zaidi na pwani ya Iran kuliko ilivyo kawaida.

    Meli hizo tatu ni meli za kubeba gesi ya petroli kimiminika zinazomilikiwa na India, Pine Gas na Jag Vasant, pamoja na meli ya kemikali inayomilikiwa na China, Bright Gold.Soma pia:

  3. Spika wa Bunge la Iran akanusha mazungumzo na maafisa wa Marekani

    Mohammad-Bagher Ghalibaf wakati wa mjadala wa TV mnamo 2024

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Mohammad-Bagher Ghalibaf wakati wa mjadala wa TV mnamo 2024

    Katika saa moja iliyopita, vyombo kadhaa vya habari vimeripoti kuwa mjumbe maalum wa Donald Trump, Steve Witkoff, pamoja na Jared Kushner, wamekuwa wakifanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Iran, Mohammad-Bagher Ghalibaf, wakinukuu vyanzo mbalimbali.

    Hata hivyo, sasa akaunti ya X inayohusishwa na Mohammad-Bagher Ghalibaf imetangaza kuwa hakujakuwa na mazungumzo yoyote na Marekani.

    Taarifa hiyo imeongeza kuwa “habari za uongo” zimetumika “kuathiri na kupotosha masoko ya mafuta”, na kwamba wananchi wa Iran “wanataka wahusika wa mashambulizi waadhibiwe kikamilifu na kwa majuto.”

    Soma pia:

  4. Trump aashiria Iran inaweza kukubali kuachana na mpango wa silaha za nyuklia

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani anaashiria kwamba Iran huenda ikakubali kuachana na mipango yake ya kutengeneza silaha za nyuklia badala ya amani.

    “Kesho asubuhi, kwa wakati wao, tulitarajia kulipua mitambo yao mikubwa zaidi ya kuzalisha umeme iliyogharimu zaidi ya dola bilioni 10 kujengwa,” anasema.

    “Ilikuwa bora sana, hakukuwa na ukosefu wa fedha. Kwa shambulio moja tu, ingetoweka. Kwa nini watake hilo litokee?”

    “Hivyo walipiga simu, si mimi niliyepiga. Wao ndio walipiga. Wanataka kufanya makubaliano,” anasema Trump.

    “Nasi tuko tayari kabisa kufanya makubaliano. Lazima yawe makubaliano mazuri, na lazima yahakikishe hakuna vita tena, na hakuna silaha za nyuklia tena.

    “Hawatakuwa tena na silaha za nyuklia. Wanakubali hilo. Bila hilo, hakuna makubaliano,” anaongeza.

    Trump pia anaashiria kuwa bei ya mafuta itashuka kwa kasi kubwa iwapo makubaliano na Iran yatafikiwa.

    Bei ya mafuta imepanda kwa kiasi kikubwa tangu mzozo huo uanze, huku Iran ikitishia meli katika njia kuu ya meli ya Strait of Hormuz.

    Anawaambia waandishi wa habari "tuna nafasi kubwa sana ya makubaliano" lakini anaongeza "hilo halihakikishi chochote; sihakikishii chochote".

    Rais wa Marekani pia anadai nchi hizo mbili zinajadili mambo 15 ya kumaliza vita, na Iran ikitoa silaha za nyuklia kama pointi "namba moja, mbili na tatu". Hata hivyo, Trump anasema anataka kuona "aina mbaya sana ya mabadiliko ya serikali".

    Soma pia:

  5. Makadirio yaonyesha mashambulizi ya Iran yalisababisha hasara ya dola milioni 800 kwa kambi za Marekani

    rr

    Chanzo cha picha, Planet labs PBC and Airbus

    Uchambuzi mpya unaonyesha kuwa mashambulizi ya Iran dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani Mashariki ya Kati yalisababisha hasara ya takribani dola milioni 800 katika wiki mbili za kwanza za vita.

    Kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Tafiti za Mikakati na Masuala ya Kimataifa pamoja na uchambuzi wa BBC, sehemu kubwa ya uharibifu huo ulitokana na mashambulizi ya awali ya kulipiza kisasi ya Iran kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel katika wiki ya kwanza baada ya vita kuanza.

    Kiwango kamili cha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Iran dhidi ya rasilimali za Marekani katika eneo hilo bado hakijabainika wazi.

    Hata hivyo, makadirio ya hasara ya dola milioni 800 kwa miundombinu ya kijeshi ya Marekani, ikiwa ni kubwa kuliko taarifa za awali, yanaonyesha gharama kubwa ambazo Marekani inaweza kubeba kadri mzozo unavyoendelea.

    “Uharibifu wa kambi za Marekani katika eneo hilo haujaripotiwa kikamilifu,” alisema Mark Kansian, mshauri mwandamizi katika Kituo cha Tafiti za Mikakati na Masuala ya Kimataifa na mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo.

    “Ingawa inaonekana uharibifu ni mkubwa, kiwango kamili hakitajulikana hadi taarifa zaidi zitakapowekwa wazi.”

    Soma pia:

  6. Habari za hivi punde, Misri yalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya miundombinu ya Lebanon

    Misri ililaani na kuita mashambulizi ya Israel dhidi ya miundombinu ya Lebanon "adhabu ya pamoja." "Uharibifu wa makusudi wa miundombinu nchini Lebanon unaonyesha sera ya wazi ya Israeli ya adhabu ya pamoja," Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilisema katika taarifa.

    Misri ilikosoa mashambulizi ya Israel "ya utaratibu na ya makusudi", ikiwa ni pamoja na kwenye madaraja ya Mto Litani kusini mwa Lebanon.

    Katika siku za hivi karibuni, picha za video zimechapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari zikionyesha kulengwa kwa madaraja kusini mwa Lebanon.

    Soma pia:

  7. Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran: Hakuna mazungumzo kati ya Iran na Washington

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Maelezo ya picha, Waziri wa Masuala ya kigeni nchini Iran Abbas Araghchi

    Katika kujibu matamshi hayo ya Donald Trump, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kuwa, hakuna mazungumzo kati ya Tehran na Washington.

    Donald Trump amesema saa moja iliyopita kwamba alikuwa na "mazungumzo mazuri sana na yenye kujenga" kuhusu "suluhisho kamili na la mwisho" la vita vya Mashariki ya Kati na Iran.

    Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kuwa, matamshi ya Rais wa Marekani yamo ndani ya fremu ya juhudi za kupunguza bei ya nishati na kupata muda wa kutekeleza mipango yake ya kijeshi.

    Baada ya Rais wa Marekani kusema kwenye mtandao wa kijamii kwamba ameahirisha shambulio lolote kwenye mitambo ya nguvu ya Iran na miundombinu ya nishati kwa siku tano, bei ya mafuta ilishuka sana na masoko ya kifedha yaliona thamani ya hisa ikipanda.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imetaja juhudi za usuluhishi: "Ndiyo, kuna mipango kutoka nchi za kieneo ili kupunguza mivutano, na majibu yetu kwa wote ni wazi: Sisi sio wahusika walioanzisha vita hivi, na maombi yote haya yanapaswa kupelekwa Washington."

    Soma pia:

  8. Trump 'asita' baada ya kusikia tutalenga vituo vyote vya umeme mashariki ya kati - IRGC

    g

    Shirika la Habari la Fars la Iran, ambalo lina uhusiano na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC), limenukuu chanzo cha Iran ambacho hakikutajwa jina kikisema "hakuna mawasiliano ya moja kwa moja au ya moja kwa moja na Trump".

    Chanzo hicho kinasema baada ya "kusikia kwamba malengo yetu yatajumuisha vituo vyote vya umeme katika Asia Magharibi, alirudi nyuma".

    Soma pia:

  9. Wairani waakisi hatua ya Trump ya kuahirisha mashambulizi dhidi ya viwanda vya umeme

    Katika hali ya kuminywa kwa mtandao lililowekwa na serikali ndani ya Iran, baadhi ya watu bado wanapata njia za kutumia intaneti. Wote waliozungumza na BBC wako dhidi ya kilichotokea sasa.

    Mwanaume mwenye umri wa miaka ishirini na kadhaa mjini Tehran ametutumia habari ya uamuzi wa Rais wa Marekani hata kabla haijathibitishwa kwenye akaunti ya Truth Social ya Donald Trump.

    Anajibu uamuzi wa Trumo kwa kusema hivi: “Mwisho wa hili utagharimu sana watu wa Iran, iwe Jamhuri ya Kiislamu itaendelea, au itatambua kuwa ipo katika siku zake za mwisho.”

    Trump “anatufanya wazimu,” anasema mwanamke mwenye umri wa miaka ishirini na kadhaa kutoka mji wa kaskazini mwa Iran.

    “Nimepiga simu kwa rafiki yangu na kucheka. Hii ni maisha gani tunayoyaishi?” anasema mwanaume mwingine mwenye umri wa miaka ishirini na kadhaa kutoka Tehran.

    Wakati huo huo, mwanamke mwingine mwenye umri wa miaka ishirini kutoka Tehran anasema: “Yeye ( Trump) hatabiriki. Sina wazo lolote la nini kitakachotokea.”

    Soma pia:

  10. Kauli ya Trump kuhusu kusitisha vita na Iran yaacha maswali muhimu bila majibu

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ujumbe wa Rais Donald Trump uliotolewa hivi punde ni labda kauli yake ya kupatanisha zaidi tangu kuanza kwa oparesheni inayoitwa ‘Epic Fury’, lakini inaacha maswali bila majibu.

    Ingawa alitaja “mazungumzo mema na yenye tija” na Iran, taarifa hiyo haijathibitishwa na Wairan, na kauli hii inapingana kabisa na kauli kali za uvamizi ambazo pande zinazopigana zilionyesha mwishoni mwa wiki.

    Zaidi ya hayo, haijulikani kwa hakika ni nini hasa mazungumzo haya yalijikita. Mada inaweza kuwa mpango wa Iran wa makombora ya balistiki au upanuzi wa nyuklia, au labda tu kuepusha mapigano, jambo ambalo Trump aliupunguza umuhimu wake Ijumaa iliyopita.

    Pia inaweza kuhusisha mlango-bahari wa Hormuz, ingawa kufungua njia hiyo kwa usafirishaji bado si jambo ambalo Wairani wameahidi hadharani. Wataalamu wengi wanaona hii haiwezekani, kwani udhibiti wa Iran juu ya Hormuz unawapa nguvu kubwa zaidi katika vita.

    Rais wa Marekani kwa sasa yupo Florida, lakini atasafiri kwenda Memphis mapema hii alasiri kutoa hotuba inayolenga juhudi za kupambana na uhalifu.

    Hata hivyo, sehemu kubwa ya dunia itakuwa ikifuatilia kwa makini habari yoyote mpya au maelezo kuhusu mazungumzo haya, na maana yake kwa mustakabali.

    Soma zaidi:

  11. Habari za hivi punde, Trump asema mazungumzo yalifanyika kuhusu 'suluhisho kamili la uhasama' na Iran

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Trump

    Donald Trump anasema kumekuwa na "mazungumzo yenye tija" kuhusu "suluhisho kamili " kwa mzozo wa Mashariki ya Kati.

    Anasema "ataahirisha mashambulizi yoyote dhidi ya mitambo ya nishati ya Iran na miundombinu ya nishati" kwa muda wa siku tano.

    Katika chapisho la TruthSocial lililoandikwa kwa herufi kubwa anasema: "NINAFURAHIA KURIPOTI KWAMBA MAREKANI, NA NCHI YA IRAN, KWA SIKU MBILI ZILIZOPITA, TUMEFANYA MAZUNGUMZO MEMA SANA NA YENYE TIJA KUHUSU USHIRIKIANO NA UTAJIRI KATIKA MASHARIKI YA KATI.

    " KULINGANA NA MAZUNGUMZO HAYA KWA KINA, NA MAZUNGUMZO YENYE KUJENGA, AMBAYO YATAENDELEA WIKI NZIMA, NIMEIAGIZA IDARA YA VITA KUAhirisha MASHAMBULIZI YOYOTE YA KIJESHI DHIDI YA IRAN KWA KIPINDI CHA SIKU TANO, HUKU MAZUNGUMZO YAKIENDELEA .

    AHSANTE RAIS DONALD J. TRUMP"

    Soma pia:

  12. Wamiliki wa magari nchini Kenya waingiwa na wasiwasi kufuatia uhaba wa mafuta

    GDJD

    Chanzo cha picha, AFP

    Uhaba wa mafuta unaendelea kushuhudiwa kote nchini Kenya, huku wamiliki wa magari wakilalamikia kuwekwa kwa viwango vya ununuzi na ugumu wa kupata vituo vyenye mafuta.

    Hali hii inajiri licha ya serikali kuwahakikishia wananchi kuwa akiba ya mafuta ya kitaifa inatosha. Hata hivyo, katika jiji la Nairobi, hususan barabara ya Lang’ata, vituo kadhaa vya mafuta vimeripotiwa kukosa mafuta.

    “Nimezunguka vituo vya mafuta vitano ndipo nimepata mafuta hapa kwa kituo hiki. Ukweli ni kwamba hakuna mafuta,” alisema Marvin Ogeta, dereva wa teksi, akizungumza na vyombo vya habari. Aliongeza kuwa alipata kiasi kidogo cha mafuta katika kituo kimoja kilichopo barabara ya Lang’ata.

    Ripoti zinaonyesha kuwa baadhi ya vituo vina upungufu mkubwa wa petroli, huku dizeli ikiwa ndiyo inayopatikana kwa kiasi fulani.

    ''Usiku wa Alhamisi nilikosa mafuta katika kituo cha mafuta cha springvalley jijini Nairobi na tulikuwa wengi sana, mmiliki wa gari aiambia BBC Swahili.

    Wakati huohuo, hali hiyo imechochewa na shinikizo la soko la kimataifa, likihusishwa na vita vinavyoendelea nchini Iran na tishio la kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz—njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

    Wachambuzi wa sekta ya viwanda wanaonya kuwa gharama za usafirishaji huenda zikaongezeka maradufu, hali itakayoongeza presha kwa uchumi.

    George Omuga, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Biashara la Afrika Mashariki, amesema kuwa vita hivyo vinaweza kuisababishia Kenya hasara ya zaidi ya asilimia 20 ya mauzo yake katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Aidha, sekta ya mauzo ya nje, hususan chai, inaweza kuathirika iwapo wanunuzi wakuu kutoka Iran, Pakistan na mataifa ya Ghuba watapunguza ununuzi wao.

    Katika bandari ya Mombasa, matarajio ya hali kuwa nafuu bado ni madogo.

    Kati ya takriban meli 60 zinazotarajiwa kuwasili ndani ya wiki mbili zijazo, ni meli chache tu zinazobeba bidhaa za mafuta, huku nyingi zikiwa zimebeba mizigo mingine kama kontena, chuma, magari, ngano na mbolea.

    Soma Pia:

  13. Mashambulizi ya Marekani na Israel yaendelea katika maeneo mbalimbali nchini Iran

    f

    Chanzo cha picha, snntv

    Kumekuwa na ripoti nyingi za mashambulizi ya anga katika mji mkuu na miji mingine ya Iran. Picha na ushuhuda wa mashahidi zinaonyesha kuwa baadhi ya mashambulizi hayo yalilenga kumuua mtu mmoja au watu fulani mahsusi, huku pia kukiripotiwa milipuko mikubwa.

    Milipuko imeripotiwa kusini mwa Iran, katika visiwa vya Kharg na Kish.

    Aidha, milipuko kadhaa imesikika mjini Tehran, hasa katika eneo la jeshi la anga.

    Wakati huo huo, Idara ya Mawasiliano ya Jeshi imesema kuwa jeshi la majini limeangamiza “ndege mbili zisizo na rubani za kivita za kujitoa muhanga” za Marekani katika eneo la Bandar Abbas.

    Kwa upande mwingine, Press TV, kituo cha televisheni cha Kiingereza cha shirika la utangazaji la Iran, kimeripoti kuwa ndege ya kivita aina ya F-15 ya Marekani imeanguka nchini Kuwait. Video inayodaiwa kuonyesha tukio hilo pia imesambazwa.

    Soma pia:

  14. Uchumi wa dunia uko katika “tishio kubwa” kutokana na mgogoro wa Mlango-Bahari wa Hormuz: Mkuu wa IEA

    G

    Chanzo cha picha, FatihBiro/X

    Uchumi wa dunia uko katika “tishio kubwa” kufuatia mgogoro wa nishati uliosababishwa na vita vya Mashariki ya Kati, na “hakuna nchi itakayokuwa salama” dhidi ya athari zake, amesema mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA), Fatih Birol, siku ya Jumatatu.

    Akizungumza katika Klabu ya Waandishi wa Habari ya Kitaifa katika mji mkuu wa Australia, Birol alifananisha mgogoro wa sasa wa nishati na ile ya miaka ya 1970 pamoja na athari za uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine mwaka 2022.

    “Kwa hali ilivyo sasa, mgogoro huu ni muunganiko wa migogoro miwili ya mafuta na anguko moja la gesi,” alisema Birol.

    “Uchumi wa dunia unakabiliwa na tishio kubwa sana leo, na ninatumaini kwa dhati kuwa suala hili litapatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.

    “Hakuna nchi itakayoweza kujiepusha na athari za mgogoro huu ikiwa utaendelea katika mwelekeo huu. Hivyo, kunahitajika juhudi za pamoja za kimataifa.”

    Rais wa Marekani, Donald Trump, na Tehran wametoa vitisho vya kujibizana huku vita vikiingia wiki ya nne, ambapo rais huyo wa Marekani anaitaka Jamhuri ya Kiislamu kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz uliokuwa umefungwa, njia muhimu ambayo takribani asilimia 20 ya usafirishaji wa mafuta na gesi duniani hupitia.

    Kuzibwa kwa njia hiyo kumekaribia kusimamisha kabisa usafirishaji wa mafuta kupitia mkondo huo mwembamba wa bahari.

    Bei ya mafuta ilipanda tena mapema Jumatatu, huku mafuta ghafi ya kiwango cha Marekani yakifikia kwa muda mfupi dola 100 kwa pipa.

    Birol aliieleza vyombo vya habari vya Australia kuwa angalau miundombinu 40 ya nishati katika eneo hilo “imeharibiwa vibaya au kwa kiwango kikubwa sana” kutokana na mzozo huo.

    Soma pia:

  15. UN watoa onyo jipya la hali ya hewa huku El Niño ikikaribia

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la hali ya hewa la Umoja wa Mataifa limeonya kwamba hali ya hewa ya Dunia imekosa usawa zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia iliyorekodiwa.

    Shirika la hali ya hewa la Umoja wa Mataifa limeonya kwamba Dunia inapata nishati zaidi ya joto kuliko inavyoweza kuitoa, ikisababishwa na uzalishaji wa gesi zenye joto kama vile kaboni dioksidi.

    "Ukosefu huu wa usawa wa nishati" uliorekodiwa uliipa bahari joto hadi kiwango kipya zaidi mwaka jana na kuendelea kuyeyusha barafu ya sayari yetu.

    Na wanasayansi wanaogopa kwamba awamu ya ongezeko la joto la asili inayoitwa El Niño - inayotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu - inaweza kuleta rekodi zaidi za joto hivi karibuni.

    Kujibu ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alirudia wito wake kwa nchi kuachana na nishati ya visukuku na kutumia nishati mbadala ili "kutoa usalama wa hali ya hewa, usalama wa nishati na usalama wa taifa".

    "Sayari ya Dunia inasukumwa kupita mipaka yake. Kila kiashiria muhimu cha hali ya hewa kinatoa tahadhari," alionya, katika ujumbe uliotumwa kwa njia ya video.

    Miaka 11 iliyopita ilikuwa yenye joto zaidi duniani katika rekodi zilizoanzia mwaka 1850, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) linasema.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Walowezi wa Israeli washambulia Wapalestina katika eneo linalokaliwa

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Walowezi wa Kiyahudi wenye msimamo mkali wamefanya mashambulizi mengi dhidi ya vijiji vya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, na kuchoma moto nyumba, magari na mashamba ya kilimo.

    Vurugu hizo zilianza baada ya kijana mmoja mlowezi - Yehuda Sherman mwenye umri wa miaka 18 - kuuawa siku ya Jumamosi, baada ya kuripotiwa kugongwa na gari lililokuwa likiendeshwa na Mpalestina akiwa kwenye baiskeli yake. Polisi walisema walikuwa wakichunguza kama shambulio hilo lilikuwa la makusudi au la bahati mbaya.

    Kujibu, vikundi vya WhatsApp vilivyotumiwa na walowezi vilitoa wito wa "kampeni ya kulipiza kisasi" kutokana na kifo chake. Zaidi ya mashambulizi 20 ya walowezi yaliripotiwa usiku kucha, kulingana na afisa wa ulinzi aliyenukuliwa na vyombo vya habari vya Israeli.

    Vurugu za walowezi zimeongezeka tangu Marekani na Israeli ziliposhambulia Iran, huku Wapalestina sita wakiuawa na walowezi tangu Machi 1, kulingana na Umoja wa Mataifa (UN).

    Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) lilisema katika taarifa kwamba wanajeshi wake na vitengo vya polisi wa mpakani vilitumwa katika vijiji kadhaa vya Wapalestina Jumamosi usiku, baada ya kupokea ripoti za raia wa Israeli "kufanya vitendo vya uchomaji moto dhidi ya miundo na mali, pamoja na kushiriki katika vurugu katika eneo hilo".

    Vijiji vya Jalud, Qaryut, al-Funduqmiya na Silat al-Dhah vilikuwa miongoni mwa vilivyolengwa.

    Video zilizosambazwa mtandaoni, ambazo BBC haikuweza kuzithibitisha kwa uhuru, zilionekana kuonyesha zaidi ya watu 90 wakiwa wamevaa nguo nyeusi - wengi wao wakiwa wamevaa barakoa - wakimkabili Jalud.

    Soma zaidi:

  17. Siku ya ukomo ya Trump kwa Iran kufungua Mlango-Bahari wa Hormuz inakaribia

    .

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Tuko karibu saa 24 kabla saa ya siku ya ukomo iliyowekwa na Rais wa Marekani Donald Trump kwa Iran kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz - mojawapo ya njia za usafirishaji wa mafuta zenye shughuli nyingi zaidi duniani.

    Trump jana alichapisha kwenye jukwaa lake la Truth Social akisema Marekani "itaangamiza" mitambo ya umeme ya Iran ikiwa haitafungua tena njia ya meli kupita baharini bila masharti.

    Trump alichapisha ujumbe saa 23:44 GMT mnamo Machi 21. Hiyo ina maana kwamba Iran ina hadi saa 23:44 GMT mnamo Machi 23 (03:14 kwa saa za Tehran ikiwa ni Machi 24), kufungua Mlango-Bahari.

    Tangu wakati huo, Tehran imesema italenga maeneo ya mafuta yanayohusishwa na Marekani katika eneo la Ghuba ikiwa ingekuwa imeshambuliwa.

    Wamarekani wahimizwa kuwa waangalifu zaidi 'duniani kote'

    Wakati huohuo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa tahadhari mpya kwa Wamarekani kote ulimwenguni kutokana na mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati.

    Akiandika kwenye mtandao wa X, idara hiyo inawataka Wamarekani "ulimwenguni kote, na haswa Mashariki ya Kati, kuwa waangalifu zaidi".

    "Kufungwa kwa anga za mara kwa mara kunaweza kusababisha usumbufu wa usafiri. Vituo vya kidiplomasia vya Marekani, ikiwa ni pamoja na nje ya Mashariki ya Kati, vimelengwa," inasema.

    "Makundi yanayounga mkono Iran yanaweza kulenga maslahi mengine ya Marekani nje ya nchi au maeneo yanayohusiana na Marekani na/au Wamarekani kote ulimwenguni."

    Soma zaidi:

  18. Wakenya wanaopigana vita kwa niaba ya Urusi dhidi ya Ukraine kusamehewa

    .

    Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images

    Raia wa Kenya waliojiunga kupigana vita kwa niaba ya Urusi dhidi ya Ukraine watapewa msamaha watakaporejea nyumbani,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi.

    Tangazo hilo linafuatia ziara ya hivi karibuni ya Mudavadi mjini Moscow, ambapo alijadiliana kuhusu suala hilo na kukubaliana kuwa hakutakuwa na ajira zaidi za Wakenya kwenda Urusi kwa ajili ya kupigana vita.

    Kwa mujibu wa sheria za Kenya, ni kinyume cha sheria kwa raia wake kujiunga na majeshi ya kigeni, kosa ambalo linaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka 10 jela.

    Wizara ya Mambo ya Nje inakadiria kuwa Wakenya 252 wamesajiliwa kinyume cha sheria kupigana mstari wa mbele hali iliyoanza takriban miezi sita iliyopita na pia kuwahusisha Waafrika kutoka nchi nyingine.

    Baadhi ya Wakenya wamesema walidanganywa kwa ahadi za kazi za kiraia zenye mishahara mizuri, lakini walipoenda wakajikuta wanalazimishwa kupigana katika vita nchini Ukraine, mara nyingi wakisaini mikataba kwa lugha ya Kirusi bila kuielewa.

    Mudavadi alisema kuwa hadi sasa:

    • Wakenya 44 wamerudishwa salama nyumbani

    • 11 wanaripotiwa kupotea au kufariki vitani

    • 38 wamelazwa hospitalini Urusi chini ya uangalizi maalum

    • Wengine 160 bado wako vitani

    Aidha, alifanikiwa kufikia makubaliano kwamba Wakenya walioko mstari wa mbele ambao hawataki kuendelea na vita wanaweza kujiondoa na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

    Urusi pia imekubali kuiweka Kenya kwenye orodha maalum ya kuzuia usajili mpya wa raia wake.

    Hapo awali, Urusi imesisitiza kuwa wapiganaji wote wa kigeni walijiunga kwa hiari na kwa kufuata sheria za nchi hiyo.

    Serikali ya Kenya na Urusi sasa zitashirikiana kukabiliana na biashara haramu ya binadamu, usafirishaji haramu na usajili usio halali unaohusiana na operesheni ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine.

    Ziara ya Mudavadi ilifuatia shinikizo kutoka kwa familia za Wakenya waliokwenda Urusi wakitaka serikali ichukue hatua.

    Mwezi uliopita, serikali ya Kenya ilifunga zaidi ya mashirika 600 ya uajiri yaliyotuhumiwa kuwadanganya watu kwa ahadi za kazi nje ya nchi.

    Ripoti ya kijasusi ya Ukraine inaonyesha kuwa zaidi ya watu 1,700 kutoka nchi 36 za Afrika wamesajiliwa kupigana kwa niaba ya Urusi.

    Soma zaidi:

  19. 'Vitisho vinaimarisha umoja wetu' - Rais wa Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema kwamba vitisho vya Marekani dhidi ya Iran vinaonyesha "kukata tamaa," kupitia mtandao wa X,

    Aliandika: "Dhana ya kujidanganya kutaka kuiondoa Iran kutoka kwenye ramani inaonyesha kukata tamaa dhidi ya mapenzi ya taifa linalotengeneza historia.

    "Vitisho na ugaidi huimarisha umoja wetu tu. Mlango-Bahari wa Hormuz uko wazi kwa wote isipokuwa wale wanaokiuka nchi yetu. Tunakabiliana vikali na vitisho vya kipuuzi kwenye uwanja wa vita."

    Uhasama katika eneo hilo umeongezeka tangu mashambulizi ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran yalipoanza Februari 28, huku Iran ikilipiza kisasi kwa mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani na makombora yanayolenga Israel na nchi za Ghuba zinazohifadhi mali za kijeshi za Marekani.

    Siku ya Jumamosi, Rais wa Marekani Donald Trump alitishia "kuangamiza" mitambo ya umeme ya Iran, kuanzia na mikubwa zaidi, ikiwa Iran haitafungua Mlango-Bahari wa Hormuz ndani ya saa 48.

    "Ikiwa Iran haitafungua kabisa, bila tishio, Mlango-Bahari wa Hormuz, ndani ya saa 48 kuanzia wakati huu, Marekani itashambulia na kuangamiza mitambo yao mbalimbali ya umeme, ikianza na ule mkubwa zaidi kwanza," Trump aliandika kwenye jukwaa lake la mitandao ya kijamii la Truth Social.

    Soma zaidi:

  20. Starmer na Trump wajadili umuhimu wa kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri Mkuu Sir Keir Starmer na Rais wa Marekani Donald Trump wamejadili kwa njia ya simu umuhimu wa kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz katika mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati.

    Msongamano wa meli kupitia njia hiyo - mojawapo ya njia zenye shughuli nyingi zaidi za meli duniani - umepungua kwa takriban 95% tangu vita vya Iran vianze tarehe 28 mwezi Februari.

    Msemaji wa serikali ya Uingereza alisema viongozi hao "walikubaliana kwamba kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz ilikuwa muhimu ili kuhakikisha utulivu katika soko la mafuta duniani" wakati wa mazungumzo siku ya Jumapili jioni.

    Haya yanajiri huku Sir Keir akitarajiwa kuongoza mkutano wa Baraza la Mawaziri, ambao utahudhuriwa na gavana wa Benki Kuu ya Uingereza Andrew Bailey siku ya Jumatatu, kujadili athari za vita hivyo kwa gharama ya maisha.

    Msemaji wa Uingereza alisema Sir Keir na Trump "wamekubaliana kuzungumza tena hivi karibuni".

    Iran imefanikiwa kufunga mlango-bahari huo tangu Marekani na Israel ziliposhambulia nchi hiyo tarehe 28 Februari.

    Takriban 20% ya mafuta na gesi asilia duniani kwa kawaida hupitia njia hiyo, na bei za mafuta duniani zimepanda kutokana na vita, huku mafuta ghafi yakipanda kwa 45% hadi $106 kwa pipa.

    Soma zaidi:

Trending Now