Vita vya Iran vimeleta mgogoro wa nishati duniani, je, China inaweza kustahimili?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

China imekuwa ikijiandaa kwa muda mrefu kwa mgogoro unaoweza kuathiri usambazaji wa mafuta kutoka mataifa ya Ghuba, lakini kufungwa kwa mlango wa bahari wa Hormuz kunaiathiri China

Usafirishaji wa mafuta kutoka Mashariki ya Kati umesitishwa kufuatia vitisho vya Iran vya kushambulia meli zinazopita kwenye njia hiyo muhimu ya bahari baada ya kushambulio na Marekani na Israel.

Mgogoro huu umesababisha uhaba wa mafuta duniani na kuathiri vibaya nchi za bara Asia zinazotegemea mafuta kutoka mataifa ya Ghuba .

Ufilipino imeamuru watu kufanya kazi siku nne pekee ili kuokoa mafuta na akiba iliyosalia.

China, ambayo ndiye mnunuzi mkubwa zaidi wa mafuta duniani, pia inahisi athari hiyo.

Mtandao wa nishati wa China

Uchumi wa dunia umeathirika pakubwa tangu Marekani na Israel kuishambulia Iran mwishoni mwa mwezi Februari.

Tangu wakati huo, bei za mafuta zimepanda hadi karibu dola 120 kwa pipa.

Takriban robo moja ya mafuta duniani hupitia kwenye mlango wa bahari wa Hormuz hii ikiwa zaidi ya mamilioni 20 ya mapipa kila siku, kulingana na makadirio ya Usimamizi wa Taarifa za Nishati ya Marekani (EIA).

Uhaba wa mafuta umefanya mataifa mbalimbali kutafuta wauzaji mbadala, huku mataifa mengine yakitumia akiba waliyonayo.

Kama mtumiaji mkubwa wa pili wa mafuta duniani baada ya Marekani, China inatumia takriban mapipa milioni 15 hadi 16 za mafuta kila siku.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Sehemu kubwa ya mafuta ghafi yanayoingia nchini China yanatoka Iran na Mashariki ya Kati kupitia Bahari ya China Kusini, yanatumika kuendesha viwanda na usafirishaji, hasa kusini mwa China.

Hata hivyo, kaskazini mwa nchi hiyo inategemea zaidi mafuta yanayozalishwa ndani ya nchi.

Mara nyingi mataifa ya bara Asia yamekuwa yakitegemea sana mafuta kutoka nchi za Ghuba, huku Urusi ikichangia takriban robo moja ya mafuta yanayotumika China. Hii inafanya Moscow kuwa muuzaji mkubwa wa mafuta kwa Beijing, licha ya vikwazo vya Marekani na Ulaya.

Makaa ya mawe pia ni chanzo kikuu cha umeme kwa sehemu kubwa ya China, na yanapatikana kwa wingi nchini humo.

China ni mzalishaji mkubwa zaidi wa makaa ya mawe duniani.

Kujiandaa kwa siku za hatari

Beijing imekuwa ikitumia faida ya bei ya chini ya mafuta ghafi wanayonunua kutoka nchi za Ghuba na kujijengea moja ya akiba kubwa zaidi ya mafuta duniani, anasema Ole Hansen, mkuu wa mkakati katika Benki ya Saxo.

Mwezi wa Januari na Februari mwaka huu, Beijing ilinunua mafuta ghafi zaidi kwa 16% ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita, kulingana na mamlaka yake ya forodha.

Iran, ambayo mafuta yake yamewekewa vikwazo na Marekani, imekuwa muuzaji mkubwa wa mafuta ghafi ya bei nafuu kwa China, na ripoti zinaashiria kwamba Beijing inununua zaidi ya 80% ya mauzo ya mafuta ya Iran.

Data ya ufuatiliaji wa meli tangu vita vya Iran vianze inaonyesha kwamba baadhi ya mafuta haya bado yanafika China ingawa si kwa kiwango kikubwa.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kujitegemea kwa China

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

China imekuwa ikitumia nishati safi kwa wingi.

Upepo, nyuklia, jua na umeme wa maji vinaunda zaidi ya theluthi moja ya umeme wa China, hii ni kulingana na idara ya takwimu ya taifa hilo.

Kutokana na juhudi za China za kuzalisha nishati mbadala, mafuta ghafi yanachangia takriban robo moja tu ya matumizi yote ya nishati ya China.

Mtafiti wa uchumi wa nishati, Roger Fouquet, anasema kwamba China kuwekeza katika nishati mbadala si tu hatua ya kulinda mazingira, bali pia imeisaidia taifa hilo kulinda uchumi wake kutokana na hatari za kimataifa kama zile zinazotokana na mgogoro wa Iran.

"Kwa kiwango fulani, China ina bahati katika miaka 25 iliyopita ilianza kuwekeza katika nishati mbadala na sasa inavuna faida zake," alisema.

Gari za umeme, ambazo zinachangia angalau theluthi moja ya magari mapya yanayouzwa China, pia zimeisaidia uchumi wa nchi hiyo kutokuwa tegemezi sana kwa mafuta.

Hii si kusema kwamba uchumi wa China hauwezi kuathiriwa na mshtuko wa uhaba wa mafuta.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula