Nepal yamuapisha aliyekuwa rapa kuwa Waziri Mkuu mpya

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Unayakumbuka maandamano ya vijana wa Gen Z ya mwaka jana nchini Nepal, ambayo yaliiangusha serikali iliyolaumiwa kwa rushwa, ubadhirifu na upendeleo?
Kilele cha azma ya vijana wa Nepal kimefikiwa Ijumaa ambapo baada ya uchaguzi wa kwanza toka maandamano hayo Waziri Mkuu mpya wan chi hiyo amaeapishwa na kuchukua hatamu za uongozi.
Mwanamuziki maaraufu wa rap (Rapa) ambaye sasa amejitosa kwenye siasa Balendra Shah ndiye aliyeapishwa kuwa Waziri Mkuu wa Nepal baada ya ushindi wake wa kishindo.
Shah ana umri wa miaka 35 na ushindi wake unaashiria mabadiliko muhimu katika siasa za Nepal. Ahadi yake ya mabadiliko iligusa wapiga kura wengi waliokuwa na hasira na ufisadi, upendeleo na utawala wa mabwanyenye wachache.
Wakati akijiandaa kuingia mamlakani, Shah, maarufu kwa jina la kisanii la Balen, alitoa wimbo uliojaa matumaini kuhusu mustakabali mpya wa Nepal.
"Wanepali wasiogawanyika, sasa historia inaandikwa upya," alirap katika wimbo ambao ulitazamwa na watu zaidi ya milioni mbili ndani ya saa moja baada ya kutolewa.
Wimbo huu unamrejesha kwenye mizizi yake katika zama zake za uanagenzi (underground) katika muziki wa rap, ambapo alitumia kipaza sauti kukemea ufisadi na matatizo mengine ya kijamii nchini Nepal.
Lakini hii si mara yake ya kwanza kushika wadhifa wa kisiasa. Baada ya miaka mitatu tu kama meya wa mji mkuu Kathmandu, Shah aliungana na chama cha siasa cha Rastriya Swatantra Party (RSP) kupeperusha bendera ya mgombea wa uwaziri mkuu, na kupata ushindi mnono katika uchaguzi mkuu mwezi huu.
Wafuasi wake wanamwona kama ishara ya mabadiliko na mwokozi kutoka kwenye madhila ya utawala uliong'olewa madarakani. Lakini wengine wanahoji kama chama chake cha RSP chenye minne tu toka kianzishwe uwezo wa kutekeleza ahadi zake za uchaguzi.
Kiongozi mpya wa Nepal ni nani?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Shah alizaliwa mwaka 1990, na ni mhandisi kitaaluma ambaye amesoma vyuo vikuu nchini Nepal na India. Ana mke na mtoto mmoja wa kike.
Alipata umaarufu mwaka 2013 baada ya kupata ushindi katika mashindano makubwa ya rap nchini humo. Mashairi yake yalikuwa mwiba mkali kwa serikali yakibeba hasira za vijana ambao walihisi kukandamizwa na kusahauliwa kabisa na watawala.
Baada ya hapo aliendelea kutoa vibao mbalimbali ambavyo vilipata umaarufu kwa kukemea ufisadi na unyonyaji wa kimatabaka katika taifa hilo linalopatikana kwenye safu za milima ya Himalaya.
Moja ya vibao vyake vilivotikisa zaidi, kiitwacho Balidan (ikimaanisha kafara), kimetazamwa na watu milioni 14 katika mtandao wa YouTube.
Mwaka 2022, akiwaa mwanasiasa mpya alishinda kinyang'anyiro cha umeya wa Kathmandu kwa kishindo kama mgombea huru, akivigaragaza vyama vikongwe ambavyo vilikuwa na uzoefu wa kisiasa na harakati za uchaguzi kwa miongo kadhaa.
Akiwa meya wa jiji, uongozi wake ulitawaliwa na juhudi za kusafisha jiji, kuhifadhi urithi wa asili, na kupambana na ufisadi. Pia alianza kampeni yenye utata ya kuvunja majengo yaliyojengwa bila vibali - ambayo ilisaidia kupunguza msongamano wa magari lakini pia ilikosolewa na wachuuzi wa mitaani na watu walioishi katika makazi yasiyo rasmi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ujumbe wa Shah uliendelea kuwagusa vijana wa nchi hiyo wakati wa maandamano ya Septemba mwaka jana, ambapo watu 77 waliuawa - wengi wao wakiwa waandamanaji waliopigwa risasi na polisi. Machafuko hayo yalisababishwa na kupigwa marufuku kwa mitandao ya kijamii lakini yakachochewa zaidi na hasira dhidi ya ufisadi, ukosefu wa ajira na kudorora kwa uchumi.
Waandamanaji waliufanya wimbo wake Nepal Haseko - ambao unamaanisha Nepal Inayotabasamu - kama moja ya nyimbo zao rasmi za maandamano.
"Nataka kuona Nepal ikitabasamu, nataka kuona mioyo ya Wanepali ikisakata densi. Nataka kuona Nepal ikitabasamu, nataka kuwaona Wanepali wakiishi kwa furaha," mashairi yake yalichezwa mitaani na ndani ya nyumba kwa wiki zote za maandamano.
Shah aliendesha kampeni zake katika mtindo usio wa kawaida, ikiwemo kuepuka mahojiano na vyombo vya habari.
Wakosoaji wake wanasema mkakati huu umemruhusu kuepuka kuchunguzwa na kuhojiwa hadharani kwa rekodi yake ya kisiasa.
Shah alichagua kuzungumza na wapiga kura kupitia mitandao ya kijamii ambapo aliahidi kupambana na ufisadi, kuleta mageuzi ya mhimili wa mahakama, na kuunda ajira mpya milioni 1.2, miongoni mwa mambo mengine.
Mwisho wa siku, mkakati ukafanikiwa na kukipatia chama cha RSP ushindi wa kishindo.
Changamoto na utata
Ushindi wa kishindo haumaanishi kila kitu kipo sawa kwa Waziri Mkuu Balendra Shah.
Akiwa meya alikosolewa na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa kutumia nguvu kubwa ya polisi dhidi ya wachuuzi wa barabarani, katika harakati za kusafisha jiji na kupambana na biashara zisizo na leseni. Timu ya kampeni ya Shah haikujibu ombi la BBC la kutoa maoni juu ya jambo hilo.
Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch ni mojawapo ya makundi yaliyoibua wasiwasi huo na kuiambia BBC kuwa ni aina ya tabia ambayo mara nyingi wameiona kwa viongozi wapya wanaotaka kuleta matokeo ya haraka.
"Tunatumai sasa akiwa Waziri Mkuu, kutakuwa na mkazo katika utaratibu wa uongozi unaozingatia sheria zaidi," alisema Meenakshi Ganguly, naibu mkurugenzi wa Human Rights Watch kanda ya Asia.
Shah pia amezua mijadala kwenye mitandao ya kijamii. Novemba mwaka jana, alichapisha andiko lililojaa maneno ya kuchukiza kwenye mtandao wa Facebook ambalo lilitaja Marekani, India, China na vyama kadhaa vya kisiasa vya Nepali, kikiwemo na RSP, ambacho alijiunga nacho Januari mwaka huu. Hatahivyo alilifuta andiko lake muda mfupi baada ya kulichapisha.
Muhimu zaidi, Shah na viongozi wa chama chake watalazimika kukabiliana na matarajio makubwa kutoka kwa wapiga kura wenye njaa ya mabadiliko, pamoja na changamoto nyengine nyingi.
![Mchwa wakubwa wa Afrika wanaokusanya nafaka, wanaoonekana hapa nchini Kenya , wanapendwa na wakusanyaji] kote duniani.](https://ichef.bbci.co.uk/ace/ws/660/cpsprodpb/7761/live/aa82d2e0-2a1b-11f1-b297-95b0a0a8331e.jpg.webp)













