Kwanini Iran inatoza ushuru meli kupita Mlango- Bahari wa Hormuz?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Asha Juma
- Nafasi, BBC Nairobi
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Mzozo wa Marekani na Israel dhidi ya Iran ulioanza 28, Februari, 2026 bado unaendelea huku miongoni mwa yaliyotokea hivi karibuni ikiwa ni pamoja na Iran kufunga Mlango- Bahari wa Hormuz na baadhi ya meli zikitozwa ushuru ili kupita kwenye njia muhimu ya usafirishaji huku Washington na Tehran zikitoa taarifa zinazokinzana.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa mazungumzo na Iran yanaendelea vizuri licha ya Tehran kukanusha hatua hiyo, pia imejitayarisha kufanya mashambulizi makubwa ikiwa Iran itakataa kufikia makubaliano. Marekani inataka Iran iachane na mpango wake wa makombora, silaha za nyuklia na ifungue Mlango – Bahari wa Hormuz.
Iran, imefunga Mlango- Bahari wa Hormuz na kusema kuwa mpango wa kusitisha vita wa Marekani haukubaliki na kutaka ilipwe fidia. Pia, imeendeleza mashambulizi dhidi ya mataifa ya Ghuba, na kujibu mashambulizi dhidi ya miundombinu yake.
Nchi zote zimeonyesha misimamo yake na kuendelea kupimana nguvu kiasi hiki kunaleta athari gani?
Iran inafanya nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kwamba njia ya Mlango-Bahari wa Hormuz imefungwa na yoyote atakayepita atakabiliwa na "hatua kali", kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Iran ilisema usafirishaji wa "kwenda na kutoka bandari za washirika na wafuasi wa "maadui" wao, Israeli na Marekani" ni marufuku kupita katika njia ya Hormuz.
Lakini kabla ya hatua hiyo, wiki hii Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisema "meli ambazo si za adui" zitaruhusiwa kupitia mradi utaratibu uwe chini ya mamlaka ya Iran.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sio meli zote zinazotozwa ushuru, na Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilisema limeonya meli tatu ikiwa ni pamoja na mbili kutoka kampuni ya China kutopita katika Mlango-Bahari wa Hormuz, kulingana na takwimu za ufuatiliaji wa meli iliyoonekana na shirika la habari la Reuters.
Wabunge wa Iran wametoa taarifa wakisema kuwa imeanza kutoza ada meli zinazopita kwenye njia ya Hormuz.
Mbunge wa Iran Alaeddin Boroujerdi alisema meli zinatozwa dola milioni 2 akitaja hatua hiyo kuwa "mfumo mpya wa kujitawala" kwasababu ya athari za vita.
Meli mbili zilizokuwa zinapita njia ya Hormuz zimetozwa ada hiyo ili kupita salama, kulingana na Lloyd's List na Bloomberg.
Boroujerdi aliongeza kuwa Iran inatumia ada inayotoza kama mkakati wake wa kivita.
"Kwa sababu vita vina gharama, lazima tuchukue ada za usafiri," Boroujerdi alisema.
Hii iliweka wazi kuwa Iran inahitaji pesa hizi kuanza kujikusanya tena wakati ambapo vita vya Marekani na Israel vimeharibu pakubwa nchi yake.
Chini ya mfumo uliopewa jina "toll booth", Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limeanzisha ukanda inaoudhibiti, hasa kaskazini mwa Kisiwa cha Larak, meli za mataifa "rafiki" zinaruhusiwa kupita mradi zipitie mchakato wa ukaguzi mkali.
Iran inatoza ada kwa makusudi ya kujiinua na kujiimarisha tena wakati mvutano na Marekani na Israeli unaendelea kuongezeka.
Kulingana na kile kinachoendelea, Iran inajaribu kuanzisha mfumo utakaoiwezesha kudhibiti njia ya Hormuz hatua ambayo huenda ikatekelezwa hata baada ya vita.
Kinachoonyesha dalili ya hilo ni wabunge wa Iran kuanza kutunga sheria ya kuanzisha utozaji ushuru katika njia ya usafirishaji meli ya Hormuz.
Bunge la Iran linafanyia kazi rasimu ya muswada utakaotoza ada kwa meli zinazotaka kupita salama kwenye Mlango wa Bahari wa Hormuz, kulingana na shirika rasmi wa habari la Fars.
Fars, akimnukuu mbunge ambaye hakutajwa jina, na kusema mpango huo utakamilika hivi karibuni, na utatambua kisheria usimamizi wa Iran wa Hormuz.
Kwa nini Iran inafanya hivi?
Iran imefunga Mlango Bahari wa Hormuz na kurejesha baadhi ya meli zilizokuwa zinataka kupita kwenye njia hiyo huku zingine zikitozwa ushuru mkubwa ili kuruhusiwa kupita.
Sababu ambazo zimechochea Iran kufikia hatua hii ya kimkakati inajumuisha shinikizo la kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kadhalika kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi yake.
Kujiongezea ushawishi katika vita

Chanzo cha picha, Gallo Images via Getty Images
Iran inatumia Mlango- Bahari wa Hormuz; njia muhimu ya usafirishaji mafuta duniani kama silaha yake kubwa dhidi ya Marekani na Israel.
Hatua hii inaiweka katika nafasi ya kujiongezea ushawishi licha ya kwamba imeshambuliwa kwa pamoja na Marekani na Israel na kuachwa na makovu kama majeraha yenyewe yatawahi kupona.
Kwa kufanya hivi, Iran inatoa shinikizo kwa dunia isikilize matakwa yake badala ya kupuuzwa na kufanywa kama tambara bovu lisilo na thamani macho pao.
Iran ifikie hatua ya kuchukua uamuzi huu, bila shaka inajiamini na pengine kushikilia kuwa iko katika msimamo muafaka wa mazungumzo badala ya kukata tamaa na kijisalimisha kwa "maadui zake."
Vile vile, Iran pia imeamua kuonyesha wazi misuli yake na kukataa hadharani kuwa kuna mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani pamoja na kupiga chini mpango wa kumaliza vita uliopendekezwa na Marekani kupitia washirika.
Inatumia Hormuz kama njia ya kimkakati
Ikiwa mwanzoni dunia ilikuwa inachukulia Mlango- Bahari wa Hormuz kama kitu cha vivi hivyi tu, leo huenda washika dau muhimu wanaotumia njia hiyo mara kwa mara wanajiuliza maswali yasiokuwa na majibu.
Imejitokea wazi kuwa njia ya Hormuz ni silaha muhimu sana yenye nguvu kijiografia ambayo wanaweza kuitumia kisiasa.
Ndani ya saa chache baada ya Iran kutoa onyo kwa meli zenye ushirika na "adui" kuwa hazitoruhusiwa kupita njia ya Hormuz na ole wake kwa atakayekiuka agizo hilo, meli nyingi zimekataa kupita ama kubadilisha mkondo huku bei ya mafuta ikapanda hadi zaidi ya $100 kwa pipa.
Washirika wa Marekani na Israel wamehisi uchungu wa mshale uliokuwa unadungwa Iran na kufanikiwa kuendelea kutikisa dunia, ingawa hili haijulikani litaendelea kwa muda gani.
Hii imeipa Iran sauti mpya na kuonyesha kwamba pia nayo ina uwezo wa kuyumbisha dunia bila kutumia silaha kama bomu.
Inalipiza kisasi mapigo ya Marekani na Israel

Chanzo cha picha, Chip Hires via Getty Images
Hatua ambazo Iran imechukua kufikia sasa zinaonekana kujibu shinikizo la kijeshi la upande wa "adui".
Tangu kuanza kwa mapigano, mbele ya macho ya wengi, Iran imeonekana kupata pigo kubwa hasa baada ya kupoteza viongozi wa ngazi ya juu zaidi ya 20 na kuhofiwa kuwa huenda ombwe hilo likasababisha mzozo wa ndani wa utawala.
Bei ya mafuta imekuwa ikipanda na kusababisha mgogoro wa kiuchumi hata baada ya washirika wa nchi 32 wanachama wa Shirika la Kimataifa la Nishati Duniani kukubali kutoa mapipa milioni 400-412 ya mafuta kutoka kwa hifadhi za kimkakati, ikiwa kiwango cha juu zaidi zaidi kuwahi kutolewa katika historia. Hii inaonyesha wazi kuwa huenda Rais Donald Trump alikadiria kimakosa athari za vita anavyoanzisha.
Baada ya Iran kutoa onyo kwa yeyote atakayepita kwenye njia muhimu ya usafirishaji ya Hormuz bila utaratibu wao, nchi nyingine zimeitikia tena kwa haraka. Kuna wale ambao wameamua kutoa ada wanayotozwa huku wengine wakibadilisha njia na hii kwa kiasi fulani imefanikiwa kuonyesha udhaifu uliopo kwenye mkakati wa mashambulizi ya Trump dhidi Iran huku Tehran ikiitumia kama njia ya kuongeza mgogoro bila kutumia silaha moja kwa moja.
Njia ya kutafuta fedha
Kudhibiti njia ya Hormuz kunafanya Iran kupata chanzo cha mapato na mamlaka. Kwa sasa Iran inahitaji vyanzo vya kujipatia mapato zaidi ya wakati mwingine wowote ili kuanza kujikwamua taratibu kutokana na athari za vita na uwezekano wa kutoza ushuru meli zinazopita njia ya Hormuz. Na kama nilivyosema awali, iwapo njia hii itafanikiwa huenda hatua hii ikaendelezwa hata baada ya vita.
Bunge la Iran ilko mbioni kupitisha sheria ambayo itahalalisha hatua hiyo na kuanza kutekelezwa mara moja.
Athari zake

Chanzo cha picha, Getty Images
Hatua iliyochukuliwa na Iran kufunga Mlango- Bahari wa Hormuz na kuanza kutoza ada, tayari imelazimisha meli kubadilisha mkondo wa usafiri na kutafuta njia ndefu mbadala pengine kwa kuhofia vitisho vya Iran hasa ukizingatia kuwa ni yenyewe pekee yenye kuamua nani ni mshirika wa "adui" au la.
Matokeo yake ni kuongezeka kwa gharama za usafiri kwasababu meli zitachukua muda mrefu kuwa Baharini ikilinganishwa na makadirio ya awali.
Njia ya Hormuz hupitisha takriban asilimia 20 ya mafuta duniani pamoja na gesi asilia lakini vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vimesababisha kupungua kwa uzalishaji wa mafuta. Mfano, Iran imepunguza uzalishaji kwa asilimia 70 huku Saudi Arabia ikifunga kiwanda chake kikubwa cha uzalishaji kutokana na mashambulizi.
Pamoja na hayo ni kuendelea kwa ukosefu wa uthabiti kikanda.
Mashambulizi ya Iran kwa nchi za Ghuba yametikisa sekta ya mafuta huku kukiwa na uwezekano wa uwepo wa wanajeshi kuongezeka kutoka Marekani baada ya kutangaza kuwa inafikiria kupelekwa wanajeshi zaidi wa ardhini nah atua kuchukuliwa iwapo itakataa kufikia makubaliano.
Niliogusia ni kiduchu tu ya athari ambazo zinaendelea kujitokeza duniani kote kutokana na vita.
Kawaida, meli huwa haziitaji ruhusa ya Iran kupita Mlango-Bahari wa Hormuz lakini katika vita ya kuonyeshana ubabe, nyasi ndizo zinazoendelea kuumia.
Kuna baadhi ya nchi ambazo zimelipa ada ya dola milioni 2 ili kuruhusiwa kupita Hormuz. Na pia, meli nyingi zitakuwa na ugumu wa kuamini Iran kwasababu ya kile ambacho kimeshuhudiwa katika nchi za ghuba.
Hii inamaanisha, dunia bado ina safari ndefu kukabiliana na changamoto ambazo sasa zinaathiri waliokuwemo na wasiokuwemo.











