Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Hatima ya kilo 440 za urani iliyorutubishwa ya Iran ni ipi? – Uchambuzi
Tunaanza kwa kuchambua magazeti ya leo na gazeti la Uingereza la Sunday Times lenye makala yenye kichwa cha habari: "Iran ina urani wa kutosha kutengeneza mabomu kadhaa ya nyuklia, inaificha wapi?", iliyoandikwa na Mark Urban.
Urban alihoji mustakabali wa miradi ya nyuklia ya Iran baada ya vita vinavyoendelea kumalizika, akionya kuwa viongozi wapya wa Iran wanaweza kuharakisha kutengeneza silaha za nyuklia, hasa baada ya kuuawa kwa Kiongozi Mkuu Ali Khamenei, aliyewahi kutoa fatwa inayokataza utengenezaji wa silaha hizo kwa misingi ya kidini.
Mwandishi alieleza kuwa Iran kwa miaka mingi imefuata sera ya "utata wa nyuklia"; ikisisitiza haitengenezi silaha za nyuklia, lakini wakati huo huo inaongeza kiwango cha urutubishaji wa urani zaidi ya mahitaji ya matumizi ya kiraia, huku ikikiuka baadhi ya kanuni za kimataifa za ukaguzi wa vituo vyake vya nyuklia.
Alirejelea pia kauli ya mkurugenzi wa ujasusi wa Marekani, Tulsi Gabbard, aliyesema wanajua mahali zilipo kilo 440 za urani iliyoboreshwa hadi asilimia 60.
Mwandishi anaibua kitendawili: Ikiwa Marekani inajua mahali ilipo urani hiyo, kwa nini ichague njia ya kijeshi? Anarejelea kauli za Rais Donald Trump kuhusu msimamo mkali wa Iran na juhudi zake za kuendeleza mpango wake wa nyuklia, akidokeza uwezekano wa kuwepo kwa miundombinu mipya ya siri karibu na kituo cha Natanz.
Aliona kauli za Trump kama ishara kwamba Iran imejenga kituo kipya ndani ya Mlima Bekas karibu na kituo cha Natanz kilichoshambuliwa, na inaendelea na tafiti zinazohusiana na silaha za nyuklia, kwa mujibu wa ujasusi wa Israel.
Mwandishi alibainisha kuwa kama Iran ilivyokataa mpango wa amani wa hoja 15 wa Trump, inaweza pia kupuuza mfumo wa uangalizi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), unaolazimisha kutotumia urani kwa madhumuni ya kijeshi.
Alinukuu onyo la Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi, kuwa hata vituo vya nyuklia vikiharibiwa, Iran inaweza kujenga vingine.
Makala hayo yalionya kuwa kilo 440 za urani iliyorutubishwa sana zinatosha kutengeneza takriban mabomu 10 ya nyuklia, na huenda zimehifadhiwa katika kontena 18 hadi 20 za chuma, kila moja ikiwa na ukubwa wa mtungi wa oksijeni unaotumiwa na wapiga mbizi.
Mwandishi alieleza ''ugumu mkubwa'' wa kujaribu kudhibiti hifadhi hiyo, akibainisha kuwa ingawa Marekani ina vikosi maalum, uwepo wa urani huo ndani kabisa ya Iran unafanya operesheni kuwa hatari sana. Alikumbusha pia kushindwa kwa operesheni ya Marekani ya mwaka 1980 ya kuwaokoa mateka nchini Iran (Operesheni Eagle Claw).
Shambulizi la Houthi lina maana gani?
Tunageukia jarida la Uingereza la Spectator, ambalo lilichapisha makala kuhusu shambulio la kombora lililozinduliwa na Wahouthi Jumamosi jioni dhidi ya kusini mwa Israeli, yenye kichwa "Shambulio la Houthi linatishia kuzidisha matatizo ya Trump," na Jonathan Sacredoti.
Mwandishi alipendekeza kuwa kuingia kwa Houthi katika vita kwa wakati huu kunaonyesha mkakati wa Tehran, na kuwa shambulizi hilo linahudumia maslahi kadhaa ya Iran.
Kwa mujibu wa makala, shambulizi hilo linatatiza uwekaji wa vikosi vya Marekani katika Bahari ya Shamu, kwani harakati za kijeshi lazima zipitie Mfereji wa Suez, Bahari ya Shamu na Mlango wa Bab al-Mandab, maeneo yaliyo katika hatari ya mashambulizi.
Saccordotti alieleza hili kama "udhaifu" ambao Iran inataka kuutumia, akiongeza kuwa Houthi wana uwezo wa kijeshi wa kutishia usafiri wa majini, ikiwemo makombora dhidi ya meli, droni, boti za kasi zenye milipuko na hata mabomu ya baharini.
Mwandishi wa makala hayo anaona kuwa hali ya sasa ya Jeshi la Wanamaji la Marekani imeunda pengo ambalo Iran inajaribu kulitumia ili kupata faida ya kimkakati. Kwa mujibu wake, manowari ya kivita USS Gerald Ford bado haijawa tayari, kwani iko katika matengenezo kwenye kisiwa cha Krete, huku manowari USS George H.W. Bush ikiwa bado inaelekea Bahari ya Mediterania.
Sacredoti anaeleza kuwa operesheni yoyote ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran itahitaji kuimarishwa kwa nguvu za majini katika eneo la Ghuba, jambo ambalo kwa upande wake litahitaji kupita katika maji yanayodhibitiwa na waasi wa Houthi.
Kwa mujibu wa mwandishi, hata kupelekwa kwa vikosi vya Marekani katika Bahari ya Shamu ya kaskazini karibu na ardhi ya Saudi Arabia hakutaondoa tishio hilo, kutokana na uwezo wa makombora ya masafa marefu ya Houthi kufikia maeneo hayo.
Mwandishi anaona kuwa shambulizi la Houthi linaweza kutafsiriwa kama "ujumbe wa kuzuia" unaolengwa kwa wapangaji wa mikakati mjini Washington, ujumbe unaobainisha kuwa Iran inaweza kuendelea kuweka shinikizo kwa kufungua nyanja nyingi za mapambano kwa wakati mmoja.
Anaongeza kuwa, ikiwa Israel na Marekani zina uwezo wa kufanya mashambulizi yaliyopangwa kwa awamu na kuonyesha uwezo wa kubadilika kulingana na hali, basi Iran nayo ina uwezo wa kuamsha washirika wake wa kikanda kwa njia ya kimakusudi.
Maandamano ya "No Kings" Marekani yana ujumbe gani?
Tunahitimisha na makala ya New York Times kuhusu wimbi jipya la maandamano ya "No Kings" nchini Marekani iliyoandikwa na Thomas Fuller.
Makala hayo yanaeleza kuwa maelfu ya watu walijitokeza mitaani siku ya Jumamosi kupinga sera za Rais Trump, zikiwemo uhamiaji, haki za kupiga kura, na masuala ya utofauti lakini pia vita dhidi ya Iran na kupanda kwa bei ya mafuta.
Mwandishi Fuller alimnukuu mwandamanaji mmoja, John Moise, akisema: "Gharama za maisha zimepanda kupita uwezo wetu… uvumilivu wetu umefikia kikomo."Moise anajitambulisha kama mtu huru, ingawa anaegemea upande wa Wanademokrasia.
Mwandishi wa makala hayo anaeleza kuwa maandamano hayo yanaonyesha mchanganyiko wa hasira ya kisiasa na kiuchumi, huku wapiga kura wakieleza kuchoshwa na sera za uhamiaji na vile vile hali ya kufadhaika miongoni mwa raia kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha, hasa kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.
Mwandishi huyo alibainisha kile ambacho matokeo ya kura ya maoni ya hivi majuzi yalionyesha: Umaarufu wa Rais Trump umeshuka hadi asilimia 36 - kiwango cha chini kabisa tangu arejee Ikulu ya White House.
Kura ya maoni ya Reuters/Ipsos iliyotolewa Jumanne iliyopita ilionyesha kuwa ni asilimia 35 tu ya waliohojiwa waliunga mkono kuanzishwa kwa mashambulizi dhidi ya Iran.
Huku uchaguzi wa katikati ya muhula ukiwa umesalia miezi saba, waangalizi wanaona maandamano haya kama kipimo cha mabadiliko ya kisiasa yanayoweza kutokea.
Ingawa idadi kubwaya waandamanaji ni wa upande wa Wanademokratic, matukio na shughuli kadhaa za "No Kings" pia zilifanyika katika majimbo ya Marekani yenye wanachama wengi wa Republican siku ya Jumamosi, kulingana na mwandishi huyo.
Wakati ambapo Warepublican wanadhibiti Ikulu ya White House, bunge, na Mahakama ya Juu, maandamano haya yalikuja kama "fursa nzuri kwa Wanademokrasia kutoa sauti zao na kujaribu kuonyesha kwamba nguvu ya Republican kwenye mamlaka inaanza kusuasua," kulingana na mwandishi huyo.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid