Vita vya Marekani, Israel na Iran: Nani atashinda na nani atashindwa?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Gazeti la Uingereza la The Times linaangazia athari za vita kati ya Marekani na Israeli na Iran, na katika tahariri yake limejaribu kujibu swali la: Nani mshindi na mshindwa katika vita vinavyoendelea?

Gazeti hilo linaonya kuhusu "dhoruba ya kiuchumi" inayokuja kutokana na athari za mzozo wa Mashariki ya Kati, ambao utaathiri vibaya watu wengi lakini utaleta faida zisizotarajiwa kwa wengine.

Kuhusu walioshindwa, gazeti hilo linasema makampuni ya madini ni miongoni mwa yaliyoathiriwa zaidi na vita hivi, kutokana na kuathirika vibaya madini kama vile ya chuma na shaba, na kusababisha kupungua kwa kasi kwa hisa za makampuni.

Orodha hiyo pia inajumuisha makampuni ya kandarasi na ujenzi, kwa sababu kuna uwezekano wa kupanda kwa viwango vya riba mwaka huu, ambayo itasababisha viwango vya juu vya mikopo ya nyumba, hilo litamaanisha mahitaji yatapungua na mauzo kuwa chini.

Mashirika ya ndege ni miongoni mwa waliopoteza, kutokana na usumbufu wa usafiri na kusafiri kwa njia ndefu ili kuepuka Mashariki ya Kati, jambo ambalo limesababisha gharama kubwa za usafiri ambazo zitaongezeka zaidi baada ya kupanda kwa bei ya mafuta.

Miongoni mwa walioathirika bila kutarajiwa ni makampuni ya teknolojia, kutokana na kutatizika kwa usambazaji wa heliamu kutoka Qatar, ambayo huzalisha theluthi moja ya heliamu duniani.

Heliamu hutokana na gesi asilia iliyoyeyuka na hutumika sana katika viwanda vya vya teknolojia, kama vile semiconductors na vifaa vingine vya elektroniki vya hali ya juu.

Kwa wauzaji rejareja wanakabiliwa na shinikizo kubwa la kupanda kwa gharama na kupungua kwa maununuzi, kutokana na usumbufu wa mnyororo wa ugavi na gharama kubwa za usafirishaji, shida ambayo inapunguza faida katika biashara zao, pamoja na matarajio ya viwango vya juu vya riba na gharama za nishati zinazoendelea kuathiri watumiaji.

Kuhusu washindi wa vita hivi, makampuni ya utafutaji wa mafuta na gesi yameibuka washindi. Ikiwa bei za sasa za mafuta na gesi zitaendelea hivi, makampuni haya yanatarajiwa kupata pesa zaidi kuliko makadirio yao ya awali, na kuwapa urahisi zaidi wa kulipa madeni, kufadhili ununuzi, au kurudisha pesa kwa wanahisa.

Vile vile, makampuni katika sekta ya fedha, hasa makampuni ya kamari, kwa kawaida hupata ongezeko la wateja wakati masoko yanapobadilika na kutokuwa na uhakika. Hali hii pia inanufaisha makampuni mengine ambayo yanaweza kunufaika na ongezeko la biashara, ikiwa ni pamoja na Soko la Hisa la London.

Mahesabu mabovu ya Trump kuhusu Iran

Makala ya gazeti la New York Times, yaliyoandikwa na mwanajeshi wa zamani wa Marekani na mwandishi wa riwaya, Phil Clay, ambaye alishiriki katika Vita vya Iraq, inajadili makosa ya Trump katika vita na Iran.

Clay anasema Vita vya Iraq, ambavyo alishiriki zaidi ya miongo miwili iliyopita, vilikuwa vimepangwa vibaya, vilitokana na kiburi, na kulikuwa na uongozi dhaifu katika ngazi za juu, lakini "nilijua kwa nini nashiriki vita hivyo." Kuhusu wanajeshi wa sasa: "Je, wanajua tunachojaribu kukifanya nchini Iran?”

Anabainisha kwamba sababu za vita hivyo zina utata mkubwa. Pengine ni kubadilisha utawala, au kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, au kudhoofisha uwezo wao wa makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani, au labda kwa sababu Israel ilikuwa karibu kuishambulia Iran na tungekuwa hatarini, au kwa sababu Marekani ilikuwa chini ya tishio kutoka Iran, au kusaka amani Mashariki ya Kati, n.k.

Clay anasema moja ya sababu zilizo wazi za vita hivi, kwa utawala wa sasa wa Marekani, ni "kuonyesha nguvu na utawala."

Ni kutokana na kauli ya Rais Trump ambapo alisema maafisa wa kijeshi walimwambia "kuzamisha meli ni jambo bora zaidi" kuliko kuzikamata... Lakini wanajeshi hawa wanaonekana kutotambua, au kutojali, kwamba lugha yao ya vurugu inaashiria kukengeuka taratibu za vita za Marekani, ambazo zilianzia wakati wa Mapinduzi ya Marekani.

Mababa wa taifa la Marekani waliweka kanuni kwa ulimwengu wote, ikiwa ni pamoja na kwamba watu wote wameumbwa sawa, na serikali hupata mamlaka kutokana na ridhaa ya watawaliwa, hilo lina maana vita haviwezi kuhalalishwa ili tu kuonyesha nguvu na utawala.

Mwandishi anagusia "vita vilivyoshindwa vya Marekani" kama vile Vita vya Vietnam na Vita vya Iraq, na anasema "kushindwa kulitokana na kushindwa kwetu kutambua kwamba watu wa nchi zingine wana hisia na maadili yao, na huenda yasiwe sawa na matamanio yetu."

Mwandishi huyo anaongeza kwamba kutegemea nguvu za kikatili kunaweza kupofusha macho, na anakosoa kauli za Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth, ambaye amesema "udhibiti wetu wa anga ya Iran na njia za majini unatufanya tudhibiti hatima yake," na "tutaamua kanuni ya vita hivi katika kila hatua."

Akizungumzia matamshi haya, anasema, "Hegseth, aliyepigana Vita vya Iraq, alipaswa kuwa mwangalifu zaidi. Adui huwa na maoni yake pia, na hata baada ya vita vya kijeshi vilivyoshindwa, athari za vita kwa watu wa kawaida zinaweza kuwa na matokeo magumu, yasiyotakikana, na wakati mwingine mabaya."

Clay anashauri kwamba mataifa yenye uadui na Marekani yanapaswa kutazamwa kama nchi zenye changamano, zilizojaa wanadamu, na hii ndiyo sababu hasa utawala wa Trump ulishindwa kutabiri matokeo ya hatua za kijeshi nchini Iran.

Baada ya Iran kupanua vita kwa kushambulia kote Mashariki ya Kati, Higseth alikiri, "Siwezi kusema kwamba tulitarajia hili kuwa hasa ndio jibu lao."

Wairani wana matumaini wakati wa sherehe ya Nowruz

Gazeti la Uingereza la The Guardian linafuatilia maisha ya kila siku ya watu wa Iran licha ya mabomu, na katika ripoti ya mwandishi wake Stephanie Glinski anasema, kutoka ndani ya Iran, Wairani wanasherehekea Nowruz, Mwaka Mpya wa Uajemi, licha ya mashambulizi kuingia wiki yake ya nne.

Gazeti hilo linasema Nowruz ni sikukuu muhimu kwa watu wengi Asia ya Kati na Mashariki ya Kati na husherehekewa na kila Wakurdi. Inaambatana na majira ya kuchipua na kwa kawaida huonekana ni wakati mpya, wa matumaini na mwanzo mpya.

Ingawa maduka mengi katika Soko la Tajrish, mojawapo ya masoko yenye shughuli nyingi mjini Tehran, yamefungwa tangu mwanzo wa vita Februari 28, lakini kuelekea Nowruz, soko lilirejea, na watu walikusanyika kununua maua, mboga, chakula, pamoja, mayai, samaki wa mapambo, bidhaa ambazo huchukuliwa kuwa alama muhimu wakati wa sherehe za Mwaka Mpya.

Ndani ya nyumba katikati mwa Tehran, Darya, mchoraji mwenye umri wa miaka 48, mumewe Mohammad, 50, na binti yao Masihah, 25, wanasisitiza kusherehekea Nowruz licha ya vita. "Lazima tuhifadhi mila zetu, haswa katika nyakati kama hizi," anasema. "Ni sehemu muhimu ya utamaduni wetu."

Lakini kwa baadhi, Nowruz imekuja na hasara. Shambulio la anga lililolenga kampuni ya usambazaji umeme ya Tehran liliharibu duka la mikate la kijana Erfan, ambalo alirithi kutoka kwa babu yake ambaye alianzisha duka hilo zaidi ya miaka 60 iliyopita.

Erfan ameamua kujenga upya duka lake la mikate la Nowruz, lakini anasema, "Tulikuwa tukisherehekea tukio hili, lakini mwaka huu nahisi hatuna nguvu na shauku ya kufanya hivyo."

Kutoka katikati ya vifusi, anasema mabadiliko nchini Iran ni "muhimu," lakini si kupitia vurugu na vita.

Irfan anakumbuka sherehe za Nowruz za mwaka jana na sherehe za Chaharshanbe Suri, tamasha la moto lililofanyika Jumatano iliyopita kabla ya mwaka mpya. Lakini mwaka huu, mitaa ilikuwa haina watu, na ni watu wachache tu waliowasha moto.

Licha ya vita na vurugu, Hassan, mwenye umri wa miaka 56, mmiliki wa duka la maua kaskazini mwa Tehran, pamoja na binti yake Sajida, mwenye umri wa miaka 26, anasema watu wanajaribu kuishi kawaida.

Hassan anasema: "Kwa kuanza kwa vita, na kabla ya Nowruz, tulinunua kiasi kikubwa cha maua. Asilimia 90 yaliharibika na tukayatupa. Huu kwa kawaida huwa msimu wetu wa mauzo makubwa, lakini sasa tunauza asilimia 5 pekee ya kiasi cha kawaida. Wateja wetu wa kawaida hawanunui, kwa hivyo biashara yetu imeathiriwa vibaya."

Katika miaka iliyopita, Hassan alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa katika duka lake, siku ambayo inaambatana na siku ya kwanza ya mwaka mpya.

"Hata wakati wa vita, hata kama hatuuzi chochote, tunapaswa kufungua duka. Tuliamua kufanya hivyo, hata wakati wa sherehe za Nowruz," Sajida anasema, akitabasamu. "Watu wanapopita na kuona maua na duka lililo wazi, ni dalili ya uwepo wa maisha na inawapa matumaini.