Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini nchi za Kiarabu hazilipizi kisasi dhidi ya mashambulizi ya Iran?
- Author, Luis Barucho
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Wakati vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vikiendelea, Tehran imeendelea na mashambulizi yake ya makombora dhidi ya nchi za Ghuba ya Uajemi.
Siku ya Alhamisi, Machi 19, 2026, baada ya Israeli kushambulia kiwanda wa gesi huko South Pars, Iran ilishambulia sehemu ya eneo la nishati la Ras Laffan la Qatar.
Qatar na mataifa mengine ya Ghuba hadi sasa yamechagua kutolipiza kisasi dhidi ya Iran, licha ya kulengwa mara kwa mara. Kwa nini wanajizuia kulipiza kisasi.
Wakati Marekani na Israeli zilipoanzisha kampeni yao ya pamoja ya kijeshi dhidi ya Iran Februari 28, Tehran ilijibu mara moja kwa kulenga sio tu Israeli bali pia washirika wa Marekani wa Ghuba.
Bahrain, Kuwait, Saudi Arabia, Qatar, Oman, na hasa Falme za Kiarabu, zote zimelengwa.
Kulingana na maafisa katika nchi za Ghuba ya Uajemi, pamoja na kushambulia kambi za kijeshi za Marekani katika eneo hilo, Iran pia imelenga miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege, hoteli, maeneo ya makazi, na hasa majengo ya nishati.
Kwa nini hazililipizi kisasi?
Lakini nchi za Ghuba ya Uajemi hadi sasa zimependelea kutoanzisha shambulio dhidi ya Iran zenyewe na kutoingia vitani moja kwa moja.
"Kwa mtazamo wao, vita hivi si vita vyao, na jibu la kulipiza kisasi lina hatari ya kuwageuza kutoka kuwa watu walio hatarini kushambuliwa na kuwa watu wanaopaswa kushambuliwa, kwa sababu bado wana mengi ya kupoteza kuliko watakayo yapata ikiwa wataingia vitani," anasema Sina Toosi, mtafiti katika Taasisi ya fikra tunduizi ya Marekani kuhusu Sera za Kimataifa
Toosi anasema kusita huku kujibu ni matokeo ya "mchanganyiko wa udhaifu, hesabu za kimkakati, na kutokuwepo kwa mafanikio."
Anabainisha kuwa uchumi wa nchi za Ghuba ya Uajemi unategemea miundombinu ya nishati, usafirishaji wa meli, na imani ya wawekezaji: "Haya yote ni maeneo ambayo Iran imeonyesha kuwa ina uwezo wa kuyavuruga."
Anasema Iran imetumia nchi za Ghuba ya Uajemi na Mlango-Bahari wa Hormuz, zote zikiwa njia muhimu za maji kwa uchumi wa dunia, kama njia ya kutoa shinikizo.
Lakini Bilal Saab, mtafiti katika Taasisi ya Utafiti na Ushauri ya Trends na afisa wa zamani wa Pentagon katika utawala wa kwanza wa Donald Trump, anasema ikiwa nchi za Ghuba ya Uajemi zitaendelea kutoishambulia Iran, "zinatuma ujumbe kwa Tehran kwamba inaweza kusababisha uharibifu zaidi bila kukabiliwa na matokeo yoyote makubwa."
Anasema: "Lengo la kujibu mashambulizi ya Iran itakuwa ni kuilazimisha kusimamisha mashambulizi yake kwa muda mfupi na kuunda kinga dhidi ya uchokozi kutoka kwa nchi hii kwa muda mrefu huko mbeleni."
Rob Geist Pinfold, mhadhiri wa usalama wa kimataifa katika Chuo cha King's London, anasema pia kuna kusita miongoni mwa mataifa ya Ghuba kuifuata Israel na malengo yake katika eneo hilo.
"Kuna hisia kwamba Israeli iliivuta Marekani katika vita hivi," anaongeza.
Mizimu wa vita vya Iraq
Pinfold anasema kwa viongozi wengi wa Ghuba, urithi wa vita vilivyoongozwa na Marekani dhidi ya Iraq bado una athari katika eneo hilo.
2003, Marekani ilipindua utawala wa Saddam Hussein baada ya kuivamia Iraq. Lakini matokeo yake yalikuwa ni ombwe la madaraka lililosababisha uasi, vurugu za kidini, na miaka mingi ya ukosefu wa utulivu nchini Iraq na kote katika eneo hilo.
"Mizimu ya mwaka 2003 bado inasumbua [eneo hilo]," anasema Pinfold.
"Wana wasiwasi kwamba vita hivi vitafungua milango ya mafuriko ya machafuko na ukosefu wa utulivu katika na pia kuruhusu Iran kupanua ushawishi wake. Wasiwasi wao ni sahihi kabisa," anaongeza.
Pinfold anasema mataifa ya Ghuba sasa yana wasiwasi kwamba Marekani inafanya "operesheni isiyo na mwisho bila malengo yaliyo wazi au njia iliyo wazi kuelekea siku ya baada ya vita" na hatimaye eneo hilo "litaachwa katika fujo hili."
Lakini licha ya nchi za Kiarabu kutoridhika na vita hivi, nchi hizo bado zinategemea sana usaidizi wa kijeshi wa Marekani.
Mbali na kuhifadhi kambi na vikosi vya Marekani, nchi kadhaa za Ghuba ya Uajemi pia zinashirikiana na Marekani katika uwanja wa ubadilishanaji wa taarifa na hutegemea mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo.
Kulingana na maafisa wa Ghuba ya Uajemi, mifumo hii ya ulinzi wa anga imezuia na kuzima mashambulizi mengi ya makombora ya Iran.
Vongozi wa Ghuba bado wanaona diplomasia ndio njia pekee ya kukomesha mvutano huu,” anasema Pinfold.
Kuvunjika kwa mahusiano ya kikanda
Pinfold anasema Iran haijalenga mataifa yote ya Ghuba kwa "nguvu sawa", jambo linaloonyesha tofauti katika uhusiano wa Tehran na kila moja ya nchi hizi.
Falme za Kiarabu imekuwa mojawapo ya nchi iliolengwa zaidi wakati wa vita hivi. UAE na Bahrain zote ziliingia katika uhusiano na Israel mnamo 2020.
Kwa upande mwingine, Oman, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikichukua jukumu la mpatanishi kati ya Iran na Magharibi, haijalengwa sana na Tehran.
"Oman ilikuwa nchi pekee ya Ghuba kumpongeza kiongozi mpya wa Iran [Mojtaba Khamenei]," Pinfold anakumbuka. "Hili halikuzifurahisha nchi nyingine za Ghuba."
Lakini Mohammed Baharoun, mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Sera za Umma chenye makao yake Dubai, anasema: "Iran inazisukuma nchi za Ghuba ya Uajemi kuelekea katika muungano mkubwa zaidi dhidi yake."
Anaongeza: "Kwa kushambulia nchi za Ghuba ya Uajemi, Iran inazigeuza kuwa maadui zake na kuongeza hatari ya vita vipana zaidi, vita ambavyo hakuna mtu anayevitaka."
Kufuatia mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Ghuba nchini Saudi Arabia siku ya Jumatano, nchi za Kiarabu zilithibitisha tena haki yao ya kujilinda, kwa mujibu wa Kifungu cha 51 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Yatafanya nini?
Dkt. H.E. Hellyer, mtafiti katika taasisi ya ushauri ya Uingereza ya Royal United Services Institute, anasema ingawa mataifa ya Ghuba hadi sasa yamejizuia kulipiza kisasi, "hesabu za kisiasa zinaweza kubadilika," hasa ikiwa mashambulizi yanayovuruga mauzo ya nje ya nishati yataendelea au kuongezeka.
Hellyer anasema jambo moja linaloweza kubadilisha hesabu hizi ni shambulio kubwa dhidi ya vituo vya nishati.
Iran ilitishia siku ya Alhamisi, baada ya kushambulia kituo cha nishati cha Ras Laffan huko Qatar, kwamba itafanya "uharibifu kamili" wa washirika wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi ikiwa mashambulizi dhidi ya vituo vyake yataendelea.
Pia, ikiwa makundi washirika ya Iran watashambulia moja kwa moja nchi za Ghuba ya Uajemi, mabadiliko mengine katika mbinu zao yanaweza kutokea.
"Ikiwa Wahouthi watawashambulia... basi mashambuliz mapya yatatokea," anasema Pinfold.
Anaongeza kwamba katika hali hii, mataifa ya Ghuba yanaweza yasione tena mzozo huu kama unaohusu Marekani na Israeli pekee, bali kama mzozo wao pia.
Kwa vyovyote vile, Pinfold anasema, ingawa mataifa ya Ghuba hayajalipiza kisasi hadi sasa, mkakati wa Iran ni "hatari sana."
Anasema: "Wairani wanaharibu madaraja yote ya uhusiano wao na nchi za Ghuba ya Uajemi."
Hellyer anasema mataifa ya Ghuba "hayatakubali" Iran kuyashambulia kwa muda usiojulikana.
Anaamini kwamba mkakati hatari wa Iran wa kulazimisha mataifa ya Ghuba ya Uajemi kuidhibiti Washington hatimaye utasababisha matokeo mabaya.
“Wanaweza kusema, ingawa mwanzoni walipinga vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran, usalama wao wenyewe sasa uko hatarini kutokana na kulipiza kisasi kwa Iran, na kwa hivyo ina mantiki zaidi kuunga mkono operesheni ya Marekani kukomesha tishio la Iran,” Hellyer anasema.