Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Menorrhagia: Hali inayokufanya utokwe na damu nyingi kuliko kawaida wakati wa hedhi
Wengi wetu hatujui kama kipindi chetu ni cha "kawaida" au la. Hii haishangazi, kwa kuwa sio tu kwamba sisi sote ni tofauti, lakini unyanyapaa bado unatuzuia kuuliza maswali au kuzungumza juu ya kile kinachotokea kwetu kila mwezi na marafiki na familia.
Lakini kuna damu nyingi sana. Kwa hakika, karibu robo ya wanawake hupata hali ya kiafya inayojulikana kama menorrhagia, pia huitwa kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi. Huu ndio wakati ambao hedhi yako ni nzito au ya muda mrefu isivyo kawaida. Hapa ndio unahitaji kujua kuhusu hali hii.
N i wakati gani damu huwa nzito?
Kwa kawaida, katika kipindi cha "kawaida", kati ya 70ml na 80ml ya kioevu hupotea . Takriban 50% ya maji yanayopotea ni damu.
Lakini watu walio na damu nyingi za hedhi wanaweza kupoteza karibu 160 ml hadi 400 ml ya maji.
Dalili za kawaida za kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi ni:
- Damu kupita kwenye taulo ya kike au tamponi kila saa moja hadi mbili.
- Damu kutoka kwa zaidi ya siku saba.
- Kutokwa na madonge ya damu zaidi ya sentimita 2.5.
D amu nzito ni mbaya?
Ingawa hali hii ni ya kawaida, wanawake wengi walio nayo hata hawajui. Wengi hata kudhani kwamba kipindi chao ni "kawaida."
Lakini njia hii ya kufikiri inaweza kuwa tatizo, kwani kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi kunaweza kuwa ishara ya tatizo la msingi, kama vile fibroids, endometriosis, maambukizi ya pelvic, au matatizo ya kutokwa na damu.
Kifaa cha intrauterine (IUD) kilichoingizwa hivi karibuni pia kinaweza kusababisha kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi.
Kwa hiyo, karibu theluthi mbili ya wanawake walio na damu nyingi wakati wa hedhi pia hupata upungufu wa damu na upungufu wa madini ya chuma.
Tunapopata hedhi, tunapoteza chembe nyekundu za damu ambazo ni muhimu kwa kubeba oksijeni (chanzo cha nishati) katika mwili wote.
Ikiwa utatoka damu nyingi kila mwezi, utapoteza seli nyekundu za damu kuliko kawaida. Upungufu wa damu unaweza kuchukua muda kukua, lakini inaweza kusababisha dalili mbalimbali ambazo zinaweza kuwa na athari kubwa katika maisha yako ya kila siku.
Ingawa ngozi iliyopauka au midomo ni dalili za kimwili, mtu aliye na upungufu wa damu anaweza pia kuhisi uchovu zaidi kuliko kawaida, kuwashwa, kizunguzungu, kuchanganyikiwa, na hata kushuka kwa mapigo ya moyo.
Pia inaweza kusababisha maumivu ya kichwa, ukungu wa ubongo, kuongezeka kwa mapigo ya moyo, na hata kupoteza uzito.
Unaweza kufanya nini ikiwa una hedhi nzito?
Ikiwa unashuku kuwa unaweza kuwa na damu nyingi za hedhi, ni muhimu kuzungumza na daktari wako haraka iwezekanavyo.
Utambuzi unaweza kuchukua miezi kadhaa baada ya kumuona daktari kwa mara ya kwanza, kwa hivyo ni muhimu kutoiahirisha.
Kwenda kwenye miadi yako ukiwa na taarifa ni muhimu kila wakati. Kwa mfano, ni vizuri kupata wazo la upotezaji wako wa kawaida wa damu, ama kwa kutumia vikombe vya hedhi kupima ujazo au kwa kufuatilia ni vitu vingapi vya usafi unavyotumia kila mzunguko.
Kuweka shajara ya hedhi au kutumia programu ya kufuatilia kunaweza pia kusaidia, na pia kujua ikiwa hali hiyo inatokea katika familia.
Ikiwa haujafanya hivi, daktari wako anaweza kukuuliza ufuatilie mambo haya kwa miezi michache kabla ya kugundua hali hiyo.
Daktari wako anaweza kukuandikia dawa fulani ambazo zinaweza kupunguza athari za kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi, kutia ndani kidonge cha kudhibiti uzazi au asidi ya tranexamic (ambayo hudhibiti kutokwa na damu na kusaidia damu kuganda).
Chaguzi za upasuaji pia zinaweza kuwa muhimu ikiwa hali hiyo inasababishwa na shida nyingine, kama vile uvimbe.
Ikiwa unafikiri unaweza kuwa na upungufu wa damu, ni muhimu pia kufuatilia kwa makini dalili zako, hasa jinsi unavyohisi kabla na baada ya kipindi chako.
Hali nyingi za kawaida, kama vile wasiwasi, kikohozi, mafua, na mzio wa chakula, huwa na dalili zinazoingiliana na upungufu wa madini ya chuma, kwa hiyo ni muhimu kupima damu, kwani daktari atakwambia ikiwa una upungufu wa damu au la.
Ikiwa utagunduliwa na upungufu wa damu, unaweza kuagiziwa virutubisho vya chuma ili kusaidia mwili wako kutengeneza seli nyekundu za damu.
Lishe yenye afya na yenye vyakula vyenye madini ya chuma, kama vile nyama nyeusi, mbaazi, maharagwe, mboga za majani, na njugu, vinaweza pia kusaidia.