Trump anapigana vita kwa kufuata hisia na hazifanyi kazi

    • Author, Jeremy Bowen
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Kushindwa kujifunza kutokana na yaliyopita kunamaanisha kwamba Donald Trump sasa anakabiliwa na chaguo gumu. Ikiwa hawezi kupata makubaliano na Iran, anaweza kujaribu kutangaza ushindi ambao hautamdanganya mtu yeyote, au atazidisha vita.

Bondia wa Marekani Mike Tyson ana msemo wake kwamba: "Kila mtu ana mipango yake, hadi pale atakapopigwa."

Maneno bora zaidi kwa Trump ni maneno ya mmoja wa watangulizi wake, Dwight D. Eisenhower, jenerali wa Marekani aliyeongoza ndege za D-Day mwaka 1944 na akatumikia mihula miwili kama rais wa Marekani kutoka Republican katika miaka ya 1950.

Eisenhower anasema "mipango haina maana, lakini kupanga ndio kila kitu." Akimaanisha nidhamu na mchakato wa kupanga mipango ya kupigana vita hurahisisha kubadilisha mwelekeo wakati jambo lisilotarajiwa linapotokea.

Kwa Trump, jambo lisilotarajiwa ni uimara wa utawala nchini Iran. Inaonekana alitarajia kudondoshwa kwa utawala kama ile operesehani ya utekaji nyara ya jeshi la Marekani mwezi Januari dhidi ya Rais wa Venezuela Nicolás Maduro na mkewe, Cilia Flores. Sasa wako gerezani New York, wanakabiliwa na kesi. Naibu wa Maduro, Delcy Rodríguez ni mrithi wake kama rais na anapokea maagizo kutoka Washington.

Kutamani ushindi kama ule wa dhidi ya Maduro kunaonyesha ukosefu mkubwa wa uelewa wa tofauti kati ya Venezuela na Iran.

Eisenhower anasema "jambo la kwanza unalofanya ikiwa mipango itakwenda kombo ni kuondoa mipango yote na kuitupa nje ya dirisha na kuanza tena.".

Licha ya kumuua Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei katika shambulio la kwanza la anga la vita, utawala wa Tehran unafanya kazi na unapigana. Unatumia vizuri udhaifu wake.

Kwa upande mwingine, Trump anatumia hisia kadiri anavyosonga mbele. Anafuata hisia zake za ndani, na si kurasa za intelejensia.

Siku kumi na tatu baada ya vita, Trump aliulizwa na Fox News Radio vita vitaisha lini. Alijibu kwamba hakufikiria kwamba "vingekuwa virefu." Kuhusu kumalizika, alisema "nitakapoihisi."

Anategemea kundi la washauri wa ndani wanao unga mkono maamuzi yake na kuyafanikisha. Inaonekana kusema ukweli kwa mamlaka sio sehemu ya kazi yao.

Mbinu za Iran

Hadi sasa vita hivyo vimewaua raia 1,464 wa Iran, kulingana na HRANA, shirika lenye makao yake Marekani linalofuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Iran.

Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu walitarajia ushindi wa haraka. Wote wawili waliwahimiza Wairani kufanya uasi wa umma ili kuiangusha serikali.

Utawala wa Tehran bado upo madarani, bado unapigana na Trump anagundua ni kwa nini watangulizi wake hawakuwa tayari kujiunga na Netanyahu katika vita vya kuiangamiza Jamhuri ya Kiislamu.

Wapinzani wa utawala huo hawajajitokeza. Wote wanajua kwamba mwezi Januari vikosi vya serikali viliwaua maelfu ya waandamanaji. Maonyo rasmi yametangazwa yakimwambia mtu yeyote anayefikiria kujaribu kurudia maandamano atahesabiwa kama maadui wa serikali.

Utawala wa Iran ni adui mgumu, mkatili, na aliyejipanga vizuri. Ulianzishwa baada ya mapinduzi ya 1979 yaliyompindua Shah, kisha ukanusurika na vita vya miaka minane na Iraq.

Utawala huo umejengwa juu ya taasisi, si watu binafsi, na umeimarishwa na imani za kidini na itikadi ya kuuawa kishahidi. Hiyo ina maana kuwaua viongozi, ingawa bila shaka ni jambo la kuumiza kwao, lakini haina maana ndio kuuawa kwa utawala huo.

Utawala wa Iran hauna nguvu kama ya Marekani na Israeli, lakini kama Tyson na Eisenhower wanavyosema, umekuwa ukipanga mipango. Ulipanua vita, ukishambulia majirani zake wa Kiarabu wa Ghuba pamoja na kambi za Marekani na Israeli, ukieneza maumivu kwa upana Kadiri iwezekanavyo.

Kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, mlango mwembamba wa kuingia Ghuba, kumepunguza takriban 20% ya usambazaji wa mafuta duniani na kuathiri masoko ya fedha duniani.

Iran ilitumia miaka na mabilioni ya dola kujenga mtandao wa washirika na wawakilishi ambao Iran inauitwa 'mhimili wa upinzani' unajumuisha Hezbollah huko Lebanon na Hamas huko Gaza na Ukingo wa Magharibi ili kuitishia na kuizuia Israeli.

Waisraeli wameishambulia vikali na kwa ufanisi mhimili huo tangu vita vya Gaza vianze kufuatia mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba 2023.

Kwahiyo Iran imeona kuwa mlango wa Bahari wa Harmuz, ndio mbinu yake ya kijeshi.

Yanayotokea yanaonesha umuhimu wa kupanga jinsi ya kuanzisha vita, jinsi ya kuimaliza na jinsi ya kukabiliana na siku inayofuata. Donald Trump na watu wake wa karibu, wakiwa wamejawa na matarajio ya ushindi wa haraka na rahisi, wanaonekana kuruka hatua hizo.

'Mhimili wa upinzani' pia unawajumuisha Wahouthi huko Yemen. Siku ya Ijumaa walirusha makombora mengi dhidi ya Israeli kwa mara ya kwanza tangu vita hivi vianze na mashambulizi ya anga dhidi ya Iran tarehe 28 Februari. Ikiwa Wahouthi wataanza tena mashambulizi yao dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu, Saudi Arabia itapoteza njia yake ya bahari kwa ajili ya usafirishaji wa mafuta kwenda Asia.

Ikiwa Wahouthi wataamua watafanya mashambulizi dhid ya meli huko Bab al Mandab na kusini, kama walivyofanya wakati wa vita vya Gaza, watakaja njia kutoka Asia hadi Ulaya kupitia Mfereji wa Suez.

Hilo litasababisha hali mbaya zaidi ya kiuchumi duniani.

Netanyahu anataka nini?

Tofauti na Trump, Netanyahu amekuwa akifikiria kuhusu vita hivi tangu aingie kwenye siasa, na kumfanya kuwa waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi nchini Israeli.

Yuko wazi juu ya anachotaka. Kupigana vita na Iran ni jambo rahisi zaidi kwa Israeli kuliko Marekani. Vurugu za kikanda ni tofauti na changamoto pana zaidi za kimataifa zinazokabiliwa na Marekani.

Netanyahu anaamini anaweza kuhakikisha usalama wa siku zijazo wa Israeli kwa kufanya uharibifu mkubwa iwezekanavyo kwa Jamhuri ya Kiislamu. Vita hivyo, alisema, ni vya "kuhakikisha uwepo wetu na mustakabali wetu."

Netanyahu amekuwa akiiona Iran kama adui hatari zaidi wa Israeli. Wakosoaji wake wanasema kushughulishwa na Iran ilikuwa moja ya sababu za Israeli kushindwa kugundua na kuzuia mashambulizi ya Hamas kutoka Gaza tarehe 7 Oktoba 2023.

"Muungano huu wa kijeshi unaturuhusu kufanya kile ambacho nimetamani kukifanya kwa miaka 40: kuipiga serikali ya kigaidi. Hiki ndicho nilichoahidi - na hiki ndicho tutakifanya."

Netanyahu na jeshi la Israeli kwa nyakati tofauti katika miaka yake mingi ofisini, wamechunguza njia za kwenda vitani na Iran, kuharibu vituo vyake vya nyuklia na makombora ya masafa marefu, na kila kitu kingine kilichoifanya kuwa tishio kwao.

Hitimisho la Israeli lilikuwa, ingawa wangeweza kuidhuru Iran, yangekuwa ni madhara madogo tu kwa utawala huo. Njia pekee ya kuvunja uwezo wa kijeshi wa Iran kwa muda mrefu au zaidi ni kuwa na ushirikiano na Marekani.

Lakini hilo lilihitaji rais katika Ikulu ya White House ambaye yuko tayari kwenda vitani pamoja na Israeli, jambo ambalo halitokea licha ya uhusiano wa karibu wa nchi hizo mbili na utegemezi wa Israeli kwa msaada wa kijeshi na kidiplomasia wa Marekani.

Netanyahu hakuweza kamwe kumshawishi rais wa Marekani kwamba ni kwa maslahi ya Marekani kwenda vitani na Iran - hadi muhula wa pili wa Donald J Trump.

Licha ya uhusiano mchungu na wenye sumu kati ya Marekani na Iran tangu Shah, mshirika imara wa Marekani, alipopinduliwa mwaka wa 1979, marais waliofuata wa Marekani waliamini kwamba njia bora ya kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuidhibiti.

Wakati wa uvamizi wa Marekani nchini Iraq, Marekani haikuingia vitani na Iran hata wakati ambao Tehran ilikuwa ikiwapa vifaa na kuwapa mafunzo wanamgambo wa Iraq waliokuwa wakiwaua wanajeshi wa Marekani. Sababu pekee ya kuingia vitani na Iran, ni kuwepo kwa tishio la karibu, hasa madai kwamba Iran inajaribu kuunda silaha za nyuklia.

Trump alijumuisha tishio la nyuklia katika orodha yya sababu za kwenda vitani. Lakini hakuna ushahidi wa kuaminika kwamba Iran ilikuwa karibu kupata silaha hizo. Hata Ikulu ya Marekani bado ina taarifa kwenye tovuti yake yenye tarehe 25 Juni 2025 chini ya kichwa cha habari “Vituo vya Nyuklia vya Iran VImeharibiwa - na Kusema Tofauti na hivyo ni Habari ya Uongo.'

Trump sasa anagundua ni kwa nini watangulizi wake waliamua kwamba hatari ya kuchagua kwenda vitani ni kubwa sana.

Vita vya mdogo na mkubwa

Vita vinaonekana kugeuka kuwa mfano halisi wa jinsi nguvu ndogo na dhaifu inavyoweza kupigana na adui mkubwa na mwenye nguvu.

Kulinganisha na vita vingine ambavyo kwenye karatasi Marekani ilikuwa ikishinda kwa idadi ya maadui waliouawa na mashambulizi ya mabomu kama nchini Vietnam, Iraq na Afghanistan. Lakini ni muhimu kukumbuka kwamba baada ya miaka mingi ya umwagaji damu na mauaji, yote yaliishia kwa njia ambazo zilisababisha kushindwa kwa Marekani.

Maamuzi yanayofuata ya Trump na Netanyahu yanaweza kuamua kama vita nchini Iran vitakuwa kosa jingine kubwa la Marekani au la. Trump sasa ameahirisha mara mbili tishio lake la kuharibu mtandao wa umeme wa Iran - ambalo kama alivyolielezea linaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Anasema hiyo ni kwa sababu Iran inatamani sana kufanya makubaliano ya kukomesha vita, kwani utawala huo umeathiriwa sana na uharibifu na vifo na inaogopa kwamba Marekani inaweza kufanya zaidi.

Mawasiliano kati ya pande hizo mbili, kupitia upatanishi wa Pakistan na wengine, yanafanyika. Wairani wanakataa madai ya Trump kwamba ni mazungumzo kamili.

Maandishi rasmi ya mpango wa rais wa mambo 15 wa amani hayajachapishwa, lakini matoleo yaliyovuja yanaonyesha hati ambayo ni mkusanyiko wa madai yote ambayo Marekani na Israel zimeyatoa kwa Iran kwa miaka mingi.

Inasomeka zaidi kama masharti ya kujisalimisha badala ya msingi wa mazungumzo. Iran imejibu kwa kutoa matakwa yake yenyewe, ambayo hayakubaliki kwa upande mwingine, ikiwa ni pamoja na kutambua udhibiti wake wa Mlango-Bahari wa Hormuz, fidia kwa uharibifu, na kuondolewa kwa kambi za Marekani kutoka Mashariki ya Kati.

Vita viko katika hatua muhimu. Ikiwa hakuna makubaliano kati ya Wamarekani na Wairani, Trump ana chaguo chache sana. Anaweza kutangaza ushindi, akisema Marekani imeharibu jeshi la Iran, kwa hivyo lengo limefikiwa, na kwamba kufungua Mlango-Bahari wa Hormuz si jukumu lake.

Au kuzidisha vita. Wamarekani wana zaidi ya wanajeshi 4,000 wa Marekani katika meli zinazoelekea Ghuba, wanajeshi wa parachuti kutoka kikosi cha 82 cha Airborne wakiwa tayari na wanajadili nyongeza zaidi.

Hakuna anayezungumzia uvamizi wa ardhini dhidi ya Iran, lakini inawezekana Wamarekani watajaribu kuteka visiwa katika Ghuba, ikijumuisha kisiwa cha Kharg, kituo kikuu cha mafuta cha Iran. Hilo litahusisha mfululizo changamoto katika utuaji. Hilo linaweza kuifaa Iran, ambayo inataka kuwavuta Wamarekani katika vita vya muda virefu. Iran inaamini kwamba uwezo wa utawala wa kuvumilia maumivu ni mkubwa kuliko ule wa Trump.

Trump amegundua kwamba ana mipaka ya mamlaka yake. Utawala wa Iran una tafsiri tofauti ya ushindi na kushindwa. Kwao, kusalimika tu ni ushindi.

Kushindwa vitani si chaguo. Kama Iran ingepigwa vibaya kama Trump na watu wake wanavyosema, utawala wa Tehran ungekuwa umeanguka kufikia sasa. Asingehitaji kuwatishia kukubali hatima yao.

Marekani na Israeli zinaweza kusababisha uharibifu mkubwa zaidi na kuua watu wengi zaidi nchini Iran. Kwa kukosekana makubaliano ya kusitisha mapigano, wanaweza kuongeza kiwango cha mashambulizi hadi Wairani watakapokuwa hawana chaguo ila kusalimu amri.

Kadiri vita vinavyoendelea kwa muda mrefu, ndivyo matokeo yake yanavyozidi kuwa makubwa kwa eneo hilo na kwa ulimwengu mzima. Mchambuzi mmoja wa Iran, Ali Vaez aliniambia kuwa yanaweza kuwa "majanga makubwa".