Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mambo 10 anayopaswa kufanya Muislam siku ya Eid El-Fitri
Eid El-Fitri ni miongoni mwa sikukuu kubwa na zenye heshima kubwa katika Uislamu, ikija mara moja kila mwaka baada ya kukamilika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ni siku ya furaha, shukrani na mshikamano kwa Waislamu duniani kote baada ya mwezi mzima wa ibada, kujinyima na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.
Mataifa kadhaa yakiwemo ya Mashariki ya Kati kama Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Qatar na Kuwait, pamoja na nchi nyingine kama Uturuki, Maldives, Lebanon, Palestina, Yemen na Iraq ymeasheherekea Eid Ijumaa ya machi 20.
Hali kama hiyo pia imeonekana katika bara la Afrika, hususan katika nchi za Afrika Kaskazini kama Morocco na Misri, ambazo zimeungana na mataifa ya Ulaya kama Ubelgiji katika kusherehekea siku hii moja.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki, nchi za Kenya, Uganda, Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia na Somalia zimeadhimisha Eid leo, tofauti na Tanzania, ambayo yenyewe Eid ni Jumamosi, Machi 21.
Katika siku hii muhimu, Waislamu husherehekea kwa nyoyo zilizojaa furaha, wakikumbuka mafanikio ya kufunga na kufanya ibada mbalimbali. Pia ni wakati wa kuimarisha mahusiano ya kifamilia na kijamii kupitia ziara, sadaka na kushirikiana chakula.
Kwa wengi, Eid ni zaidi ya sherehe; ni siku ya kuonesha ucha Mungu, upendo na mshikamano kwa jamii. Watu huvaa nguo nzuri, kuandaa vyakula maalum na kuwakaribisha ndugu, jamaa na marafiki.
Hata hivyo, pamoja na furaha yake, siku ya Eid pia ina taratibu na mambo muhimu ambayo Muislam anapaswa kuyazingatia ili kuhakikisha anaitimiza kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Mambo 10 anayopaswa kufanya Muislam siku ya Eid
1. Kula kabla ya Swala ya Eid
Ni Sunna kwa Muislam kuanza siku ya Eid kwa kula kitu kidogo kabla ya kuelekea msikitini kwa ajili ya Swala ya Eid.
2. Kumshukuru Mwenyezi Mungu
Siku ya Eid ni ya shukrani, hivyo ni muhimu kumshukuru Mungu kwa kukuwezesha kufunga Ramadhani na kufanya ibada.
3. Kulipa Zakatul-Fitr
Kabla ya Swala ya Eid, Muislam anapaswa kuhakikisha ametoa Zakatul-Fitr kwa ajili ya kuwasaidia wenye uhitaji.
4. Kuoga na kujipamba
Usafi ni muhimu siku ya Eid. Inashauriwa kuoga, kuvaa nguo safi au mpya na kujipaka manukato (hasa kwa wanaume).
5. Kwenda msikitini na familia
Ni vyema kwenda kuswali pamoja na familia, wakiwemo watoto, wanawake na wanaume.
6. Kusoma Takbira
Takbira ni sehemu muhimu ya siku ya Eid, zikianza tangu usiku wa Eid hadi pale Swala itakapoanza.
7. Kusikiliza khutba ya Eid
Baada ya Swala, ni muhimu kubaki na kusikiliza khutba ya Sheikh kwa ajili ya mawaidha.
8. Kubadilisha njia ya kwenda na kurudi msikitini
Ni Sunna kwa Muislam kutumia njia tofauti anaporudi kutoka msikitini ili kuonesha furaha ya Eid kwa jamii.
9. Kusherehekea na ndugu na marafiki
Baada ya ibada, Waislamu hukutana na ndugu, marafiki na majirani kusherehekea pamoja.
10. Kutoa sadaka na kusaidia wahitaji
Eid ni siku ya kugawana furaha, hivyo ni muhimu kuwasaidia wenye uhitaji ili nao washiriki kikamilifu katika sherehe.