Moto katika kiwanda cha magari Korea Kusini: Watu 14 wafariki

Mamlaka za Korea Kusini zinasema kwamba watu 14 walifariki na wengine 25 kujeruhiwa vibaya baada ya moto kuzuka katika kiwanda cha kutengeneza vipuri vya magari katika mji wa Daejeon.
Moto huo ulizuka wakati wa chakula cha mchana siku ya Ijumaa na ulidhibitiwa kufikia saa 5:48 usiku, wizara ya usalama ilisema. Watu wengine 35 walipata majeraha madogo.
Mamlaka ilisema kuwa kiwanda hicho kinamilikiwa na Anjun Industrial, ambayo hutengeneza vifaa vya injini kwa ajili ya makampuni ya Hyundai Motor, Kia Corp miongoni mwa mengine, kwa mujibu wa tovuti yake.
Katika taarifa kwenye tovuti ya kampuni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji Sohn Ju-hwan aliomba radhi, akisema kwamba watashirikiana kikamilifu na mamlaka katika kuchunguza chanzo cha ajali hiyo, kukagua tena mifumo yake ya usalama, na kutekeleza kwa haraka hatua zote muhimu ili kuzuia tukio hilo kutokea tena.
Serikali ilitumia timu ya pamoja ya kudhibiti majanga kutoka idara kadhaa baada ya Rais Lee Jae Myung kuamuru rasilimali zote zilizopo zitumike kukabiliana na moto huo na kuokoa maisha.








