Iran yasema haitajadili juu ya uwezo wake wa makombora
Marekani kwa muda mrefu imekuwa ikitaka kupanua mazungumzo kuhusu uwezo wa nyuklia wa Iran pia kujumuisha mpango wake wa makombora.
Muhtasari
- Mahakama yaridhia pingamizi moja la Lissu
- Edwin Sifuna: Katibu Mkuu wa ODM atimuliwa
- Watu wapoteza maisha kwa kimbunga Madagascar
- Vikwazo vya Marekani kwa Urusi juu ya biashara ya mafuta ya Venezuela ni ubaguzi - Lavrov
- Ghana yatangaza Jumatano 'Siku ya kuvaa Fugu' vazi la kitamaduni baada ya kejeli mtandaoni
- Iran yasema haitajadili juu ya uwezo wake wa makombora
- Shambulizi la Urusi laua baba na watoto watatu, Ukraine inasema
- Marubani wauawa baada ya ndege iliyobeba abiria kufyatuliwa risasi ikitua huko Papua
- Netanyahu kukutana na Trump huku mazungumzo ya nyuklia ya Iran yakifikia hatua muhimu
- Mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zambia Lungu aamriwa kusalimisha magari 79, kituo cha mafuta na nyumba za kifahari
- Mpango wazinduliwa kuongeza muhula wa Rais Zimbabwe
- Britney Spears auza haki zote za muziki wake
- Tunachojua kufikia sasa kuhusu shambulio la Shule nchini Canada
- Baba alimpiga risasi binti yake baada ya 'kubishana kuhusu Donald Trump'
- Watu tisa wauawa kwa kupigwa risasi, wakiwemo saba shuleni Canada - Polisi
- Wabunge wa Marekani wamtaka kakake mfalme wa Uingereza kutoa ushahidi juu ya faili za Epstein
- Trump atangaza uwezekano wa kutuma meli nyengine ya kubeba ndege za kivita katika Ghuba ya Uajemi
- Trump: Makubaliano ya Iran lazima yajumuishe silaha za nyuklia, makombora na kila kitu kingine
Moja kwa moja
Na Abdalla Seif Dzungu & Asha Juma
Mahakama yaridhia pingamizi moja la Lissu

Chanzo cha picha, Getty Images
Na, Eagan Salla, Dar es salaam.
Kesi ya uhaini inayomkabili mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu imeahirishwa hadi siku ya kesho Alhamisi 12/02/2026, baada ya mahakama kuu ya Tanzania kuridhia pingamizi moja kati ya matano yaliyokuwa yamewekwa na Tundu Lissu.
Mahakama imeridhia kizimba maalumu cha kulinda utambulisho wa mashahidi wa kiraia kuwa hakikidhi vigezo vya kisheria, hivyo basi, kirekebishwe kuendana na matakwa ya kisheria na kesho shauri liendelee kwa upande wa mashitaka kuwalaeta mashahidi wao wawe wa siri au wale walio wa siri ambao ni wamoja na askari 19.
November 12, 2025, mshatakiwa Tundu Lissu aliweka mapingamizi matano akijikita zaidi kwenye namna ambavyo mashahidi wa siri walivyopatikana na namna ambavyo wangetumika kwenye shauri hili.
Pingamizi la kwanza la Lissu lilijikita kwenye kizimba maalumu kilichopo mahakamani hapo, kwa ajili ya kuwaficha mashahdi wa siri, Lissu alisema kizimba hicho hakiendani na matakwa ya kisheria.
Pingamizi la pili lilikuwa juu ya namna mashahidi hao wa siri walivyopatikana na kuombewa kibali cha mahakama, Lissu akisisitiza sheria inaelekeza mashahidi hao ni lazima wafahamike na mahakama na ijiridhishe kabla ya kutoa amri hiyo ya ulinzi.
Pingamizi la tatu Lissu alisema DDP hakueleza namna mashahidi hao wangelindwa na hakuomba matumizi ya kizimba hicho cha siri na matumizi yake yatamnyima nafasi ya kuwauliza mashahidi maswali ya dodoso kwa undani.
Kwenye pingamizi la nne Lissu alisisitiza juu ya haki na usawa iwapo mashahidi hao watalindwa kwa namna hiyo basi huenda asingetendewa haki.
Na mwisho Lissu alihoji juu ya uhalali wa sheria na kanuni zilizotumika kuwapata na kuwapatia amri ya ulinzi mashahidi hao akisisitiza yeye alikamatwa mwezi Aprili na kanuni zikapatikana mwezi Julai, hivyo, ni kama ziliandaliwa mahususi kwa ajili yake.
Maamuzi ya majaji watatu wakiongozwa na jaji Dastan Ndunguru, yakawa kizimba hicho cha siri mahakamani hapo kirekebishwe hii leo na kesho kiwe tayari kulingana na sheria inavyoelekeza ili kiweze kutumika na mashahidi hao wa siri.
Kwa upande wa viongozi wa chama chake cha Chadema wameendelea kusisitiza kwa wanachama na wapenzi wa Lissu wasivunjike moyo, bali washikamane na kuendelea kupambania demokrasia kwa nguvu.
Pia unaweza kusoma:
Habari za hivi punde, Edwin Sifuna: Katibu Mkuu wa ODM atimuliwa

Chanzo cha picha, INSTAGRAM/SIFUNA
Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimemfukuza Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kama Katibu Mkuu wa chama hicho.
Uamuzi wa kumuondoa Sifuna ulifikiwa wakati wa mkutano wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya Chama uliofanyika Mombasa Jumatano.
Chama hicho kilisema kimeazimia kumwondolea Sifuna majukumu yake mara moja.
Catherine Omanyo ambaye ni mmoja wa Naibu Katibu Mkuu, atahudumu katika nafasi hii hadi mtu anayeshikilia wadhifa huo achaguliwe.
Soma zaidi:
Watu wapoteza maisha kwa kimbunga Madagascar
Takriban watu tisa wameuawa baada ya dhoruba ya kitropiki kupiga taifa la Bahari ya Hindi la Madagascar.
Kimbunga Gezani kilitua Jumanne katika mji wa pili kwa ukubwa kisiwani na bandari kuu ya Toamasina, kwa kasi ya upepo inayozidi kilomita mia mbili kwa saa.
Ofisi ya usimamizi wa majanga ya Madagascar ilisema 'hali ilikuwa mbaya' - ikiripoti kwamba nyumba zilianguka katika eneo lililoathirika, ambapo miili ilipatikana.
Ilisema barabara hazifikiki huku miti iking'olewa, nguzo za umeme zimeanguka na asilimia tisini ya paa ziking’olewa.
Hili limetokea chini ya wiki mbili baada ya dhoruba nyingine ya kitropiki, Fytia, kuua watu 14.
Vikwazo vya Marekani kwa Urusi juu ya biashara ya mafuta ya Venezuela ni ubaguzi - Lavrov

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema Jumatano kwamba vikwazo vipya vya Marekani kuhusu jukumu la Urusi na nchi zingine katika biashara ya mafuta ya Venezuela ni ubaguzi wa wazi.
Urusi ilisema mapema Jumatano kwamba Moscow ilipanga kutafuta ufafanuzi kutoka Marekani kuhusu vikwazo hivyo vipya.
Wizara ya Fedha ya Marekani siku ya Jumanne ilitoa leseni ya jumla ili kuwezesha utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi nchini Venezuela. Leseni hiyo haikuidhinisha miamala inayohusisha raia au vyombo vya Urusi na China.
Lavrov alisema Urusi ilikuwa inawasiliana na Marekani kuhusu suala hilo na ilitaka ushirkiano unaoheshimu pande zote "bila wazo la kutawala".
Soma zaidi:
Iran yasema haitajadili juu ya uwezo wake wa makombora

Chanzo cha picha, European Photopress Agency
Mshauri wa kiongozi mkuu wa Iran alisema siku ya Jumatano, uwezo wa makombora ya Iran ni suala ambalo "si mada ya kujadiliwa", huku Iran na Marekani zikitarajia kufanya duru mpya ya mazungumzo ili kuepusha migogoro.
Wanadiplomasia wa Marekani na Iran walifanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja wiki iliyopita huko Oman, huku kukiwa na ongezeko la meli za kikanda kutokana na Marekani kutishia Iran.
"Uwezo wa makombora wa Jamhuri ya Kiislamu hauwezi kujadiliwa," Ali Shamkhani alisema kulingana na vyombo vya habari vya serikali wakati akionekana katika hafla ya kuadhimisha miaka 47 ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Marekani kwa muda mrefu imekuwa ikitaka kupanua mazungumzo kuhusu uwezo wa nyuklia wa Iran pia kujumuisha mpango wake wa makombora.
Iran imesema iko tayari kujadili vikwazo dhidi ya mpango wake wa nyuklia kwa mabadilishano ya kuondolewa vikwazo, lakini imekataa mara kwa mara kuhusisha suala hilo na masuala mengine ikiwemo makombora.
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu anatarajiwa kutumia mkutano na Trump huko Marekani kushinikiza makubaliano yoyote kati ya Marekani na Iran yajumuishe vikwazo kwenye makombora ya Tehran.
Siku ya Jumapili, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Abbas Araqchi alisema mpango wa makombora wa Tehran haujawahi kuwa sehemu ya ajenda ya mazungumzo.
Soma zaidi:
Ghana yatangaza Jumatano kuwa 'Siku ya kuvaa Fugu' vazi la kitamaduni baada ya kejeli mtandaoni

Chanzo cha picha, Zambia's Ministry of Information and Media/X
Ghana imetenga kila Jumatano kama siku ya kuvaa vazi la kitamaduni la nchi hiyo, fugu, siku chache baada ya kuzua mjadala mtandaoni na Wazambia.
Vazi hilo lilipata umaarufu wiki iliyopita wakati Rais John Dramani Mahama alipolivaa wakati wa ziara ya kitaifa nchini Zambia, ambapo baadhi waliliita kwa kejeli "blauzi," na kusababisha mwitikio mkali kutoka kwa Waghana mtandaoni.
Waziri wa Utalii wa Ghana Abla Dzifa Gomashie alisema Jumanne kwamba kuvaa vazi hilo kila wiki kutasaidia kuonyesha utambulisho wa nchi hiyo "kwa fahari katika jukwaa la kimataifa".
Alihimiza kuvaa vazi hilo "aina zake zote, miundo, na mishono yake mbalimbali, likiongezewa na nakshi zake zake za kipekee zenye kuvutia".
Fugu, ambayo pia inajulikana kama batakari, ni nguo ya kitamaduni inayovaliwa seheme ya juu ya mwili kutoka kaskazini mwa Ghana iliyotengenezwa kwa vipande vyembamba vya kitambaa kinene cha pamba vilivyoshonwa pamoja ili kuunda vazi lenye muundo wa mtindo wa poncho.
Zaidi ya umuhimu wake wa kitamaduni, Gomashie alisema maonyesho ya kila wiki ya mavazi hayo "yataleta faida kubwa za kijamii na kiuchumi" hasa kwa wafumaji, wabunifu, mafundi na wafanyabiashara wa ndani.
"Serikali inatumai kwamba mtindo wa kuvaa Fugu kutaimarisha umoja wa kitaifa, kuchochea uchumi wa ubunifu, na kutumika kama ishara yenye nguvu ya kujiamini kitamaduni na kujieleza Kighana," waziri huyo aliongeza.
Mavazi hayo yamekuwa maarufu kwenye mitandao ya kijamii kwa siku kadhaa kufuatia utani kati ya Waghana na Wazambia.
Mjadala huo uliwafanya Waghana, wakiwemo wabunge, kufurika kwenye mitandao ya kijamii wakionyesha kwa fahari nguo zao aina ya fugu, huku Wazambia wakionekana wakiwa wamevaa mavazi yao ya kitamaduni yanayojulikana kama siziba.
Mazungumzo hayo ya mtandaoni yalivutia nadhari ya Rais wa Zambia Hakainde Hichilema, ambaye alitangaza kwamba nchi yake ingeagiza nguo za fugus kutoka Ghana.
Pia unaweza kusoma:
Shambulizi la Urusi laua baba na watoto watatu, Ukraine inasema

Chanzo cha picha, Ukraine's DSNS emergencies service/Kharkiv region
Mashambulizi ya anga ya usiku kucha ya Urusi yamesababisha vifo vya takriban watu wanne, wakiwemo watoto wadogo watatu katika mkoa wa kaskazini-mashariki wa Kharkiv nchini Ukraine, maafisa wa eneo hilo wamesema.
Afisa wa eneo hilo Oleh Synegubov amesema wavulana wawili, wote wenye umri wa miaka miwili, msichana wa mwaka mmoja na mwanamume wa miaka 34 walifariki baada ya ndege isiyo na rubani kushambulia nyumba yao.
Mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka 35 na mwanamke mwingine, 73, walijeruhiwa katika shambulizi hilo, Synegubov alisema.
Shambulio la anga la Urusi linatokea wakati Moscow ikifanya mashambulizi mapya baada ya kuyasitisha kwa wiki moja ambayo Donald Trump alikuwa amemtaka Vladimir Putin azingatie msimu wa baridi kali unaoendelea Ukraine.
Bohodukhiv, kaskazini-magharibi mwa mji wa pili kwa ukubwa wa Kharkiv nchini Ukraine, imekuwa ikishambuliwa karibu kila siku na Urusi katika siku za hivi karibuni.
Siku ya Jumatatu, mwanamke mwenye umri wa miaka 41 na mvulana mwenye umri wa miaka 10 waliuawa katika mji huo, Synegubov alisema.
Urusi ilianzisha mashambulizi nchini Ukraine mnamo Februari 2022.
Soma zaidi:
Marubani wauawa baada ya ndege iliyobeba abiria kufyatuliwa risasi ikitua huko Papua

Chanzo cha picha, Smartair
Polisi wa Indonesia wamesema Jumatano kwamba rubani na rubani msaidizi wa ndege ndogo ya kibiashara wamefariki baada ya washambuliaji wasiojulikana kuifyatulia risasi ndege yao ilipokuwa ikitua katika eneo la mashariki mwa nchi ya Papua.
Ndege ya Smart Air, iliyokuwa na abiria 13 pamoja na marubani, ilitua katika uwanja wa ndege wa Korowai huko Boven Digoel, eneo la Papua Kusini, Jumatano saa 11.17 asubuhi kwa saa za eneo, msemaji wa polisi wa eneo hilo Cahyo Sukarnito aliambia Reuters.
Wakati ufyatuaji risasi ulipoanza, marubani na abiria waliiacha ndege hiyo na kuelekea eneo la msitu karibu na uwanja wa ndege, Ndege ya Smart Air ilisema.
Rubani na rubani msaidizi waliuawa lakini abiria wote walikuwa salama.
Cahyo alisema haijafahamika ni nani aliyetekeleza shambulio hilo, baada ya kuulizwa kuhusu uwezekano wa kuhusika kwa makundi ya waasi ya Papua.
Smart Air haikujibu mara moja ombi la Reuters la kutoa maoni.
Pia unaweza kusoma:
Netanyahu kukutana na Trump huku mazungumzo ya nyuklia ya Iran yakifikia hatua muhimu

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Ziara ya Netanyahu siku ya Jumatano inaashiria safari yake ya sita nchini Marekani tangu Trump arejee ofisini (Picha ya faili) Rais Donald Trump atakuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya White House siku ya Jumatano, huku mvutano ukiendelea kuongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati na mazungumzo yakizidi kupamba moto kuhusu kuzuia mpango wa silaha za nyuklia wa Iran.
Netanyahu anatarajiwa kumshinikiza Trump kutekeleza makubaliano ambayo yatasimamisha urutubishaji wa uranium ya Iran, na kudhibiti uungaji mkono wake kwa vikundi vya wakala kama Hamas na Hezbollah.
"Nitawasilisha kwa rais mtazamo wetu kuhusu kanuni za mazungumzo haya," Netanyahu aliwaambia waandishi wa habari kabla ya kuondoka kuelekea Marekani.
Iran imesema haitazuia urutubishaji wa madini ya uranium isipokuwa mataifa ya Magharibi yatapunguza vikwazo ambavyo vimezorotesha uchumi wake.
Ziara ya Netanyahu siku ya Jumatano inaashiria safari yake ya sita nchini Marekani tangu Trump arejee madarakani - zaidi ya kiongozi yeyote duniani.
Mshirika wa karibu wa Trump, Netanyahu kwa muda mrefu amekuwa akisema kuwa Iran inawakilisha tishio la usalama lililopo kwa Israeli na ameisukuma Marekani kuzuia ushawishi wa Tehran katika eneo hilo.
"Waziri Mkuu anaamini kwamba mazungumzo yoyote lazima yajumuishe kupunguza makombora ya balestiki na kukomesha msaada kwa mhimili wa Iran," ofisi ya Netanyahu ilisema katika taarifa kabla ya safari yake.
Ziara hiyo inakuja huku Marekani ikiongeza uwepo wake wa kijeshi katika Mashariki ya Kati, huku Trump akiionya Tehran kuchukua hatua iwapo itashindwa kufikia makubaliano ya nyuklia.
Mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zambia Lungu aamriwa kusalimisha magari 79, kituo cha mafuta na nyumba za kifahari

Chanzo cha picha, The National Prosecution Authority of Zambia
Maelezo ya picha, Waendesha mashtaka wa serikali walichapisha picha kadhaa kwenye Facebook za mali iliyoporwa ya Dalitso Lungu, kikiwemo kituo cha mafuta. Mahakama Kuu ya Zambia imeamuru kukamatwa kwa mali zenye thamani ya zaidi ya $1.3m (£923,000) kutoka kwa Dalitso Lungu, mtoto wa Rais wa zamani Edgar Lungu.
Agizo la unyakuzi linajumuisha magari 79 na vipande 23 vya ardhi na mali isiyohamishika, ikiwa ni pamoja na maduka makubwa, kituo cha petroli, "ghorofa za kifahari na makao makuu" katika mji mkuu, Lusaka.
Hukumu hiyo ilisema mtu huyo mwenye umri wa miaka 39 na kampuni yake wameshindwa kutoa maelezo ya kuaminika na yanayoweza kuthibitishwa kuhusu jinsi mali hizo zilivyopatikana kihalali.
Edgar Lungu, ambaye aliongoza Zambia kwa miaka sita kutoka 2015, alifariki nchini Afrika Kusini Juni mwaka jana lakini bado hajazikwa kwa sababu ya vita vya kisheria vinavyoendelea kati ya familia yake na serikali ya sasa.
Inafuatia mzozo wa muda mrefu kati ya Lungu na mrithi wake, Rais Hakainde Hichilema, ambaye alimshinda katika uchaguzi wa 2021 kwa tofauti kubwa.
Serikali ya Hichilema inataka mabaki yake kurejeshwa nyumbani na kufanyiwa mazishi ya serikali, kwa heshima kamili ya serikali - na mahakama ya Afrika Kusini iliamua kuwaunga mkono mwezi Agosti.
Lakini familia inataka mazishi ya kibinafsi nchini Afrika Kusini kwani wanasema rais huyo wa zamani hakutaka Hichilema ahudhurie mazishi yake.
Mpango wazinduliwa kuongeza muhula wa Rais Zimbabwe

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Emmerson Mnangagwa, aliyewahi kuwa makamu wa Robert Mugabe, anatarajiwa kuachia ngazi mwaka 2028 Baraza la mawaziri la Zimbabwe limeidhinisha rasimu ya sheria ambayo itamruhusu Rais Emmerson Mnangagwa, 83, kuongeza muda wake wa kukaa madarakani hadi angalau 2030.
Marais wangechaguliwa na wabunge badala ya kura ya moja kwa moja na wanaweza kuhudumu kwa muda usiozidi mihula miwili ya miaka saba, badala ya mihula ya sasa ya miaka mitano, chini ya mapendekezo hayo.
Waziri wa Sheria Ziyambi Ziyambi alisema mashauriano ya umma yatafanyika kabla ya mswada huo kuelekea bungeni kwa mjadala, ambapo mabunge yote mawili yanaongozwa na chama tawala cha Zanu-PF.
Changamoto za kisheria zinawezekana kwani wataalam wa kikatiba wanahoji kuwa kura ya maoni inahitajika ikiwa ukomo wa muda utabadilishwa - na pia wanasema kuwa marekebisho hayo hayawezi kumnufaisha rais aliyepo.
Mnangagwa, ambaye aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2017 baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe, alishinda uchaguzi wa urais mwaka uliofuata na muhula wa pili 2023 - ingawa matokeo yalipingwa.
Anajulikana kama "mamba" kwa sababu ya ujanja wake wa kisiasa, muhula wake wa mwisho wa miaka mitano unatarajiwa kumalizika mnamo 2028.
Katika kura ya maoni iliyofanyika miaka 13 iliyopita, Wazimbabwe waliipigia kura kwa wingi katiba mpya ambayo ilianzisha ukomo wa mihula ya urais wakati ung'ang'anizi wa Mugabe madarakani ulionekana kuimarika - aliiongoza nchi hiyo tangu uhuru mwaka 1980.
Britney Spears auza haki za muziki wake

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Mwanamuziki Britney Spears Mwimbaji nyota wa muziki aina ya Pop Britney Spears ameuza haki za orodha yake yote ya muziki, BBC imebaini.
Spears, 44, inasemekana aliuza haki hizo kwa mchapishaji huru wa muziki wa Primary Wave tarehe 30 Desemba kwa karibu $200m (£146m).
Mwimbaji huyo - ambaye uhifadhi wake wa muda mrefu uliamuru maisha yake ya kibinafsi na kitaaluma - anajulikana kwa vibao ...Baby One More Time, Oops!... I Did It Again, Toxic na Gimme More.
Primary Wave haikujibu mara moja maombi ya BBC ya kutoa maoni.
Wawakilishi wa Spears walikataa kutoa maoni.
Mnamo Januari 2024, mwimbaji huyo alisema "hatarudi tena kwenye tasnia ya muziki".
Wimbo wake wa mwisho aliimba pamoja na mwanamuziki Elton John mnamo 2022.
Habari za hivi punde, Tunachojua kufikia sasa kuhusu shambulio la Shule nchini Canada
Iwapo unajiunga nasi, haya ndiyo mapya zaidi kuhusu ufyatuaji risasi wa watu wengi ambao ulifanyika katika jumuiya tulivu ya Tumbler Ridge, British Columbia:
- Polisi wanasema mshambuliaji aliwaua watu tisa kabla ya kujiua siku ya Jumanne
- Waathiriwa sita walipatikana wakiwa wamekufa ndani ya shule ya Sekondari ya Tumbler Ridge, huku mtu wa saba akifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali.
- Mwili wa mshambuliaji pia ulipatikana shuleni
- Watu wawili zaidi walipatikana wamekufa ndani ya makazi ya karibu
- Polisi walimtaja mshukiwa kama "mwanamke aliyevalia nguo na nywele za kahawia" katika tahadhari ya mpiga risasi iliyotumwa kwa jamii.
- Watu wengine wawili walipelekwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya au ya kutishia maisha kufuatia shambulio hilo, na takriban watu 25 walikuwa wakitibiwa majeraha yasiyo ya kutishia maisha, polisi walisema.
- Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, alisema "amehuzunishwa" na ufyatuaji risasi na kwamba serikali yake "inasimama na wakaazi wa eno hilo wanapokabili janga hili baya"
- Waziri Mkuu alighairi safari yake ijayo ya Mkutano wa Usalama wa Munich kutokana na shambulio hilo
Baba alimpiga risasi binti yake baada ya 'kubishana kuhusu Donald Trump'

Chanzo cha picha, Facebook
Maelezo ya picha, Lucy Harisson Mwanamke wa Uingereza ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na babake alipokuwa akizuru nyumbani kwake huko Texas alikuwa amebishana naye kuhusu Rais wa Marekani Donald Trump mapema siku hiyo, uchunguzi umeelezwa.
Lucy Harrison, kutoka Warrington huko Cheshire, alipigwa risasi kifuani tarehe 10 Januari 2025 huko Prosper, karibu na Dallas.
Polisi katika mji huo walichunguza kifo cha kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 kama mauaji ya bila kukusudia lakini hakuna kesi ya jinai iliyoletwa dhidi ya Kris Harrison baada ya mahakama kuu katika kaunti ya Collin kukataa kumfungulia mashtaka.
Uchunguzi wa kifo cha Lucy Harrison ulianzishwa mapema katika Mahakama ya Cheshire Coroner, ambapo mpenzi wake Sam Littler alielezea "mabishano makubwa" kuhusu Trump, ambaye alikuwa akijiandaa kuapishwa kwa muhula wake wa pili
Watu tisa wauawa kwa kupigwa risasi, wakiwemo saba shuleni Canada - Polisi

Takriban watu tisa wameuawa kwa kupigwa risasi magharibi mwa Canada, kulingana na maafisa wa polisi wa Royal Canadian Mounted Police (RCMP).
Waathiriwa sita waligunduliwa katika Shule ya Sekondari ya Tumbler Ridge kaskazini-mashariki mwa British Columbia, RCMP inasema.
Mmoja wa saba alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali.
Wengine wawili walikutwa wamekufa katika eneo lingine, ambalo polisi wanaamini kuwa lina uhusiano na tukio hilo. Takriban watu wengine 25 wamejeruhiwa.
Mtu anayeaminika kuwa mpiga risasi pia alipatikana amekufa na kile kilichoonekana kuwa ni jeraha la kujidhuru, polisi wanasema.
Wabunge wa Marekani wamtaka kakake mfalme wa Uingereza kutoa ushahidi juu ya faili za Epstein

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Mfalme Charles III wa Uingereza na ndugu yake Andrew kushoto Andrew Mountbatten-Windsor Kakake mfalme wa Uingereza anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa maafisa wa Marekani na familia ya mshtaki wake mashuhuri Virginia Giuffre kutoa ushahidi nchini humo juu ya uhusiano wake na mfadhili wa wanaonyanyasa watoto kingono Jeffrey Epstein.
Mbunge wa Democrat Ro Khanna alisema Familia ya Kifalme "haikuwa wazi", wakati mbunge Teresa Leger Fernandez, pia Mdemokrat, alisema "Mfalme anapaswa kumuelekeza kaka yake" kwenda Marekani kujibu maswali.
Mapema Jumanne, Mfalme Charles III alisema Familia yake ilikuwa "tayari kusaidia" polisi katika maswali yao.
Andrew amerudia kukana kosa lolote na kufikia suluhu nje ya mahakama na Giuffre mnamo 2022.
Trump atangaza uwezekano wa kutuma meli nyengine ya kubeba ndege za kivita katika Ghuba ya Uajemi

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Rais wa Marekani ametangaza uwezekano wa kutuma chombo kingine cha kubeba ndege pamoja na meli yake kwenye Ghuba ya Uajemi na wakati huo huo akaeleza matumaini yake kuhusu manufaa ya mazungumzo hayo na Iran.
Axios aliandika Jumanne, Februari 10, kwamba Donald Trump alisema: "Tuna meli ya wanamaji inayoelekea huko na nyingine inaweza kutumwa."
Hii inamaanisha kuwa pamoja na shehena ya ndege ya Abraham Lincoln na meli inayoandamana nayo, ambayo ni pamoja na waangamizi kadhaa na makombora ya Tomahawk, kundi lingine linatumwa kwenye Ghuba ya Uajemi.
Rais wa Marekani aliiambia Axios kwamba kwa kuwa viongozi wa Iran hawakukataza mashambulizi ya kijeshi katika mazungumzo kabla ya vita vya siku 12, wakati huu itakuwa "tofauti sana."
Bw. Trump, akiwa na matumaini kuhusu njia ya diplomasia, alisema Iran "inataka sana" makubaliano na imeingia kwenye mazungumzo kwa umakini zaidi wakati huu kwa sababu ya tishio la kijeshi.
Duru ya kwanza ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Tehran na Washington ilifanyika Ijumaa iliyopita huko Muscat, mji mkuu wa Oman, na pande hizo mbili zilikubaliana kuendelea na mazungumzo hayo.
Trump: Makubaliano ya Iran lazima yajumuishe silaha za nyuklia, makombora na kila kitu kingine

Chanzo cha picha, Reuters/Getty
Maelezo ya picha, Rais Donald Trump na mwenzake wa Iran Ali Khamenei Rais wa Marekani Donald Trump amesema katika mahojiano na Fox News kwamba makubaliano yoyote na Iran lazima yajumuishe mpango wa makombora wa Tehran pamoja na mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.
Bw. Trump, ambaye Jumanne pia alizungumza kuhusu uwezekano wa kutuma meli nyingine kwenye Ghuba ya Uajemi, alifafanua katika mahojiano na Fax News kwamba: "Watu wengi wanasema hapana, lakini nasema ningependelea kufanya makubaliano; bila shaka lazima uwe mpango mzuri.
Hakuna silaha za nyuklia, hakuna makombora, hakuna hili na hakuna vile; kila kitu unachotaka. Lakini wengine wana wasiwasi kwa sababu, kama wanavyosema Iran, Hawakuchukua hatua miaka mingi ."
Matamshi ya Bw.Trump kuhusu maudhui ya mazungumzo na Iran yanakuja wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araqchi na viongozi wengine wa Iran wanasema kwamba mpango wa makombora wa nchi hiyo "hauwezi kujadiliwa" na kwamba nchi hiyo haitaacha haki yake ya kurutubisha madini ya uranium, lakini inaweza kusitisha au kupunguza kwa muda ili kujenga imani.
Jana, J.D. Vance, makamu wa rais wa Bw. Trump alisema mjini Yerevan kwamba suala la kukandamizwa kwa umwagaji damu maandamano ya Januari nchini Iran pia liliibuliwa katika mazungumzo kati ya Tehran na Washington.
Natumai hujambo
