Ndege ya abiria yatua baharini kwa dharura Mogadishu
Vikundi vya kutoa msaada vilitumwa mara moja, na watu wote 55 walihamishwa hadi eneo salama
Muhtasari
- Milio ya risasi karibu na gereza Guinea inahusishwa na operesheni ya usalama, mamlaka inasema
- Ndege iliyobeba raia yatua baharini kwa dharura Mogadishu
- Marekani kujiondoa UN kutakuwa na athari kubwa - Kenya
- Wabunge Marekani waishutumu idara ya sheria kwa 'kuhariri' faili za Epstein 'vibaya'
- Marekani yatoa mwongozo mpya kwa meli zake zinazopita njia ya Iran
- Eswatini yakasirisha uongozi wa kijeshi Madagascar kwa kumkaribisha kiongozi aliyeondolewa madarakani
- Wabunge Burkina Faso waidhinisha marufuku ya vyama vya kisiasa
- China iko tayari kuisaidia Cuba kutokana na uhaba wa mafuta ya ndege
- Shambulio la Urusi laharibu kituo cha nishati Ukraine
- Afisa Mkuu wa Usalama wa Iran asafiri Oman, akibeba ujumbe muhimu kuhusu nyuklia kwa Marekani
- Mfalme wa Uingereza 'ana wasiwasi' huku polisi wakichunguza mashtaka yanayohusiana na Epstein dhidi ya kaka yake
- Chadema haitambui siku 100 za madaraka ya Rais Samia -Heche
- Wamiliki wa Instagram na YouTube waliunda 'mashine za uraibu', kesi inaendelea
- Albanese asikitishwa na vurugu za maandamano dhidi ya ziara ya rais wa Israel huko Sydney
- Starmer awaambia nini wabunge wake kuhusu kushinikizwa kujiuzulu?
- Nchi ya Kiislamu inakuwa ya kwanza kutuma wanajeshi Gaza
- Baridi kali jijini New York yasababisha vifo vya watu 18
- Trump atishia kuzuia kufunguliwa kwa daraja linalounganisha Marekani na Canada
- Wapalestina waituhumu Israel kwa 'kunyakua ardhi' katika Ukingo wa Magharibi
- Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki: Utawala wa Iran hauwezi kuangushwa kwa shambulio la anga
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Asha Juma
Milio ya risasi karibu na gereza Guinea inahusishwa na operesheni ya usalama, mamlaka inasema
Mamlaka nchini Guinea imesema milio ya risasi iliyosikika karibu na gereza kuu la Conakry inahusishwa na operesheni ya usalama ndani ya kituo hicho.
Katika taarifa ya Jumanne, mwendesha mashtaka mkuu katika mahakama ya Rufaa ya Conakry, Fallou Doumbouya, alisema vikosi vya usalama vilifanya "operesheni ya ukaguzi na msako ambayo haikutangazwa" siku ya Jumatatu.
Lengo lilikuwa kukamata vitu vilivyopigwa marufuku, ikiwa ni pamoja na simu za mkononi na silaha kama vile visu, mikasi na uma.
Doumbouya alisema mfungwa mmoja, Aboubacar Diakité, anayejulikana pia kama "Toumba," alikataa kutoa ushirikiano na kutoa vitisho dhidi ya maafisa wa usalama. Tabia yake ilizua mvutano kati ya wafungwa wengine na, kulingana na mwendesha mashtaka, "ilihatarisha usalama wa kituo hicho."
Hakutoa maelezo kuhusu ni kwa nini milio ya risasi iliripotiwa kusikika Jumanne asubuhi wala hakutoa maelezo ya kina ya kile ambacho kituo hicho ilikabiliana nacho.
Diakité amehamishwa hadi Gereza Kuu la Coyah, katika eneo la Kindia, ili "kudumisha utulivu wa umma na kuhakikisha usalama wa wafungwa wengine na wafanyakazi wa magereza," Doumbouya alisema.
Aboubacar Diakité ni msaidizi wa zamani wa Kapteni Moussa Dadis Camara, rais wa zamani wa muda wa Guinea. Kwa sasa yuko kizuizini kuhusiana na mauaji ya uwanjani mwaka 2009 na amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela.
Ndege ya abiria yatua baharini kwa dharura Mogadishu

Chanzo cha picha, Starsky
Ndege ya raia iliyokuwa na watu 55 imetua baharini karibu na uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Adde mjini Mogadishu baada ya rubani kufanya uamuzi wa kutua karibu na ufuo kufuatia hitilafu ya kiufundi, abiria na wafanyakazi wote wameokolewa salama.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Somalia imesema ndege hiyo ilipaa kutoka Mogadishu kuelekea Galkayo, mji mkuu wa mkoa wa Mudug, wakati hitilafu iliporipotiwa muda mfupi baada ya kupaa na marubani waliomba kurejea.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Ahmed Macalin Hassan, ndege hiyo ilitua lakini haikuweza kusimama kwenye barabara yake, na kuelekezwa hadi eneo la baharini karibu na uwanja wa ndege.
Abiria wapatao 50 na wafanyakazi watano walikuwa ndani ya ndege hiyo.
Vikundi vya kutoa msaada vilitumwa mara moja, na watu wote 55 walihamishwa hadi eneo salama. Hakuna vifo au majeraha makubwa yaliyoripotiwa.
Shirika la ndege, Starsky, lilisema limeanzisha uchunguzi kuhusu tatizo la kiufundi na kupongeza uamuzi wa kijasiri wa rubani kutua karibu na bahari, ikibaini kuwa hatua hiyo ilikuwa muhimu katika kuokoa maisha ya watu wote ndani ya ndege hiyo.
Maafisa wa usafiri wa anga wanasema uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini sababu hasa na kutathmini athari zozote kwa usalama wa ndege.
Pia unaweza kusoma:
Marekani kujiondoa UN kutakuwa na athari kubwa - Kenya

Chanzo cha picha, State House Kenya/Facebook
Rais wa Kenya William Ruto amesema kuwa uamuzi wa Marekani kujiondoa kwenye Umoja wa Mataifa utakuwa na athari kubwa duniani katika kukabiliana na majanga.
Rais Ruto alisema kuwa Kenya inatambua umuhimu wa shirika la Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu na kwamba kupungua kwa ufadhili kwa shiriki hilo kunalemaza utendakazi wake.
"Kupunguza ufadhili kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa kunadhoofisha ushirikiano wa kimataifa na kupunguza uwezo wa jumuiya ya kimataifa kukabiliana na mizozo, mgogoro y a kibinadamu, vitisho vya afya duniani na changamoto za maendeleo", alisema Rais Ruto.
Ruto alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuungana na nchi kama Kenya katika juhudi za kuimarisha mfumo wa shirika la UN.
Hili linatokea mwezi mmoja tangu Rais wa Marekani Donald Trump kutia saini amri ya kujiondoa kutoka kwa mashirika na tume 66.
Pia unaweza kusoma:
Wabunge Marekani waishutumu idara ya sheria kwa 'kuhariri' faili za Epstein 'vibaya'

Chanzo cha picha, Reuters
Wabunge wa Marekani wanasema faili zinazohusiana na mhalifu wa kingono aliyehukumiwa Jeffrey Epstein zilihaririwa vibaya kabla ya kutolewa kwake na Idara ya Sheria (DOJ).
Wabunge siku ya Jumatatu waliruhusiwa kuanza mapitio ya matoleo ambayo hayajahaririwa ya takriban kurasa milioni tatu za faili zilizotolewa chini ya Sheria ya Uwazi wa Faili za Epstein (EFTA) tangu mwezi Desemba.
"Suala kuu ni kwamba hawazingatii... sheria yangu, kwa sababu hizi zilihaririwa mnamo mwezi Machi na FBI ya Donald Trump," Mwakilishi wa wa chama cha Democratic Ro Khanna aliiambia MS NOW.
Nyaraka moja haijahaririwa tangu malalamiko ya wabunge, huku Naibu Mwanasheria Mkuu Todd Blanche akisema kwenye X: "DOJ imejitolea kwa uwazi."
Baada ya kutazama nyaraka ambazo hazijahaririwa, Massie na Khanna, ambao waliunga mkono sheria iliyolazimisha kutolewa kwa faili za Epstein mwaka jana, waliwaambia waandishi wa habari kwamba walikuwa na orodha ya watu wapatao 20 ambapo kila jina lilifutwa isipokuwa la Epstein na mshirika wake wa biashara haramu ya ngono aliyehukumiwa Ghislaine Maxwell.
Majina sita kati ya hayo yanaweza hata kuwa ya wanaume ambao "huenda wametiwa hatiani kwa kuingizwa kwao katika faili hizi", Massie alisema nje ya Ofisi ya Waziri Mkuu Jumatatu usiku, kabla ya kuchapisha faili iliyohaririwa mtandaoni na kudai maelezo zaidi.
Majina haya "yalihaririwa" kwa njia isiyofaa, Khanna alisema kwenye MS NOW.
Kujibu wasiwasi wao, Blanche alisema idara yake "imerejesha majina yote yasiyo ya waathiriwa kutoka kwenye nyaraka hizi. DOJ imejitolea kuwa na uwazi."
Soma zaidi:
Marekani yatoa mwongozo mpya kwa meli zake zinazopita njia ya Iran

Chanzo cha picha, Press Eye
Marekani imetoa mwongozo mpya Jumatatu kwa meli za kibiashara zinazopitia Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya meli kwa ajili ya usambazaji wa mafuta Mashariki ya Kati, huku mvutano ukiendelea kati ya Washington na Tehran kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Iran hapo awali ilitishia kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao sehemu fulani iko ndani ya maji yake ya eneo, na kuna kipindi ilikamata meli za kibiashara na meli za mafuta zinazopita katika eneo hilo kwa madai ya usafirishaji haramu.
Idara ya Uchukuzi ya Marekani ya Utawala wa Baharini ilizishauri meli za kibiashara zenye bendera ya Marekani kukaa mbali na eneo la bahari ya Iran iwezekanavyo na kukataa kuruhusu vikosi vya Iran kuingia ikiwa itaombwa kufanya hivyo, kulingana na mwongozo uliotolewa.
"Inapendekezwa kwamba meli za kibiashara zenye bendera ya Marekani zinazopita kwenye maji haya zisalie mbali iwezekanavyo kutoka kwenye eneo la bahari ya Iran bila kuathiri usalama wa baharini," kulingana na mwongozo uliowekwa kwenye tovuti yake.
Pia ilisema wafanyakazi hawapaswi kutumia nguvu iwapo vikosi vya Iran vitaingia kwenye meli zao.
"Ikiwa vikosi vya Iran vitaingia kwenye meli ya kibiashara yenye bendera ya Marekani, wafanyakazi hawapaswi kupinga kwa kutumia nguvu ili wao wasipande," ilisema.
Mwanadiplomasia mkuu wa Iran alisema Ijumaa kwamba mazungumzo ya nyuklia na Marekani yaliyosimamiwa na Oman yameanza vizuri na yanatarajiwa kuendelea, katika matamshi ambayo yanaweza kusaidia kupunguza wasiwasi kwamba kushindwa kufikia makubaliano kunaweza kuisukuma Mashariki ya Kati karibu na vita.
Pia unaweza kusoma:
Eswatini yakasirisha uongozi wa kijeshi Madagascar kwa kumkaribisha kiongozi aliyeondolewa madarakani

Chanzo cha picha, Eswatini government / X
Serikali ya kijeshi ya Madagaska imekosoa Eswatini kwa kumkaribisha Rais aliyeondolewa madarakani Andry Rajoelina wiki iliyopita, ikielezea ziara hiyo kama "ukiukwaji mkubwa wa uhuru wake".
Ijumaa iliyopita, serikali ya Eswatini ilishirikisha picha za Mfalme Mswati wa III akikutana na Rajoelina, ambapo mfalme alitoa wito kwa jeshi la Madagascar kurejesha utekelezaji wa katiba.
Katika taarifa yake, kiongozi wa kijeshi wa Madagascar Kanali Michael Randrianirina "alishutuma vikali" ziara hiyo na kusema kuwa "haikubaliki kisiasa".
Rajoelina alipinduliwa Oktoba iliyopita na jeshi la wasomi kufuatia wiki kadhaa za maandamano yaliyoongozwa na vijana.
Pia unaweza kusoma:
Wabunge Burkina Faso waidhinisha marufuku ya vyama vya kisiasa

Chanzo cha picha, AFP
Wabunge wa Burkina Faso waidhinisha kupigwa marufuku kwa vyama vya kisiasa huku uongozi wa kijeshi ukijaribu kuimarisha mamlaka yake katika taifa hilo uliochukuwa madaraka baada ya mapinduzi.
Wakati wa kikao cha bunge siku ya Jumatatu, wabunge 69 waliohudhuria kwa kauli moja walipiga kura kuunga mkono mswada uliowasilishwa na serikali. Muswada huo pia ulitupilia mbali sheria inayosimamia ufadhili wa vyama vya siasa na kampeni.
Kulingana na Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Émile Zerbo, hatua ya Januari 29 ilichochewa na hitaji la kupanga upya mazingira ya kisiasa ya kitaifa, kufuatia kile alichokiita mgawanyiko na mifarakano ya kijamii inayochochewa na kuzidisha kwa vyama vya kisiasa.
Ilifuatia kusimamishwa kwa mara ya kwanza kwa vyama vya kisiasa tangu 2022, wakati jeshi lilipochukua mamlaka katika mapinduzi.
Muda mfupi baada ya muswada huo kupitishwa bungeni, Zerbo alisema uamuzi huo utakaribishwa na watu wa Burkinabe, akisisitiza kuwa unaungwa mkono na mfumo wa kisheria.
Wachambuzi wanasema hii sasa inafungua njia kwa serikali ya kijeshi kufanya kazi bila upinzani - hatua iliyoshtumiwa na makundi kadhaa ya kutetea haki za binadamu.
Wiki iliyopita, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk alielezea marufuku hiyo kama hatua isiyo sahihi, na kuzitaka mamlaka kubadili uamuzi wao.
Bw. Türk alisema hatua hiyo inaondoa uwezo wa utendaji wa mashirika ya kutetea haki za binadamu.
"Badala ya kupiga marufuku vyama vya kisiasa na kuwafunga watu jela kwa kutoa maoni yao, mamlaka nchini Burkina Faso zinahitaji kutoa fursa kwa mashirika ya kiraia, ikiwa ni pamoja na watetezi wa haki za kibinadamu," alisema.

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso Wanajeshi katika nchi jirani za Mali na Niger walichukua hatua kama hizo mwaka jana, na kuibua wasiwasi kuhusu kurudi nyuma kwa demokrasia katika Afrika Magharibi.
Serikali za kijeshi za nchi tatu za AES zimeshutumiwa kwa kukandamiza mashirika ya kiraia, wapinzani wa kisiasa na waandishi wa habari.
Soma zaidi:
China iko tayari kuisaidia Cuba kutokana na uhaba wa mafuta ya ndege

Chanzo cha picha, Reuters
Wizara ya mambo ya nje ya China siku ya Jumanne ilisema hakukuwa na ripoti zozote za raia wake kukwama Cuba kutokana na mashirika ya ndege kusimamisha safari za ndege kwenda nchini humo kwa sababu ya uhaba wa mafuta ya ndege, kufuatia Marekani kuzuia usafirishaji kutoka Venezuela.
"China inaunga mkono Cuba kwa dhati katika kulinda uhuru na usalama wake wa kitaifa, na inapinga kuingiliwa na wageni," Lin Jian, msemaji wa wizara ya mambo ya nje, aliambia mkutano wa mara kwa mara na waandishi wa habari. "Siku zote tutatoa msaada na usaidizi kwa upande wa Cuba kwa uwezo wetu wote."
Cuba inategemea Venezuela kwa kiasi kikubwa cha mafuta ya ndege, lakini yamekuwa vigumu kupatikana tangu katikati ya Desemba wakati Marekani ilipozuia usafirishaji wa mafuta kwa nchi hiyo ya Amerika Kusini.
Hatua hiyo inakuja huku kukiwa na hali mbaya zaidi kisiwani humo na vitisho vinavyoendelea kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump.
Nchi hiyo imekabiliwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara, na kuwaacha Wacuba wakiwa na wakati mgumu kukabiliana na kutokuwa na umeme wa uhakika.
Kuzuiliwa kwa meli za mafuta za Venezuela zilizowekewa vikwazo na utawala wa Trump kumezidisha mgogoro wa mafuta na umeme nchini Cuba.
Trump pia ametishia ushuru kwa nchi zinazosambaza mafuta kwa Cuba, akisema Cuba "itaporomoka hivi karibuni" kwani Venezuela haitumi tena mafuta au pesa kwa mshirika wake huyo wa muda mrefu.
Ushuru huo unaweza kulenga nchi yoyote "ambayo inauza au kutoa mafuta yoyote kwa Cuba moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Rodríguez Parrilla hivi majuzi alisema kwamba taifa la Cuba lilikuwa na "haki ya kuagiza mafuta" kutoka kwa muuzaji yeyote wa mafuta aliye tayari kumuuzia "bila kuingiliwa au kutii hatua za kulazimisha za upande mmoja za Marekani".
Soma zaidi:
Shambulio la Urusi laharibu kituo cha nishati Ukraine

Chanzo cha picha, t.me/dsns_telegram
Shambulio la Urusi limaharibu kituo cha nishati katika eneo la kusini mwa Bahari Nyeusi la Ukraine la Odesa, kampuni ya umeme ya DTEK ilisema siku ya Jumanne.
"Uharibifu ni mkubwa. Matengenezo yatachukua muda mrefu kuhakikisha vifaa vinafanyakazi tena," DTEK ilisema kwenye programu ya ujumbe ya Telegram.
Gavana wa Mkoa Oleh Kiper awali alisema baadhi ya makazi katika eneo hilo yameachwa bila umeme kwa kiasi fulani.
"Usiku, adui alianzisha shambulio lingine dhidi ya miundombinu ya nishati ya eneo la Odesa," Kiper aliandika kwenye Telegram.
Miundombinu muhimu inaendesha jenereta na kazi inaendelea kurejesha usambazaji wa umeme, Kiper alisema.
Moscow imeongeza mashambulizi yake kwenye gridi ya umeme ya Ukraine na miundombinu mingine ya nishati tangu Oktoba, na kuwaacha mamilioni bila umeme hali ya hewa ikiwa baridi.
Mji wa Odesa na maeneo yanayouzunguka umekuwa ukilengwa mara kwa mara na mashambulizi.
Pia unaweza kusoma:
Uchaguzi wa Bangladesh: Kampeni zafikia kikomo

Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kufanya kampeni kwa wagombea katika uchaguzi wa 13 wa bunge nchini Bangladesh, utakaofanyika Februari 12, umekamilika.
Kampeni za uchaguzi nchini Bangladesh zilianza rasmi Januari 22, lakini kulingana na miongozo ya Tume ya Uchaguzi, lazima ziishe saa 48 kabla ya kupiga kura.
Kwa hivyo, muda wa kampeni za uchaguzi ulimalizika saa 7:30 asubuhi ya Jumanne.
Tume ya Uchaguzi ya Bangladesh imesema katika taarifa yake kwamba hakuna mikusanyiko ya hadhara au mikutano ya hadhara itakayofanyika katika eneo bunge lolote hadi saa 4:30 jioni mnamo Februari 14.
Upigaji kura nchini Bangladesh utaanza saa 7:30 asubuhi Alhamisi, Februari 12, na utaendelea hadi 4:30 jioni.
Upigaji kura utafanyika kwa wakati mmoja katika maeneo bunge 299 kati ya 300 ya nchi siku hiyo.
Hii ni mara ya kwanza kwa uchaguzi nchini humo tangu Sheikh Hasina Wajid kuondolewa mamlakani.
Chama cha Sheikh Hasina, Awami League, hakiwezi kushiriki katika chaguzi hizi kwa sababu shughuli zake zimepigwa marufuku.
Jumla ya wagombea 2,000 wanashiriki katika uchaguzi huu, wakiwemo wagombea wakujitemea zaidi ya 250.
Soma Pia:
Afisa Mkuu wa Usalama wa Iran asafiri Oman, akibeba ujumbe muhimu kuhusu nyuklia kwa Marekani

Chanzo cha picha, ISNA
Maelezo ya picha, Ali Larijani {katikati} Afisa mkuu wa usalama wa Iran amesafiri leo Jumanne kuelekea Oman, jimbo la Kiarabu Mashariki linalokuwa kimbilio la mazungumzo kati ya Tehran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu, unaolenga kuzuia shambulio linalowezekana la Marekani.
Ali Larijani, rais wa zamani wa Bunge la Iran ambaye sasa anahudumu kama katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, kimsingi ataeleza jibu la nchi yake kuhusu duru ya kwanza ya mazungumzo ya moja kwa moja yaliyoanza wiki iliyopita mjini Muscat na Wamarekani.
Larijani anatarajiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr al-Busaidi, ambaye ndiye mpatanishi mkuu katika mazungumzo hayo, pamoja na Sultan wa Oman, Haitham bin Tariq, ripoti ya shirika la habari la serikali ya IRNA iliashiria.
IRNA ilieleza mazungumzo hayo kama “ya muhimu,” bila kufafanua ujumbe ambao Larijani atabeba. Iliripoti kuwa alitoka Tehran kuelekea Muscat Jumanne asubuhi.
Iran na Marekani zilishiriki mazungumzo mapya kuhusu nyuklia wiki iliyopita huko Oman.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alipokuwa akizungumza Jumapili na wanadiplomasia mjini Tehran, alionyesha kuwa Iran itaendelea kushikilia msimamo wake kwamba inapaswa kuwa na uwezo wa kuongeza kiwango cha urani, hoja kuu ya mgongano na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye alirushia mabomu maeneo ya nyuklia ya Iran Juni mwaka jana wakati wa vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel.
Vita hivyo vilisababisha usumbufu kwa duru za awali za mazungumzo ya nyuklia kati ya Washington na Tehran.
Maelezo zaidi:
Mfalme wa Uingereza ‘ana wasiwasi’ huku polisi wakichunguza mashtaka yanayohusiana na Epstein dhidi ya kaka yake

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Mfalme wa Uingereza Mfalme Charles amezungumza kwa mara ya kwanza katika mlolongo wa maelezo mapya yanayochipuka kuhusu kashfa ya Epstein, akisema Ikulu ya Buckingham iko tayari kutoa usaidizi kwa polisi wanapochunguza madai dhidi ya kaka yake, Andrew Mountbatten-Windsor.
Msemaji wa Kasri alibainisha: “Mfalme ameonyesha wazi, kwa maneno na vitendo visivyo vya kawaida, wasiwasi wake mkubwa kuhusu madai yanayoendelea kujitokeza kuhusu mwenendo wa Bwana Mountbatten-Windsor.”
Aliongeza: “Ingawa madai maalum ni kwa Bwana Mountbatten-Windsor kuyashughulikia, tutakapofikishwa na Polisi wa Thames Valley tuko tayari kuwasaidia na kutoa usaidizi unaotarajiwa.”
Polisi wa Thames Valley wameripoti kuwa wanakagua msingi wa malalamiko yaliyotolewa na kundi linalopingana na kifalme, Republic, ambalo liliwahi kumripoti Mountbatten-Windsor kwa tuhuma za ukiukaji wa ofisi ya umma na uvunjaji wa siri rasmi.
Barua pepe kutoka kwenye faili mpya zilizotolewa za Epstein zinaonyesha mwanamfalme huyo wa zamani akiwasilisha taarifa za ziara zake Singapore, Hong Kong na Vietnam, pamoja na maelezo ya siri kuhusu fursa za uwekezaji.
Pia Unaweza Kusoma:
Chadema haitambui siku 100 za madaraka ya Rais Samia -Heche

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Upinzani Tanzania Chadema, John Heche, amesema chama chao hakitambui siku 100 za Rais Samia Suluhu madarakani na kusisitiza kwamba hatua za kurekebisha hali ya sasa zinapaswa kuanzia na uchaguzi mpya.
Akizungumza katika mahojiano na BBC Swahili, Heche alieleza kuwa “kwa sababu uchaguzi haukufanikiwa, hatutambui waliopo madarakani kwa sababu wamejipachika kiholela. Kinyume na Katiba yetu, wametumia nguvu na silaha kudhibiti madaraka na kuua watu wengi.”
Alisisitiza kuwa tatizo halipo kwenye upinzani, bali kwenye ukosefu wa utaratibu: “Hatujasusia uchaguzi; hakuna kura zilizopigwa na kuhesabiwa ipasavyo, hakuna utaratibu uliofuatwa. Uchaguzi wa kweli unapaswa kuruhusu wananchi kupiga kura kwa huru, matokeo kuhesabiwa na kutangazwa kwa uwazi.”
Alipoulizwa kuhusu mustakabali wa maridhiano nchini Tanzania, Heche alisisitiza kuwa tume zilizoundwa na serikali ili kuchunguza matukio ya Oktoba 29 hazina mamlaka, kwani “huwezi kuwa hakimu wa kesi yako mwenyewe. Huu ni uhalifu, kuua na kuuharibu utu wa nchi yetu, na serikali inajiita yenyewe haki.”
Aidha, alibainisha changamoto zinazokumba maridhiano ya kisiasa, akisema: “Hali ya maridhiano yenyewe imedhihirisha kuwa haijalindwa na Katiba mpya. Hatuna suluhisho la kweli mpaka wananchi waamue kiongozi wao kupitia uchaguzi huru na wa haki.”
Aliongeza kuwa Chadema haiwezi kufanya maamuzi makubwa bila vikao vya chama na kuzingatia maoni ya wanachama: “Watu wamepoteza ndugu zao na bado hawajapewa haki. Waliotekeleza uhalifu bado wako kwenye madaraka bila kuadhibiwa. Hali hii haiwezi kuendelezwa kupitia maridhiano tu.”
Heche aliishia kwa kusisitiza kuwa suluhisho la moja kwa moja ni “kuwapa wananchi nafasi ya kufanya uchaguzi mpya, ili wateue kiongozi wanayempenda. Ndiyo njia rahisi na salama ya kutoka kwenye mgogoro huu.”
Pia unaweza kusoma:
Wamiliki wa Instagram na YouTube waliunda 'mashine za uraibu', kesi inaendelea

Chanzo cha picha, Reuters
Kampuni kubwa zaidi za mitandao ya kijamii duniani zimeshutumiwa kwa kuunda "mashine za uraibu" huku kesi ya kihistoria likianza kusikilizwa huko California Marekani, kuchunguza athari za afya ya akili za Instagram na YouTube.
Katika hoja yake ya ufunguzi mbele ya Jaji wa Mahakama ya Juu ya Los Angeles, Carolyn B. Kuhl, Mark Lanier amedai mteja wake, ambaye ni mlalamikaji "K.G.M.," alikumbwa na matatizo ya afya ya akili kutokana na uraibu wake wa mitandao ya kijamii.
Mawakili wa Meta na YouTube wameiambia mahakama kwamba uraibu wa K.G.M. ulitokana na masuala mengine maishani mwake, wala si uzembe wao.
K.G.M. itakuwa ni jina litakalotumika wakati wa kesi hiyo, au kama Kaley G.M., kwa sababu madhara yanayodaiwa yalifanyika alipokuwa mtoto.
Lanier pia alishtaki kuwa Meta na YouTube zilishindwa kuonya juu ya hatari kwa watumiaji wachanga inayoletwa na muundo wa majukwaa yao.
Pia unaweza kusoma:
Albanese asikitishwa na vurugu za maandamano dhidi ya ziara ya rais wa Israel huko Sydney

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Waziri mkuu wa Australia, Anthony Albanese Waziri mkuu wa Australia, Anthony Albanese, amesema amesikitishwa sana kuona mapambano makali kwenye maandamano ya kupinga ziara ya rais wa Israel.
Polisi waliwakamata takriban watu 30 katika mkutano wa hadhara huko Sydney siku ya Jumatatu.
Bw Albanese alitetea uamuzi wake wa kumwalika Isaac Herzog na kusema wale ambao hawakukubaliana na ziara hiyo walipaswa kutoa maoni yao kwa amani.
Herzog alianza ziara kwa kuzuru eneo la ufyatulianaji risasi wa halaiki katika ufukwe wa Bondi, uliozilenga sherehe za Kiyahudi Disemba 2025.
Waandamanaji wanamtuhumu kwa kuchochea mauaji ya halaiki huko Gaza, tuhuma ambazo anazikana.
Wakati huo huo, idara ya polisi imejitetea ilivyodhibiti waandamanaji hao.
Video iliyoonekana ikionyesha polisi wakikabiliana kwa nguvu na kupiga waandamanaji wakati wa maandamano mjini Sydney Jumatatu usiku, huku Mbunge wa bunge la jimbo akiwemo miongoni mwa waliodaiwa kujeruhiwa katika mabishano hayo.
Kamishna wa Polisi wa NSW, Mal Lanyon, alieleza Jumanne kwamba maafisa walionesha "uwezo wa kushangaza wa kujizuia," akiongeza kuwa walifanya "walichohitajika kufanya."
Soma Pia:
Starmer awaambia nini wabunge wake kuhusu kushinikizwa kujiuzulu?

Chanzo cha picha, PA Media
Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, amewaambia wabunge wa chama chake cha Labour kwamba hatajiuzulu baada ya kiongozi wa chama chake nchini Scotland kumtaka aachie ngazi.
Waziri Mkuu Starmer alitoa maoni hayo alipokuwa akiwahutubia wabunge wa chama chake kwa zaidi ya saa moja.
Hali ya kushtusha imeendelea nchi Uingereza kutokana na kile wengi wanaona kama kushindwa kuamua kwa usahihi pale alipomteua Peter Mandelson kuwa balozi wa Uingereza mjini Washington mwaka wa 2024.
Lord Mandelson alijulikana kuwa rafiki wa Jeffrey Epstein aliyehukumiwa kwa unyanyasaji wa kingono.
Lakini barua pepe zilizotolewa na Wizara ya Sheria ya Marekani mwezi uliopita zilifichua undani wa urafiki huo hata baada ya Epstein kuhukumiwa mwaka 2008.
Soma zaidi:
Nchi ya Kiislamu inakuwa ya kwanza kutuma wanajeshi Gaza

Chanzo cha picha, Fadel Senna/AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio akisalimiana na Brigedia Jenerali wa Israel Yaakov Dolf katika Kituo cha Uratibu wa Kijeshi mnamo Oktoba 24, 2025. Shirika la utangazaji la umma la Israel linasema wanajeshi kutoka Indonesia, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu duniani, watakuwa wanajeshi wa kwanza wa kigeni kutumwa kujiunga na kikosi cha kimataifa cha kuleta utulivu huko Gaza.
Shirika hilo limesema wanajeshi hao wanatarajiwa kuwa kusini mwa Gaza, kati ya Rafah na Khan Younis.
Mkuu wa jeshi la Indonesia amewaambia waandishi wa habari kwamba maandalizi ya kutumwa kwa wanajeshi hao yameanza. Amesema askari kati ya 5,000 na 8,000 wanaweza kutumwa; lakini hakutoa maelezo ya kina ikiwemo tarehe ya kutekelezwa kwa hatua hiyo.
Soma Zaidi:
Baridi kali jijini New York yasababisha vifo vya watu 18

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Halijoto inaongezeka baada ya siku za baridi kali na theluji jijini Jumla ya watu 18 wamefariki dunia kutokana na kipindi cha baridi kali jijini New York, kwa mujibu wa meya wa jiji hilo.
Tangu mwishoni mwa Januari, jiji hilo limekumbwa na wimbi la baridi kali, likiwemo siku 13 mfululizo ambapo joto lilikuwa nyuzi joto 0°C au chini ya hapo, moja ya vipindi virefu zaidi vya baridi kali kuwahi kushuhudiwa New York katika kipindi cha miaka 60.
Mwishoni mwa wiki, mtu mwingine “alipoteza maisha mitaani katika jiji letu,” alisema Zohran Mamdani siku ya Jumatatu, akiongeza kuwa, “kila maisha yanayopotea ni msiba, na tutaendelea kuyakumbuka familia zao katika mawazo yetu.”
Alisema, “Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii kuhakikisha usalama wa wakazi wa New York, na tutaendelea kufanya hivyo. Kwa sababu joto halitarajiwi kupanda zaidi ya nyuzi 32 za Fahrenheit hadi kesho, na nyuzi 35 si hali ya joto ya kufurahisha hata kidogo.”
Ingawa joto linatarajiwa kupanda kidogo wiki hii, bado lipo chini ya wastani.
Mamdani aliwahimiza wakazi “kuendelea kuwa salama, kukaa ndani ya nyumba inapowezekana, na kujuliana hali kila mmoja.”
Shirika la Usimamizi wa Dharura la Jiji la New York (NYC Emergency Management) limesema kuwa baada ya siku kadhaa za baridi kali na theluji, hatari kubwa za kiusalama bado zipo katika maeneo mengi ya jiji.
Shirika hilo limeonya kuwa theluji na barafu vinavyoyeyuka vinaweza kudondoka kutoka juu ya majengo bila onyo, na kwamba barabara na njia za wasio tunia magari zinaweza kuganda tena wakati wa usiku.

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Jiji la New York lilikuwa chini ya onyo baridi kali mwishoni mwa juma Pia unaweza kusoma:
Trump atishia kuzuia kufunguliwa kwa daraja linalounganisha Marekani na Canada

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Daraja la Kimataifa la Gordie Howe litaunganisha kusini mwa Detroit, Michigan, Marekani, na Windsor, Ontario, Kanada litakapokamilika. Rais wa Marekani, Donald Trump, ametishia kuzuia kufunguliwa kwa daraja linalounganisha Marekani na Canada hadi Washington “ilipwe kikamilifu kwa kila kitu” ilichokitoa kwa jirani yake wa kaskazini.
Daraja la Kimataifa la Gordie Howe, linalounganisha jimbo la Ontario nchini Canada na jimbo la Michigan nchini Marekani, halitafunguliwa hadi Ottawa “itakapoitendea Marekani kwa haki na heshima tunayostahili,” Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa tovuti ya mradi huo, daraja hilo linafadhiliwa na serikali ya Canada, lakini litamilikiwa na raia wa Canada na jimbo la Michigan kwa pamoja.
Haijulikani wazi ni kwa namna gani Trump anaweza kuzuia kufunguliwa kwa daraja hilo, lakini amesema mazungumzo yataanza mara moja, bila kutoa maelezo zaidi.
Trump aliandika: “Serikali ya Canada inatarajia mimi, kama Rais wa Marekani, NIWARUHUSU tu ‘kuitumia vibaya Marekani!’”
Aliongeza: “Sitakubali daraja hili lifunguliwe hadi Marekani ilipwe kikamilifu kwa kila kitu tulichowapa.”
Daraja hilo, linalovuka Mto Detroit, linatarajiwa kufunguliwa kwa matumizi ya usafiri mapema mwaka 2026, baada ya kukamilika kwa majaribio na idhini rasmi.
Ujenzi wake ulianza mwaka 2018, lakini mradi huo umekuwa chanzo cha mvutano kati ya nchi hizo mbili kwa zaidi ya muongo mmoja.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Canada (CBC), gharama ya ujenzi wa daraja hilo inakadiriwa kufikia dola bilioni 6.4 za Canada (sawa na pauni bilioni 3.4 za Uingereza).
Soma Pia:
