Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon yaongezwa kwa wiki tatu

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon yamesogezwa mbele kwa muda wa wiki tatu, lakini akasisitiza kuwa hatakimbilia kufikia makubaliano yoyote na Iran.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga & Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Usiku mwema.

  2. Wafanyabiashara Uganda walalamikia ongezeko la kodi ya mitumba

    Wafanyabiashara wa nguo za mtumba nchini Uganda wameonyesha wasi wasi wao kuhusu hatua ya bunge kuongeza kodi kwa bidhaa hizo. Baadhi yao wanasema huenda hatua hiyo ikasababisha wengi wao kulemewa biashara hiyo.

    Haya yanajiri baada ya Bunge la Uganda mapema wiki hii kupitisha muswada ambao utaongeza maradufu kodi ya nguo za mitumba zinazoagizwa kutoka nje kutoka asilimia 15% hadi asilimia 30%.

    Iwapo raisi atatia saini muswada huo na kuidhinisha kama sheria utaanza kutekelezwa Julai Mosi mwaka huu.

    Serikali inasema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana zaidi wa kuendana na malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuondoa uagizaji wa nguo za mitumba kutoka nje na baadala yake kuvipa nafasi viwanda vya ndani vinavyotengeneza nguo.

    Kwa muda mrefu mamlaka nchini Uganda zimekuwa zikidai kwamba uagizaji wa nguo za mitumba unadhoofisha viwanda vya nguo zinazotengenezwa nchini humo na pia kuchangia uchafuzi wa mazingira kutokana na taka za nguo hizo.

    Wakosoaji wanasema kwamba kupunguza uagizaji wa mitumba unaweza kusababisha ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana walioajiriwa katika sekta ya nguo za mitumba.

  3. Kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa DRC awasili Goma inayodhibitiwa na waasi

    James Swan, Mkuu mpya wa ujumbe wa MONUSCO, amewasili Goma leo asubuhi katika ziara yake ya kwanza mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo tangu kuteuliwa kwake wiki tatu zilizopita.

    Amesema kipaumbele cha ujumbe huo ni kusukuma mbele utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, kulinda raia na kuimarisha mchakato wa amani.

    Akiwa Goma, mwanadiplomasia huyo wa Marekani anatarajiwa kukutana na timu za MONUSCO, viongozi wa waasi wa muungano wa Alliance Fleuve Congo unaojumuisha kundi la M23, pamoja na vyombo vya uthibitishaji. Amesisitiza kuwa ufuatiliaji wa amani wenye ufanisi unahitaji uhuru wa kusafiri, upatikanaji wa uwanja wa ndege, na kusitishwa kwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani pamoja na uingiliaji wa mifumo ya GPS.

    Bw. Swan alianza ziara yake mashariki mwa DRC kwa kutembelea Beni mapema wiki hii, Aprili 21, 2026, ambako Gavana aliyeteuliwa na serikali alihamishia makao yake kufuatia kuanguka kwa Goma zaidi ya mwaka mmoja uliopita, kabla ya kuendelea na ziara katika eneo la Ituri.

    James Swan aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, AntĂłnio Guterres, tarehe 6 Machi 2026 kuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa MONUSCO, akimrithi Bintou Keita wa Guinea.

  4. NATO yakataa uwezekano wa kufukuza wanachama kufuatia ripoti kuhusu Uhispania

    NATO inasema hakuna kipengele cha nchi wanachama kusimamishwa au kufukuzwa katika muungano wa kijeshi baada ya ripoti kusema kuwa Marekani inaweza kutaka kusimamisha uanachama wake wa Uhispania kutokana na msimamo wake wa vita vya Iran.

    Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez amesisitiza Ijumaa kuwa Uhispania ni mwanachama “wa kuaminika” wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, kufuatia taarifa kwamba Marekani inaweza kuwa inafikiria kuifukuza nchi hiyo kutokana na kutounga mkono vita dhidi ya Iran.

    Shirika la habari la Reuters, likinukuu afisa wa Marekani ambaye hakutajwa jina, liliripoti kuwa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilipendekeza kupitia barua pepe kwamba Uhispania ifukuzwe NATO kama njia ya kuwaadhibu washirika waliotofautiana na msimamo wa Marekani na Israel katika vita dhidi ya Iran.

    Akizungumza na waandishi wa habari pembeni ya mkutano wa Umoja wa Ulaya nchini Cyprus, Sánchez alisema:

    “Uhispania ni mwanachama wa kuaminika wa NATO na inatekeleza kikamilifu majukumu yake.”

    “Kwa hiyo sina wasiwasi hata kidogo,” aliongeza.

    Pia alisisitiza kuwa:

    “Hatuendeshi sera zetu kwa kuzingatia barua pepe, bali nyaraka rasmi na msimamo wa serikali ya Marekani.”

    Aliongeza kuwa sera ya serikali yake ni “ushirikiano kamili na washirika, lakini daima ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa.”

    Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa akikosoa mara kwa mara nchi wanachama wa NATO kwa kutoshiriki katika vita hivyo, akivitaja vitendo hivyo kama “usaliti.”

    Baadhi ya nchi kama Ufaransa, Uhispania na Italia hazikuruhusu ndege za kijeshi za Marekani kupita katika anga zao au kutumia vituo vyao vya kijeshi. Uingereza awali ilipinga, lakini baadaye iliruhusu matumizi ya vituo vyake kwa safari za Marekani zilizoelezwa kuwa za “ulinzi.”

    Trump pia alijaribu kushinikiza nchi za Ulaya wanachama wa NATO kutuma meli za kivita katika Mlango wa Hormuz, lakini juhudi hizo hazikufanikiwa. Mlango huo ambao Iran imeudhibiti kwa kiasi kikubwa kupitia vitisho na mashambulizi ya kijeshi.

    Soma zaidi:

  5. Makundi ya haki za binadamu yaonya wageni wa Kombe la Dunia Marekani

    Makundi ya haki za binadamu yamewataka mashabiki, wachezaji, waandishi wa habari na wageni wengine wa Kombe la Dunia la majira ya kiangazi kuchukua “tahadhari” wanaposafiri kwenda Marekani.

    Zaidi ya mashirika 120 yameungana kutoa tahadhari ya safari yakisema inachochewa na kile wanachokiita “ukandamizaji mkali na wa kikatili wa uhamiaji unaofanywa na utawala wa Rais Donald Trump”.

    “Kuongezeka kwa siasa za kiimla na matumizi ya nguvu kupita kiasi katika utawala wa Trump kunaleta hatari kubwa kwa wote,” imesema taarifa hiyo.

    Pia imeeleza kuwa makundi ya wachache yako katika hatari kubwa ya madhara makubwa, huku ikimkosoa Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Gianni Infantino kwa uhusiano wake wa karibu na Rais wa Marekani Donald Trump.

    Muungano huo, unaojumuisha Umoja wa Uhuru wa Kiraia wa Marekani, umeitaka FIFA kushinikiza mamlaka za Marekani kuheshimu haki za msingi za binadamu za kila mtu atakayetembelea na kuhudhuria michezo hiyo.

    Mamlaka za Marekani bado hazijatoa kauli kuhusu tahadhari hiyo, lakini FIFA imesema imejikita katika kuheshimu haki zote za binadamu zinazotambuliwa kimataifa na itajitahidi kuzilinda.

    FIFA imesema ina “ahadi ya kuheshimu haki za binadamu katika shughuli zote muhimu na wadau wote wanaohusiana na mashindano hayo,” ikitaja nyaraka na vikundi vya ushauri ilivyoanzisha kushughulikia masuala ya haki za binadamu.

    Makundi hayo ya haki za binadamu yanaonya kuhusu uwezekano wa wageni kuzuiwa kuingia nchini, kukamatwa, vizuizi vya safari kwa raia kutoka nchi kadhaa, uchunguzi wa mitandao ya kijamii, ubaguzi wa kijamii na ufuatiliaji mkali zaidi.

    Kuna marufuku ya kusafiri kwa raia kutoka nchi nne zinazoshiriki mashindano hayo: Iran, Haiti, Senegal na Ivory Coast.

    Makundi hayo yameshauri wasafiri kuchukua hatua kama kuondoa taarifa nyeti kwenye simu zao na kuwajulisha marafiki na familia mipango yao ya safari.

    Marekani itakuwa mwenyeji mwenza wa mashindano hayo pamoja na Kanada na Mexico, huku mechi 78 kati ya 104 zikitarajiwa kufanyika Marekani.

    Mwezi uliopita, ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International ilionya kuwa Kombe la Dunia linaweza kuwa “jukwaa la ukandamizaji na njia ya kuhalalisha mifumo ya kiimla”.

    Soma zaidi:

  6. Familia ya Lungu yalaani kuondolewa kwa mwili na uchunguzi bila idhini

    Familia ya aliyekuwa Rais wa Zambia Edgar Lungu imeshutumu mamlaka za Afrika Kusini na maafisa wa Zambia kwa kuondoa mwili wake kinyume cha sheria na kufanya uchunguzi wa maiti bila idhini, kwa mujibu wa taarifa yao.

    Familia hiyo imesema polisi na wawakilishi wa Zambia waliuchukua mwili huo kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti jijini Johannesburg tarehe 22 Aprili, wakitaja amri ya mahakama ya mwaka 2025. Imesema amri hiyo iliruhusu tu urejeshaji wa mwili nchini Zambia na haikuruhusu uchunguzi wa kitaalamu wa kitabibu.

    Mwili huo ulipelekwa katika kituo cha serikali jijini Pretoria, ambapo maafisa walifungua jalada wakitaja “shaka ya sumu,” madai ambayo familia hiyo imeyapinga.

    Mawakili wa familia walipata amri ya dharura ya Mahakama Kuu baadaye siku hiyo, ikiagiza mamlaka kurejesha mwili na kueleza kwa nini hawapaswi kudharauliwa mahakama.

    Familia imesema licha ya amri hiyo, uchunguzi wa maiti ulifanyika siku iliyofuata kabla ya mwili kurejeshwa tarehe 23 Aprili.

    Mamlaka za Afrika Kusini na serikali ya Zambia bado hazijatoa majibu ya hadharani kuhusu tuhuma hizo.

    Lungu, aliyekuwa Rais wa Zambia kuanzia mwaka 2015 hadi 2021, alifariki miezi kumi iliyopita.

  7. Waziri wa Iran Araqchi afanya mazungumzo ya simu na viongozi wa Pakistan

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amezungumza kwa njia ya simu na Mkuu wa Majeshi ya Pakistan, Field Marshal Asim Munir, pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Ishaq Dar, huku mustakabali wa mazungumzo ya amani na Marekani ukiwa bado haujafahamika.

    Kituo rasmi cha Telegram cha Bw. Araghchi kimesema kuwa walijadili “mabadiliko ya kikanda na masuala ya kusitisha mapigano.”

    Pakistan imeibuka kama mpatanishi mkuu katika juhudi za kumaliza vita vinavyohusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran, lakini baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo ya Aprili 11, Tehran hadi sasa imekataa kutuma ujumbe kwenda Islamabad kwa duru ya pili ya mazungumzo.

    Kituo hicho pia kimesema Bw. Araghchi alijadili pia maendeleo ya kikanda na Rais wa Mkoa wa Kurdistan wa Iraq, Nechirvan Barzani.

    Soma zaidi:

  8. ACT Wazalendo yakosoa vikali Tume ya Chande, yataka uchunguzi huru wa kimataifa

    Chama cha ACT Wazalendo kimesisitiza kuwa kimeendelea kuikataa Tume ya Chande, kikidai tangu mwanzo kuwa ilikosa uhuru na ilianzishwa kama njia ya kuwalinda wahusika badala ya kutoa haki.

    “Tume hii haikuwa huru na imethibitisha kile tulichosema tangu mwanzo,” imesema ACT Wazalendo.

    Chama hicho kimesema ripoti hiyo imefufua majeraha mapya na kuongeza maumivu kwa Watanzania kufuatia matukio ya tarehe 29 Oktoba 2025 na athari zake.

    ACT Wazalendo imesema inaendelea kuomboleza kila maisha yaliyopotea na iko pamoja na familia zote zilizoathirika na tukio hilo.

    “Tunaungana na familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika matukio ya 29 Oktoba,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

    Chama hicho pia kimeelezea wasiwasi wake kuhusu mpango wa kuundwa kwa tume nyingine ya uchunguzi wa jinai kuhusu tukio hilo hilo, kikisema hatua hiyo ni njia ya kuchelewesha haki na kupoteza fedha za walipa kodi.

    “Watanzania hawatakubali ujanja huu wa kuchelewesha haki,” imesisitiza ACT Wazalendo.

    ACT Wazalendo imesisitiza kuwa suluhu ya kweli ya kitaifa itapatikana tu kupitia uchunguzi huru, wa haki na unaokubalika na wananchi.

    Chama hicho kimependekeza kuundwa kwa uchunguzi huru wa kimataifa chini ya taasisi kama Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika au SADC.

    Chama hicho kimesema msimamo wa kina zaidi utatolewa baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Uongozi wa Taifa kitakachofanyika wiki ijayo.

    Soma zaidi:

  9. Rais wa Uganda apuuza wasiwasi wa bei ya mafuta, aeleza vipaumbele vipya

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni amepuuza wasiwasi kuhusu bei ya juu ya mafuta kwa madereva, akisema wale wasioweza kumudu wanapaswa kubaki nyumbani na kwamba hahusiki na watu wanaosafiri kwa burudani, ikiwemo kwenda vilabu vya usiku.

    Akizungumza katika Mkutano wa Africa We Build Summit 2026, Museveni alisema wasiwasi wake mkuu katika mazungumzo yake ya hivi karibuni na Rais William Ruto haukuwa ongezeko la gharama ya mafuta ya magari, bali bei ya mafuta ya ndege.

    Alieleza kuwa mafuta ya ndege yana nafasi muhimu zaidi ya usafiri wa anga, akibainisha mchango wake katika sekta ya utalii na biashara ya mauzo ya nje, akionya kuwa gharama kubwa zinaweza kupunguza idadi ya wageni na kuathiri biashara.

    Museveni alisisitiza umuhimu wa kupunguza bei ya mafuta ya ndege ili kuimarisha sekta muhimu za uchumi, huku akipuuza athari za bei ya juu ya mafuta kwa wamiliki wa magari.

    “Msingemhangaisha sana Rais Ruto kuhusu mafuta, hasa watu wanaoendesha magari barabarani. Kama mafuta ni ghali, kaeni nyumbani, mnaenda wapi,” alisema.

    “Sijali sana kuhusu nyinyi. Nilichokuwa nachojali ni mafuta ya ndege, kwa sababu si ya safari tu, bali pia utalii. Kama gharama ya mafuta ya ndege ni kubwa, watalii hawatakuja. Pia hutumika katika usafirishaji wa bidhaa nje kwa kuwa ndege zinatumika. Watu wanaoenda vilabu vya usiku na mambo mengine, siwajali sana. Kama huna fedha, kaa nyumbani. Unaenda wapi?”

    Kiongozi huyo wa Uganda aliongeza kuwa amezitaka Kenya na Uganda kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu usimamizi wa bomba la mafuta, hasa katika kuhakikisha uthabiti wa upatikanaji na bei ya mafuta ya ndege.

    “Ndiyo maana nilizungumza na Rais Ruto ili serikali za Kenya na Uganda ziwe na sauti moja kuhusu bomba la mafuta, hasa kwa sababu ya mafuta ya ndege,” alisema.

    Kauli yake inajiri wakati ambapo nchi za Afrika Mashariki zinakabiliwa na gharama ya juu ya maisha, inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na bei ya juu ya mafuta.

    Soma zaidi:

  10. Meta yapanga kupiga kalamu wafanyakazi wake na kugeukia AI

    Meta yapanga kupunguza wafanyikazi wake kwa kiwango kikubwa mwezi ujao huku ikiwekeza zaidi kwenye miradi ya akili unde(AI)

    Kampuni ya Meta imewaandikia wafanyakazi wake barua Alhamisi ikitangaza mpango wa kupunguza asilimia 10 ya wafanyakazi wake, sawa na takribani wafanyakazi 8,000. Pia imesema haitajaza nafasi nyingine elfu kadhaa zilizo wazi ambazo ilikuwa inazifanyia ajira.

    Meta inatarajiwa kutumia dola bilioni 135 (takribani pauni bilioni 100) kwenye miradi ya akili mnemba mwaka huu.

    Kiasi hicho ni sawa na matumizi yote ya sekta ya AI katika miaka mitatu iliyopita kwa pamoja.

    Msemaji wa Meta amethibitisha mpango huo wa kupunguza ajira lakini amekataa kutoa maelezo zaidi.

    Mkurugenzi mtendaji na mwanzilishi wa Meta, Mark Zuckerberg, alikuwa tayari ametoa kauli ya wazi mwezi Januari kwamba kampuni hiyo itapunguza ajira mwaka huu.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Maharamia wa Somalia wateka meli ya mafuta ya Pakistan

    Maharamia wa baharini kutoka Somalia wanaripotiwa kuteka meli ya mafuta ya Pakistan karibu na Ghuba ya Aden na kuwateka wafanyakazi wake.

    Wasiwasi umeibuliwa kuhusu usalama wa raia wa Pakistan waliokuwa ndani ya meli hiyo.

    Taarifa hizo zimeripotiwa na magazeti kadhaa nchini Pakistan.

    Gazeti la Daily Pakistan linaripoti kuwa meli hiyo ilikuwa na wafanyakazi 11 kutoka Pakistan ambao bado wanashikiliwa na haramia hao, kwa mujibu wa gazeti hilo.

    Kwa mujibu wa vyanzo, meli hiyo inayojulikana kama Owner 25 ilishambuliwa na kutekwa na haramia wa baharini.

  12. Rais wa Kenya azua mjadala kwa kauli kuhusu Kiingereza cha Wanigeria

    Rais wa Kenya William Ruto amezua mjadala mkali mtandaoni baada ya kutoa kauli iliyotafsiriwa kama kudharau lafudhi ya Waingereza wa Nigeria, akisema kuwa wakati mwingine haiwezi kueleweka bila mkalimani.

    Akizungumza na Wakenya wanaoishi nchini Italia siku ya Jumatatu, Ruto alisema: “Ukimsikiliza Mnigeria akizungumza, huwezi kuelewa anachosema unahitaji mkalimani,” huku akijigamba kuwa Wakenya huzungumza Kiingereza “miongoni mwa wazungumzaji bora zaidi duniani.”

    Kauli hiyo ilizua ukosoaji mkali kutoka kwa Wanigeria na Waafrika wengine mitandaoni, waliomshutumu kwa kuidhalilisha nchi nyingine ya Afrika.

    Mwandishi wa habari wa Zimbabwe, Hopewell Chin'ono, aliandika: “Kiingereza ni lugha ya kikoloni, si kipimo cha akili, uwezo au maendeleo ya taifa.”

    Kama nchi zilizokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza, Kenya na Nigeria zote zinatumia Kiingereza kama lugha rasmi, lakini kila moja imekuza lahaja yake ya kipekee yenye tofauti za matamshi.

    Tofauti hizi zinachangiwa na lugha za asili. Nigeria ina zaidi ya lugha 500 zinazoathiri mdundo na lafudhi ya Kiingereza chake, wakati Kenya ina mchanganyiko wa lugha za Kibantu, Kiniloti na Kikushiti unaozalisha lafudhi zake.

    Hata hivyo, katika hotuba hiyo kwa wanaoishi ughaibuni, Ruto alisisitiza kuwa mfumo wa elimu wa Kenya unazalisha umahiri mzuri wa Kiingereza, akidai kuwa mara nyingi ni vigumu kuwaelewa Wanigeria wanapozungumza lugha hiyo, kauli iliyozua vicheko miongoni mwa hadhira.

    Soma Pia:

  13. EU yataka wataalamu wa nyuklia washirikishwe katika mazungumzo ya amani na Iran

    Mbali na kuongezwa kwa muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon, mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa vitisho kutoka Iran vinaweza kuwa “hatari zaidi” ikiwa wataalamu wa nyuklia hawatahusishwa katika mazungumzo ya amani.

    Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa EU huko Cyprus, Kaja Kallas anasema kuna hatari kwamba makubaliano yoyote yanaweza kuwa dhaifu kuliko makubaliano ya nyuklia ya Iran yaliyokubaliwa mwaka 2015 wakati wa utawala wa Obama, ambayo Rais Trump alijiondoa katika muhula wake wa kwanza.

    Chini ya makubaliano hayo Iran ilikubali kupunguza shughuli zake nyeti za nyuklia na kuruhusu wakaguzi wa kimataifa kuingia nchini humo ili kuondoa vikwazo vya kiuchumi.

    "Ikiwa mazungumzo hayo yanahusu tu mpango wa nyuklia na hakuna wataalamu wa nyuklia wanaohusishwa, basi tutaishia kuwa na makubaliano dhaifu kuliko JCPOA," Kallas anasema.

  14. Hezbollah na Israel zalaumiana kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano

    Jeshi la Israel na kundi la Hezbollah wameshutumiana kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Awali, Israel ilisema ilifanikiwa kuzuia makombora kadhaa yaliyofyatuliwa kutoka Lebanon, huku ving’ora vya tahadhari vikisikika katika eneo la Shtula.

    Kwa upande wake, Hezbollah ilithibitisha kupitia Telegram kwamba ililenga eneo hilo kwa shambulio la makombora.

    Katika taarifa yake kupitia mtandao wa X, IDF ilisema pia imewaua watu watatu inaowataja kama “wanamgambo wa Hezbollah” baada ya kushindwa kufyatua kombora kuelekea ndege ya Jeshi la Israel.

    IDF pia ilidai kuwa katika matukio mawili tofauti, Hezbollah ilifyatua makombora dhidi ya wanajeshi wake walioko kusini mwa Lebanon, ikisema kuwa hatua hizo ni “uvunjaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano.”

    Hata hivyo, Hezbollah ilijibu Alhamisi jioni ikisema ilifyatua makombora kuelekea kaskazini mwa Israel kama kujibu kile ilichokiita “uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano” uliofanywa na Israel.

    Wakati huohuo, Shirika la Habari la Taifa la Lebanon linaripoti kuwa Israel imefanya mashambulizi katika mji wa Tyre ulioko kusini mwa nchi hiyo asubuhi ya leo.

    Unaweza kusoma pia:

  15. Mataifa ya Afrika Mashariki kuanzisha mradi wa pamoja wa kiwanda cha mafuta

    Nchi za Afrika Mashariki zinaendelea kujadili mpango wa kujenga kiwanda cha pamoja cha kusafishia mafuta katika bandari ya Tanga, Tanzania, kwa mfano wa kiwanda cha Dangote cha Nigeria, amesema rais wa Kenya William Ruto siku ya Alhamisi.

    Kwa sasa, Afrika Mashariki huagiza mafuta yote yaliyosafishwa, hasa kutoka Mashariki ya Kati, hali inayofanya eneo hilo kuwa katika hatari ya kupanda kwa bei na usumbufu wa upatikanaji wa mafuta, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa mzozo wa Iran.

    “Tutakuwa na kiwanda cha pamoja cha kusafishia mafuta Tanga ambacho kitawanufaisha wote, kwani kitachakata mafuta kutoka Jamhuri ya demokrasia ya Congo, Kenya, Sudan Kusini na Uganda,” alisema Ruto katika mkutano wa ufadhili wa miundombinu uliofanyika Nairobi.

    Mfanyabishara tajiri zaidi barani Afrika, Aliko Dangote, ambaye pia alihudhuria mkutano huo, alisema anaweza kuanzisha mradi Afrika Mashariki kama wa kiwanda chake cha Nigeria kinachozalisha mapipa 650,000 ya mafuta kwa siku, endapo serikali za eneo hilo zitaunga mkono mpango huo.

  16. Mwanajeshi wa Marekani aliyeshiriki operesheni ya Maduro akamatwa baada ya kushinda kamari

    Serikali ya Marekani inamshikilia wanajeshi mmoja aliyeshiriki katika operesheni ya kumkamata aliyekuwa rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, kwa tuhuma za kutumia taarifa za siri kufanya biashara katika kamari za kidijitali maarufu kama Polymarket.

    Mamlaka nchini Marekani imemfungulia mashitaka Gannon Ken Van Dyke, mwanajeshi wa kikosi maalum, kwa kutumia taarifa za siri kufanya biashara kwenye masoko yanayohusiana na mpango wa kumwondoa Maduro madarakani.

    Serikali imesema kitendo hicho kinahesabika kama biashara kwa kutumia taarifa za siri chini ya sheria za shirikisho ni kosa la jinai.

    Van Dyke, aliyekuwa akifanya kazi katika kambi ya Fort Bragg, North Carolina, anadaiwa kupata zaidi ya dola 409,000 kutokana na mchezo huo.

    Unaweza kusoma pia:

  17. Muda wa ziada wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon haujashusha bei ya mafuta

    Bei ya mafuta ilipanda Ijumaa barani Asia licha ya kutangazwa kwa kuongezwa kwa muda wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon.

    Brent, kiwango cha kimataifa cha mafuta ghafi, iliongezeka kwa 0.7% hadi dola 105.80 (ÂŁ78.60) kwa pipa, huku mafuta ya Marekani yakipanda kwa 0.6% hadi dola 96.50 kwa pipa.

    Hata hivyo, mapigano kati ya Israel na Lebanon yanatishia kudhoofisha usitishaji huo dhaifu wa mapigano unaohusisha Marekani na Iran, baada ya Tehran kusema masharti ya makubaliano hayo yamekiukwa.

    Bei ya mafuta imekuwa ikipanda tangu Donald Trump alipotangaza kuwa Marekani itasitisha mashambulizi hadi Iran itakapowasilisha “pendekezo la pamoja.”

    Wakati huohuo, usafirishaji katika Mlango wa Bahari wa Hormuz bado unasuasua kwa kiasi kikubwa, hali inayovuruga usafirishaji wa mafuta duniani.

    Unaweza kusoma pia:

  18. Usitishaji mapigano Lebanon si wa uhakika kwa 100% - Israel

    Balozi wa Israel katika umoja wa mataifa anasema hana uhakika kuhusu hatua ya kusogezwa mbele usitishaji mapigano kama itakomesha mzozo kati ya Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon.

    "Serikali ya Lebanon haidhibiti Hezbollah," Danny Dannon anasema katika mahojiano na CNN.

    "Hezbollah inatuma makombora kujaribu kuhujumu usitishaji mapigano, na Israel - tunapaswa kulipiza kisasi. Kila wakati tunapoona tishio, tunachukua hatua."

    Maoni yake yanakuja baada ya mabalozi wa Israeli na Lebanon nchini Marekani kukutana katika Ikulu ya White House ambapo Trump alitangaza kuongeza wiki tatu za usitishaji mapigano baada ya siku 10 za sasa.

    "Hayana uhakika wa 100%," anasema akimaanisha makubaliano mapya.

    "Natumai ... kuona kwamba jeshi la Lebanon linaweza kutekeleza usitishaji huu wa mapigano."

    Unaweza kusoma pia:

  19. Papa alaani mauaji ya waandamanaji nchini Iran, asisitiza msimamo wake dhidi ya vita

    Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Leo siku ya Alhamisi alilaani vikali mauaji ya waandamanaji nchini Iran, kufuatia ukosoaji kutoka kwa rais wa Marekani Donald Trump wiki iliyopita kwa madai kuwa hakuchukua msimamo huo wazi alipokuwa akizungumzia vita vinavyohusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Akiwa papa wa kwanza kutoka Marekani, Leo pia alilaani vifo vya raia wengi katika mzozo huo na kueleza masikitiko yake kuhusu kuvunjika kwa mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Iran.

    Alitoa kauli hizo akiwa ndani ya ndege akirejea Roma baada ya ziara yake barani Afrika.

    “Ninalaani vitendo vyote visivyo vya haki. Ninalaani kuuawa kwa watu,” alisema papa alipokuwa akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu ripoti za kuuawa kwa waandamanaji nchini Iran.

    Aliongeza kusema kuwa pale ambapo serikali au taifa linachukua maamuzi yanayosababisha vifo vya watu bila haki, hatua hiyo inapaswa kulaaniwa wazi.

    Hapo awali, Aprili 12, Trump alimshambulia Papa Leo kupitia mitandao ya kijamii akimuita “asiyefaa,” baada ya kiongozi huyo wa kanisa Katoliki kuonekana kukosoa vikali vita vya Iran pamoja na sera za kupinga uhamiaji za rais huyo.

    Katika chapisho lingine siku mbili baadaye, Trump alihoji ikiwa kuna mtu angemfahamisha Papa Leo kuhusu vifo vya waandamanaji nchini Iran.

    Unaweza kusoma pia:

  20. Iran haijazuiwa kushiriki Kombe la Dunia - Marekani

    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema hakuna mamlaka yoyote ya Marekani iliyowaambia wanamichezo wa Iran kuwa hawaruhusiwi kushiriki mashindano ya kombe la dunia FIFA yatakayofanyika nchini humo msimu huu wa joto.

    Amesema kumekuwa na uvumi kuwa Iran huenda isishiriki na kwamba Italia inaweza kuchukua nafasi yao, lakini akaongeza kuwa ikiwa Iran haitashiriki, huo utakuwa uamuzi wao wenyewe.

    Rubio alieleza kuwa tatizo si wanamichezo wa Iran, bali ni baadhi ya watu wanaoweza kuandamana nao.

    “Wasichoweza kufanya ni kuingiza magaidi wa IRGC nchini kwetu na kujifanya waandishi wa habari au wakufunzi wa michezo,” alisema.

    Unaweza pia kusoma:

Trending Now