"Hili ni zaidi ya soka" - DR Congo yapambania kuvunja ukame wa miaka 52 Kombe la Dunia

    • Author, Ian Williams
    • Nafasi, BBC Sport Africa
  • Muda wa kusoma: Dakika 9

Mashabiki wa soka nchini DR Congo wamekuwa wakisubiri kwa hamu na ghamu kwa zaidi ya miaka 50 kurudi kwenye Kombe la Dunia tangu ushiriki wao wa 1974. Safari yao ilianza kwa changamoto kubwa, lakini sasa wana nafasi ya kuandika historia mpya.

Huo ulikuwa mwaka ambao Rais wa Marekani Richard Nixon alijiuzulu kufuatia kashfa ya Watergate, kifaa cha Rubik's Cube kilibuniwa, na Muhammad Ali alimshinda George Foreman katika pambano la 'Rumble in the Jungle' lililofanyika Kinshasa.

Ushindi kwa timu ya Leopards dhidi ya Jamaica katika mechi ya mchujo wa mabara, unamaanisha tiketi ya DR Congo kushiriki Kombe la Dunia litakalofanyika Canada, Mexico na Marekani na kuipatia Afrika mwakilishi wa 10 katika mashindano hayo.

"Ninaiona hii kama mechi kubwa zaidi katika maisha yangu ya soka," alisema beki wa Burnley Axel Tuanzebe, huku nahodha wa zamani Gabriel Zakuani akiitaja kama "mechi kubwa zaidi katika historia yetu."

Iwapo DR Congo itashinda, zaidi ya watu milioni 110 nyumbani pamoja na ughaibuni watakuwa na matumaini kwamba safari hii mambo yatakuwa bora kuliko mwaka 1974 waliposhiriki kama Zaire nchini Ujerumani Magharibi.

Safari hiyo ilianza vibaya kwa kufungwa 2-0 na Scotland, ikazidi kuwa mbaya kwa kipigo cha 9-0 dhidi ya Yugoslavia, na kuishia kwa fedheha katika kipigo cha 3-0 dhidi ya Brazil kilichozalisha moja ya matukio ya kukumbukwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia.

"Hii alikuwa anafanya nini duniani?" ndilo swali lililoulizwa na mtangazaji wa BBC, John Motson, baada ya beki wa kulia Mwepu Ilunga kutoka kwenye ukuta wa ulinzi na kuupiga mpira mbele wakati Brazil wakiandaa mpira wa kufunga pembezoni mwa eneo la penalti la Zaire.

Ilunga alionyeshwa kadi ya njano, lakini madhara yaliyotokea yalikuwa makubwa zaidi kwa taswira ya soka la Afrika, yakiacha hisia kwamba wachezaji wa bara hilo hawakuzijua hata sheria za mchezo.

"Hatukuwa timu mbaya," alisema Mohamed Kalambay, mmoja wa makipa wa kikosi cha 1974, katika mahojiano ya mwaka 2022.

"Ukitazama timu za Afrika, ni chache tu zilizowahi kufika Kombe la Dunia, lakini sisi tulifika na tulistahili."

Hata hivyo, matukio kama ya Ilunga yamekuwa yakihusishwa na sababu mbalimbali, kuanzia malimbikizo ya posho hadi madai ya vitisho, yakichangia mwenendo hafifu wa kikosi hicho.

Sasa kizazi kipya kinaingia uwanjani kikiwa na dhamira ya kuandika historia yao na kufuta kumbukumbu hizo za zamani.

Ushindi dhidi ya Jamaica utawaingiza kwenye kundi linalojumuisha timu kama Portugal, Uzbekistan na Colombia.

"Hatutaki tu kushiriki," alisema Gabriel Zakuani, ambaye ni kocha msaidizi wa timu ya vijana ya DR Congo. "Tunalenga kushindana, kuonyesha kiwango bora, na kuandika historia, si kuwa washiriki tu wa mashindano."

Vita, madikteta na uwezo wa soka wa 'kuunganisha'

Walipofuzu mwaka 1974, Zaire ilikuwa timu ya tatu kutoka Afrika kufika Kombe la Dunia baada ya Egypt (1934) na Morocco (1970).

Tangu wakati huo, taifa hili kubwa lenye rasilimali nyingi likiwa la pili kwa ukubwa barani Afrika kwa eneo na la nne kwa idadi ya watu lililazimika kushuhudia kwa wivu wapinzani wake wadogo kama Ghana, Senegal na Tunisia wakicheza mara kadhaa kwenye mashindano makubwa ya soka duniani.

Hali hiyo inahusishwa kuchochewa na rushwa, ukosefu wa utulivu wa kisiasa na vita, mambo ambayo yameendelea tangu mwisho wa utawala wa kikoloni wa Ubelgiji mwaka 1960.

Kikosi cha 1974, ambacho pia kilikuwa mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), kiliungwa mkono na Rais Mobutu Sese Seko, dikteta aliyekuwa na mamlaka makubwa aliyelitawala taifa hilo kuanzia 1971 hadi 1997, akitumia madaraka yake kujilimbikizia utajiri mkubwa binafsi, ambao sehemu yake aliwekeza katika soka.

"Tulikuwa Ikulu. Tulikwenda kumwona kwa sababu alitaka kututia moyo," alisema Mohamed Kalambay, akimkumbuka kiongozi huyo ambaye aliwazawadi nyumba na gari kwa kila mchezaji wa kikosi kilichotwaa Afcon.

Tangu wakati huo, Congo haijawahi tena kufika fainali za Afcon.

"Athari katika kipindi cha miaka 50 iliyopita zimekuwa kubwa," alisema mwanahabari wa michezo Jean-Jacques Akengelaka, akibainisha miundombinu iliyoharibiwa pamoja na rushwa na usimamizi duni katika sekta ya michezo.

"Tofauti na nchi nyingine za Afrika, DR Congo kwa muda mrefu imekosa vituo vya mafunzo vilivyopangwa vizuri, viwanja bora, miundombinu ya kisasa na makocha wenye weledi."

Utawala wa Mobutu ulimalizika kutokana na migogoro, ambapo vita mbili za Congo (1996–2003) zilihusisha mataifa tisa ya Afrika na kusababisha vifo vya hadi watu milioni sita.

Mapigano bado yanaendelea mashariki mwa nchi, ambapo kundi la waasi la M23 linadhibiti miji muhimu ikiwemo Goma na Bukavu. Hali hiyo imechochea kikosi cha DR Congo kutumia ushiriki wao katika nusu fainali ya AFCON 2023 kama wito wa amani.

Wakati wa wimbo wa taifa, wachezaji walifunika midomo yao kwa mkono mmoja huku wakitumia mkono mwingine kuashiria kama bunduki kwenye mahekalu yao.

Mshambuliaji wa Newcastle United, Yoane Wissa, alisema wakati huo kwamba alitarajia safari yao hadi hatua ya nusu fainali ingewasaidia walioguswa "kutabasamu kidogo", huku Axel Tuanzebe akielezea soka kama "kutoa pumzi ya hewa safi kwa nchi".

Freddy, shabiki kutoka Bukavu, aliambia BBC Sport Africa kwamba ingawa si kila mtu anaiona kwa namna hiyo, wengi "wanaishi kupitia soka" na nguvu yake ya "kuunganisha watu".

"Kweli itakuwa na athari kubwa katika maisha yangu na ya majirani zangu," alisema kabla ya mechi dhidi ya Jamaica inayochezwa nchini Mexico.

Hata hivyo, licha ya Bukavu kuwa na maeneo mengi ya kijamii, tofauti ya saa ambapo mechi huanza katikati ya usiku nchini Congo itafanya mashabiki wengi watazame wakiwa nyumbani.

"Ni hatari sana na inaweza kuwa ya kuhatarisha maisha kwenda kwenye vilabu au baa kutazama mechi," Freddy alieleza.

"Wakati wowote mtu anatoka usiku wa manane, kwa kawaida anaweza kuuawa. Eneo letu hapa Bukavu ni hatari sana kutokana na kuwepo kwa waasi wanaolidhibiti."

"Hili ni kubwa kuliko soka"

DR Congo ilifika hatua ya mchujo wa mabara baada ya kumaliza ya pili nyuma ya Senegal, kisha ikaishinda Cameroon na Nigeria kwa mikwaju ya penalti.

Mafanikio yao yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwasajili wachezaji kutoka ng'ambo. Mfano ni Aaron Wan-Bissaka na Axel Tuanzebe, ambao waliwahi kuichezea England katika ngazi za vijana.

"Sikuwa na shaka hata kidogo. Mara tu nilipojiunga nao walinipokea vizuri, walinikubali, nikajisikia furaha na tangu hapo mambo yamekuwa laini," alisema beki wa West Ham United, Aaron Wan-Bissaka, akizungumza na BBC Sport Africa wakati wa AFCON iliyofanyika Morocco, ambapo DR Congo ilitolewa katika hatua ya 16 bora.

"Hapo ndipo wazazi wangu wanakotoka. Nilikulia katika familia ya Kongo, na nilijivunia sana kuiwakilisha nchi yao."

Kati ya kikosi cha sasa cha wachezaji 26, wachezaji 10 wamezaliwa nchini Ufaransa, nyumbani kwa kocha mkuu Sebastien Desabre; watano wamezaliwa Ubelgiji, wawili Switzerland na mmoja Uingereza.

Ni wachezaji wanane tu waliozaliwa nchini Congo, huku wengi wao wakikulia barani Ulaya.

Wachezaji wawili pekee, kiungo Meschak Elia na mshambuliaji Fiston Mayele, ndio waliowahi kucheza soka la kiwango cha juu katika klabu za ndani ya Congo.

"Wachezaji wengi wenye vipaji hulazimika kwenda nje ya nchi wakiwa na umri mdogo," alieleza Jean-Jacques Akengelaka.

"Kuna ukosefu wa utulivu katika uendeshaji, ufadhili mdogo na pia mashindano ya ndani hayapati nafasi ya kutosha kutangazwa kwenye vyombo vya habari."

Inaonekana vigumu kwa mfumo wa ligi ya ndani kuzalisha wachezaji wa kiwango cha kimataifa katika siku za karibuni.

Msimu wa 2022/23 wa Linafoot haukukamilika baada ya serikali kusitisha ruzuku zilizokuwa zikiisaidia klabu kugharamia safari za ndege njia kuu ya usafiri katika nchi hiyo kubwa huku baadhi ya timu zikishindwa hata kupata fedha za kumalizia kampeni zao.

Shirikisho la soka la taifa, Fecofa, nalo limeshindwa kurekebisha hali hiyo, likiwa halina kiongozi aliyechaguliwa tangu aliyekuwa rais wake, Constant Omari, alipofungiwa kujihusisha na shughuli za soka kwa mwaka mmoja mnamo Juni 2021.

Tangu Aprili 2023, Fecofa imekuwa ikiendeshwa na kamati ya mpito iliyoteuliwa na FIFA, huku uchaguzi uliopangwa ukiahirishwa mara kwa mara.

Wakati huo huo, serikali imewekeza mamilioni ya fedha katika mikataba ya udhamini na vilabu vikubwa barani Ulaya kama FC Barcelona, AC Milan na AS Monaco, hatua iliyozua hasira kwa wengi wanaoamini fedha hizo zilipaswa kuelekezwa kuendeleza soka la ndani.

Aidha, baadhi ya watumishi wa umma ambao hawajalipwa mishahara yao wameeleza kutoridhishwa na matumizi ya fedha kusaidia kampeni ya Leopards kuelekea Kombe la Dunia.

"Hakika tuna kila tunachohitaji kama timu. Hatukosi kitu, na hilo linatuwezesha kuonyesha kiwango chetu bora uwanjani," alikiri Axel Tuanzebe, akitumaini sasa timu itatimiza wajibu wake uwanjani.

"Hii ni moja ya nyakati ambazo ni zaidi ya soka. Ni suala la kuacha alama, kuandika historia ambayo tutai kumbuka na kuithamini daima."

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid