Tundu Lissu awauliza maswali mashahidi waliofichwa

Kesi ya kiongozi wa chama cha CHADEMA nchini Tanzania Tundu Lissu imeendelea leo kwa ushahidi kutolewa. Baadhi ya wafuasi wake walikuwepo mahakamani kufuatilia kesi hiyo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Asha Juma & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

    Na hapa ndio mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja, tukutane kesho.

  2. Baadhi ya nchi kuanza mfungo wa Ramadhan kesho

    mm

    Chanzo cha picha, Getty

    Saudi Arabia, Falme za Kiarabu na Qatar zilitangaza kwamba Ramadhani itaanza kesho baada ya kuona mwezi mpya.

    Kuwait imethibitisha rasmi kwamba Jumatano, Februari 18, itaanza Ramadhani. Mamlaka za uchunguzi wa mwezi mpevu zimethibitisha.

    Iraq, Yemen, Lebanon, na Palestina zimethibitisha rasmi kwamba Jumatano, Februari 18, itakuwa mwanzo wa Ramadhani. Kufuatia kuonekana kwa mwezi.

    Bahrain imethibitisha rasmi kwamba Jumatano, Februari 18, itakuwa mwanzo wa Ramadhani. Kufuatia kuonekana kwa mwezi.

  3. Wanajeshi wa Marekani wawasili Nigeria

    k

    Chanzo cha picha, dvidshub

    Takriban wanajeshi 100 wa Marekani wamewasili Nigeria kutoa mafunzo kwa vikosi vya jeshi vya taifa hilo la Afrika Magharibi na kuwasaidia kwa taarifa za kijasusi katika vita vyao dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu na makundi mengine yenye silaha.

    Msemaji wa Wizara ya ulinzi wa Nigeria Meja Jenerali Samaila Uba amesema wanajeshi na vifaa vyao wametua kwenye uwanja wa ndege katika jimbo la Bauchi kaskazini-mashariki.

    Ameisitiza kwamba wanajeshi hao hawatoshiriki katika shughuli za mapigano na wamekuja kwa ombi la serikali la Nigeria.

    Hatua hii inafuatia mashambulizi ya anga ya Siku ya Krismasi yaliyofanywa na Marekani kwenye kambi mbili zinazoendeshwa na kundi la wanamgambo wa Kiislamu kaskazini magharibi mwa Nigeria.

    Nigeria inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiusalama ikiwa ni pamoja na uasi wa makundi ya Kiislamu, mashambulizi ya magenge ya wahalifu wanaopora na kuteka nyara na mapigano kuhusu ardhi na machafuko ya wanaotaka kujitenga.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Arsenal yamtangaza Saka kuwa mchezaji anayelipwa zaidi

    k

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Bukayo Saka amefunga mabao saba na kutoa pasi sita za mabao msimu huu

    Winga wa Uingereza Bukayo Saka amesaini mkataba mpya wa miaka mitano na Arsenal hadi 2031.

    Vyanzo vimeiambia BBC Sport makubaliano hayo yatamfanya Saka kuwa mchezaji anayelipwa zaidi klabuni hapo kwa mshahara wa zaidi ya pauni 300,000 kwa wiki.

    Saka alisaini mkataba wake wa awali, ambao ulitarajiwa kuisha mwaka 2027, mwaka 2023 lakini kuongezwa kwake kunamaanisha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ataendelea kubaki Gunners.

    Saka amefunga mabao saba katika mechi 33 alizocheza akiwa na Gunners msimu huu.

    Kikosi cha Mikel Arteta kiko mbele kwa pointi nne kileleni mwa Ligi Kuu na kitakabiliana na Manchester City katika fainali ya Kombe la EFL mwezi Machi.

    Gunners pia wamefuzu hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa, pamoja na raundi ya tano ya Kombe la FA.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Mazungumzo ya nyuklia kati ya Marekani na Iran yamalizika Geneva

    ,wds

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mazungumzo hayo yanafanyika katika jengo la misheni la Oman mjini Geneva

    Duru ya pili ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani, yenye lengo la kutatua mzozo kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran, yamemalizika katika jiji la Geneva, Uswisi.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi amesema nchi hizo mbili zimefikia makubaliano kuhusu "kanuni kuu za kuongoza mazungumzo," lakini kazi bado inahitajika. Marekani bado haijatoa maoni.

    Majadiliano hayo yasiyo ya moja kwa moja yanakuja kufuatia vitisho vya kijeshi vya Washington dhidi ya Iran kuhusu ukandamizaji wa nchi hiyo dhidi ya maandamano ya kupinga serikali, pamoja na shughuli zake za nyuklia.

    Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya Air Force One kabla ya mazungumzo, Rais wa Marekani Donald Trump amesema anaamini Iran inataka kufikia makubaliano.

    Wakati huo huo, wizara ya mambo ya nje mjini Tehran imesema inaamini msimamo wa Marekani kuhusu suala la nyuklia “unaeleweka.”

    Kabla ya mkutano wa Jumanne, uliosimamiwa na Oman, Iran ilisema itajadiliana juu ya mpango wake wa nyuklia na uwezekano wa kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani.

    Washington imeonyesha pia inataka kujadili masuala mengine, kama vile maendeleo ya makombora ya Iran.

    Vitisho vya Trump vimekuja wakati ambapo jeshi la Marekani linajikusanya Mashariki ya Kati.

    BBC Verify imethibitisha eneo ilipo meli ya Marekani ya USS Abraham Lincoln karibu na Iran kwa kutumia picha za setilaiti.

    Marekani pia imeripotiwa kutuma meli ya kivita ya USS Gerald R Ford, meli kubwa zaidi ya kivita duniani, Mashariki ya Kati, ambayo inaweza kufika katika eneo hilo ndani ya wiki tatu zijazo.

    Mbali na kuwasili kwa Abraham Lincoln, BBC Verify pia imefuatilia ongezeko la ndege za kivita za Marekani, meli za kivita na ndege za kivita katika eneo hilo.

    Iran imejibu ongezeko la jeshi la Marekani kwa kuonyesha nguvu zake. Siku ya Jumatatu Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kilifanya mazoezi ya baharini katika Mlango-Bahari wa Hormuz, ulioko katika Ghuba kati ya Oman na Iran.

    Mlango huo unachukuliwa kuwa njia muhimu ya kimataifa ya maji na njia ya kusafirisha mafuta kutoka nchi za Ghuba ya Kiarabu.

    Mazungumzo ya kwanza yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yalifanyika Oman mapema mwaka huu, ambayo Araqchi aliyaelezea kama "mwanzo mzuri."

    Pia unaweza kusoma:

  6. Duru ya tatu ya mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine yaanza Geneva

    l

    Chanzo cha picha, State Emergency Service of Ukraine/Anadolu via Getty Images

    Maelezo ya picha, Zima moto wa Ukraine baada ya mashambulizi ya Urusi katika maeneo ya makazi ya mji wa Sumy kaskazini-mashariki mwa Ukraine

    Wajumbe wa Urusi na Ukraine wanakutana jijini Geneva kwa ajili ya duru ya tatu ya mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani, wiki moja kabla ya maadhimisho ya miaka minne tangu uvamizi wa Moscow dhidi ya Ukraine.

    Licha ya mazungumzo hayo, mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine yanaendelea, na kuharibu zaidi gridi ya umeme ya nchi hiyo ambayo tayari imeharibika huku baridi kali ikiendelea.

    Saa chache kabla ya wajumbe hao kukutana nchini Uswisi, Moscow ilifanya shambulio kubwa la angani dhidi ya Ukraine, ikipiga maeneo 12 kwa kutumia ndege zisizo na rubani 400 na karibu makombora 30. Takribani watu watatu wameuawa.

    Urusi imesema mifumo yake ya ulinzi wa anga imedungua ndege zisizo na rubani zaidi ya 150, huku kiwanda cha kusafishia mafuta kikiwaka moto baada ya shambulio la ndege zisizo na rubani za Ukraine.

    Mazungumzo ya Jumanne yanasimamiwa na Steve Witkoff, mjumbe maalum wa Donald Trump, na Jared Kushner, mkwe wa rais wa Marekani.

    Ukraine inawakilishwa na Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa Rustem Umerov na mkuu wa wafanyakazi wa Rais Volodymyr Zelensky, Kyrylo Budanov.

    Ujumbe wa Urusi unajumuisha msaidizi wa Rais Vladimir Putin, Vladimir Medinsky na maafisa wa ujasusi wa kijeshi.

    Urusi inakalia takriban 20% ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa za eneo la mashariki mwa Donbas. Kremlin inataka Ukraine ikabidhi eneo lote lililobaki, Ukraine imekataa.

    Kyiv inataka dhamana za usalama kutoka nchi za Magharibi - ikiwa ni pamoja na Marekani.

    Majadiliano haya yanakuja baada ya mazungumzo ya pande tatu mwezi uliopita huko Abu Dhabi, ambayo yalikuwa mazungumzo ya kwanza ya pande tatu kati ya Urusi, Ukraine na Marekani tangu Moscow ilipoanzisha uvamizi dhidi ya jirani yake Februari 2022.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu yaahirishwa hadi kesho

    Kesi dhidi ya mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Tundu Lissu iliyokuwa ikiendelea leo jijini Dar es Salaam, imeahirishwa hadi kesho saa tatu asubuhi.

  8. Kwa nini unatoa ushahidi ukiwa umejificha kwenye mbao?

    ll

    Chanzo cha picha, Mtandao

    Lissu: Mimi najua kukinukisha ni kukifanya kinukie vibaya au vizuri

    Shahidi: Hapana mimi sijasema kukinukisha haifanyi itoe harufu nzuri ni wewe ndiyo umeeleza

    Lissu: Waeleze majaji kama unaelewa kwenye uchgauzi mdogo wa serikali za mitaa wa 2024 wagombea wote wa upinzani walifutwa na CCM ikashinda kwa asilimia 100?

    Shahidi: Siwezi kujua nchi zima labda eneo nililotoka

    Lissu: Wagombea wote wa CHADEMA Arusha walifanyaje?

    Shahidi: Hawakuwepo

    Lissu: Kwa hiyo ninavyosema wasimamizi wa uchgauzi wanafuta wagombea wakati upo upinzani ni mambo ya hovyo kusema hivyo ni makosa?

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Baada kutoa maelezo yako Polisi tarehe 18 kama umewahi kuwasiliana na polisi juu ya shauri hii

    Shahidi: Ndiyo nimewahi juzi wakati wameniita kituioni

    Lissu: Kwa hiyo walikuita polisi?

    Shahidi: Ndiyo waliniambia nina wito wa mahakama

    Lissu: Kwa hiyo baada ya tarehe 17 hukuwahi kuwasiliana na polisi kwa chochote

    Shahidi: Sikuwahi

    Lissu: Umewahi kuwasiliana na kiongozi yoyote wakati upo CHADEMA katika kipindi hiki?

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Waeleze majaji kama kuna kiongozi, mfuasi au mwanachama wa CHADEMA aliyewahi kukutishia maisha

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Waeleze majaji kama kuna kiongozi, mwanachama, mfuasi wa CHADEMA aliyekutishia kukudhuru kwa sababu ya kukubali kuwa shahidi

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Waeleze majaji kama kuna kiongozi, mwanachama, mfuasi wa chadema kama aliwahi kutishia kuharibu mali yako?

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Waeleze majaji kama kuna kiongozi, mwanachama wa Chadema aliwahi kumtishia maisha ndugu au rafiki yako?

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Waeleze majaji kwa nini unatoa ushahidi ukiwa umejificha kwenye mbao hizo?

    Shahidi: Nahofia maisha yangu

    Lissu: Nani alikufundisha kusema hivyo wakati hujatishiwa maisha yako?

    Lissu: Waeleze majaji kuwa polisi walipeleka ombi mahakamani wakisema kwamba viongozi, wanaachama wa chadema walitishia wewe kukudhuru ndiyo maana inabidi ujifiche

    Shahidi: Sifahami inteljesia yao

    Lissu: Nani alikuhoji

    Shahidi: Askari Arusha mjini

    Lissu: Una mfahamu jina?

    Shahidi: Simkumbuki jina

    Lissu: Waeleze majaji kama umesema kwenye maelezo yako ya polisi hiyo video ilikuwa kwenye mtandao gani?

    Shahidi: Habari24

    Lissu: Waeleze majaji kama uiandika kwenye maelezo yako kuwa hiyo habari uliona Habari24

    Shahhidi: Hapana

    Lissu: Ni hayo tu

  9. Waeleze majaji kama unafahamu maana ya neno kunuka - Tundu Lissu

    kk

    Chanzo cha picha, Mwananchi

    Baada ya kusoma maelezo Lissu anamtajia shahidi maeneo ambayo anataka kumuhoji

    Lisuu: Ulikuwa unaperuzi kwa simu yako hili ni eneo la kwanza, eneo la pili unasema ulivyoniona nazungumza kwenye mitandao ukasema “akasema watakinukisha” haya maneno nitakuhoji kwa ‘uelewa wako, eneo la tatu ni ulisema ‘alisema watafanya fujo kuzuia uchaguzi’ vile vile nataka nikuhoji kwenye ushahidi wako ambako ulisema ukiandikaa maelezo alafu ukawekwa ndani na eneo la tano kwenye ushahidi wako ulisema kwamba ulipopewa dhamana 4-4-2025 uliambiwa unatakiwa kuripoti kila siku sawa?

    Na eneo la mwisho ni pale ulipoulizwa unafahamuje Tundu Lissu ukasema unafahamu kama mwanasiasa mkubwa nchi hii sasa naomba ueleze majaji kwamba maelezo yako yatumike kama ushahidi mahakamani

    Shahidi: Ningependa maelezo haya yatumike kama ushahidi mahakamani

    Lissu: Asante……

    Jaji: Itakuwa D9

    Lissu: Naomba shahidi apewe kielelezo D9. Una nakala ya hayo maelezo yako?

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Umesema hiyo 3-4-2025 ulikuwa unaperuzi mtandao wa Youtube kwa simu yako kweli sio kweli?

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Waeleze majaji kama kuna mahala popote ambako umesema ulikuwa na simu? Kama sehemu ipo sema, kama haipo sema

    Shahidi: Haipo

    Lissu: Kwenye ushahidi wako leo umesema kwamba wakati huyu Tundu Lissu anahutubia mkutano alisema watakinukisha naomba uangalie kwenye maelezo yako kama kuna hayo maneno umeyaandika

    Shahidi: Haya maneno naona hayajaandikwa

    Lissu: Kwenye ushahidi wako ulisema kwamba alisema watafanya fujo kuzuia uchaguzi haya maneno uliyasema kwenye ushahidi wako au hukusema?

    Shahidi: Sikusema kufanya fujo nilisema watakinukisha

    Lissu anaomba kumbukumbu za mahakama.

    Lissu: Baada ta kukamatwa na kupelekwa central umesema hivi “ Tulipofika tuliambiwa makosa yetu kuzuia uchaguzi na tukawekwa ndani” halafu baadae ukasema “tuliandikwa maelezo alafu tukawekwa ndani” unakumbuka hilo?

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Waambie majaji kama maneno “tulihojiwa tukawekwa ndani” kama yapo kwenye maelezo yako

    Shahidi: Hapa hayapo

    Lissu: Twende 4-4-2025 ambako kwenye ushahidi wako umeeleza kwamba dada na mdogo wako walikuja kukuwekea dhamana alafu ukasema ulitakiwa uripoti kila siku waeleze majaji kama hayo maneno “kutakiwa kuripoti kila siku” yapo kwenye maelezo

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Ni kweli kwamba siku hiyo ya tarehe 4-4-2025 Wakati unahojiwa na polisi, walikuuliza kama una mfahamu Tundu Lissu?

    Shahidi: Ndiyo waliniuliza nikajibu namfahamu kama mwanasiasa mkubwa

    Lissu: Naomba uwaambie majaji kama hayo yapo kwenye maelezo yako

    Shahidi: Hapana hayapo

    Lissu: Umesema ulikuwa unaperuzi mtandani waeleze majaji kama ulitumia computer kuperuzi maana simu haipo?

    Shahidi: Nilitumia simu siwezi kusema kitu ambacho siwezi kumiliki

    Lissu: Kwa hiyo nikikuuliza tablate nayo utasema huijui

    Shahidi: Ndiyo siijui

    Lissu: Umeeleza kwenye ushahidi wako maandishi umesema kwamba wakati upo kwa Mrombo mnajadili hotuba ya Tundu Lissu …swali langu kwako kuzungumza hayo maneno ni kosa la jinai?

    Shahidi: Kwa sababu mimi sio mwanasheria siwezi kujua

    Lissu: Kuhamasika na maneno ya mwenyekiti ni kosa la jinai

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Na kauli kwamba Majaji ni vibaraka wa CCM ni kosa la jinai?

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Na kusema kwamba mapolisi wanashiriki kuiba kura ni kosa la jinai?

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu maana ya neno kunuka

    Shahidi: Kunuka ni kitu kinachotoa harufu mbaya

    Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu maana ya neno kunukia?

    Shahidi: Ni kitu kinachotoa harufu nzuri

    Lissu: Kwakua kunuka ni kutoa harufu mbaya mtu akisema nitakinukisha maana yake nitafanya kitoe harufu mbaya?

    Shahidi: Inategemea na muktadha

    Lissu: Waleze majaji hiyo maana yako ya kufanya fujo umeitoa wapi?

    Shahidi: Ni lugha ya mtaani

    Lissu: Mtaa upi mimi mtaani kwangu sijawahi kusiki

  10. Tundu Lissu aanza kumuhoji Shahidi P4

    [

    Chanzo cha picha, MITANDAO

    Lissu: Naomba ujibu maswali yangu na uyajibu kama unajua sema unajua kama hujui sema sijui. Usilete maelezo mengine

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Umeileza mahakama kwamba wewe unakaa Arusha ni kweli sio kweli?

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Waeleze majaji hapa Dar es salaam umekuja lini?

    Shahidi: Nina siku ya pili leo

    Lissu: Kwa hiyo ulikuja Jumapili ya juzi?

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Nani aliyekuambia uje Dar es salaam waeleze majaji?

    Shahidi: Nilipigiwa simu nikaambiwa nije

    Lissu: Ulipigiwa simu na nani?

    Shahidi: Na mtu aliyejitambukusha yeye ni wakili wa Serikali

    Lissu: Alikuambia jina lake?

    Shahidi: Siwezi kulisema kwa sababu binafsi

    Lissu: Hivyo majaji waandike umekataa kusema kwa sababu zako binafsi?

    Lissu: Waeleze majaji kama ulipata wito wa mahakama wa kuja Dar es salaam?

    Shahidi: Taarifa nilipata maana nilikwenda kituoni

    Lissu: Ulipata barua ya mahakama

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Unaweza kutuonesha

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Nani alikulipia nauli ya kuja Dar?

    Shahidi: Nilijilipia mwenyewe maana nilikuwa nakuja kwa shughuli zangu binafsi

    Lissu: Una nyumba Dar?

    Shahidi: Hapana nimefikia kwa ndugu yangu

    Lissu: Nani analipa gharama za kukuleta

    Shahidi: Leo nimekuja kwa gari la wanasheria

    Lissu: Umeeleza kuwa uliandika maelezo tarehe 3-4-2025, waeleze majaji ni makosa gani yalifanya uandikie maelezo

    Shahidi: Walisema ni kuzuia uchaguzi

    Lissu: Waeleze majaji kama uliwahi kupelekwa mahakamani huko Arusha kwa kosa hilo

    Shahidi: Sikuwahi kupelekwa mahakamani

    Lissu: Waeleze majaji hiyo kesi ya kuzuia uchaguzi iliishia wapi?

    Shahidi: Hilo sijui

    Lissu: Waeleze majaji hayo maelezo ya tarehe 3-4-2025 yapo wapi

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Nikikuambia kwamba ulikamatwa bure, kutaka kuzuia uchaguzi sio kosa ndiyo maana hukupelekwa mahakamani

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Umesema 03-4-2025 ulkuwa kwenye kijiwe cha Mrombo mlikuwa mnazungumza kuhusu maneno kwenye mtandao, waeleze kama nyinyi kuzungumza hilo ilikuwa kosa

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Maelezo yako ya 18-04-2025 eleza kama ukionyeshwa hayo maelezo yako utayatambua

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Naomba onyeshwe maelezo yake

    Lissu: Naomba ueleze majaji kama hiyo karatasi uliyonayo ni maelezo yako uliyotoa polisi tarehe 17-4-2025

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu anamsomea shahidi maelezo yake aliyoandika tarehe 18-04-2025

  11. Shahidi P4 amaliza kuhojiwa na Wakili

    k

    Chanzo cha picha, MwanaHalisi

    Wakili: Endelea kueleza baada ya kutakiwa kuripoti kila siku kitu gani kiliendelea?

    Shahidi: Tuliripoti mpaka ilifika tarehe 17

    Wakili: Tarehe 17 ya mwezi gani mwaka gani?

    Shahidi: 17-04-2025 wakatuambia tusiondoke kuna maelezo watatumbia

    Wakili: Nani aliyewaambia?

    Shahidi: Yule Afande aliyekuwa mpelelezi wetu

    Wakili: Baada ta kuambiwa msiondoke nini kiliendelea?

    Shahidi: Nilisubiri nikaandikwa maelezo

    Wakili: Walikuandika maelezo gani? Na nini kiliendelea?

    Shahidi: Baada ya kuandika maelezo waliniambia niondoke wakasema watanipigia simu wakinihitaji

    Wakili: Baada yapo

    Shahidi: Niliondoka kwenda nyumbani kuendelea na shughuli zangu

    Wakili: Kuna mtu unasema ulimuona kwenye mtandao wa Youtube. Je unafahamu vipi Tundu Lissu?

    Shahidi: Namtambua kama wanasiasa mkubwa kwenye hii nchi

    Wakili: Maswali yangu ni hayo

  12. Kila mtu alianza kukimbia - Shahidi P4

    ll

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wakili: Shahidi Endelea

    Shahidi: Baada ya hapo dakika ishirini kidogo wakatokea polisi

    Wakili: Hao polisi walitokea wapi?

    Shahidi: Hatukujua walikotokea wapi, tunashangaa walifika wakatuweka chini ya ulinzi

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Kila mtu alianza kukimbia

    Wakili: Nini kiliendelea baada ya kila mtu kukimbia?

    Shahidi: Nikakamatwa mimi pamoja na mwenzangu P7

    Wakili: Kwa hiyo walikimbia wote mkakamatwa wewe na P7?

    Shahidi: Ndiyo

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Tulipelekwa kituo cha Polisi cha Miret tukapelekwa kituo kikuu Arusha mjini

    Wakili: Baada ya kupelekwa Nini kiliendelea?

    Shahidi: Baada ya kufika pale tukaambiwa makosa yetu

    Wakili: Mliambiwa makosa gani?

    Shahidi: Tuliambiwa kwamba tunazuia uchaguzi tukawekwa ndani

    Wakili: Nini kiliendelea baada ya kufikishwa central

    Shahidi: Tulivyoambiwa kosa letu tuliandika maelezo tukawekwa ndani

    Wakili: Baada ya kuwekwa ndani nini kilifuata

    Shahidi: Kesho yake asubuhi walikuja dada yangu na mdogo wangu ilikuwa tarehe 4-4-2025

    Wakili: Baada ya dada ako na mdogo wako walipataje taarifa

    Shahidi: Tulikamatwa wakati kila mtu anaona

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Walituwekea dhamana wakatupa utaratibu tuwe tunaripoti kila siku.

  13. Shahidi P4 aanza kuhojiwa katika kesi ya Tundu Lissu

    ['

    Chanzo cha picha, MTANDAO

    Jaji: Shahidi una miaka mingapi?

    Shahidi: Nina miaka 29

    Jaji: Dini yako

    Shahidi: Mkristo

    Shahidi: Anaapishwa ili kianza kutoa ushahidi

    Wakili: Unaweza kuikambia mahakama wewe ni mkaazi wa wapi

    Shahidi: Mimi ni mkazi wa Arusha

    Wakili: Unajishughulisha na nini?

    Shahidi: Mimi ni dereva bajaji

    Wakili: Shughuli zako za kuendesha bajaji unazifanyia wapi?

    Shahidi: Nazifanyia kwa Mroboo

    Wakili: Unakumbuka nini tarehe 3-04-2025?

    Shahidi: Nakumbuka majira ya saa 6 mchana nikiwa natoka nyumba nilisimama nikimsubiri mteja

    Wakili: Nini kiliendelea

    Shahidi: Nilikuwa naperuzi kwenye simu yangu

    Wakili: Endelea

    Shahidi: Nikaingia kwenye mtandao wa Youtube

    Wakili: Baada ya kuingia

    Shahidi: Nilikutana na habari za Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, ambazo alikuwa anaelezea kwamba wamejipanga, kuzuia uchaguzi, baada ya hapo akasema watakinukisha

    Wakili: Mwenyekiti alikuwa anafanya nini?

    Shahidi: Alikuwa anafanya mkutano na waamdiashi wa habari

    Wakili: Uliona nini?

    Shahidi: Niliona anasema watakinukisha wamejipanga kuzuia uchaguzi

    Wakili: Uliona nini kingine?

    Shahidi: Anasema wao watakinukisha kwa sababu hawana imani na uchaguzi sababu hata uende wapi huwezi kupata haki kwamba hata majaji ni vibaraka wa CCM

    Wakili: Nini kingine ulikisikia?

    Shahidi: Kwamb tume ya uchgauzi ilipanga kuharibu uchaguzi kwa kukata majina ya wanachama wa Chadema

    Wakili: Kuyakata vipi?

    Shahidi: Kuyaondoa majina ya viongozi hao kwenye uchgauzi mdogo

    Wakili: Uchaguzi gani?

    Shahidi: Uchaguzi mdogo wa 2024

    Wakili: Tuendelee

    Shahidi: Maana walikuwa wakiona hata polisi wakishiriki kuiba kura

    Wakili: Kitu gani kiliendelea

    Shahidi: Nikaona ni kitu ambacho kinaleta ushawishi kwangu

    Wakili: Kivipi?

    Shahidi: Maneno yale yaliweza kunishawishi mimi kuunga mkono alichokuwa anakisema

    Wakili: Baada ya kusikiliza kitu gani kiliendelea

    Shahidi: Baada hapo abiria wangu walifika nikawapeleka kwa Mromboo baada ya kuwafikisha nikarudi kijiweni

    Wakili: Unaweza kueleza mahakama ni maneno gani yalikushawishi

    Shahidi: Kwamba tutakinukisha na vyombo vyote alivyosema haviamini

    Wakili: Maneno hayo yalikushawishi vipi?

    Shahidi: Kutokana na hali ya kimaisha ilivyo

    Wakili: Baada ya kufikisha wateja nini kiliendelea?

    Shahidi: Baaada ya kuwafikisha wateja wangu kwa Mrombo nilirudi kijiweni kwangu hapo hapo kwa Mrombo

    Wakili: Ulivyorudi kwa Mromboo nini kiliendelea?

    Shahidi: Nilivyorudi nilikuta mada hiyo inaendelea

    Wakili: Ilikuwa inaendelea kivipi?

    Shahidi: Nilikuta wanajadili juu ya maneno ya Mwenyekiti

    Wakili: Ulieleza mahakama ulirudi kijiweni, ni kijiwe cha nini?

    Shahidi: Ni kijiwe cha bajaji

    Wakili: Unaweza kuelezea ni mada gani ilikuwa inaendelea?

    Shahidi: Mada ya wenyekiti wa CHADEMA akizungumza kuhusu kukinukisha

    Wakili: Je, nini kiliendelea?

    Shahidi: Watu wengi walikuwa wanasapoti wakisema bora kinuke kutakuwa na unafuu wa maisha

    Wakili: Ni watu wengi walikuwa wakisema?

    Shahidi: Wengi walikuwepo madereva wa bajaji na mmoja mwenye kiduka pembeni

    Wakili: Kilichoendelea baada ya hapo?

    Shahidi: Baada ya dakika zisizopungua 20 walitokea askari

  14. Tundu Lissu amaliza kumuhoji shahidi PW9

    L

    Lissu: Itakushangaza nikikuambia kwamba hao waliokamatwa na kesi yao kuisha, hivi sasa ni mashahidi kwenye kesi hii?

    Shahidi: Hainishangazi

    Lissu: Hamshangazi kwa sababu ndiyo utaratibu wenu kubambikiza makosa

    Lissu: Umewahi kuona video ambapo mimi nilizungumza kuhusu kuzuia uchaguzi mkuu wa. 2025 ambao imefanya leo nashtakiwa?

    Shahidi: Sikumbuki

    Lissu: Unajua kwa nini nashtakiwa kwa uhaini waeleze majaji?

    Shahidi: Ni kweli nafahamu kutokana na kauli uliyotoa

    Lissu: Hiyo kauli uliiona

    Shahidi: Sikumbuki

    Lissu: Sina maswali zaidi

  15. Umeshaingia kwenye 18 zangu – Tundu Lissu

    O

    Chanzo cha picha, MWANANCHI

    Lissu: Waeleze majaji ni sheria gani inasema kuzuia uchaguzi kwa mujibu sheria gani?

    Shahidi: Siwezi kujua

    Lissu: Asante huwezi kujua….kama PGO inasema uzingatie sheria zilizopo ulienda kukamata watu kwa kosa gani kama hujui kama ni kosa

    Shahidi: Tuliwakamata kwakua walikiwa wanaleta uchochezi…..

    Lissu: Nimekuuliza ulienda kukamata watu kwa kosa gani?

    Shahidi: Kama nilivyoeleza kuwa walikula njama

    Lissu: Tuendelee…umeshaingia kwenye 18 zangu

    Lissu: Twende kwenye maelezo yako nani aliyekuruhusu wewe kujiandika maelezo wewe mwenyewe?

    Shahidi: Niliandika kwa sababu nilikuwepo

    Lissu: Nani aliyekuambia unaweza kujiandikia maelezo?

    Lissu: Majaji shahidi amekaa kimya…nani aliyekuambia unaweza kujiandikia wewe mwenyewe?

    Shahidi:…..

    Lissu: Nani aliyekuambia unaweza kujishuhudia wewe mwenyewe ASP

    Shahidi:…..

    Lissu: Hilo halina jibu ngoja nikupeleke kwenye PGO. Ni kweli au si kweli kwamba PGO imeweka utaratibu wa namna ya kuchukua maelezo ya shahidi?

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Ninachotaka kuuliza sasa hivi ni kuhusu kilichopo kwenye PGO 236 ni kweli au si kweli kwamba mtu anayeandika maelezo ya shahidi anakuwa tofauti na anayemuandikia huyu shahidi?

    Shahidi: Shahidi unaweza kuandika maelezo yako

    Lissu: Tueleze ni PGO gani inaeleza hivyo

    Shahidi: Siwezi kukumbuka

    Lissu: Nikupe hiki kitabu upitie…(shahidi anapelekewa PGO)

    Lissu: Kwenye hiyo PGO eleza kama kuna kifungu chochote kinachokuruhusu kujiandikia maelezo mwenyewe, kujishuhudia wewe mwenyewe?

    Shahidi: Siwezi kukumbuka?

    Lissu; Huwezi kukumbuka au hujui kusoma…kwenye maelezo yako umesema uliandika maelezo kwa mujibu wa kifungu cha makosa ya jinai cha 103 D cha sheria ya mwenendo wa kesi za jina kinakuruhusu wewe kujiandika maelezo, kujitolea onyo na kujishuhudia wewe?

    Shahidi: Naruhusiwa

    Lissu: Kwa hiyo kina kuruhusu kifungu hicho? Shahidi kwanza hakuna kifungu cha 103 kinachoruhusu. Hakuna

    Shahidi: Sikumbuki

    Lissu: Ni kweli au si kweli maelezo yako yanatakiwa kuandikwa na askari mwingine?

    Shahidi: Yanaweza kuandikwa na askari mwimgine au mimi mwenyewe

    Lissu: Ni kweli au si kweli kwamba ni askari mwingine anatakiwa kukupa wewe onyo?

    Shahidi: Sijaelewa swali lako

    Lissu: Swali langu ni fupi nimeuliza: Je, ni kweli si kweli askari mwingine anayekuandikia onyo la kusema ukweli?

    Shahidi: Kama naandika mwenyewe naweza

    Lissu: Ni kweli kwamba wewe mwenyewe unaweza kujipanga onyo?

    Shahidi: Labda sijaelewa maswali

    Lissu: Nataka kujua kama ni utaratibu wa kujiandikia mwenyewe, kujipa onyo mwenyewe….huna jibu…naomba nimsomee shahidi PGO

  16. Tundu Lissu anaendelea kumuhoji shahidi PW9

    kk

    Chanzo cha picha, Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

    Baada ya kumsomea maelezo yake Lissu anauliza kwa shahidi kama yapo sawa na shahidi anaunga mkono.

    Lissu: Nataka kujua kwenye maelezo yako ni wapi uliposomea na pili ni eneo la uzoefu wako halipo kwenye maelezo yako, eneo la tatu ni sehemu ulizopitia Oysterbay, Ofisi ya RCO Geita na Arusha eneo la nne ni hicho kikosi chako cha watu 9, eneo la tano ya kuwa ulipata maelezo kupitia radio call, nimeangalia kwenye maelezo yako hakuna.

    Eneo jingine ni ukiwa unawapeleka watuhumiwa kwenye ofisi ya RCO uliwahoji kwenye gari kwenye maelezo yako hayapo. Eneo jingine ni baada ya mahojiano yako ya kwenye gari walikujibu kuwa wao wanaunga mkono kauli ya kuuzuia uchaguzi mkuu kwenye maelezo yako hakuna.

    Eneo la 13 ni huyo kaimu RCO alitaka wachukuliwe maelezo lakini kwenye maelezo hayo hakuna. Sasa ningependa uieleze mahakama kama ungependa hayo maelezo yako yaingie kama ushahidi.

    Shahidi: Ndiyo ningependa

    Majaji: Maelezo hayo yatakuwa D8

    Lissu: Naomba shahidi apewe kielelezo D8. Shahidi hicho sasa ndiyo kielelezo. Shahidi kwenye ushahidi wako hapo kizimbani umeeleza kwamba ulingia Jeshi la polisi mwaka 2003 ukasomea nyota ya kwanza mwaka 2013 ukasomea mratibu wa polisi mwka 2023 ni kweli sio kweli?

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Umeyasema hayo mahakamani kwa sababu ni mambo muhimu kuingia kwenye rekodi za mahakama au umeongeza tu haya umuhimu

    Shahidi: Hayo ni muhimu

    Lissu: Kama ni muhimu kama unavyodai waeleze majaji kama yapo kwenye maelezo uliyotoa polisi?

    Shahidi: Kwenye hii karatasi siwezi kuandika kila kitu

    Lissu: Eleza kama yapo au hayapo?

    Lissu: Umesemakuwa una uzoefu wa miaka 15 kweli sio kweli?

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Eleza majaji kama hilo ni jambo muhimi kuandika kwenye maelezo yako

    Shahidi: Nimesema siwezi kuandika maelezo yote

    Lissu: Uliandika au laa?

    Shahidi: Sikuandika

    Lissu: Umeeleza kuwa ulifanya kazi Oysterbay kisha ofisi ya RCO GEITA na ukahamishiwa Arusha ni kweli sio kweli?

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Waeleze majaji kama uliandika hayo kwenye maelezo yako polisi?

    Shahidi: Sikuandika

    Lissu: Umeelza kwamba wakati unafanya hiyo Patrol ulipokea maelezo toka kwa kaimu RCO kwa kutumia radio call?

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Waeleze majaji kama kwenye maelezo yako maneno hayo yapo?

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Wakati unawapeleka watuhumiwa uliwahoji kwa kula njama wakitaka uchaguzi wa 2025 usifanyike?

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Waeleze majaji kama maneno hayo yapo kwenye maelezo yako

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Na unasema walikuambia wanaunga mkono na kula njama uchaguzi mkuu usifanyike ni kweli sio kweli?

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Waeleze majaji kama hayo yapo kwenye maelezo yako

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Unasema ulipowafikisha kwenye ofisi ya RCO ulipewa maelekezo wahojiwe

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Eleza kama maelezo hayo yapo kwenye maelezo yako ya polisi?

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Ni sahihi nikisema umeongeza maneno ambayo hukusema polisi lakini umeeeleza hapa

    Shahidi: Nimejaribu kufafanua mahakamani, siwezi kuandika kila kitu niliandika vitu muhimu

    Lissu: Ulitoa maelezo polisi kwa nini kuna tofauti kati ya maelezo yako polisi na ushahidi wako hapa mahakamani?

    Lissu: Wewe katika cheo chako cha Polisi unafahamu mashariti ya PGO?

    Shahidi: Nayafahamu masharti ya PGO lakini sasa…..

    Lissu: Hiyo lakini sasa ni swali la nani….?

    Lissu: Naomba nimuelekeze shahidi katika order 1 para 25 ya PGO za 2021(anasoma PGO)

  17. Tundu Lissu aanza kumuhoji shahidi PW9

    l

    Chanzo cha picha, Mwananchi

    Lissu: Nashukuru mheshimiwa Jaji. Shahidi naomba nikuulize maswali naomba ujibu maswali yangu kadri ninavyouliza. Naomba uwaeleze majaji kama huko polisi mnakojifunzia hizo kazi kama mnafundishwa kuwa waongo

    Shahidi: Hapana hatufundishwi kuwa waongo

    Lissu: Naomba ueleze kama mnavyokuwa mnafundishwa kutoa ushahidi mahakamani kuongoeza maneno ambayo hayapo

    Shahidi: Hatufundishwi

    Lissu: Waeleze majaji kama huko Polisi unafundishwa kutokuwa watu wa heshima

    Shahidi: Sio kweli

    Lissu: Hamfundishwi hivyo. Waelezo majaji kama huko Polisi mnafudishwa au hamfudishwi kuwa watu wenye maadili

    Shahidi: Tunafundishwa kuwa watu wenye maadili

    Lissu: Unafahamu kitu kinaitwa polis general order (PGO) hii (anamuonesha)?

    Shahidi: PGO Naifahamu

    Lissu: Sawa

    Lissu: Waeleze majaji kama ni sahihi au sio sahihi kwamba PGO inasema polisi wanatakiwa watu wenye weledi kwenye kazi zao

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Waeleze majaji kuwa kwa mujibu wa PGO polisi anatakiwa awe muaminifu, wasiwe na upendeleo, wasiwe mafisadi ni kweli sio kwel?

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Ulieleza mahakama kuwa ukiandika maelezo yako 18-04-2025 ni kweli sio kweli?

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Na unaweza kuyatambua ukioneshwa

    Shahidi: Naeweza

    Lissu: Naomba apewe maelezo yake

    Lissu: Maelezo hayo ndiyo uliyoandika tarehe 18-04-2025

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Waeleze majaji nani alikuandikia maelezo

    Shahidi: Maelezo niliandika mwenyewe

    Lissu: Waeleze majaji nani aliyekupa onyo wakati unaandika hayo maelezo

    Shahidi: Mimi ni shahidi nimeandika mwenyewe

    Lissu: Nimeuliza swali nani aliyekupa onyo wakati unaandika maelezo?

    Shahidi: Hakuna

    Lissu: Nitaanza kumsoea maelezo yake. Sasa nakusomea maelezo yako kama kuna sehemu nimekosea utasema baadae utaeleza kwa majaji kama nilivyosoma ndivyo (anasoma maelezo ya shahidi PW9).

  18. Wakili wa serikali Renatus Mkude anaendelea kumhoji shahidi PW9

    l

    Chanzo cha picha, MTANDAO

    Maelezo ya picha, Renatus Mkude

    Wakili: Baada ya hapo?

    Shahidi: Tuliwafikisha katika ofisi za upelelezi mkoa wa Arusha

    Wakili: Ilikuwa muda gani?

    Shahidi: Saa 2:00

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Nilipewa maelekezo tena na kaimu upelelezi mkoa wa Arusha kwamba nifungue jarada la uchunguzi

    Wakili: Nini kilifuata

    Shihidi: Nilifungua jarada namba ARS/DCLD/P40/2025

    Wakil: Baada hayo?

    Shahidi: Nilipewa maelekezo tena na kaimu mpelelezi mkoa wa Arusha

    Wakili: Maelekezo hayo yalikuwa yanakutaka ifanye nini?

    Shahidi: Aliniambia watuhumiwa wahojiwe na kuchukuliwa maelezo yao

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Niliwapangia askari wengine wa RCO baada ya hapo nikaendelea na majukumu yangu mengine

    Wakili: Baada ya kuwaacha kwa RCO kuna kingine kiliendelea?

    Shahidi: Nakumbuka niliandika tu malezo yao kama shahidi 18-04-2025

    Wakili: Mhe Majaji ni hayo tu kwa sasa kwa shahidi

  19. Wakili wa serikali Renatus Mkude anaanza kumhoji shahidi PW9

    .

    Wakili: Unafanya kazi wapi?

    Shahidi: Nafanya kazi katika ofisi ya upelelezi mkoani Arusha kama kiongozi wa anti-robber.

    Wakili: Hii anti- robber ni nini?

    Shahidi: Ni kikosi cha kuzuia uhalifu.

    Wakili: Kazi yako kama askari polisi au mpelelezi hii kazi una mafunzo yoyote?

    Shahidi: Ndiyo nina mafunzo.

    Wakili: Ni mafunzo gani, uliyapata wapi na lini?

    Shahidi: Kwanza nakumbuka nilipata mafunzo 28/04/2003 katika chuo cha Polisi Moshi.

    Wakili: Baada ya mafunzo nini kiliendelea?

    Shahidi: Nilijifunza mafunzo mbalimbali ikiwemo upelelezi.

    Wakili: Ulimaliza lini?

    Shahidi: 2003 mwezi 11

    Wakili: Kuna mafunzo mengine ulipata?

    Shahidi: Ndiyo

    Wakili: Ulipata wapi na lini?

    Shahidi: Nilienda kusomea nyota ya kwanza kutoka chuo cha Polisi mwaka 2013.

    Wakili: Baada ya hapo?

    Shahidi: Nilipata mafunzo ya cheo cha mratibu msaidizi polisi.

    Wakili: Kutoka wapi?

    Shahidi: Chuo cha Polisi cha Dar-es-salaam nilimaliza mwezi 11 mwaka 2023.

    Wakili: Kwa upande wa mafunzo kuna kingine kilichotokea?

    Shahidi: Ni masomo tu mengine tulikuwa tunafundishwa tukiwa kazini.

    Wakili: Polisi kama kazi una uzoefu wa miaka mingapi?

    Shahidi: Kwa upelelezi nina uzoefu wa miaka 15

    Wakili: Ukiacha mafunzo na uzoefu tukirudi kwenye ofisi ya upelelezi mkoani Arusha upo pale toka lini?

    Shahidi: Nipo pale tangu mwaka 2023

    Wakili: Kabla ya hapo ulikuwa wapi?

    Shahidi: Mimi kazi nilianza Oyster Bay Dar es salaam nilianza kama askari wa kawaida

    Wakili: Baada ya hapo?

    Shahidi: Baada ya hapo nilihamishwa kwenda Geita ofisi ya mkuu wa upelelezi makosa ya jinai mkoani Arusha.

    Wakili: Baada ya hapo?

    Shahidi: Baada ya hapo ndiyo nikahamia mkoa wa Arusha

    Wakili: Majukumu yako ni yapo kwenye ofisi ya mpelelezi mkoa wa Arusha?

    Shahidi: Kufanya doria katika maneno mbalimbali mkoani Arusha, kufanya upelelezi wa makosa jinai na kufikisha watuhumiwa mahakamani.

    Wakili: Mahakama inataka kujua siku ya tarehe 3/4/2025 majira ya saa 11 jioni ulikuwa wapi.

    Shahidi: Nilikuwa naendelea na shughuli zangu kushika doria katika maeneo ya jiji la Arusha.

    Wakili: Unakumbuka ulikuwa na nani na mlikuwa wangapi?

    Shahidi: Tulikuwa askari 9 (section 1).

    Wakili: Hii section moja inakuwa na askari wangapi?

    Shahidi: 9 ukijumuisha na dereva.

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Wakati tunafanya doria kwa gari aina ya Toyota, nikapata maelezo toka kwa kaimu mkuu wa upelelezi Arusha, Boni Mgogo.

    Wakili: Maelekezo hayo ulipata kwa njia gani?

    Shahidi: Maelekezo hayo nilipata kupitia radio call.

    Wakili: Hii radio call ni nini??

    Shahidi: Sijui Kiswahili chake lakini sisi mapolisi ni kifaa cha mawasiliano.

    Wakili: Maelekezo hayo yalikuwa ya nini?

    Shahidi: Alipata taarifa kuwa kwa mrombo kuna vijana wanahamasishana kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

    Wakili: Baada ya kupata maelekezo nini kiliendelea?

    Shahidi: Kwakua hatukua mbali na eneo hili (tulikuwa mbauda) tuliweza kufika kwa haraka eneo hilo.

    Wakili: Baada ya kupata maelekezo kutoka kwa kiongozi wako na kufika hapo nini kiliendelea?

    Shahidi: Baada ya kufika kweli tulikuta vijana wengi wakiwa wanakula njama juu ya uchaguzi mkuu wa 2025.

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Tuliwambia wapo chini ya ulinzi

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Baada ya kuwaambia wapo chini ya ulinzi walianza kukimbia lakini tulikamata watuhumiwa wawili P4 na P7.

    Wakili: Baada ya kuwakamata nini kiliendelea?

    Shahidi: Baada ya hapo nikatoa maelekezo wawapeleke katika kituo cha polisi cha Muret.

    Wakili: Walikuwa askari wangapi?

    Shahidi: Walikuwa wanne.

    Wakili: Baada ya kutoa maelekezo wapelekwe polisi nini kiliendelea?

    Shahidi: Sisi tulibakia ili kumata waliosalia lakini hatukuwapata.

    Wakili: Nini kiliendelea kwa upande wenu?

    Shahidi: Walivyokimbia waliacha bajaji zao hivyo tulifanikiwa kukamata bajaji zao na kuzipeleka kituo cha Polisi cha Muret.

    Wakili: Bajaji zilikiwa ngapi?

    Shahidi: Bajaji zilikuwa nne lakini mbili ni za watuhumiwa tulio wakamata

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Tulipeleka bajaji kituo cha polisi cha Muriet majira ya saa 1 usiku.

    Wakili: Baada ya kufika kituo cha polisi nini kiliendelea?

    Shahidi: Nilipata maelekezo kutoka kwa kaimu mkuu wa upelelezi mkoa wa Arusha.

    Wakili: Maelekezo hayo yalikuwa yanakutaka kufanya nini?

    Shahidi: Maelekezo hayo yalikuwa yananitaka kupeleka watuhumiwa wawili katika ofisi za mkuu wa upelelezi Arusha.

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Nilipeleka watuhumiwa.

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Nikiwa nawapeleka mimi niliwahoji P4 na P7.

    Wakili: Uliwahoji nini?

    Shahidi: Kwa nini wanakula njama wakitaka uchaguzi wa 2025 usifanyike?

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Baada ya kuwahoji wote walikiri wanamuunga mkono Mwenyekiti wa chama cha Demkrasia na Maendeleo Tundu Lissu.

    Wakili: Walikuambia wanamuunga mkono vipi?

    Shahidi: Walidai kwamba wanaunga mkono kauli ya Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu kwa kauli yake aliyotoa kwenye mitandao kuwa watazuia uchaguzi wa 2025 na watakinukisha.

    Soma zaidi:

  20. Kesi ya Kiongozi wa chama cha CHADEMA Tundu Lissu imeanza

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kesi ya kiongozi wa chama cha CHADEMA nchini Tanzania Tundu Lissu inaendelea leo.

    Baadhi ya wafuasi wake wapo mahakamani kufuatilia kesi hiyo.

    Wakili upande wa serikali amesema leo upande wao wameleta mashahidi watatu ili kuendelea na usikilizwaji wa kesi.

    Shahidi wa kwanza leo ni afisa polisi ASP Geoffrey Mtufe ambaye ni shahidi wa PW9 mwenye umri miaka 47 mkaazi wa Arusha.

    Soma zaidi:

Trending Now