Changamoto za kisiasa zinazomkabili Netanyahu nchini Israel

Chanzo cha picha, EPA
Kumekuwa na nguvu za pamoja kutoka jeshi la Israel na viongozi wa kisiasa kujenga taswira kuwa vita vya Iran vimeleta mabadiliko eneo la Mashariki ya kati, ingawa Israel bado haijatimiza malengo yake ya kubadilisha utawala wa Iran.
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ametumia miongo kadhaa kujiandaa kwa makabiliano haya na Iran, na maisha yake ya kisiasa yamejengwa juu ya ahadi ya kuilinda Israel dhidi ya adui wake, Iran.
Baada ya kuanzisha vita vya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Iran pamoja na Marekani, kauli za Netanyahu kuhusu vita hivyo hazijakuwa na ufasaha, anaelezea kuwa mashambulizi hayo ni "kampeni ya uwepo wetu wenyewe."
Mkuu wa majeshi ya Israel ameelezea mashambulizi hayo kama "operesheni ya kulinda Maisha ya baadaye katika ardhi ya mababu zetu kwa vizazi vijavyo."
Mmoja wa washauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Netanyahu amesema kuwa hii ni "fursa ya kipekee ya kubadilisha mwelekeo wa Mashariki ya Kati."

Chanzo cha picha, GPO
"Hii ni kilele cha kile ambacho Netanyahu amejaribu kukipa jina jipya kama 'Vita vya Ukombozi,' ambavyo kwa mtazamo wake vilianza tarehe 7 Oktoba 2023. Na hii kama si vita vya mwisho, basi vita kubwa dhidi ya Iran," anaeleza Neri Zilber, mwandishi wa habari wa Tel Aviv na mshauri wa kisiasa wa Israel Policy Forum, taasisi ya utafiti ya Marekani.
Mabadiliko ya utawala nchini Iran yatasaidia kuangamiza maadui wa Israel katika eneo hilo (kama Hezbollah nchini Lebanon au Hamas huko Gaza) kwani watakosa ufadhili, mafunzo na silaha kutoka Iran, jambo ambalo linaweza kubadilisha usalama wa Israel.
Lakini baada ya kumuua kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, kupitia shambulio la angani, na kutoa wito wa mara kwa mara kwa raia wa Iran kutumia fursa hii kuiasi taifa lao, huenda kubadilisha utawala wa Iran kikamilifu ukakuwa vigumu.

Chanzo cha picha, WANA/via Reuters
Baadhi ya watu nchini Israel wanatafsiri hili kama ishara kwamba nchi yao inaombwa kumaliza vita pamoja na Marekani,kipindi hiki ambacho bei ya mafuta imepanda.
Katika vita vya mwaka uliopita dhidi ya Iran, Waziri mkuu wa Israel alitangaza "ushindi wa kihistoria" ambao utadumu hadi vizazi vijavyo na kwamba ameondoa vitisho viwik vya kimsingi hasa silaha za nyuklia na makombora yake ya masafa marefu.
Miezi minane baadaye, Israel ilirudi tena vitani, Netanyahu akisema, akidai Iran ilikuwa ikijenga upya na kwa kasi mpango wake wa makombora na ilikuwa inapanga kuuhamishia, pamoja na mpango wake wa nyuklia, chini ya ardhi.
Kutakuwa na vita vingine?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Changamoto ambayo Netanyahu anakabiliwa nalo sasa nibila mabadiliko ya utawala mjini Tehran, itachukua muda gani kabla ya mashambulizi mengine?
Vyanzo vya kijeshi vinasema kwamba uharibifu uliosababishwa kwa mipango ya silaha ya Iran safari hii ni mkubwa zaidi kuliko nyakati zilizopita, kwani vituo vya kutengeneza silaha na vituo vyao vya kutoa maagizo ya kijeshi, pamoja na ghala za makombora na vifaa vya kurushia, vimeshambuliwa.
Meja Jenerali Yaakov Amidror, mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Israel na mwanachama wa Taasisi ya Jerusalem ya Mkakati na Usalama, anaeleza kuwa hata bila Wairani kuingia mitaani, Israel inaweza kufikia malengo yake ya msingi kwa kuacha utawala huo ukiwa dhaifu sana kiasi cha kutoweza kuwa tishio.
"Iwapo tungeweza kufanikisha mabadiliko ya utawala, hilo lingeibadilisha Mashariki ya Kati. Lakini tunajua mipaka yetu, sisi si dola yenye nguvu kubwa duniani, na tunapaswa kuwa wapole katika maamuzi yetu," alieleza.

Chanzo cha picha, Reuters
Mwandishi wa habari za ulinzi kwa moja ya magazeti yanayosomwa sana nchini Israel, Yedioth Ahronoth, anasema kwamba vyanzo vya kijeshi visivyojulikana vinaripoti dalili ya kuwepo na mvutano ndani ya mfumo wa uongozi usalama wa Iran, "ikijumuisha mivutano ya ndani katika Kikosi cha Mapinduzi.
Netanyahu amependekeza kuwa, baada ya kuunda hali inayoweza kuleta mabadiliko ya utawala, Israel sasa inaweza kujiondoa na kusubiri shinikizo za ndani za Iran zichukue mkondo wake.
Lakini kwake, kuna hatari ya kisiasa ikiwa ataacha utawala ukiwa salama.
Mchambuzi Neri Zilber anaamini kuwa hatari kwa Netanyahu ni kwamba matamko yake makubwa kuhusu "ushindi wa jumla" dhidi ya Iran ni maneno tu yakujigamba.
"Hamas bado inadhibiti takriban nusu ya Gaza. Hezbollah sasa inaendesha mapigano yenye ukali zaidi kuliko watu wengi walivyotarajiwa hata baada ya kusitishwa kwa mapigano mnamo 2024, na baada ya mashambulizi ya Juni mwaka uliyopita dhidi ya Iran, Israel na Marekani tena wamerejelea katika vita kubwa zaidi dhidi ya Tehran," anasema.

Chanzo cha picha, Reuters
Vita Vya kujirudia
Migogoro isiyokamilika ya Israel na Hamas na Hezbollah kwenye mipaka yake ni kielelezo cha wazi kuhusu nguvu za kijeshi za Israel, hata baada ya mabadiliko makubwa katika mkakati wa ulinzi wa Israel kufuatia mashambulizi ya Hamas mnamo Oktoba 7, 2023.
Kihistoria, imekuwa rahisi kuanzisha vita kuliko kuyamaliza.
Hivi sasa Israel inapigana kwenye upande wa pili dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon, baada ya kundi hilo linaloungwa mkono na Iran kujibu kifo cha Khamenei na kujiunga na mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel.
Baada ya miongo kadhaa ya vita vya mara kwa mara na Hezbollah, na kampeni kali ya kuwatokomeza mnamo mwaka wa 2024 iliiweka kundi hilo katika hali dhaifu, wengi nchini Israel wanaona wakati huu kama fursa ya kumaliza tishio kwenye mpaka wake wa kaskazini .
Vikosi vya Israel vinaendelea kuingia kusini mwa Lebanon katika kile wanachodai kuwa, hadi sasa, ni operesheni ya kujilinda.
Lakini mkuu wake wa majeshi, Luteni Jenerali Eyal Zamir, ametangaza kuwa lengo lake ni kupokonya silaha za Hezbollah."
"Hii itachukua muda mrefu sana," alisema, alielezea kuwa "Hizi ni vita vya vita vya kizazi chetu ,vita muhimu, vita vya maamuzi vitakavyobainisha mustakabali wetu na usalama wetu kwa miaka ijayo."

Chanzo cha picha, Reuters
Swali kuu ni kama Israel itaendelea kupigana kwenye upande huu, hata kama Washington itamua kumaliza vita vyake dhidi ya Iran.
Licha ya uchovu mkubwa kutokana na vita baada ya zaidi ya miaka miwili ya mgogoro wa mara kwa mara, maoni ya umma nchini Israel yanaunga mkono kwa nguvu vita hivi vya kikanda.
Inatarajiwa kwamba Netanyahu atatumia wakati huu kukarabati urithi wake wa kisiasa,katika uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.













