Washirika wa Marekani na China wanasemaje kuhusu kutuma meli za kivita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz?

.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Meli moja iliyokwama katika Mlango Bahari wa Hormuz kwa wiki mbili
Muda wa kusoma: Dakika 3

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Marekani haihitaji usaidizi wowote kutoka mataifa mengine katika vita vya Iran, siku chache tu baada ya kutoa wito kwa washirika wa Marekani kumsaidia kufungua mlango wa bahari wa Hormuz.

Kupitia mtandao wake wa Truth Social alisema "Mataifa mengi ambao ni wanachama wa Nato walikuwa wametuambia kuwa hawataki kuhusika"

"sijashtushwa na hatua yao, kwasababu naiona Nato ikuwa ya upande mmoja tu, tutawalinda lakini hawawezi kutusaidia na chochote" aliandika

Tarehe 14 mwezi Machi, alisema kuwa "natumai china, Ufaransa, Japan, Korea Kusini na Uingereza, ambao wameathirika na mgogoro huu watatuma meli zao za vita"

Mlango wa bahari wa Hormuz umefugwa na Iran, isipokuwa meli chache tu ambazo zimebeba mafuta ya Iran kuelekea India na China zinaruhusiwa kupita tangu mashambulizi hayo kuanza.

20% ya mafuta yote duniani hupitia eneo hilo, na kufungwa kwa mlango huo wa bahari kumesababisha kupanda kwa bei ya mafuta.

Katika chapisho lake siku ya Jumanne, Trump hakusema ni taifa gani ambaye ni mwanachama wa kujihami wa Nato amekubali kumuunga mkono katika vita hivyo.

Uingereza

Akiwahutubia wanahabari, Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer alisema wanakuja na mpango maalum utakao jumuisha Marekani, Ulaya na mataifa ya ghuba ila bado hawajaafikia mpango huo.

Alipoulizwa na BBC iwapo atatuma droni na meli eneo hilo, Waziri wa nishati Ed Miliband alisema "tutatumia njia yoyote ambayo itatuwezesha kuufungua mlango wa Hormuz pamoja na washirika wetu"

Aidha Waziri huyo alisisitiza kuwa njia bora ni kumaliza mzozo huo.

Ujerumani

Msemaji wa serikali alisema vita vya Iran "havihusiani na Nato"

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius aliuliza kuwa "Trump anatarajia nini kutoka kwa mataifa ya ulaya ambalo jeshi lake la Maji haliwezi kufanya?"

"Hivi si vita vyetu, hatukuvianzisha"

Ufaransa

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema ako tayari kusindikiza meli za mafuta na ulinzi zinazopitia mlango wa bahari wa Hormuz iwapo hali itakuwa tulivu.

"Ufaransa ina jukumu katika eneo hili,la kulinda raia wetu na maslahi yetu, na kuwa mtu wa kuaminika kwa washirika wetu na kusaidia katika kusitisha vita hivyo" alisema Macron.

Meli ya kivita ya Ufaransa tayari iko katika bahari ya mediterenia kwa kile walikiita "utayari wa kujilinda"

China

Alipoulizwa na wanahabari iwapo taifa lake limepokea ombi la kutuma meli za kivita karibu na Iran, Waziri wa mambo ya kigeni wa China Lin Jian alisema "China inawataka pande zinazopigana kusitisha vita hivyo ili kuzuia mzozo wa kimataifa na kuathiri uchumi wa dunia"

Aliongezea kuwa China inawasiliana na pande husika kutafuta njia ya kusitisha vita hivyo.

Korea Kusini

Waziri wa mambo ya kigeni wa Korea Kusini alisema "wanafuatilia kwa karibu" semi za Trump na mataifa hayo mawili yatazidi kuwasiliana kabla ya kufanya uamuzi wowote.

Waziri wa ulinzi Ahn Gyu-back aliaambia bunge kuwa kutuma meli ya kivita eneo la Hormuz kutahitaji idhini ya bunge la taifa hilo.

Japan

Waziri mkuu wa Japan Sanae Takaichi alisema siku ya Jumatatu kuwa hajapokea ombi lolote la kuwataka kutuma meli za kivita katika mlango wa bahari wa Hormuz.

"Serikali ya Japan bado inatathmini hatua dhabiti za kuchukua, na lazima iwe chini ya sheria za Japan. Bado tunazingatia jinsi ya kulinda maisha ya raia wa Japan na wanajeshi wa maji."

Takaichi anatarajiwa kukutana na Trump mjini Washington tarehe 19 mwezi Machi.

Umoja wa Ulaya

Naibu rais wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas alisema siku ya Jumatatu kuwa "kwa sasa hatuna hamu" kubadilisha kazi maalum ya wanajeshi wa maji eneo hili.

"Hakuna mtu ambaye yuko tayari kuhatarisha Maisha ya watu wake katika mlango wa bahari wa Hormuz, lazima tutumie njia ya kidiplomasia kuhakikisha mlango huo wa bahari unasalia wazi" aliiambia shirika la habari la Reuters.