Shirika la Ndege Tanzania laendelea kuendeshwa kwa hasara

Chanzo cha picha, AIR TANZANIA
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa leo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Dkt. Charles Kichere, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linaendelea kujiendesha kwa hasara.
Amesema shirika hilo limepata hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 191 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Kwa ujumla, tangu kuanzishwa kwake, shirika hilo limekusanya hasara ya takribani shilingi bilioni 748.
Katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, shirika limelipa zaidi ya shilingi bilioni 310 kwa abiria kama fidia kutokana na safari zilizositishwa au kuahirishwa. Hasara hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na gharama za uendeshaji kuwa kubwa kuliko mapato yanayopatikana.
Aidha, matumizi yasiyoridhisha ya ndege ya mizigo yameelezwa kuwa miongoni mwa sababu za hasara. Katika miezi ya hivi karibuni, ndege hiyo ilifanya safari nyingi zisizo na tija na hatimaye kusimamishwa, hali iliyoongeza kiwango cha hasara.
Akizungumzia mashirika mengine ya umma yanayoendeshwa kwa hasara, Dkt. Kichere alilitaja Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Alisema licha ya mapato ya reli ya kisasa (SGR) kuongezeka, reli ya zamani imeendelea kupata hasara kutokana na kuongezeka kwa ajali. Ndani ya mwaka mmoja, jumla ya ajali 328 zimeripotiwa, na kusababisha uharibifu wa miundombinu.
Kuhusu hali ya deni la taifa, Dkt. Kichere alisema limeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 110 likijumuisha deni la ndani na la nje. Ndani ya mwaka mmoja, deni hilo limeongezeka kwa zaidi ya shilingi trilioni 12, sawa na asilimia 13.4.
Ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa mikopo ya nje pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani.
Hata hivyo, alibainisha kuwa pamoja na ongezeko hilo, deni la taifa bado ni himilivu kwani lipo katika kiwango cha asilimia 40.7, ambacho ni chini ya ukomo wa asilimia 55.
Akisoma taarifa ya ukaguzi wa hesabu za vyama vya siasa, Mkaguzi Mkuu alisema vyama viwili CUF na NRA vimepata hati zenye mashaka kutokana na kutokuwasilisha nyaraka zote zinazohitajika. Wakati huo huo, chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, hakijakaguliwa kutokana na mashauri yaliyopo mahakamani yanayohusiana na mali za chama hicho.
Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali itafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali haraka iwezekanavyo.
Baada ya kusomwa kwa taarifa hizo, zinatarajiwa kuwasilishwa bungeni ndani ya siku saba kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa mapendekezo.
Unaweza kusoma pia:

















