Wanawake wajuta kuingia kwenye "mtego" wa uzazi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Carmen anampenda mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka 10, ila anasema kama angekuwa na uwezo wa kurudi nyuma kiwakati, hangekubali kuwa mama.

Anasema "kuwa mama kumenidhoofisha kiafya,kifedha,kinguvu,kimwili na wakati. Gharama hiyo inadumu milele.

Carmen ambaye ni mwalimu akiwa na umri wa miaka 40, ni miongnoni mwa kundi fiche la kina mama ambao huongea kuhusu hisia zao za kujutia kuwa mama.

Kujuta huku huwa hakusemwi waziwazi mbele ya wat, na wanawake hawa wakubali kuzungumza na BBC iwapo majina yao yatabanwa kwa kuhofia kuhukumiwa na jamii na familia zao ambazo hawana ufahamu wowote.

Miaka michache iliyopita, Carmen alielezea mbele ya umma kuwa anajutia kuwa mama, maneno ambayo wengi walimhurumia huku wengine wakimshambulia.

Katika filamu iliyoteuliwa katika tuzo za Oscars "if I had legs I would kick you" inaangazia shinikizo na kujitolea kwa kina mama katika kuwalea Watoto wao.

Rose Byrne anaigiza kwenye filamu hiyo alitoa hotuba kuhusu anvyojihisi mpweke katika juhudi zake za kutimiza mahitaji ya mwanawe na familia yake.

.

Chanzo cha picha, Logan White/A24

Carmen anasema Maisha yake inaendana na maudhui ya filamu hiyo akisema, "Kuwa mama ni kazi isiyo na mwisho, unaifanya hata kama hujataka kwa sababu kuna kiumbe kidogo kinachokutegemea. Inahisi kama mtego usioweza kutorokeka."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Carmen anazungumza kwa uwazi sana kuhusu jinsi anavyohisi "kuchoka", lakini sauti yake inachangamka anapoulizwa kuhusu mwanawe "Theo"

Theo hana uhusiano wowote na majuto yangu. Yeye ni mvulana mzuri sana anayependwa, na ninampenda sana na naweza kutoa maisha yangu kwa ajili yake bila kusita, ni mkarimu, mtulivu, na anafuta maelekezo.

Mtaalamu wa saikolojia ya tabia, Anna Mathur, anasema, "Wakati wanawake wanapohisi salama vya kutosha kuzungumza kuhusu majuto yao ya ulezi, mara nyingi kinachojitokeza si ukosefu wa upendo, bali hisia ya upweke, uchovu, au kupoteza utambulisho wao binafsi."

Kwa Carmen, ambaye anajieleza kama mtu anayependa vitu viende anavyotaka yeye, jukumu la kumlea "mtoto mzuri na mwenye furaha" linaonekana kama mzigo mkubwa kwake.

Alijiahidi kuwa "Theo" hatajua alichokihsi akiwa mtoto.

Alitoka katika mazingira maskini na yenye changamoto nyingi "ambapo vurugu ilikuwa suala la kawaida," na hakuwahi kujihisi kupendwa.

Anaelezea kuwa mwanzoni kuwa mama ilikuwa raha, na Theo alikuwa mtoto mtulivu.

Hata hivyo, mambo yalibadilika mwanawe alipoanza kuonyesha dalili za kuchelewa kua, na "kila tukio dogo likaanza kuleta wasiwasi," anaongezea kuwa "Nilijihisi vibaya, na niliogopa kuwa maisha yake yangekuwa magumu."

Mwishowe, Theo hakupatikana na magonjwa ambayo Carmen alikuwa ameogopea na sasa yuko vizuri kiafya, lakini msongo wa mawazo wa kila mara ulimfanya apate ugonjwa unaoathiri misuli ya mwili.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mtaalamu wa masuala ya jamii kutoka nchini Israeli, Orna Donath, na mwandishi wa kitabu cha (A Study: Regret for Motherhood), anaamini kwamba majuto hutokana na malezi makali au yenye changamoto aliyoyapata mama.

Donath aliwahoji wanawake 23, kila mmoja akielezea tofauti kati ya hisia za majuto kuhusu kuwa mama na hisia wanazo kwa watoto wao.

Mmoja wa wanawake hao anasema"Ninajuta kuwa mama, lakini ninawapenda watoto wangu. Sitaki waondoke au wasikuwepo. Ninachotaka tu ni mimi kuto kuwa mama."

Takwimu zinaonyesha kuwa hisia hii si ya kawaida.

Tafiti ya mwaka 2023 nchini Poland ilikadiria kuwa kati ya asilimia 5 hadi 14 ya wazazi wanajuta uamuzi wao wa kuwa na watoto na wangechagua kuto kuwa na watoto kama wangepewa nafasi ya kufanya uamuzi huo tena.

Licha ya ukimya wa umma, wanapata Faraja katika kundi moja la mitandaoni. Carmen alijiunga na kikundi cha Facebook kilichoitwa "Ninajuta Kuwa na Watoto," ambacho kina wanachama wapatao 96,000.

Mmoja wa wanawake wanaofuatilia kikundi hicho aliambia BBC, "kuwa mama kumejaa nyakati nzuri, lakini hauna uhuru. Ninavaa naficha mengi mbele ya binti yangu, lakini anapolala, nakuwa huru na napendelea kuwa peke yangu."

Anaongeza kuwa imebidi aweke kando maono yake ya kusafiri au kufungua biashara kutokana na fedha kuwa chache."Nimepoteza motisha kwa kila kitu, isipokuwa kujaribu kumlea mwanangu."

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwanamke mwingine kutokea nchini Uingereza anasema anahisi "kudhalilishwa" wakati watu wanadhani mama asiye na furaha lazima awe na huzuni inayokuja baada ya kujifungua. Watoto wangu sasa ni watu wazima, lakini bado naomboleza maisha niliyoshindwa kupata nafasi ya kuyaishi."

"Sasa pia nina wasiwasi kuhusu kuwalea wajukuu wangu siku za usoni, kwani jukumu la kulea halina mwisho."Anasema.

Kikundi cha Facebook "Ninajuta Kuwa na Watoto" kiliundwa mwaka 2007, na maudhui yake hutoka moja kwa moja kwa wazazi, wengi wao ni wanawake, ambao hutoa hadithi zao kupitia ujumbe wa faragha ili kuchapishwa baadaye bila kutambulika.

"Lengo halikuwa kamwe kudhalilisha wazazi au kukuza mtindo fulani wa maisha," anasema Giannina, msimamizi wa kikundi na mwanasayansi wa maabara nchini Marekani mwenye umri wa miaka 44.

Giannina anasema kuwa alikuwa na shaka kuhusu kuzaa watoto, na kwamba kusoma hadithi kwenye jukwaa hilo kulimsaidia kuamua kutozaa watoto.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mshauri na mtaalamu wa saikolojia kutoka Ireland, Margaret O'Connor, ambaye ni mtaalamu wa kuwasaidia watu kufanya uamuzi wa kuwa na watoto, anaamini kwamba vijana wa sasa wanamtazamo tofauti kuhusu kuwa na watato ikilinganishwa na vizazi vya awali.

O'Connor anasema: "Leo kuna uelewa mkubwa kwamba ni chaguo, si kitu cha moja kwa moja unachopaswa kufanya."

"Watu walio kati ya miaka 20 na 30 huja kwangu wakiwa wanataka kuwa na watoto, lakini wanahofu kuhusu changamoto, na wanataka msaada wa kuwasaidia kukabiliana nazo."

Lakini O'Connor anasema kwamba ni vigumu kutambua ishara wazi kwamba mwanamke atajutia uamuzi wake wa kutaka kuwa mama, kwa sababu kila mtu anapitia changamoto tofauti.

"Unapaswa kuwa na uhakika zaidi kuhusu uamuzi huu na kufanya kwa sababu zako binafsi, si kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa mpenzi wako au wazazi wako."Anasema

Anaongezea kuwa "ujumbe mara nyingi wengi huambiwa ni kwamba wote tutakuwa hapa kumtunza mtoto, lakini mara nyingi hali si hivyo. Ni mtoto wako, na wewe utakuwa na jukumu la kumhudumia binafsi."

O'Connor anaamini kwamba hisia za majuto kwa baadhi ya wazazi ni za kawaida kabisa, ikizingatia jukumu hili la uzazi na mahitaji yake makubwa.

Anashauri kushauriana na mtaalamu wa saikolojia ili kujaribu kuelewa mizizi ya majuto haya, na kuzungumza "katika nafasi bila kuhisi unahukumiwa."

Mtaalamu wa saikolojia Anna Mathur anasema kwamba majuto kuhusu kutotaka kuwa mama si hisia ambayo inaweza "kubadilishwa kikamilifu au kwa urahisi."

"Kwa baadhi ya wanawake, hisia hizi hupungua au kubadilika sana kwa msaada wa washauri, faraja,na muda unavyokwenda hali hubadilika"

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula