'Alinidunga na sindano iliyokuwa na virusi vya HIV baada ya kukataa kuolewa naye'

Chanzo cha picha, Getty Images
Tukio la kushangaza limetokea jimbo la Telangana nchini India, baada ya mwanaume mmoja aliyekuwa amejawa na hasira kumdunga sindano iliyo na damu mwanamke mmoja aliyekataa kuoleka na yeye.
Sindano hiyo ilikuwa imebeba damu iliyokuwa na virusi vya HIV.
Polisi wa eneo hilo wanasema mwanamke huyo kwa sasa anapokea matibabu.
Kulingana na polisi miezi michache iliyopita, familia ya mwanamke wa miaka 24 wanaoishi eneo la Annojiguda nje ya mji wa Hyderabad, na familia moja ya kijana mwenye umri wa miaka 25 ambao walikuwa majirani, walikuwa wamekubali kuwaoza wawili hao. Familia hizi ni jamaa moja.
Mshukiwa alikuwa akiishi na mamayake baada ya kifo cha babake. Mshukiwa huyo anafanya kazi ya uchukuzi.
"Kwasababu wazazi wa mshukiwa walikuwa wakishukiwa kuwa na virusi vya HIV, wazazi wa wasichana walitaka kijana huyo kupimwa kwanza kabla ya harusi kufanyika. Ukaguzi wa maabara ulibaini kwama kijana huyo ana virusi vya HIV. Harusi hiyo ilisimamishwa" hii ni kulingana na ripoti iliyoandikiwa na familia ya msichana katika kituo cha polisi.
"Kijana huyo alikasirika baada ya harusi hiyo kusitishwa"alisema polisi mmoja katika kituo cha polisi cha Pocharam.
"Uchunguzi wetu umebaini kijana huyu alimdunga msichana huyo na sindano, ili kubadilishana damu yake iwe ya msichana huyo pia. Alidhani akimdunga na virusi vya HIV hataweza kuoleka na mtu mwingine."
"Aliingia kwa nyumba kwa nguvu"

Chanzo cha picha, UGC
Wazazi wa msichana huyo wanasema tukio hilo lilitokea tarehe 11 mwezi Machi.
"Alijua msichana wetu yuko nyumbani pekee yake. Aliingia kwa nyumba na kumpea posa nyingine, alipokataa alimdunga sindano iliyokuwa na damu kwa nguvu."
Msichana huyo alikuwa amejawa na wasiwasi kuhusu tukio hilo kwa hivyo hakuripoti kwa wazazi wake.
Siku chache baadaye, alianza kuhisi na joto jingi na mwili kuuma, wazazi wake walimpeleka hospitalini, alipoulizwa maswali na daktari alisimulia kilichotokea.
"Kijana huyo alitaka kumuua msichana wetu kwa kumdunga na virusi vya HIV. Sheria kali inafaa kuchukuliwa" wazazi wa msichana huyo walisema.
Alijua yuko na virusi vya HIV
Polisi walipokea kesi hiyo tarehe 13 mwezi Machi. Mshukiwa alikamatwa, alisema polisi wa upelelezi Vijay Bhaskar Reddy.
"Tunachunguza kujua alipataje virusi vya HIV. Mara anasema alizaliwa navyo, mara anasema aliambukizwa, tunachunguza suala hilo" walisema polisi.
Mwanamke aliyeathirika sasa anapokea matibabu. Kulingana na polisi, vipimo vya damu vya msichana huyo kwa sasa vinaonyesha hajapata virusi vya HIV, ila uchunguzi zaidi bado unafanyika.
Kulingana na madaktari uhakika zaidi utapatikana baada ya miezi miwili.
BBC ilijaribu kumtafuta baba ya msichana huyo ila alikataa kuzungumza nasi.

Chanzo cha picha, UGC
"Dalili huwa hazionekana mara moja"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Dkt. Pratik Patil Yashwant, mtaalamu wa magonjwa ambukizi aliiambia BBC kwamba ingawa mwanamke huyo kwa sasa hana virusi, vipimo zaidi vinahitajika katika hatua tofauti.
Dkt. Patil alisema, "Ikiwa damu ya mtu mwenye virusi vya HIV itaingizwa moja kwa moja kwa mtu mwingine, uwezekano wa maambukizi ni zaidi ya 90%. Katika hatua ya kwanza, vipimo vya PCR na serolojia haviwezi kugundua maambukizi. Vipimo hivyo vinapaswa kurudiwa mara kadhaa."
"Wakati mwingine virusi hujificha ndani ya seli za damu, hali inayofanya vipimo visionyeshe mara moja. Kwa hiyo, ufuatiliaji wa mara kwa mara na vipimo vya kawaida vinahitajika," alisema.
Aina hii ya tabia inachukuliwa kuwa "tabia potovu", alisema Meena Hariharan, profesa katika idara ya saikolojia Chuo Kikuu cha Hyderabad.
"Kesi hii inaonyesha mtazamo wa 'ikiwa siwezi kukipata, basi hakuna mwingine atakayekipata.' Inaendeshwa na hulka ya ubinafsi na umiliki kupita kiasi," alisema.
Tukio kama hilo liliwahi kutokea katika mji wa Kurnool, ambapo mwanamke alishtakiwa kwa kumdunga sindano ya virusi vya HIV mke wa mwanaume aliyekuwa akimpenda.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula











