Silaha hatari zinazotumiwa na Marekani dhidi ya Iran

Chanzo cha picha, U.S.Central Command
Mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani kwa kushirikiana na Israel dhidi ya Iran yalianza tarehe 28 Februari 2026, yakifungua sura mpya ya mvutano mkali katika Mashariki ya Kati. Operesheni hiyo ilihusisha matumizi ya silaha za kisasa zenye uwezo mkubwa wa kushambulia kwa usahihi na umbali mrefu.
Katika saa 48 za mwanzo, mashambulizi hayo yalitekelezwa kwa nguvu kubwa ya anga, yakihusisha ndege za kivita, makombora ya masafa marefu pamoja na mifumo ya kisasa ya kijasusi. Hatua hiyo ilionyesha wazi kiwango cha maandalizi ya muda mrefu yaliyofanywa na Marekani kabla ya kuanzisha operesheni hiyo.
Taarifa za kijeshi zinaonyesha kuwa maandalizi ya mashambulizi hayo yalianza tangu Januari mwaka huu, yakihusisha usambazaji wa vifaa, kuimarisha vituo vya kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, pamoja na kupelekwa kwa manowari na ndege za kivita.
Ushirikiano kati ya Marekani na Israel umeonekana kuwa wa karibu zaidi katika operesheni hii, huku kila upande ukitoa mchango wake katika mashambulizi ya anga na ya kimkakati dhidi ya malengo muhimu ndani ya Iran.
Katika makala hii, tunaangazia baadhi ya silaha kuu zilizotumika katika mashambulizi hayo, ambazo zinaonyesha mwelekeo wa vita vya kisasa vinavyozidi kutegemea teknolojia ya hali ya juu.
Ndege ya kisasa ya B-2 Spirit

Chanzo cha picha, US-Air force
Moja ya silaha muhimu zaidi iliyotumika katika mashambulizi haya ni ndege ya kivita ya masafa marefu aina ya B-2 Spirit. Ndege hii ni miongoni mwa teknolojia za juu zaidi katika Jeshi la Anga la Marekani, ikiwa na uwezo wa kuepuka kugunduliwa na rada za adui.
B-2 Spirit hutengenezwa na kampuni ya Northrop Grumman na imeundwa mahsusi kwa ajili ya mashambulizi ya kimkakati dhidi ya malengo yenye ulinzi mkali, kama vile vituo vya nyuklia na maghala ya silaha.
Katika operesheni hii, ndege hizi ziliruka kwa zaidi ya saa 30 kutoka Marekani hadi Iran, zikifanya mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya malengo muhimu. Uwezo wake wa kuruka umbali mrefu bila kujaza mafuta unaiwezesha kufikia karibu eneo lolote duniani.
Ndege hii inaweza kubeba mabomu mazito, ikiwemo yale ya kuvunja ngome (bunker busters), ambayo hutumika kushambulia maeneo yaliyofichwa chini ya ardhi. Hii inaifanya kuwa silaha muhimu katika kushambulia miundombinu iliyolindwa sana.
Matumizi ya B-2 Spirit yanaonyesha jinsi Marekani inavyotegemea teknolojia ya stealth katika kuhakikisha mashambulizi yake yanafanikiwa bila kugunduliwa mapema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Makombora ya Tomahawk
Mbali na ndege za kivita, Marekani ilitumia na inatumia makombora ya masafa marefu aina ya Tomahawk, ambayo hurushwa kutoka kwenye meli za kivita au manowari.
Makombora haya yana uwezo wa kusafiri umbali mrefu sana na kulenga shabaha kwa usahihi mkubwa, yakitumia mifumo ya kisasa ya uongozaji (navigation systems).
Katika mashambulizi dhidi ya Iran, Tomahawk zilitumika kulenga vituo muhimu vya kijeshi na miundombinu, hasa katika hatua za mwanzo za operesheni.
Faida kubwa ya makombora haya ni uwezo wake wa kurushwa kutoka mbali bila kuhatarisha maisha ya marubani, jambo linalopunguza hatari kwa vikosi vinavyoshambulia.
Matumizi ya Tomahawk yanaonyesha mkakati wa Marekani wa kutumia mashambulizi ya mbali (stand-off strikes) ili kudhoofisha ulinzi wa Iran kabla ya kuingia moja kwa moja katika anga yake.
'Droni' za MQ-9 Reaper

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndege zisizo na runani ama drone aina ya MQ-9 Reaper ni moja ya silaha muhimu katika vita vya kisasa, ikitumika kwa upelelezi na mashambulizi kwa wakati mmoja.
Ndege hii isiyo na rubani ina uwezo wa kukaa angani kwa zaidi ya saa 27, ikikusanya taarifa muhimu za kijeshi na pia kushambulia malengo inapohitajika.
Katika mashambulizi dhidi ya Iran, MQ-9 ilitumika kufuatilia mienendo ya majeshi pamoja na kulenga malengo kwa usahihi mkubwa.
Ina uwezo wa kubeba makombora na silaha nyingine, jambo linaloiwezesha kufanya mashambulizi ya ghafla bila kutoa onyo.
Matumizi ya drone za MQ-9 Reaper kwa Marekani yameleta mabadiliko makubwa ya ambapo teknolojia hii ya kushambulia kwa mbali isiyohusisha binadamu kuwa mstari wa mbele imechukua nafasi kubwa kuishambulia Iran.
Silaha nyingine za Marekani dhidi ya Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbali na silaha hizo kuu, Marekani ilitumia pia ndege mbalimbali za kivita kama F-15, F-16, F-18, F-35 pamoja na A-10, ambazo zilihusika katika mashambulizi ya anga na ulinzi wa vikosi.
Aidha, mifumo ya ulinzi ya Patriot na THAAD ilitumika kukabiliana na makombora ya Iran, huku ndege za EA-18 Growler zikitumika kuvuruga mawasiliano na mifumo ya rada.
Katika operesheni hiyo pia kulikuwa na matumizi ya mifumo ya makombora ya HIMARS, ndege za upelelezi kama P-8, pamoja na manowari kubwa kama USS Abraham Lincoln na USS Gerald R. Ford, zilizosaidia mashambulizi kutoka baharini.














