Ligi ya Mabingwa Ulaya: Arsenal, PSG zatinga robo fainali, Chelsea, Man City nje

Chanzo cha picha, Getty Images
Arsenal imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya baada ya kuiondoa Bayer Leverkusen kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1. Ushindi huo ulinogeshwa na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano uliochezwa usiku wa kuamkia leo Emirates, ambapo mabao mazuri ya Eberechi Eze na Declan Rice yalihitimisha ubabe wa Arsenal baada ya sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza uliopatikana kupitia penalti ya kuchelewa ya Kai Havertz.
Licha ya mashambulizi makali ya Arsenal, kipa wa Leverkusen Janis Blaswich alifanya kazi kubwa kuokoa michomo kadhaa hatari kutoka kwa Gabriel, Bukayo Saka na Leandro Trossard, na kuifanya timu yake kuepuka kipigo kikubwa zaidi. Ushindi huo unaifanya Arsenal kukutana na Sporting Lisbon katika robo fainali.
Sporting Lisbon walifika hatua hiyo kwa njia ya kusisimua baada ya kufanya moja ya 'comeback' kubwa katika historia ya michuano hiyo kwa kuiondoa Bodo/Glimt. Licha ya kufungwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza nchini Norway, Sporting walirejea nyumbani na kushinda 5-0, na kufuzu kwa jumla ya mabao 5-3.
Hii ilihitimisha safari ya kihistoria ya Bodo/Glimt ambao walivutia wengi kwa kufika hatua ya mtoano katika msimu wao wa kwanza, wakizifunga timu kubwa kama Manchester City na Atlético Madrid.
Madrid yaendeleza ubabe dhidi ya Man City, Chelsea hoi

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika mechi nyingine iliyovuta hisia kubwa, Real Madrid waliendeleza ubabe wao dhidi ya Manchester City kwa kuwaondoa kwa mara ya tatu mfululizo katika michuano hii. Madrid walishinda 2-1 katika mchezo wa marudiano uliochezwa Etihad, na kukamilisha ushindi wa jumla wa mabao 5-1 baada ya ushindi mkubwa wa kwanza wa mabao 3-0 nchini Hispania.
Vinicius Jr alikuwa shujaa wa Madrid akifunga mabao mawili, likiwemo penati iliyotokana na kadi nyekundu aliyopata Bernardo Silva kwa kuunawa mpira katika kipindi cha kwanza. Licha ya mashabiki wa City kumzomea, nyota huyo wa Brazil Vinicius Jr, alithibitisha ubora wake kwa kufunga bao la pili dakika za lala salama, akimalizia usiku mzuri kwa Madrid.
Kwa upande mwingine, Paris Saint-Germain walionesha ubora mkubwa kwa kuiangamiza Chelsea kwa jumla ya mabao 8-2. Baada ya kushinda 5-2 katika mchezo wa kwanza jijini Paris, PSG walikamilisha kazi hiyo kwa ushindi wa mabao 3-0 katika uwanja wa Stamford Bridge.
Ndani ya dakika 14 za mwanzo, PSG tayari walikuwa wamefunga mabao mawili na kuzima kabisa matumaini ya Chelsea kurejea, huku bao la tatu likihakikisha kuwa Chelsea wanapokea kipigo chao kikubwa zaidi kuwahi kutokea katika hatua ya mtoano ya michuano hii.
Liverpool, Barcelona zitafanikiwa leo kuvuka?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati huo huo, michezo mingine ya hatua ya 16 bora inaendelea leo, ambapo Liverpool watakuwa nyumbani dhidi ya Galatasaray wakihitaji kubadili matokeo baada ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza, huku mshindi wa mchezo huo akitarajiwa kukutana na PSG katika robo fainali.
Bayern Munich wao wanasafiri kwenda Italia kukabiliana na Atalanta wakiwa na faida kubwa ya ushindi wa mabao 6-1 walioupata nyumbani, na mshindi wa jumla atakutana na Real Madrid.
Katika mechi nyingine, Barcelona wanakutana na Newcastle United baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza, huku mshindi wake akitarajiwa kucheza na atakayefuzu kati ya Tottenham Hotspur na Atlético Madrid, ambapo Atlético wanaongoza kwa jumla ya mabao 5-2 kufuatia ushindi mkubwa katika mchezo wa kwanza.












