Marekani kuishambulia Cuba?

Chanzo cha picha, Aaron Schwartz/UPI/Bloomberg/Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump, amedai kuwa Cuba, ambayo kwa muda mrefu imekumbwa na uhaba wa mafuta kutokana na vikwazo, ni "nchi dhaifu," alisema anaamini ataweza "kukipata" kisiwa hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari katika White House, Trump alisema:
"Katika maisha yangu yote, nimekuwa nikisikia kuhusu ajenda ya Marekani dhidi ya Cuba. Watu walikuwa wakisema, 'Marekani itachukua hatua lini?' Ninaamini nitakuwa na heshima ya kuichukua Cuba."
Alipoulizwa alimaanisha nini kwa kusema "kuichukua Cuba," Trump alisema:
"Ndiyo, kuichukua kwa namna fulani, kuikomboa au kuimiliki. Naweza kufanya chochote ninachotaka nayo. Ni nchi dhaifu sana," na akaongeza kuwa Cuba ni "kisiwa kizuri."
Cuba imekuwa kwenye ajenda ya Trump kwa muda mrefu. Rais huyo wa Marekani mara nyingi amekuwa akisema kwamba wataishughulikia Cuba baada ya kufanikisha malengo yao Iran. Serikali ya Cuba, hata hivyo, imeonesha kutoridhishwa na kauli hizo kutoka Marekani.
Wakati huo huo, Rais wa Cuba Miguel Díaz-Canel amesema kuwa mazungumzo yameanza kati ya nchi hizo mbili ili kupunguza mvutano unaoongezeka kati ya Cuba na Marekani.
Rais wa Cuba Miguel Díaz-Canel alisema tarehe 12 Machi kuwa mazungumzo hayo yanafanyika "kwa lengo la kutafuta suluhisho la tofauti za pande mbili kati ya mataifa hayo mawili kupitia mazungumzo."
Kulikuwa pia na tetesi kwamba mazungumzo hayo kwa niaba ya Cuba yalikuwa yanaendeshwa na mjukuu wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, ambaye pia ana jina linalofanana naye.

Chanzo cha picha, Yamil Lage/ AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Raúl Guillermo Rodríguez Castro mwenye umri wa miaka 41 ni mjukuu na mlinzi binafsi wa Rais wa zamani wa Cuba mwenye umri wa miaka 94, Raúl Castro.
Havana bado haijathibitisha taarifa hii.
BBC Mundo inaeleza kuwa uwepo wa Rodríguez Castro katika mazungumzo hayo pia unaibua swali la "nani hasa hufanya maamuzi nchini Cuba?"
Rais wa Cuba Miguel Díaz-Canel alitangaza tarehe 12 Machi kuwa yeye pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu wanaongoza mazungumzo hayo kwa niaba ya Cuba.
Saa chache kabla ya kauli ya Díaz-Canel, serikali ya Cuba pia ilitangaza kuwaachilia huru wafungwa 51, bila kutoa maelezo zaidi.
Aidha, imeripotiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, ambaye ana asili ya Cuba, alikutana na Rodríguez Castro katika mkutano wa kilele uliofanyika Karibiani mwezi Februari.
Rubio aliwaambia waandishi wa habari tarehe 25 Februari: "Cuba inahitaji mabadiliko makubwa kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuboresha maisha ya watu wake."
Mgogoro ulizidi kuongezeka
Uchumi wa Cuba uliingia katika hatua mpya baada ya kiongozi wa Venezuela Nicolás Maduro kuchukuliwa kwa nguvu na kupelekwa nchini Marekani.
Baada ya mtiririko wa mafuta kutoka Venezuela kupungua katika kipindi cha baada ya Maduro, Cuba imekumbwa na uhaba mkubwa wa mafuta pamoja na kukatika kwa umeme kwa kiwango kikubwa kote nchini.
Baada ya kukatika kwa umeme kwa saa 24 nchini Cuba tarehe 6 Machi, Rais wa Marekani Donald Trump alitoa kauli akidai kuwa "Cuba itaanguka hivi karibuni."
Trump pia alikuwa amesema kuwa Havana ilitaka kufanya mazungumzo na Marekani, kauli ambayo serikali ya Cuba iliikanusha.

Chanzo cha picha, Cubavision
Rais wa Cuba Miguel Díaz-Canel, ambaye alithibitisha kwa mara ya kwanza mazungumzo hayo tarehe 12 Machi, alisema katika hotuba yake kuwa kipaumbele kikuu ni kutatua tatizo la nishati nchini humo.
Kukatika kwa umeme kwa muda mrefu na uhaba wa mafuta kote nchini Cuba kumeathiri vibaya sekta nyingi, kuanzia huduma za afya hadi utalii.
Rais huyo alisema kuwa kutokana na hali hiyo, makumi ya maelfu ya watu wamelazimika kuahirisha shughuli za upasuaji.
Mashirika mengi ya ndege pia yamelazimika kufuta safari kutokana na uhaba wa mafuta.
Chanzo kikuu cha mgogoro huo ni vikwazo vya kiuchumi na zuio la mafuta vilivyowekwa na Marekani, ambavyo vimepunguza sana upatikanaji wa mafuta nchini Cuba.
Mnamo tarehe 3 Januari 2026, Marekani ilimkamata kiongozi wa Venezuela Nicolás Maduro katika operesheni ya kijeshi na kumpeleka New York, jambo lililochangia kusitishwa kwa usambazaji wa mafuta kutoka Venezuela kwenda Cuba.
Wakati huo huo, zuio la kijeshi la majini liliwekwa ili kuzuia usafirishaji wa mafuta kutoka Venezuela.

Chanzo cha picha, YAMIL LAGE / AFP / Getty Images
Baada ya operesheni hiyo, tarehe 11 Januari 2026, Rais wa Marekani Donald Trump alitoa taarifa akielekeza kauli yake dhidi ya Cuba akisema, "Hakutakuwa tena mafuta wala pesa zitakazokwenda Cuba.
Ninawaonya sana wafanye makubaliano kabla hawajachelewa." Hii ilijumuisha ahadi ya kuzuia mtiririko wa mafuta na fedha kutoka Venezuela.
Pia serikali ya Marekani ilitangaza kwamba itaweka vikwazo kwa nchi yoyote inayouza mafuta kwa Cuba.
Cuba kwa miaka mingi ilitegemea karibu nusu ya mahitaji yake yote ya mafuta kutoka Venezuela, ikipokea takriban mapipa 35,000 ya mafuta ghafi.
Rais Díaz-Canel alisema kuwa hakuna mafuta yoyote yaliyoingia kisiwa hicho kwa miezi mitatu iliyopita.
Kukosa mafuta na umeme kumeathiri sana uchumi wa Cuba, ingawa nchi hiyo imejaribu kuongeza uzalishaji wa mafuta na gesi ndani ya nchi na kupanua uwezo wake wa nishati ya jua.
Mnamo tarehe 26 Februari, Marekani ilitangaza itaruhusu kiasi cha mafuta kiingie nchini humo "kwa sababu za kibinadamu," hatua iliyofanywa ili kujaribu kupunguza baadhi ya athari mbaya za vizuizi vya nishati.













