Siku 100 za Rais Samia zenye uzuri na simanzi

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 6

Leo, Februari 10, 2026, ni siku ya 100 tangu Rais Samia Suluhu Hassan aapishwe kuanza awamu yake ya pili ya uongozi wake Novemba 03, 2025. Siku 100 ni muda mfupi katika uongozi wa taifa, lakini mara nyingi ndiyo kioo cha kwanza cha mwelekeo wa mamlaka.

Kwa Rais Samia, siku hizi hazikupita kimya; zilikuja na matumaini makubwa, maswali mazito, na tukio moja lililobadilisha kabisa namna kipindi hiki kinavyotazamwa.

Ni siku 100 zilizoanza na mjadala wa ushindi mkubwa wa kisiasa, akitoka kushinda kwa karibu asilimia 98 katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025. Siku hizi pia zilisindikizwa na hoja mbili kuu: haki na amani zilizojengwa kwa hatua za ahadi nzito za mabadiliko, maridhiano, na mageuzi ya taasisi hasa zinazosimamia demokrasia, uchaguzi na haki. Lakini zaidi, matukio ya Oktoba 29 yalikuwa mstari wa kugawanya simulizi ya siku hizi 100.

Tangu matukio hayo ya maandamano yaliyohusiana na uchaguzi yalipopelekea ghasia, vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali, tathmini ya siku 100 haikuwa tena juu ya ahadi au utekelezaji wake pekee, bali jinsi taifa linavyokabiliana na usalama, haki, amani, na maridhiano baada ya machafuko.

Makala hii haizitazami siku 100 hizi kwa macho ya sifa wala lawama, bali kwa mizani ya uhalisia. Ni jaribio kuelewa kwa nini siku 100 za Rais Samia zinaweza kuitwa zenye uzuri, lakini uzuri uliobeba simanzi.

Tofauti ya siku 100 za urithi wa 2021 na za sasa

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Samia wakati huo akiwa makamu wa rais na Rais John Magufuli, wakizungumza na aliyekuwa rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa njia ya simu, Ikulu Dar es Salaam, Tanzania, Julai 24, 2019.

Siku 100 za kwanza za Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2021 zilikuwa za aina ya kipekee. Aliingia madarakani kupitia urithi wa kikatiba kufuatia kifo cha ghafla cha Rais John Pombe Magufuli. Lengo kuu la siku zile 100 halikuwa kasi ya utekelezaji wa ahadi mpya, bali kurejesha utulivu wa kisiasa, kujenga imani ya kimataifa na kuonesha kuwa dola ilikuwa imesimama imara.

Katika kipindi hicho cha 2021, msisitizo mkubwa ulikuwa katika maridhiano ya kimyakimya, kufungua kidogo nafasi ya kisiasa, kurejesha mahusiano ya kidiplomasia na jumuiya ya kimataifa, pamoja na kuhimiza umoja wa kitaifa. Hakukuwa na shinikizo kubwa la kutimiza ahadi mahsusi za kampeni, kwa kuwa Rais Samia hakuwa amepitia mchakato wa uchaguzi kama mgombea mkuu. Alikuwa mgombea mwenza wa Magufuli. Alitazamwa zaidi Magufuli kuliko yeye aliyekuwa msaidizi wake.

Siku 100 za sasa za awamu ya pili ni tofauti kabisa. Hizi ni siku 100 za uongozi uliopata kupitia uchaguzi uliompa ushindi wa asilimia 98. Kabla ya Oktoba 29, siku hizi zilibeba matarajio makubwa ya utekelezaji wa ahadi, mageuzi ya wazi na mwelekeo mpya wa kisiasa. Ndiyo maana tathmini ya sasa ni nzito zaidi na yenye mizani mikubwa ya matumaini na kutupiana lawama.

Ndani ya tofauti hii ndipo uzito wa matukio ya Oktoba 29 unapoonekana zaidi. Tofauti na 2021 ambako Rais Samia alitarajiwa kuwa msuluhishi na mpatanishi, siku 100 za sasa zimemkuta akiwa katikati ya jukumu la kutekeleza ahadi, kudhibiti dola, usalama na wakati huo huo kushughulikia jeraha la kisiasa lililofungua maswali mapya kuhusu haki, maridhiano na mustakabali wa mageuzi.

Rais Samia alihaidi nini katika siku 100 za kwanza?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati wa uzinduzi wa kampeni zake za uchaguzi mkuu wa 2025, Rais Samia aliahidi kwamba ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa angeanza utekelezaji wa mambo kadhaa muhimu kwa manufaa ya Watanzania.

Miongoni mwa ahadi hizo ni kuajiri jumla ya watumishi 12,000 katika sekta za afya na elimu, kuanza kwa majaribio mpango wa bima ya afya kwa wote, kugharamia kwa asilimia 100 vipimo vya magonjwa makubwa kwa wananchi wasiokuwa na uwezo, pamoja na kupiga marufuku hospitali kuzuia miili ya marehemu kwa sababu ya madeni ya matibabu.

Kwa upande wa elimu na ajira, Rais aliahidi kuajiri walimu 7,000 wa masomo ya hisabati na sayansi. Ahadi nyingine zilihusu kutenga Sh bilioni 200 kwa ajili ya mitaji kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, kuanzisha programu ya viwanda vya wilaya, kuendeleza nishati safi ya kupikia, kuanza ujenzi wa gridi ya taifa ya maji na kuweka mifumo rafiki ya uwajibikaji kwa viongozi wa umma.

Hata hivyo, katika ahadi zote hizo, macho ya wengi yalielekezwa zaidi kwenye ahadi mbili kubwa: Kuanzishwa kwa mchakato wa maridhiano ya kitaifa na kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya ndani ya siku 100.

Uzuri wa siku 100 ulivyofunikwa na Oktoba 29

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Baada ya matukio ya Oktoba 29, upepo wa utekelezaji na ufuatiliaji wa serikali ulibadilika. Siku 100 zilianza kusikika kwa wimbo wa haki na amani kila upande ukizungumza kwa tafsiri yake ya haki na amani. Suala la usalama likachukua nafasi kubwa kuhakikisha nchi inarejea katika hali yake ya kawaida.

Mgawanyiko wa kimtazamo ukaanza kujitokeza, hata kama haukuzungumzwa kwa sauti kubwa katika siku za mwanzo. Akizungumza kwa niaba ya serikali, Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa alisisitiza kuwa suala la msingi kwa wakati huo lilikuwa ni usalama wa taifa.

"Katika siku 100 hizi Tanzania imeonesha namna ambavyo inaweza kuhakikisha nchi iko salama", Msigwa ameiambia BBC.

Wakati wizara na taasisi za serikali zikiendelea na shughuli zake kama kawaida, ajira zikitangazwa, miradi ya ujenzi ikiendelea, bima ya afya kwa wote ikianza kutekelezwa na timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kufuzu 16 bora AFCON kwa mara ya kwanza, mafanikio hayo yalibaki kuwa hayana sauti kubwa katika mjadala wa umma. Yalifunikwa na uzito wa matukio ya Oktoba 29.

Maridhiano, katiba mpya na hoja zingine

a

Chanzo cha picha, MrokiM

Maelezo ya picha, Rais Samia akizungumza na kiongozi wa chama cha upinzani (CHADEMA) Tundu Antiphas Lissu ambaye yuko jela kwa tuhuma za uhaini. Wakati huo walikutana Brussels nchini Ubelgiji, Februari 16 2022, Lissu akiwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho alikuwa uhamishoni

Miongoni mwa mambo makubwa yaliyotarajiwa kuanza ndani ya siku 100 ni mchakato wa maridhiano ya kitaifa na maandalizi ya mchakato wa katiba mpya. Hata hivyo, mambo haya hayajapata mwanzo uliotarajiwa.

Rais Samia, ambaye katika kampeni zake aliahidi kuunda Tume ya Kitaifa ya Maridhiano ndani ya siku 100, amelazimika kubadili mwelekeo wa haraka. Badala ya kuanza moja kwa moja na maridhiano, serikali iliunda kwanza Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29 ili kuchunguza kilichotokea. Kwa mujibu wa serikali, matokeo ya tume hiyo ndiyo yatakayotoa mwelekeo wa maridhiano ya kitaifa.

Kwa upande wa wadau wa siasa, bado kuna mashaka. Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Bara), John Heche, ameeleza wasiwasi wake kuhusu mchakato huo akisema: "Hatuwezi kuingia kwenye maridhiano kukiwa bado kuna wafungwa wa kisiasa." Kauli hiyo inaakisi mtazamo wa sehemu ya upinzani kuwa maridhiano hayawezi kutenganishwa na masuala ya haki na uhuru.

Kwa mtazamo wa kitaaluma, Dk. Onesmo Kyauke wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama alivyonukuliwa na gazeti la Mwananchi, anasisitiza kuwa maridhiano hayawezi kujengwa juu ya kimya. Kwa mujibu wake, maridhiano ya kweli "lazima yatangulize ukweli kwanza kabla ya lawama."

Tazama hapa
Maelezo ya video, Siku 100 za Rais Samia zenye uzuri na simanzi

Ahadi ya kuanza mchakato wa Katiba Mpya ndani ya siku 100 bado imebaki kuwa matarajio ambayo hayajapata mwonekano wa wazi katika utekelezaji wake. Serikali imeeleza kuwa hayajatupwa, lakini kwa wadau wa jamii ya kiraia na siasa, mashaka ya utashi wa kisiasa yanaendelea kutawala.

"Hatukutarajia yangetokea yaliyotokea tarehe 29. Kwa sababu yale yametokea, tunayatatua kwanza. Baada ya muda mfupi tutaendelea na utekelezaji wa ahadi nyingine," alisema Msigwa.

Kwa kauli ya Msigwa, siku 100 zilikuwa za kushughulika na ya oktoba 29 zaidi, ila Katiba mpya na maridhiano nafasi bado ipo na serikali ina utayari wa kuyasimamia kuhakikisha yanafanyika kama yalivyohaidiwa na Rais Samia na chama chake cha CCM kupitia ilani yake ya uchaguzi.

Kwa jumla, siku 100 za Rais Samia katika awamu yake ya pili ni siku zenye sura mbili: uzuri wa mafanikio na uzito wa simanzi. Ni kipindi kinachoacha taifa likiwa katika tafakari, baada ya uchunguzi wa Oktoba 29 na simanzi zake, je, maridhiano na mageuzi yaliyosubiriwa kwa muda mrefu yataanza kuchukua nafasi yake?