Fahamu nchi zinazosheherekea Eid leo

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati Tanzania ikitarajiwa kusherehekea Eid El-Fitri kesho Jumamosi, Machi 21, 2026, baada ya kutokuwepo kwa muandamo wa mwezi wa Shawwal, nchi nyingi duniani zinasheherekea sikukuu hiyo leo Ijumaa.
Taarifa ya Mufti wa Tanzania ilithibitisha kuwa mwezi haukuonekana, hivyo Waislamu nchini watakamilisha siku 30 za Ramadhani kabla ya kusherehekea kesho Jumamosi.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki, tofauti hiyo imejitokeza wazi, ambapo nchi jirani na Tanzania kama Kenya Kaimu Kadhi Mkuu wa Kenya Sukyan Hassan alisema mwezi huo ulionekana katika maeneo kadhaa ya nchi, na uthibitisho wa kutosha kutoka Kaunti ya Kwale hivyo wanakula Eid leo.
Uganda, Sudan, Somalia na nchi zingine ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zinaadhimisha Eid leo. Hali hii imewafanya waumini katika eneo hili kusherehekea kwa nyakati tofauti licha ya ukaribu wao wa kijiografia.
Nchi zinazosherekea Eid leo

Chanzo cha picha, Getty Images
Nchi nyingi zimeadhimisha Eid al-Fitr leo Ijumaa, Machi 20, 2026, baada ya kuthibitisha kuonekana kwa mwezi wa Shawwal.
Miongoni mwa mataifa hayo ni yale ya Mashariki ya Kati kama Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Qatar na Kuwait, pamoja na nchi nyingine kama Uturuki, Maldives, Lebanon, Palestina, Yemen na Iraq.
Hali kama hiyo pia imeonekana katika bara la Afrika, hususan katika nchi za Afrika Kaskazini kama Morocco na Misri, ambazo zimeungana na mataifa ya Ulaya kama Ubelgiji katika kusherehekea siku hii moja.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki, nchi za Kenya, Uganda, Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia na Somalia zimeadhimisha Eid leo, tofauti na Tanzania.
Katika mji wa Mogadishu nchini Somalia, waumini walikusanyika kwa wingi kuswali Swala ya Eid katika misikiti mbalimbali ikiwemo Alliance Mosque, wakionesha furaha na mshikamano mkubwa katika siku hii muhimu ya Kiislamu.
Nchi zinazosherekea Eid kesho

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati huo huo, baadhi ya nchi zimepanga kusherehekea Eid siku ya Jumamosi, Machi 21, 2026, baada ya kutokuonekana kwa mwezi wa Shawwal katika maeneo yao. Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo, kufuatia tangazo rasmi la Mufti wa taifa.
Nchi nyingine zitakazofuata utaratibu huo ni pamoja na India, Bangladesh, Sri Lanka na Malaysia, ambako mamlaka za kidini zimethibitisha kukamilika kwa siku 30 za Ramadhani kabla ya kuanza kwa sikukuu ya Eid.
Aidha, katika baadhi ya mataifa kama Iran, maadhimisho ya Eid pia yameahirishwa hadi siku inayofuata, kufuatia taratibu zao za kidini na uthibitishaji wa mwezi.
Hali kama hii imekuwa ya kawaida kila mwaka, ambapo baadhi ya nchi huadhimisha sikukuu kwa nyakati tofauti kulingana na maamuzi ya mamlaka zao.
Kwanini siku ya Eid hutofautiana

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Eid al-Fitr huanza baada ya kuonekana kwa mwezi wa Shawwal. Kutokuwepo kwa mwangaza wa mwezi au hali ya hewa tofauti husababisha baadhi ya nchi, kama Tanzania, kusherehekea Eid siku tofauti. Mamlaka za Tanzania zilisema mwezi Shawwal haujaonekana Alhamisi ya Machi 19 hivyo Eid itakuwa Jumamosi, wakikamilisha siku 30 za mwezi Ramadhani.
Kwa ujumla tofauti ya siku ya kusherehekea Eid al-Fitr hutokana na mbinu mbalimbali zinazotumika kuthibitisha kuanza kwa mwezi mpya wa Kiislamu. Katika baadhi ya nchi, hususan zile zinazotegemea ushuhuda wa moja kwa moja, mwezi wa Shawwal lazima uonekane kwa macho ndipo sikukuu ithibitishwe. Endapo hauonekani, Ramadhani huongezwa kwa siku moja zaidi.
Kwa upande mwingine, baadhi ya mataifa hutumia hesabu za kisayansi za anga kutabiri muandamo wa mwezi, jambo linalowawezesha kutangaza mapema tarehe ya Eid.
Mbali na hilo, tofauti za kijiografia pia huathiri muonekano wa mwezi, kwani unaweza kuonekana katika eneo moja na usionekane katika eneo lingine duniani.
Vilevile, tofauti za kimadhehebu na mifumo ya mamlaka za kidini huchangia utofauti huu, ambapo baadhi ya jamii hufuata maamuzi ya viongozi wao wa kidini au taasisi maalum katika kuthibitisha siku ya sikukuu.
Hata hivyo, licha ya tofauti hizi, Eid El-Fitri hubaki kuwa siku ya furaha, mshikamano na shukrani kwa Waislamu duniani kote baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.













