Afrika inavyohaha kwenye mpangilio mpya wa dunia

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Damian Zane
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Wakuu wa nchi za Afrika wanakusanyika mwishoni mwa wiki hii katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kwa mkutano wao wa kila mwaka katika wakati ambao nafasi ya bara hili katika siasa za kimataifa inaonekana kubadilika kwa kasi.
Mwezi uliopita huko Davos, Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, alitoa taswira yenye mvuto kuhusu mustakabali wa uhusiano wa kimataifa: Ima mataifa yako mezani yakishiriki maamuzi, au yako kwenye menyu yakisubiri kuliwa.
Kwa viongozi wa Afrika, ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakisisitiza kuwa wanastahili kuketi katika "meza kuu" ya maamuzi ya dunia, tamko hilo si geni.
Hata hivyo, katika muhula wake wa pili, Rais wa Marekani, Donald Trump, ameongeza kasi ya mwelekeo wa siasa za nguvu za mataifa makubwa na kupunguza uzito wa ushirikiano wa kimataifa (multilateralism).
Mkakati uliosasishwa wa usalama wa Ikulu ya Marekani unaeleza wazi kuwa si kila kanda ya dunia inaweza kupewa kipaumbele sawa.
Mwelekeo wa Trump kuelekea zaidi Amerika Kaskazini na kusini pamoja na Mashariki ya Kati umeashiria kupungua kwa umakini kwa Afrika.
Kwa mataifa yenye nguvu kidogo, ambayo hapo awali yalitegemea kanuni na ufadhili wa taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa, Benki kuu ya Dunia, Shirika la Biashara Duniani, hali hii inalazimisha tathmini upya ya mahusiano yao ya kimataifa.
Hatua hizi zimeongeza uharaka wa swali: Afrika inapaswa kushughulika vipi na dunia katika zama hizi mpya?
Kwa mujibu wa Tighisti Amare wa taasisi ya Chatham House, kuna hatari ya nchi za Afrika "kuachwa nyuma" ikiwa hazitaendeleza mkakati wa pamoja na madhubuti.
Wakati huo huo, kwa mtazamo wa Marekani, tayari kuna "menyu" iliyojaa mikataba ya moja kwa moja (bilateral) inayohusu madini na rasilimali asilia, mikataba inayopunguza nafasi ya Afrika kujadiliana kwa pamoja kama bara.
Linapokuja suala la Afrika, mabadiliko ya sera yanayoakisiwa katika matamshi kutoka Washington yanatia kizunguzungu.

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Miaka mitatu iliyopita, Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden, aliwaambia viongozi wa Afrika mjini Washington kwamba "Marekani imejitoa kikamilifu kwa mustakabali wa Afrika."
Hii ilifuatia waraka wa mkakati wa Ikulu kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara uliolitaja eneo hilo kuwa muhimu kwa vipaumbele vya kimataifa vya Marekani.
Hata hivyo, wakosoaji walihoji iwapo kauli hizo ziliakisi dhamira ya kweli ya kisera, hasa ikizingatiwa kuwa ziara yake pekee ya rais katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ilifanyika mwishoni mwa muhula wake Cape Verde na Angola.
Kinyume chake, sera ya "America First" ya Trump ina mtazamo finyu zaidi kuhusu maslahi ya Marekani.
Mkakati wa usalama wa taifa wa Novemba uliopita ulisisitiza kuwa ''Marekani haiwezi kuwa makini kwa kiwango sawa kwa kila kanda au kila tatizo duniani''.
Aya chache zilizoihusu Afrika zilieleza ushirikiano na "nchi zilizoteuliwa" kupunguza migogoro, kukuza biashara ya manufaa ya pande zote, na kuhamisha mkazo kutoka misaada kwenda uwekezaji na ukuaji wa uchumi.
Kwa Peter Pham, ambaye alikuwa mjumbe maalum kwa Afrika wakati wa utawala wa kwanza wa Trump, hii ni njia ya uaminifu zaidi.
"Nilifunzwa katika shule ya uhalisia ya mahusiano ya kimataifa," aliiambia BBC, "na sidanganyi vya kutosha kufikiri kwamba Afrika ni mbele na kitovu cha maslahi ya Marekani kama vile pengine mbele na katikati ya maisha yangu.
"Hakuna jinsi nchi yoyote, hata inayotajwa ina nguvu zaidi duniani, inaweza kuwa mambo yote kwa kila mtu. Ukweli ni kwamba hatuna uwezo mpana au rasilimali zakutosha, kuwa wakarimu kama watu wa Amerika, kufanya kila kitu kwa kila mtu.
"Kwa hivyo inabidi tuzimiliki rasilimali hizo na kuzisimamia kadri tuwezavyo ili kufikia matokeo bora kwa raia wetu, lakini pia washirika wetu wakubwa."

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwelekeo huu umejidhihirisha wazi katika makubaliano ya madini kati ya Marekani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaliyosainiwa mwezi Desemba mwaka jana, sambamba na makubaliano ya amani na Rwanda.
Lengo lilikuwa kujenga minyororo salama na ya kuaminika ya usambazaji wa madini muhimu kwa viwanda vya teknolojia vya Marekani, huku yakihamasisha uwekezaji nchini DR Congo, yenye akiba kubwa ya madini muhimu kwa utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki.
Pham mwenyewe ni sehemu ya makubaliano mengine, kwani yeye ni mwenyekiti wa Ivanhoe Atlantic, kampuni inayohusika na maendeleo ya "Liberty Corridor" - mradi wa kujenga miundombinu mipya inayounganisha migodi mikubwa ya madini ya chuma ya Guinea na bandari ya Liberia, kwa lengo la kuongeza mauzo ya malighafi hiyo nje ya nchi.
Hata hivyo, wachambuzi kama Ken Opalo wa Chuo Kikuu cha Georgetown wanaonya kuwa mbinu hii ya kibiashara ya moja kwa moja inaweza kudhoofisha uwezo wa nchi za Afrika kujadiliana kwa manufaa makubwa zaidi.
Aliiambia BBC kwamba ikiwa "mfano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni kigezo cha kuangalia, basi mkazo wa Marekani kwenye madini unalenga zaidi kupata haki za uchimbaji kwa kampuni za Marekani, na si zaidi ya hapo katika suala la ushirikiano mpana wa kiuchumi, jambo ambalo halihitajiki na ukanda huu."
''Afrika inahitaji zaidi ya haki za uchimbaji, inahitajika upatikanaji mpana wa masoko, mikataba ya uwekezaji, na uwezo wa kuvutia mtaji katika sekta zote, si madini pekee'', anasema Opalo.
Waziri wa Madini wa DR Congo, Louis Watum Kabamba, akiwa Afrika kusini wiki hii, amekanusha hofu hizo, akisisitiza kuwa nchi yake "haitauza kila kitu bure kwa Marekani."
Ni wazi kuwa Marekani si mhusika pekee.
Kwa zaidi ya muongo mmoja, China ilizidi Marekani kwa uwekezaji wa moja kwa moja barani Afrika, ingawa hali hiyo ilibadilika mwaka jana.
Aidha, mataifa kama Urusi, Uturuki na Falme za Kiarabu (UAE) pia yamekuwa yakisaini mikataba yao ya uwekezaji na usalama.
Kwa mujibu wa Opalo, tatizo si lazima liwe katika asili ya mikataba ya kibiashara, bali katika ukosefu wa mkakati wa kina na utaalamu wa kidiplomasia ndani ya serikali nyingi za Afrika.
Hatari iliyopo ni viongozi kutafuta ushindi wa haraka bila kuzingatia athari za muda mrefu.
Katika uwanja wa usalama, kushindwa kwa Afrika kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, ambavyo Umoja wa Mataifa imevitaja kama janga baya zaidi la kibinadamu duniani kwa sasa ni mfano wa changamoto hiyo.
Licha ya msimamo wake wa kutangaza kutopendelea upande wowote, Uturuki imetuhumiwa kuipatia silaha jeshi la Sudan. Iran na Urusi pia zinakabiliwa na tuhuma kama hizo. Mataifa yote hayo yamekanusha madai hayo, lakini Februari mwaka jana Urusi ilisaini makubaliano na serikali ya kijeshi ya Sudan ya kuanzisha kambi ya kijeshi ya majini nchini humo.
Kwa upande mwingine, Falme za Kiarabu (UAE) imetuhumiwa kuyaunga mkono Vikosi vya Msaada wa Haraka (Rapid Support Forces), jambo ambalo pia imelikanusha.
"Imeshindikana kwa Afrika kutatua mgogoro wa Sudan ni dalili ya ukosefu wa uwezo wa bara kujitawala na kuamua hatma yake yenyewe," amesema Opalo.

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Ghana, John Mahama, anajaribu kubadili mwelekeo huu.
Akiwa pia Davos, alionya kuwa dunia iko katika "wakati wa mgeuko" huku kukiwa na "mshirika asiyeweza kutabirika" ng'ambo ya Atlantiki na kupungua kwa misaada ya maendeleo.
Afrika lazima ijikomboe na kujinasua kwa nguvu zake yenyewe'' anaeleza.
Kwa msisitizo mkubwa, Mahama alisema Afrika imepoteza sehemu ya uhuru wake na kunaswa katika mtego wa utegemezi iwe katika sekta za afya na elimu au masuala ya usalama.
Kuhusu rasilimali asilia, alibainisha: "Tunatoa madini muhimu kwa dunia, lakini hatupati thamani inayostahili."
Kupitia mpango wake wa "Accra Reset", anapendekeza uwekezaji mkubwa katika ujuzi unaohitajika, viwanda vilivyoratibiwa kikanda, na majadiliano ya pamoja ya bara zima na washirika wa nje.
Hata hivyo, kauli kama hizi zimewahi kusikika hapo awali. Swali linalobaki ni kama safari hii kutakuwa na utekelezaji wa dhati.
Kwa mujibu wa mchambuzi Tighisti, changamoto kuu ni kwamba ili kuunda sauti ya pamoja, viongozi wanapaswa kuweka mbele maslahi ya kikanda, hata kama wakati mwingine italazimu kuweka pembeni baadhi ya maslahi ya kitaifa. Bila kufanya hivyo, uwezo wa Afrika kushawishi majadiliano ya kimataifa utabaki mdogo.
Barani Afrika, mataifa yenye uzito wa kati yanayoweza kuongoza juhudi hizo ni pamoja na Nigeria, Misri, Ethiopia, Kenya na Afrika Kusini. Hata hivyo, changamoto za ndani katika nchi hizi mara nyingi huwafanya viongozi kujikita zaidi katika siasa za nyumbani kuliko ajenda ya muungano wa bara.
Tayari kuna mifumo ya ushirikiano kama Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika- mpango kabambe wa mageuzi ya bara, lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.
Akiwa Davos, Mahama alisisitiza kuwa "Afrika inakusudia kuwa mezani" katika kuamua sura ya utaratibu mpya wa dunia. Lakini kufikia hapo kunahitaji kazi kubwa: kuimarisha mshikamano wa bara, kujenga uwezo wa majadiliano, na kuhakikisha kuwa mikataba ya kimataifa inaleta manufaa endelevu kwa wananchi wake.
Kwa sasa, mwaliko wa chakula bado haujatumwa na hatma ya Afrika itategemea kama itaweza kuketi mezani kama mshiriki kamili au kubaki kwenye menyu ya wengine.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












