Je, Wahouthi watasababisha mshtuko mwingine wa soko la mafuta huko Bab al-Mandab?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Vita vya Iran vimefikia kilele katika bahari ya shamu, mlango bahari ambao ukifungwa unaweza kusababisha mzozo kamili wa nishati duniani.

Wikiendi hii, mwezi mmoja baada ya Marekani na Israel kuanza vita na Iran, washirika wa Iran nchini Yemen, Houthis, hatimaye wameingilia vita hivyo.

Hadi sasa mashambulizi yao yamekuwa yakionya zaidi na yameilenga Israel, lakini Wahouthi wanaweza kupanua mashambulizi yao kwenye bomba la mafuta la Saudi Arabia na kituo cha mafuta cha nchi hiyo katika Bahari ya shamu wakati wowote.

Baada ya Iran kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz, njia pekee sasa kutoka Ghuba ya Uajemi ambapo asilimia 25 ya mafuta duniani na asilimia 20 ya gesi inapita ni mlango bahari wa Bab -al - Mandab.

Awali, Saudi Arabia ilihamisha karibu theluthi moja ya mauzo yake kwenda kwenye kituo chake cha Bab -al Mandab ambacho kilikuwa kimejengwa wakati wa vita vya Iran na Iraq.

Kwa mabadiliko haya ya njia, bei ya mafuta duniani haikupanda kama ilivyotarajiwa. Saudi Arabia, ambayo ni miongoni mwa nchi tatu zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani pamoja na Marekani na Urusi, ilisafirisha takriban mapipa milioni 6 ya mafuta kwa siku kupitia Hormuz kabla ya vita hivyo na sasa inafikisha takriban mapipa milioni 5 sokoni kupitia njia ya Yanbu.

Sehemu kubwa ya mafuta hayo husafiri hadi Asia kupitia Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab, njia ambayo imevurugwa mara kwa mara katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na Wahouthi, kundi la Washia nchini Yemen wanaodhibiti sehemu kubwa za nchi hiyo na kuungwa mkono na Iran.

Lakini pamoja na kuanza kwa vita vya Iran, Houthis walikuwa kimya kwa muda.

Ukimya huo ulivunjwa mwishoni mwa juma. Jumamosi asubuhi, walirusha makombora kuelekea Israel na kuonya kwamba hawataacha kushambulia maadamu vita vinaendelea. Usiku huohuo, shambulio jingine lilifanywa.

Wachambuzi walikuwa wametabiri hali kama hiyo mapema. Kwa mujibu wao, Wahouthi, licha ya kuungwa mkono na Iran, ni jeshi huru na wataingia vitani tu iwapo Iran itakabiliwa na tishio kubwa na muhimu.

April Ely, mtaalamu wa Yemen katika taasisi ya wataalam ya Washington, alisema kabla ya mashambulizi ya kwanza: "Uamuzi wa kwenda vitani utafanywa Yemen, sio Tehran."

Alitabiri kwamba Wahouthi wangeilenga Israel kwanza, kama walivyofanya, na kisha kuelekea kwenye mvutano unaozidi.

"Pamoja na Mlango-Bahari wa Hormuz kufungwa, shambulio dhidi ya meli katika Bahari ya shamu linaweza kuweka shinikizo kubwa zaidi kwa soko la nishati na usafirishaji wa meli duniani, haswa wakati huu ambao Saudi Arabia imeongeza mauzo yake ya mafuta kupitia njia hii."

"Mapinduzi ya Kiislamu yenye rangi na ladha ya Yemen"

Uamuzi wa Wahouthi kuingia vitani uliambatana na kuwasili kwa meli ya kivita ya Marekani kutoka Japan hadi Mashariki ya Kati; meli ambayo hubeba maelfu ya Wanamaji na, ikihitajika, inaweza kutumika katika shughuli kama vile kukamata Kisiwa cha Kharg (moyo wa mauzo ya mafuta ya Iran).

Baada ya mwezi mmoja wa majaribio bila mafanikio ya kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu kusalimu amri kwa njia ya mashambulizi ya mabomu na mauaji ya viongozi wake, Donald Trump anaendelea kusema kuwa hana nia ya kutuma wanajeshi kwa ajili ya operesheni za ardhini nchini Iran, ingawa anaongeza kuwa iwapo atachukua uamuzi huo, hatatangaza mapema.

Wakati huo huo, majibu ya ongezeko hili yametoka kwa washirika wa Iran: Houthis. Tishio lao ni kubwa. Ikiwa Saudi Arabia pia itapoteza njia yake mbadala ya kusafirisha mafuta, uhaba wa usambazaji unaweza kusababisha kupanda kwa bei mpya, ambayo imepanda kutoka karibu dola 70 hadi $ 115 kwa pipa katika mwezi mmoja tu wa vita.

"Wahouthi wametangaza vita na kuishambulia Israel, lakini swali la kweli ni ikiwa lengo lao lifuatalo litakuwa kituo cha mafuta cha Yanbu au bomba la Saudi Mashariki-Magharibi," alisema Gregory Brough, mtaalam wa mafuta na Iran katika kampuni ya kimataifa ya ushauri.

"Ikiwa miundombinu hii itashindwa, uhaba wa mafuta utaongezeka kutoka mapipa milioni 10 kwa siku hadi mapipa 13 hadi milioni 15 kwa siku."

Mtaalamu wa Yemen Michael Knights anaonya kuwa sio tu Wahouthi, lakini pia Iran yenyewe inaweza kulenga miundombinu hii ikiwa ni lazima.

Anasema hata kama Iran itashindwa katika vita hivyo, Wahouthi watasalia kuwa nguvu inayovuruga utulivu katika eneo hilo.

"Nimekuwa nikisoma Houthis kwa umakini tangu miaka ya 1980," asema Bw. Knights. "Hao ndio wafuasi wa kweli wa Mapinduzi ya Kiislamu, na wanaweza kushinda hata Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Hezbollah huko Lebanon, na kuwa ngome ya mwisho ya mapinduzi haya - ingawa kwa ladha ya Yemeni."