Tarique Rahman Waziri mkuu wa Bangladesh ni nani?

Chanzo cha picha, Bangladesh Nationalist Party (BNP)/Reuters
Tarique Rahman amechaguliwa kuwa Waziri mkuu wa Bangladesh kupitia chama cha Bangladesh Nationalist Party (BNP) ambacho kilishinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Februari 2026.
Rahman,mwenye umri wa miaka 60, anatokea kwenye familia yenye ushawishi mkubwa ya Zia, ambao wamekuwa katika ulingo wa siasa kwa miongo kadhaa. Babake na mamake wamewahi kuwa viongozi nchini Bangladesh.
Katika safari yake ya siasa Rahman ametuhumiwa na wapinzani wake kuwa na mapendeleo, ufisadi, na kuishi uhamishoni baada ya kuuawa kwa babake.
Alichukua uongozi wa chama cha BNP wiki chache tu kabla ya uchaguzi mkuu wa Bangladesh, baada ya kifo cha mamake Khaleda Zia, ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri mkuu nchini humo kuanzia mwaka wa 1991 hadi 1996.
Babake Ziaur Rahman ambaye alikuwa mwanajeshi, baadaye akawa rais wa taifa hilo, aliuawa katika mapinduzi ya serikali yaliyotokea mwaka wa 1981. Alikuwa ameongoza mapambano ya kupata uhuru nchini humo na kuanzisha chama cha BNP mwaka wa 1978.
Rahman alijiunga rasmi na siasa na kujihusisha na siasa za chama cha BNP mwaka wa 2001.
Mwaka wa 2002, Rahman alianza kufuata nyayo za wazazi wake, na kupewa cheo katika chama cha BNP.
Wakati huo upinzani ulitaja hatua hiyo kama mapendeleo na kuonekana kama mtu aliyekuwa na msimamo tofauti na kuwaadhibu walioenda kinyume na maadili ya chama hicho.
Rahman pia ametuhumiwa hapo nyuma kwa kutumia madaraka aliyonayo kwa maufaa yake binafsi, na amekanusha kuhusika na ufisadi wowote.
Alikamatwa mwaka wa 2007 kwa madai ya ufisadi na serikali ya mpito ya kijeshi. Alizuiliwa kwa miezi 18 gerezani kabla ya kuachiliwa na kutorokea mjini London, Uingereza.
Rahman alirejea Bangladesh baada ya miaka 17 ya kuwa uhamishoni.

Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya kuishi nje ya nchi, Rahman aliendelea kujihusisha na kuunda sera na mikakati ya chama cha BNP, na alikuwa anakaimu kama mwenyekiti wa chama hicho kuanzia mwaka wa 2018, baada ya mamake kufungwa jela.
Alirejea nchini Bangladesh tarehe 25 mwezi Disemba 2025. Siku tano baadaye, mamake mzazi aliaga dunia.
Tarehe 9 Januari alitangazwa kama kiongozi wa BNP.
Katika uchaguzi uliofanyika tarehe 12 Februari 2026, chama cha BNP kiliongoza kwa kupata kura nyingi zaidi.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula












